Tafuta

 Melbourne nchini Australia Melbourne nchini Australia 

Jumuiya za Wakatoliki wa Korea nchini Australia,Kukuza imani na tamaduni

Zaidi ya miaka arobaini imepita tangu 1984,wakati Padre mmisionari kutoka Sydney alianza kusafiri mara moja kwa mwezi kwenda Canberra kusherehekea Misa na jumuiya ya Wakatoliki wa Korea.

Na Sr. Christine Masivo, CPS - Vatican.

Nchini Australia, Wakatoliki wa Korea wanaunda Jumuiya zenye nguvu na za karibu zinazoakisi utambulisho wa tamaduni nyingi wa nchi hiyo. Kuanzia Sydney hadi Canberra na Melbourne, mapadre wa Korea wakileta pamoja vizazi tofauti na asili za kiutamaduni, wakikuza hisia ya umoja na kuwa sehemu ya wahamiaji wa Korea na familia zao. Padre Andrea Yang Myeong-sik, anayehudumia Jumuiya ya Wakorea huko Canberra, ni mmoja wa mapadre wengi waliotumwa na Jimbo la Daejeon nchini Korea, ambaye anatafakari changamoto na manufaa ya kufanya kazi na kundi dogo lakini tofauti la wahamiaji wa Kikorea wa kizazi cha kwanza na cha pili, wenye idadi ya watu wapatao 130.

"Nimevutiwa kuona jinsi imani ya Kikristo inavyoishi katika jamii yenye tamaduni nyingi," Padrw Myeong-sik alisema. Mbali na huduma yake na jamii ya Wakorea, pia anahudumu katika parokia za wenyeji, akisaidia kuunganisha Jumuiya  ya Wakorea na Kanisa Katoliki la Australia. Idadi ya kipekee ya watu wa Canberra, ikiwa mji mkuu wa utawala wenye idadi ndogo ya watu na uhamaji mkubwa, inatoa changamoto na fursa. Jamii inabadilika kila mara, kwani Wakorea wengi huja jijini kwa ajili ya kazi na wanaweza kukaa kwa miaka michache tu.

Changamoto za dhaurua ni kudumisha mwendelezo wa kichungaji

Padre Myeong-sik alibainisha kuwa moja ya changamoto za dharura ni kudumisha mwendelezo katika kazi yao ya kichungaji licha ya mabadiliko ya mara kwa mara katika jamii. Hata hivyo, kanisa la Kikorea linaendelea kukua, likiwa na wanachama wapya, kama vile mwanamke kijana wa Kichina ambaye alianza safari yake ya imani na jamii ya Wakorea baada ya kusoma Korea.

Wakati huo huo, huko Sydney, makazi ya jamii kubwa zaidi ya Wakatoliki wa Kikorea nchini Australia, parokia ya Mashahidi wa Kikorea na Mtakatifu Stanislaus inasherehekea miaka 50 ya huduma. Ilianzishwa mwaka wa 1976 kwa msaada wa Mababa wa Franciscan na Columban, parokia hiyo sasa inahudumia zaidi ya wanachama 6,000 waliosajiliwa, huku takriban 1,400 wakihudhuria Misa ya Jumapili. Padre Andrea Kim Yoon Jae, mmoja wa mapadre wanne wa Korea wanaohudumia parokia hiyo, anaelezea kwamba jamii imeona mawimbi ya uhamiaji: wafanyakazi wenye ujuzi katika miaka ya 1960, maveterani wa Vita vya Vietnam katika miaka ya 1970 na 80, wanafunzi na wataalamu vijana katika miaka ya 2000, na hivi karibuni, familia ambazo zimehama kwa ajili ya kazi au elimu.

Elimu kwa wazazi ili kubatiza watoto

Padre Yoon Jae alisema kwamba sifa tofauti ya parokia yao ni msisitizo wa elimu, huku wazazi wengi wakichagua kuwabatiza watoto wao katika muktadha wa shule za Kikatoliki, ambazo zina jukumu muhimu katika jamii. Licha ya changamoto kama vile mapengo ya vizazi na tofauti za kitamaduni, jamii ya Wakatoliki wa Korea huko Sydney inabaki kuwa imara, na ongezeko linaloendelea la wahamiaji wapya linahakikisha jamii itaendelea kukua.

Melbourne, jumuiya zina uhusiani wa karibu

Huko Melbourne, Padre Michele Kong anahudumia jamii ndogo ya Wakatoliki wa Korea katika Parokia ya Sacred Heart huko Kew. Tofauti na parokia kubwa ya Sydney, jamii ya Melbourne ina uhusiano wa karibu zaidi, ikijumuisha zaidi familia ambazo watoto wao huhudhuria shule ya parokia.Padre Kong, ambaye ameishi Australia kwa karibu miaka 20, anaona tofauti za kitamaduni katika jinsi waumini wanavyoelezea imani yao. "Katika makanisa ya Kikorea, waumini huwa na tabia ya kujizuia zaidi, ilhali katika parokia za Australia, watu huwa na tabia ya kuzungumza na watu wengine na isiyo rasmi," anasema. Kadri jamii ya Wakatoliki wa Kikorea nchini Australia inavyoendelea kukua, dhamira ya mapadri hawa inabaki wazi: kukuza imani, kujenga madaraja kati ya tamaduni, na kusaidia vizazi mbalimbali vya Wakorea wanaoita Australia nyumbani. Iwe ni katika Sydney yenye shughuli nyingi au Canberra tulivu, hisia ya jumuiya na imani inabaki kuwa imara, kuhakikisha kwamba urithi wa Ukatoliki wa Kikorea utaendelea kwa miaka ijayo.

10 Novemba 2025, 17:31