Tafuta

Injili ya Dominia ya 33 ya Mwaka C. Injili ya Dominia ya 33 ya Mwaka C. 

Dominika ya 33 ya Mwaka C:Nyakati za mwisho na ujio wa Pili wa Yesu

Tuweke juhudi katika kujitayarisha na kujiweka katika hali ya neema na“tusichoke wala kukata tamaa katika kutenda mema”(2The 3:13),kwa sababu tukivumilia mpaka mwisho katika kuisimamia kweli na haki,hautapotea hata unywele mmoja wa vichwa vyetu (Lk 21:18),bali thawabu yetu ni kubwa mbinguni(Mt 5:11-12),kwa maana tuwe hai au tumekufa,tu mali ya Bwana(Rum 14:8).

Na Padre Paschal Ighondo, – Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya 33 mwaka C wa kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Ujumbe mkuu umejikita katika nyakati za mwisho za maisha ya kila mtu hapa duniani kwa njia ya kifo, na hukumu yake kadiri alivyoishi maisha yake. Ujumbe huu sio wa kuogofya, bali kutukumbusha kuishi vizuri maisha yetu kwa kutenda mema kama Mungu anavyotuwazia mema daima. Ni katika muktadha huu zaburi ya wimbo wa mwanzo inavyosema; “Bwana asema: Mawazo ninayowawazia ninyi ni mawazo ya amani wala si ya mabaya. Nanyi mtaniita nami nitawasikiliza, nami nitawarudisha kutoka mahali pote watu wenu waliofungwa” (Yer. 29:11, 12, 14). Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali; “Ee Bwana Mungu wetu, tunakuomba utujalie tufurahi daima katika kukutumikia, maana kama tunapokutumikia daima wewe Mwumba wa mema yote, tunayo heri iliyo kamili siku zote”.

Somo la kwanza ni la kitabu cha Nabii Malaki (Mal 3:19-20). Hiki ni moja ya vitabu vya manabii wadogo 12, na ni cha mwisho kwenye orodha ya vitabu vya Agano la Kale.  Malaki, jina la Kiebrania, maana yake ni “mjumbe wangu”, ni kifupisho cha jina “Malakia”, lenye maana ya “Mjumbe wa Bwana” (Mal 1:1). Nabii huyu aliishi katika nusu ya pili ya karne 5 KK, baada ya uhamisho wa Babeli na kujengwa tena kwa hekalu la Yerusalemu. Ni kipindi ambapo waisraeli walitegemea maisha bora, yenye amani, utulivu, ustawi na haki, kama walivyoahidiwa na Mungu kwa njia ya manabii wengine. Ahadi hii ilibaki kuwa ndoto, kwani maskini, idadi kubwa ya watu, walionewa na viongozi na matajiri, watu wachache waliojitajirisha kwa kuwatumikisha wengine kazi za suluba na dhuluma. Maisha ya kiimani na kimaadili yalizorota, watu walikengeuka, wakaacha kutoa zaka na dhabihu hekaluni, wakaoa wanawake wa mataifa mengine, wakaabudu miungu yao, wakatenda maovu mengi.

Katika hali hii nabii Malaki anatabiri ujio wa Siku ya Bwana, siku ya hukumu ya haki, ambapo waovu wataadhibiwa, na waaadilifu kuponywa. Hii ni siku ambapo wenye haki watasitawi na kushangilia, waovu watateseka na kuomboleza, hasira ya Mungu itakuwa juu yao, nao wataiona ghadhabu yake. Fadhaa, ukiwa, giza, dhiki, uharibifu na maombolezo vitawashukia watu waovu. Fedha na dhahabu zao zitakuwa bure, hazitaweza kuwaokoa, vyote vitakuwa na ukomo wa kutisha. Lakini walio waadilifu na waaminifu kwa Mungu, jua la haki litawazukia na kuwaponya majeraha yao. Hii ni siku ambayo Mungu atajibu kilio cha waadilifu, na kuwaangamiza waovu, siku ya kutangaza ushindi dhidi ya dhambi na mauti.

Huu ni ujumbe wa matumaini kwa wanaodhulumiwa na kuteswa, kuwa siku inakuja, Mungu atanyoosha mkono wake kuwaokoa na kuwapa heri, nao waovu watakiona cha mtema kuni. Hivyo tusife moyo, bali tujae matumaini tukiingojea Siku ya Bwana, kwani Mungu hawezi kukaa kimya kwa wanyofu wa moyo, wala kuziba masikio kwa kilio chao. Ni katika muktadha huu zaburi ya wimbo wa katikati inasema; “Mwimbieni Bwana zaburi kwa kinubi, kwa kinubi na sauti ya zaburi, kwa panda na sauti ya baragumu, shangilieni mbele za Mfalme, Bwana. Bahari na ivume na vyote viijazavyo, ulimwengu nao wanaokaa ndani yake. Mito na ipige makofi, milima na iimbe kwa furaha mbele za Bwana. Kwa maana Bwana anakuja aihukumu nchi, atauhukumu ulimwengu kwa haki, na mataifa kwa adili” (Zab. 98:5-9).

Somo la pili la waraka wa pili wa Mtume Paulo kwa Wathesalonike (2Thes 3:7-12). Ni mawaidha kuhusu ujio wa pili wa Yesu Kristo. Wakristo wa Kanisa la mwanzo waliisubiri kwa shauku kubwa sana siku hivyo. Lakini kadiri mda ulivyozidi kusonga mbele, waliona kuwa Yesu anachelewa sana kurudi na pengine harudi tena kabisa. Hivyo wapo waliokata tamaa na kuanza kuiacha imani yao na wengine kwa kufuata mafundisho ya uongo waliona kuwa mda ulibaki mfupi sana wa Yesu kurudi kuja kuwachukuwa. Hivyo walioona hakuna sababu ya kufanya kazi, wala kuhangaika na nyajibu za maisha ya kila siku.

Ni katika mazingira hayo mtume Paulo anatoa mawaidha na mafundisho sahihi na kukanusha mafudhisho potofu kuhusu ujio wa pili wa Kristo. Kwa kuwa hakuna anayejua siku, saa, mda wala namna atakavyo kuja Kristo, ni kazi bure kuwaza juu ya hilo. Vitu vya msingi ni hivi; kutokukata tamaa, kudumu katika imani, kutenda mema bila kukoma, na kufanya kazi kwa bidii ili kujipatia mahitaji ya kila siku, na mtu asiyefanya kazi hastahili kula. Hili ni onyo kwa wasio na utaratibu katika maisha, wasiopenda kufanya kazi, wanajishughulisha na mambo ya wengine, waache tabia hiyo, wafanye kazi kwa bidii, wapate chakula na mahitaji yao ya kila siku. Ndivyo tunavyopaswa kuishi maisha yetu, tukijua kuwa kuna siku tutakufa na kuhukumiwa mbele za Mungu kwa haki, kadiri tulivyoishi.

Injili ni ilivyoandikwa na Luka (Lk 21:5-19). Sehemu hii ya Injili inahusu utabiri wa Yesu kuhusu mambo na matukio yanayoambana na nyakati za mwisho, ujio wake wa pili: Kuharibiwa kwa mji wa Yerusalemu, kubomolewa hekalu lake, kutokea kwa vita, matetemeko ya ardhi, njaa, na magonjwa, kuzuka kwa dhulumu, fitina, chuki, usaliti, kukamatwa kamatwa, kuteswa na kutupa gerezani, na kuuawa kwa wanaopigania ukweli, haki na amani kwa jina la Yesu. Katika mazingira haya watatokea manabii wa uongo wanaohubiri na kutabiri kwa jina la Yesu, na wengine kujifanya wao ni Yesu, wakisema mimi ndiye. Tahadhari, tunaposikia habari hizi, sisi tulio wafuasi wake Kristo hatupaswi kuyumbishwa na mafundisho potovu ya manabii wa uongo, tusiwafuate wala kuwasikiliza, watatupoteza. Tena tukiona mambo haya yanatokea, tusisikitike wala kuogopa, maana hayo hayana budi kutokea kwa sababu ya udhalimu na uovu wa mwanadamu. Lakini hayo sio ishara ya nyakati za mwisho.

Lengo la utabiri wa mambo ya kutisha sio kututisha, bali kutufanya tuishi vyema maisha yetu na ikitokea tumekosea, tukatenda dhambi, tuzijutie na kuzitubu haraka iwezekanavyo, ili siku hii itukute tuko tayari kuingia katika ufalme wa Mungu mbinguni. Lakini pia ni ujumbe wa kututia moyo kuwa tunapokumbwa na mateso na madhulumu, tusimame imara, tusifadhaike, tusiogope wala kuwa na wasi wasi, bali tuwe jasiri na imara, tuweke bidii katika sala, maombi, na mafungo, tukijibidisha kutenda matendo mema kwa upendo, tujivike moyo wa msamaha, ili tuwe na muunganiko na Mungu Baba Yetu, na tukiwa na muunganike naye, tutakuwa na ujasiri, tutafurahi kwa kurukaruka na kushangilia, kwa kuwa Mungu yupo pamoja nasi, hakuna cha kutushinda. Hivyo tuweke juhudi katika kujitayarisha na kujiweka katika hali ya neema, na “tusichoke wala kukata tamaa katika kutenda mema” (2The 3:13), kwa sababu tukivumilia mpaka mwisho katika kuisimamia kweli na haki, hautapotea hata unywele mmoja wa vichwa vyetu (Lk 21:18), bali thawabu yetu ni kubwa mbinguni (Mt 5:11-12), kwa maana tuwe hai au tumekufa, tu mali ya Bwana (Rum 14:8).

Basi tukumbuke daima kuwa subira yetu itaziponya nafsi zetu kwani mwenye subira hufikiri vyema tena kwa undani na upana wake. Hivyo yatupasa kukesha kila wakati ili Bwana ajapo tuwe tayari kumlaki naye kutushirikisha Ufalme wa mbingu aliotuandalia kabla ya kuumbwa Ulimwengu. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali hivi; “Ee Bwana, tunaomba sadaka tuliyotoa mbele ya macho yako wewe mtukufu, itupatie neema ya kukutumikia na kutuletea heri ya milele”. Na katika sala baada ya komunyo anasali; “Ee Bwana, tumepokea mapaji ya fumbo hili takatifu; na sasa tunakuomba kwa unyenyekevu, hayo aliyotuamuru Mwanao tuyafanye kwa ukumbusho wake, yafae kutuongezea mapendo yako”. Na hili ndilo tumaini letu.

Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari neno la Mungu Dominika XXXIII
14 Novemba 2025, 11:40