Tafuta

Injili ya Dominika ya XXXIII ya Mwaka C. Injili ya Dominika ya XXXIII ya Mwaka C. 

Dominika ya XXXIII ya Mwaka C:“Kwa uvumilivu wenu mtaziponya nafsi zenu”

Ukristo sio tu orodha ya mambo mengi bali Ukristo ni maisha.Yatupasa kuendelea kujifunza imani yetu na kushika mwenendo mwema.Kujua lipi ni la muhimu kwa wokovu na lipi hapana,njia ipi ni sahihi na ipi sio ili wakati utakapotimia tuweze kumfikia Mungu mwenyeweEe Bwana wa matumaini,jua la haki,tupe neema ya kuvumilia hadi mwisho.Tuimarishe tuwe mashahidi wa tumaini katika dunia yenye machungu.Tusaidie tusikate tamaa,bali tukae imara kwa kazi njema na uaminifu.

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

Karibu mpenzi msikilizaji na msomaji wa tafakari ya neno la Mungu kutoka hapa radio vatican leo Dominika ya 33 MWAKA C, Tunakaribia mwisho wa mwaka wa kiliturujia, na masomo ya leo yanatualika kutafakari kuhusu mwisho wa dunia hii na matumaini ya milele. Hii si habari ya kutisha, bali ya kutia moyo, hasa tunapoelekea Jubilei ya Matumaini mwaka 2025. Dunia imejaa magumu, lakini tumaini la Kikristo halikomi. Kristo ndiye sura halisi ya huruma ya Baba aliye ukamilifu wa kila mwenye mwili. Katika Yeye vyote vinaishi, vinajimudu na kuwa na uhai wake, vyote vimeumbwa kwa ajili yake, vipo kwa ajili yake na kwake vinarejea... Huyo Yesu alishuka kutoka mbinguni mara ya kwanza akaudhihirisha upendo na huruma isiyo na kikomo ya Mungu Baba yetu kwa maisha yake, kwa kuhubiri Habari njema, kwa miujiza mingi na hatimaye kwa kuteswa, kufa, kufufuka na kupaa mbinguni kwa utukufu... Kutoka huko atakuja tena nyakati zitakapotimia ayakamilishe yote yaliyoanza katika uumbaji na kuyaweka yote miguuni pa Mungu Baba kusudi Mungu awe yote katika yote… Siku hiyo ya Bwana ipo kwa hakika, ni siku njema sana lakini ngumu pia,

Nabii Malaki anasema:“Tazama, siku inakuja inayowaka kama tanuru...”Lakini pia anatoa ahadi:“Kwenu ninyi mnaolicha jina langu, jua la haki litachomoza, lenye kuponya katika mbawa zake. … kila jicho litamuona, hatakuja tena katika unyonge na umasikini bali kama Mfalme na Hakimu wa utukufu na kitisho akimpa kila mmoja kadiri ya matendo yake… itakuwa lini? tarehe ngapi? tutakusanyikia kijiji gani? hayatuhusu, ni Yake mwenyewe… lakini kwa kutupenda ametupa dalili zake za matukio ya uharibifu, vita, matetemeko, moto, uwepo wa mpinga Kristo na manabii wa uongo… kwamba mwanadamu katika unyonge wake atapita vipindi vigumu vya changamoto aina kwa aina, iwe kutoka kwa wanawe na ndugu zake, jumuiya yake, mifumo ya kiutawala na mitazamo mipya ya kiulimwengu kiasi cha kujiona njia panda asijue lipi ni lipi… katika mazingira hayo leo Kristo anatupa moyo sana akisema, “nanyi kwa subira yenu mtaziponya nafsi zenu!”…

Subira iwe katika Mwana wa Mungu ambaye kifo chake Msalabani kimeangamiza dhambi na mauti ya milele, atang’oa yote yenye kuudhi katika mioyo ya wanaomwamini na kuuthibitisha Ufalme wa Mungu kwa wote wenye kumtumainia… tupige moyo konde tumngoje Bwana, Mkristo anatakiwa kuitamani siku hiyo, aone inachelewa kufika, asiiogope siku tukufu ya Bwana bali aifurahie na kuishangilia (Zab 118:24).

UFAFANUZI

Hata kama dunia itatikisika, mataifa yataingia vitani, na mateso yatakuja, Bado Mungu ni mwaminifu. Jua la haki linachomoza kwa wale wanaomcha Bwana. Tumaini letu si katika utulivu wa dunia hii, bali katika ahadi ya uzima wa milele Wakati tukimsubiri Kristo ‘tuwajibike kutenda mema’... kila mbatizwa ni taa, chumvi, chachu na njia kwa ulimwengu, uwepo wetu duniani uwe ni habari njema ya wokovu kwetu na wengine. Tunapomsubiri Kristo tutakumbana na mateso, ‘basi jiangalieni, mioyo yenu isije ikaelemewa na ulafi, na ulevi na masumbufu ya maisha haya siku ile ikawajia ghafla, kama mtego unasavyo’ (Lk 21:34). Ikiwa Kristo aliteswa sisi ni nani yasitupate hayo? mahangaiko yetu yatuimarishe, tunapambana na nguvu za giza [rushwa, ufisadi, uongo, wivu, tamaa, wizi na dhuluma, siasa zisizo safi, mipasuko katika ndoa na familia na imani za ushirikina].

Ushindi wa hayo yote upo katika KUSALI NA KUFUNGA... Sala ni ‘chemchemi ya Hekima’ ya Mungu katika utendaji wetu, katika kusali tunapata nguvu ya kuendelea na matumaini ya ushindi. Tunapokesha tujue hakika kuwa uaminifu ni njia ya kuelekea uzima. Uaminifu katika kushika imani yetu na viapo vyake, uaminifu katika kushika amri za Mungu na za Kanisa lake. Tumngoje Bwana kwa kujenga maisha yetu juu ya Neno la Mungu, kujilisha kwa Ekaristi takatifu, kujitajirisha kwa maisha ya fadhila, kujitibu kwa kitubio na kuambatana na Mama Kanisa katika ibada na liturjia. Tupunguze kujihurumia na kujipenda kupita kiasi, safari ya mbinguni inatudai ukakamavu na utimamu kamili.

Injili ya leo inaonekana kama ripoti ya habari zetu za kila siku: vita, ghasia, mitetemeko, mateso, Yesu hakuwa mtabiri wa hofu, bali mjumbe wa matumaini. Kama Wakristo, hatuogopi mwisho wa mambo, tunauitikia kwa imani na tumaini. Utawala wa Sheria Wakati sheria nyingi duniani zinavunjwa au kugeuzwa kwa manufaa ya wachache, ujumbe wa Malaki ni wazi, Siku ya Bwana italeta haki kamili kwa wote. Hatupaswi kuchanganyikiwa na mifumo ya dunia bali kuendelea kuwa waaminifu kwa Mungu. Tunapoingoja siku ya hukumu tusiweke mioyo yetu kwenye fedha, mali au vitu. Watu waliposhabikia uzuri wa hekalu Yesu aliwaonya ‘haya mnayoyatazama, siku zitakuja ambapo halitasalia jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomoshwa’... yote tuliyonayo yasitufunge hivi kiasi cha kushindwa kumuhudumia Kristo katika ndugu zetu walio wadogo. Kubomolewa kwa hekalu ni kubomoa hali, tabia na mazoea mabaya ya dhambi na kujipatia hali njema.

Tunakesha tukimngoja Kristo kwa kuuishi upendo kwa wote. Hatuwezi kujiita wakristo tunaomngoja Bwana aje kutuchukua wakati kuna watu hatuwapendi, hatuna amani nao, tumewachoka, hatutamani hata kuwaona… katika matendo yote ya upendo na msamaha Kristo ndio awe kipimo chetu, na matendo hayo huonekana katika mambo madogomadogo ya kawaida. Mfano unapoamua kufungua muziki kwa kelele hadi asubuhi, ni kweli hupangiwi maisha, radio ni yako, kibali umekata kwa fedha zako lakini je, unamfikiria kweli huyu jirani yako anayehitaji walau masaa machache ya usiku apumzike kwa utulivu baada ya mahangaiko ya jua kali siku nzima? Muziki unaokesha kwa kelele ni dalili wazi ya kupungukiwa fikra za upendo na kuwajali wengine.

MASWALI YA KUJIULIZA LEO: Je, naishi kwa tumaini au kwa hofu ya mambo yajayo? Je, ninafanya kazi kwa bidii na uaminifu, au nataka kula pasipo jasho? Je, ninasimama imara katika imani hata ninapopitia mateso au changamoto? Je, maisha yangu yanaonyesha uvumilivu na ushuhuda wa matumaini? Tunaingoja siku ya Bwana kwa kusamehe makosa tuliyotendewa. Sote ni wakosefu mbele ya Mungu na mbele ya wenzetu. Kama sisi tunavyotamani tusamehewe vivyo hivyo nasi imetupasa kuwasamehe wenzetu. Tunapojaribu kusameheana, tutazame zaidi mapungufu yetu wenyewe kuliko ya wenzetu na hapo tutakuwa na nafasi nzuri zaidi ya kutubu kuliko kuhukumu wengine. Tuingoje siku ya Bwana tukisali na Biblia iliyo wazi. Yaani kuisoma Biblia sio tu kwa lengo la kutafakari na kuelewa lakini pia tukiweka nafsi zetu katika yale maneno na kuyafanya sala (Lectio Divina), yatatuinua na kutuunganisha na Mungu na kutupa nguvu na neema tunayoihitaji.

Paulo anawakaripia wale wanaoishi bila kufanya kazi, na wanaotumia muda kwa mambo ya ovyo. Anasema “Yeyote asiyetaka kufanya kazi, na asile, Mt. Paulo amesema tunapoingoja siku ya Bwana tusimuelemee mtu, bali kwa taabu na masumbufu, usiku na mchana tutende kazi makusudi tuwe mfano na kielelezo bora kwa wenzetu, amesema tusipofanya kazi hata chakula tusile... inawezekana tupo tunaongojea ‘ufufuko wa wafu na uzima wa milele ijayo’ kwa kukaa tu na kusubiri. Ujio wa 2 wa Kristo utukute tunawajibika. Katika ulimwengu wa sasa, tunaalikwa kuwa watu wa nidhamu, kiroho na kimwili. Tumaini halimaanishi kubweteka au kuishi kwa uvivu, bali kufanya kazi kwa bidii huku tukingoja ujio wa Kristo. Katika kipindi cha taabu duniani, tunaalikwa kuendelea kufanya kazi ya kujenga familia, jamii, na Kanisa, kuutunza na kuuendeleza ulimwengu aliotupatia, kutunza familia na ndugu zetu, kuifadhi salama rasilimali na kufanya yote yanayowezekana ili dunia istawi na watu wote waifurahie. Hivi mkristo uwe hodari, upige moyo konde, sali kama leo ni siku yako ya mwisho kuishi na tenda kazi kama utaishi milele

Ukristo sio tu orodha ya mambo mengi bali Ukristo ni maisha. Yatupasa kuendelea kujifunza imani yetu na kushika mwenendo mwema. Kujua lipi ni la muhimu kwa wokovu na lipi hapana, njia ipi ni sahihi na ipi sio ili wakati utakapotimia tuweze kumfikia Mungu mwenyewe. Ee Bwana wa matumaini, jua la haki, tupe neema ya kuvumilia hadi mwisho.Tuimarishe tuwe mashahidi wa tumaini katika dunia yenye machungu. Tusaidie tusikate tamaa, bali tukae imara kwa kazi njema na uaminifu.Kwa uvumilivu wetu, tuzibebe nafsi zetu kwa uzima wa milele. AMINA.

Dominika ya 33 ya mwaka C
15 Novemba 2025, 11:25