Tafuta

Kristo ni Mfalme wa Ulimwengu. Kristo ni Mfalme wa Ulimwengu. 

Dominika ya XXXIV ya Mwaka C:Kristo Mfalme wa Amani,si kwa Silaha bali kwa Msalaba

Yesu Kristo ni Mfalme wa mbingu na wa ulimwengu wote, ni Mfalme wetu,sio kwa hila au dhuluma, wala kwa kupigiwa kura,wala kwa mapinduzi ya kijeshi, wala kwa kurithi bali kwa asili. Ufalme wake ni ufalme uzidio falme zote na enzi na tawala na usultani na utwa na uchifu na mamlaka.Ni ufalme ulio utimilifu wa ahadi ya Mungu,kilele cha ufalme wa enzi na fahari ya Kiti cha kifalme cha Daudi mtumishi wake.

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

“Kristo Mfalme wa Amani, si kwa Silaha bali kwa Msalaba.” Karibu mpenzi msikilizaji/Msomaji  na msomaji wa tafakari ya neno la Mungu kutoka hapa Radio Vatican leo Dominika ya 34, ambayo ni Dominika ya mwisho katika kalenda ya liturujia ya mwaka wa kanisa na tukumbuke ndio tumehitimisha mwaka C, daima hii dominika tunamwadhimisha Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu leo ni sherehe kubwa sana kwetu wakristo. Leo tunasherehekea Sherehe ya Kristo Mfalme, tukifunga rasmi mwaka wa liturujia. Hili ni somo la imani yetu: kwamba mwisho wa yote, Kristo ndiye atakayeshika hatamu ya dunia na mioyo ya wanadamu. Alleluia, ni ufalme wa Mungu na wa Kristo wake… ufalme wa zamani zote, za kale, za sasa na zamani zijazo, milele na milele, alleluia!

Yesu Kristo ni Mfalme wa mbingu na wa ulimwengu wote, ni Mfalme wetu… sio kwa hila au dhuluma, wala kwa kupigiwa kura, wala kwa mapinduzi ya kijeshi, wala kwa kurithi bali kwa asili. Ufalme wake ni ufalme uzidio falme zote, na enzi, na tawala, na usultani, na utwa, na uchifu, na mamlaka… ni ufalme ulio utimilifu wa ahadi ya Mungu, kilele cha ufalme wa enzi na fahari ya kiti cha kifalme cha Daudi mtumishi wake (rej. Somo I- 1Sam 5:1-3). Kristo Mfalme ni kimbilio letu na nguvu yetu, yu tayari kusaidia wakati wa taabu, kwa hiyo hatutaogopa chochote. Mungu ananguruma dunia yayeyuka, mataifa yagadhibika na tawala zatikisika, Bwana wa majeshi yu pamoja nasi, Mungu wa Yakobo ni ngome yetu (Zab 46: 1-7). Katika mwaka wa Jubilei ya Matumaini 2025, sherehe hii ni mwaliko wa kuimarisha tumaini letu kwa Mfalme asiye na silaha, bali msalaba; asiye na kiti cha kifalme cha dhahabu, bali ni cha kuni kilichopigiliwa misumari

Somo la Kwanza, 1 Sam 5:1‑3 Katika sura hii, tukio kubwa linachukuliwa kutoka kitabu cha Samweli: Warumi wa Wafilisti walichukua Sanduku la Agano (liloashwa makuhani wa Israeli), na kuiweka ndani ya hekalu la sanamu ya Dagon. Wakati wa asubuhi, waliojua walipata kustaajabishwa, sanamu ya Dagon ilikuwa imedondoka uso chini mbele ya Sanduku la Bwana. Sanamu ilikuwa imeangushwa, kichwa chake na mikono ilikuwa imevunjika. Hata sanamu inayodai utawala inashindwa mbele ya Mwenyezi Mungu Mungu ana uwezo wa kupindua mifumo ya uongozi, sanamu za utawala, nguvu za kisiasa, na miundo ya utawala uliochukuliwa kuwa “ngome.”  Je, tunaanza kuona kwamba kutambua uongozi wa Kristo ni kupinga “sanamu” za utawala wa wazimu, dhuluma au giza katika dunia? Katika muktadha wa jubilei ya matumaini, hii inatuelimisha kwamba hata wakati utawala wa haki hautadumu, Mungu bado yuko, yuko juu, atapindua hali,  na atamulika Mfalme.

Uhusiano na matukio ya leo, Dunia inateseka kwa vita, majanga, mgogoro wa kiuchumi, utawala wa kidikteta, rushwa, halifu, kwa mara nyingi wengi wanaogopa “senario zimezidi nguvu zetu.” Zaburi 46 inatualika kutambua: Mungu si mbali, ni ngome yetu, msaada wetu, nguvu yetu.Katika Jubilei ya Matumaini, tunapokaribia Noeli ya kristo na mwisho wa mwaka wa liturujia Zaburi hii anatuita tusimame imara, kukumbuka ulinzi wa Mungu na kutawala kwake kwa rehema, si kwa silaha.

Mtume Paulo anatuonyesha kwamba Kristo ndiye Mfalme wa ulimwengu mzima ,si tu wa Kanisa, bali wa ulimwengu wote, Yesu Kristo ni mfano wa Mungu asiyeonekana, Mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote. Kwa kuwa katika Yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana (somo II- Kol 1:11-20)… Yeye, Mfalme, ndiye Mwanakondoo halisi, kwa upendo na utii amechinjwa sadaka, tuile karamuye na tuimbe alleluia… kwa sababu hiyo, kwa damu yake azizi na takatifu sana amemnunulia Mungu watu kutoka kila kabila, na taifa, na jamaa, na lugha, na tamaduni zote za kale, za sasa na zijazo… hivi kwa haki kabisa Yeye peke yake ndiye mwenye kukitwaa kile kitabu na kuivunja mihuri yake… hakika amestahili kupokea utukufu na heshima, uweza na nguvu hata milele na milele, amina (Ufu 5:9,12)… na tuanguke fudifudi mbele ya Mfalme huyu wa ajabu katika utukufu na uweza, tumshukuru, tumsifu, tumuabudu Bwana aliye Jana na Leo, Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho, nyakati ni zake na karne pia, utukufu ni wake na enzi pia, milele na milele (rej. Baraka ya Mshumaa wa Pasaka).

Maana ya Mfalme Kristo, Utaalamu wake hauko tu katika ngao ya Roho, bali Madaraka ya ulimwengu wote , anasimamia makundi, nguvu za kijeshi, utawala, siasa, maadili. Kristo si “mfalme wa upande mmoja” bali mfalme wa upatanisho: alipatanisha vitu vilivyoko mbinguni na duniani kwa damu yake ya msalaba. Katika dunia inayovurugika na kukiuka sheria, mgawanyiko, migogoro ya kimataifa, huu ni ujumbe wa matumaini, Kwamba si nguvu za wanadamu wala makubaliano ya dunia yatakayodumu,  bali utawala wa Kristo. Hii inatupatia ujasiri kuishi chini ya utawala wake utawala wa upendo, utawala wa haki, utawala wa unyenyekevu. Bwana Mfalme ameketi milele… kadiri ya somo la Injili (Lk 23:35-43) Yupo juu ya kiti cha enzi cha Msalaba na anuani kichwani pake ikimthibitisha HUYU NDIYE MFALME WA WAYAHUDI, na kutoka pale juu alipoangikwa anamjalia wokovu mwizi anayetubu na kutoka palepale juu anatubariki watu wake kwa amani… hima tufungue mioyo yetu, roho na akili zetu kupokea baraka hizo, neema hizo, ulinzi huo, nafuu hizo na manono hayo tunayoyapewa pasi idadi na pasi mastahili kutoka Msalaba wa Mfalme wetu… Ameketi katika utukufu pindo la vazi lake zalijaza hekalu na maserafi wakisifu juu yake, “Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatiffu” (Isa 6:1-2), anatutazama ‘mtazamo’ mwema kwa macho yake ya kibuluu yenye kupenya moyo na nafsi lakini mapole na yenye kualika… ni hamu ya Moyo wake Mtakatifu sote tumkaribie na magotini pake tujipatie faraja na pumziko tunalohitaji.

Wakati ulimwengu unateseka kwa vita (Ukraine, Gaza, Sudan, DRC,hata kwenye familia zetu nk.), Wahalifu wa leo hujaribu kudhibiti kwa nguvu, nguvu za silaha na ukandamizaji wa sheria za mabavu. Lakini hii sheria  ya Sherehe ya leo inatukumbusha Ufalme wa Kristo hauji kwa silaha, bali kwa upendo, msalaba, na ufufuo. Katika muktadha wa jubilei ya matumaini, hii ni fursa ya kutangaza, “Ufalme wake ni wa milele, haufanyiki na majeshi ya wanadamu lakini wanavyomwabudu na kutangaza ni nani Mfalme wa kweli.” Ni kwa Huyu tu Mfalme wa utukufu kuna mema ya milele, Kwake hakuna ahadi ongo za kisiasa au matata yatokanayo na kusema iliyo kweli, hali njema ya wote, ustawi na uhuru wa wanawe ndivyo viujazavyo Moyo wake Mtakatifu… Ni katika maskani za Mfalme wetu Mkuu iko iliyo haki, iliyo amani, iliyo matumaini, iliyo upendo… Tunaona fahari kuliungama Jina lake, tunamkiri Mfalme wetu, Bwana wetu na Mungu wetu… na tumwamini, tumpokee, tumsikilize, tumtii nasi tutafika tupendapo kufika kwa vile Yeye ni mwaminifu wa daima, nao “ufalme ni wake, na nguvu, na utukufu hata milele, amina.

Viongozi wengi duniani wanatumia sheria kwa maslahi yao wenyewe, wanadanganya, kuangamiza haki. Kuzaliwa kwa Kristo Mfalme kunataka kutumiwa kama changamoto – kwamba sheria kamili ya maisha ni ile ya Kristo, upendo, adhabu na wongofu – si sheria tu ya kifalme. Mfalme Kristo anatualika kuwa wawekaji wa sheria ya rehema, upendo, huruma na msamaha wala si sheria ya giza. Katika kazi, familia, utumishi wa kijamii, watu mara nyingi hujisikia kwamba “wana utawala mdogo juu ya maisha yao.” Lakini tukumbuke kwamba Kristo ni Mfalme wa maisha yetu, na tunapomwachia madaraka, yeye anaweza kuingilia. Inawezekana kutuweka tumaini badala ya hofu Inawezekana kutuongoza katika haki na huduma, Inawezekana kutuhifadhi na kutumiwa kwa utukufu wa utawala wake

Katika Sherehe hii, Baba Mtakatifu analialika Kanisa kuchukua msimamo wa hadhi ya mamlaka ya Kristo juu ya mataifa. Hii ina maana,Kanisa na waamini wasiogope kutoa ushuhuda wa Kristo kwa umma, hata wanapokabiliwa na vurugu au ukandamizaji. Kanisa kuenzi neema ya “sabato ya waaminifu” ambapo Kristo anatawala mioyoni yetu – si kwa kujilazimisha bali kwa utu wa huduma. Waamini kutambua kwamba wakiwa chini ya utawala wa Kristo, hawatakosa nguvu, msaada, au hukumu ya mwisho isiyokiuka haki. Katika muktadha wa migogoro ya dunia, kanisa linapewa wajibu wa kuwa cerubin wa tumaini, kueneza misaada, haki, amani, na kutetea wanyonge chini ya utawala wa Kristo. Kristo ametupenda upeo, ametuondolea dhambi zetu kwa damu yake, ametushirikisha ufalme na ukuhani ili tumtumikie Mungu…

Kama zilivyo falme na tawala nyinginezo, utawala wa Kristo unazo Katiba na amri na sheria zake, dhamiria leo kutulia kwake, usiwe na uraia pacha, mwananchi wa Kristo Mfalme kwa upande mmoja na mwananchi wa wengine wasio Kristo, na walio kinyume na Kristo, japo wanaonekana na kunena na kutenda kama wakristo… sheria ya Bwana ni kamilifu, ni sheria ya upendo.. na amri yake ni amri ya haki… Neno lake ni amini huburudisha moyo, hilo ndilo “imani” yetu, hilo ndilo “maadili” yetu, tulijue, tulishike, tuliishi, tulisali nayo yote yatakuwa yetu, kwa milele, amina alleuia. Kristo Mfalme ni ushindi wa upendo dhidi ya uovu, ushindi wa sheria ya upatanisho mbele ya sheria ya giza, na ushindi wa matumaini dhidi ya hofu. Hata wakati dunia inavurugika kwa vita, udhalilishaji, tawala za mabavu na ukandamizaji, Kristo anakaa juu ya ngome yake ya haki na huruma. Leo tunapofunga mwaka wa liturujia, tukikaribia Jubilei ya Matumaini, tuitike wito: kumruhusu Kristo aingie mbinguni na duniani  aite mataifa yetu, mioyo yetu, maisha yetu.

Dominika ya 34 ya nwaja C 23 Novemba
BABA YETU
22 Novemba 2025, 09:06