Tanzania,Nyaisonga:Ninatoa rai ya kujitathmini kama taifa na kuomba uponyaji na maridhiano
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya nchini Tanzania, kama kama ilivyokuwa imetoa mwaliko katika Dominika ya 32 ya Mwaka C wa Kanisa, kwa maparokia yote ya Jimbo kuu, kusali kwa ajili ya marehemu wote vile vile alasiri hiyo ilifanyika Misa maalumu ya kijimbo katika Kanisa la Bikira Maria wa Fatima, Mwanjelwa jijini Mbeya, tarehe 9 Novemba 2025, iliongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya, Gervas Nyaisonga.
Katika mahubiri yake pamoja na kufafanua mashujaa wa kibiblia waliotambua kutetea imani yao bila kuteleleka katika somo la kwanza lililoseoma, alielezea hali halisi iliyoikumba nchi ya Tanzania wakati wa Uchaguzi Mkuu wa tarehe 29 Oktoba 2025. “Nchi yetu imekumbwa na ambayo ni unpresidented. Katika madhira hayo kumetokea vifo vya watu, wengine wamejeruhiwa, kumetokea uharibifu wa mali na kadhalika. Jimbo letu la mbeya linalotandaa ndani ya Mkoa wa Mbeya na Songwe ni kati ya maeneo yaliyo athirika kwa kiasi cha kuhuzunisha sana. Ndiyo maana tumeona ni vema tuadhimishe Misa hii kumuomba Mungu atupe tunayotamani katika maisha yetu. Madhumuni ya Misa hii yako Sita, kwanza kuwaombea marehemu, waliopoteza maisha katika migogoro na kuwapa pole wafiwa; Lengo la pili ni kuwaombea majeruhi waliojeruhiwa kwa namna mbalimbali kutokana na migogoro ya uchaguzi mkuu na waathiriwa…” haya na mengine yamo katika mahubiri ambayo tunayachapisha.
Kristo tumaini letu….
Ndugu wapendwa, hii ni Misa maalum inayotupa fursa ya kuwaombea wahanga wa machafuko ya Uchaguzi Mkuu na fursa ya kutafakari juu ya fumbo la kifo na ufufuko. Imani juu ya uzima baada ya kifo ipo kati ya wanadamu tangu uwepo wa wanadamu. Ndo maana kuna madokezo mengi ya uwepo wa uzima baada ya kifo katika mila na disturi zetu za kijadi. Imani hiyo ilikuwepo pia katika dini ya kiyahudi na somo la Kwanza la kitabu cha Pili cha Makabayo, linaelezea juu ya Imani hiyo katika dini ya kiyahudi. Katika dini ya kiyahudi ilikuwa ni marufuku kwa muaamini kula nyama ya nguruwe. Na wale ambao hawakuwa wayahudi, akiwemo aliyekuwa Mfalme nyakati hizo, aliamua kuwalazimisha waamini wa dini ya kiyahudi kula nguruwe na aliye kataa alistahilishwa adhabu ya kifo.
Katika somo la Kwanza ni similizi ya tukio la vifo vya watoto saba wa Familia moja walionyesha uimara katika kushika Imani yao. Nina nukuu chache hapa, yule wa Kwanza alipohojiwa na kulazimishwa, alijibu “sisi tuko tayari kufa kuliko kuzivunja amri za wazee wetu.” Basi aliuawa. Wa Pili alipofikiwa zamu yake, akamwambia yule muuwaji: “wewe mdhalimu unatufarikisha na maisha ya sasa lakini mungu atatufufua tupate uzima wa milele.” Anataja wazi Imani yake juu ya ufufuko juu ya uzima baada ya maisha haya ya duniani. Wa Tatu akasema, “Kutoka mbinguni nilipewa haya yote ninayoyaona na ninayo yastahili hapa duniani, na kwa ajili za Amri za mungu na hesabu yote kuwa sio kitu kwani naamini nitavipata tena.”
Anaamini atapata uzima wa milele baada ya kifo. Yule wa nne akasema: “Ni vema kufa katika mikono ya wanadamu na kuzitazamia ahadi za mungu.” Somo letu linaishia alipoteswa yule wa nne. Lakini tungeangalia yule wa tano, Kitabu cha Pili cha Makabayo Sura ya Sita, yeye alimwambia Mfalme moja kwa moja kuwa “ wewe ingawa ni mtu tu, lakini una mamlaka na unayatumia upendavyo lakini usifikiri hata siku moja kwamba Mungu amelitupa taifa hili.” Na hivyo ukiendelea kusoma Sura ya Saba ya Kitabu cha Makabayo utaona vijana wote saba kila mmoja alionyesha utayari wake wa kufia dini yake. Na mama yao shujaa alishuhudia watoto wake wote, na yeye ilipofika zamu yake aliendelea kubaki shujaa. Hakulia tu na kupoteza matumaini, lakini alikuwa shujaa alivyowambia watoto wake kwamba “jinsi mlivyo ingia tumboni mwangu mimi sijui ni huyo mungu aliyewaleta ndiyo Yeye anayewaita na anayetaka muwe mashujaa.”
Somo hili linatueleza wazi juu ya imani, juu ya ufufuko. Walikuwa tayari kufa kwa sababu walijua Kuna ufufuo. Dhana hii ya kifo na ufufuko imetajwa tena kwenye Somo la Injili. Ambapo watu wasiokuwa na imani juu a ufufuko walimuuliza Bwana Yesu swali la mtego, wakielezea desturi juu ya ndoa kwamba: “ndugu akifariki, mdogo wake amridhi mkewe, na sasa walikuwa ndugu saba na wote walirithi, na wote waliaga dunia bila kuacha uzao, sasa unatueleza juu ya ufufuko atakuwa mke wa nani sasa.” Walimuuliza swali la kejeli. Nia si kutafarisha juu ya ndoa, lakini jibu la Yesu alisema wana wa dunia wanaoa na kuolewa lakini katika ufufuo, kuna fahari kubwa zaidi ambayo mnafikiri kuna fahari kubwa kuliko zote.” Kwamba duniani humu tunashindania mambo mengi, tunautafuta utukufu, kwa bidii zote. Na hata kusahau kwamba upeo wa utukufu uko kwa Mungu. Ambapo sasa binadamu huyo atafanana na Malaika na kufikia utimilifu wa lengo wa kuumbwa kwake.
Bwana Yesu anatukumbusha kwamab mahangaiko ya duniani ni ya muda tu na kamwe yasitusahaulishe fahari ile ya milele. Binadamu wengine wanajisahaulisha kuwa kuna upeo Miele wa Mungu. Hivyo wanatumia mbinu zote hasa chafu kuhakikisha kwa wanapata fahari na utukufu hapa duniani na wanasahau kujiuliza kwamba itakuwaje mbele ya mwenyezi Mungu. Hayo yaliyoambatana na harakati za uchaguzi mkuu, uliofanyika tarehe 29 mwaka huu, uliofanya Tanzania izungumzwe kwenye vyombo vya Habari. Hususan vyombo vya Kimataifa- AL Jazeera, BBC na vinginevyo. Kama Habari zetu zingekuwa njema tungefurahi. Habari zilizovuma zilielezea kuwa Tanzania imekumbwa na machafuko, na hayo machafuko yalipewa kivumishi, “unpresidented” kumaanisha “hayajawahi kutokea” na “hayakutegemewa.” Ndivyo yalivyotangazwa. Nchi yetu imekumbwa na ambayo ni ‘unpresidented.’ Katika madhira hiyo kumetokea vifo vya watu, wengine wamejeruhiwa, kumetokea uharibifu wa mali na kadhalika.
Jimbo letu la Mbeya linalotandaa ndani ya Mkoa wa Mbeya na Songwe ni kati ya maeneo yaliyo athirika kwa kiasi cha kuhuzunisha sana. Ndiyo maaana tumeona ni vema tuadhimishe Misa hii kumuomba Mungu atupe tunayotamani katika maisha yetu. Madhumuni ya Misa hii yako Sita, Kwanza kuwaombea marehemu, waliopoteza maisha katika migogoro na kuwapa pole wafiwa. Lengo la Pili ni Kuwaombea majeruhi waliojeruhiwa kwa namna mbalimbali kutokana na migogoro ya uchaguzi Mkuu na waathiriwa. Lengo la Tatu ni kumuomba Mungu asaidie jitihada za kuwapata waliopotea kutokana na migogoro hiyo. Tunamwomba atusaidie kuwapata wakiwa hai ni vema sana. Wakiwa wafu basi walau tuwapate. Lengo la Nne ni kuwapa pole waliopoteza mali zao kutokana na migogoro hiyo. Lengo la Tano ni kutoa rai ya kujitathmini na lengo la Sita ni kuomba uponyaji kutoka kwa Mungu wetu. Mimi binafsi naamini kuwa kwenye migororo ya Uchaguzi Mkuu wa Taifa letu, mwaka huu, kumetokea vifo vya watu wenye hatia na wasio na hatia. Kati ya waliouawa, kuna watoto, kuna vijana na wazee, kuna wanawake na wanaume, kuna raia na askari. Makundi yote hayo kuna waliouawa.
Tarehe 4 Novemba nimeshuhudia kwa macho yangu wingi wa watu usio wa kawaida waliokuwa wananunua Majeneza kwenye mitaa ya wauza Majeneza. Nimeshuhudia pia misafara ya magari, ikisafirisha miili kwende nje ya jiji la Mbeya. Marehemu walio wengi waliuawa kupitia silaha za moto, yaani bunduki. Ambazo kwa sheria hutumiwa na Askari, walioaminiwa na kuapishwa, kutumia silaha hizo kwa kuzingatia kanuni za usalama. Ninaamini kuwa, wako waliopoteza maisha kwa sababu walikosa chakula, matibabu na fursa ya kusikilizwa. Wapo waliofariki dunia kwa adhabu kali kutoka kwa walio wakabidhi, wapo waliopoteza uhai wakiwa wamejihifadhi ndani ya nyumba zao, kwani baadhi ya washika bunduki hawakusita kuzivamia nyumba hizo. Wapo waliopoteza maisha kutokana na kiwewe, (trauma), au msongo wa mawazo. Baadhi ya wahanga walitekwa nyara au kushambuliwa kabla ya Uchaguzi na wengine mpaka sasa haijulikani waliko.
Wengine wamekutwa na Madhira haya wakati uchaguzi ukifanyika au ukiendelea. Hao na wengineo ni wahanga wa Uchaguzi Mkuu. Wahanga hawa wanaleta simanzi kubwa nchi Tanzania. Kwa kuwa matukio ni mengi kwa wakati mmoja, hatujuhi tumpe nani pole na tumuache nani. Misa hii ipo kwa lengo la kutoa pole kwa wote. Mwanamuziki mmoja maarufu nchini Tanzania kwa jina TX Moshi William na mwenzake Ngurumo wakipiga bendi ya ‘Msondongoma’ waliwahi kuimba hivi: “ukiona mtu mzima analia, ujue kuna jambo.” Na wakaongeza maneno “tunatoana roho kwa mali alizoziacha Baba.” Maneno ya Muziki huu tuyatoe kwenye muktadha wa Familia, tuyaweke kwenye muktadha wa Taifa letu. Nafasi ya Baba weka jina la Mwalimu Nyerere, poleni sana waombolezaji wote. Tunatoa pole kuonesha heshima na pole kwa wahanga kwani, tunajua kuwa kila mwanadamu anastahili heshima katika hali yeyote ile, na katika tuhuma zozote zile, asizoweza kuzikataa kwani ameondolewauhai kabla ya kujitetea. Tunasukumwa na imani kuwa, Mungu alimuumba mwanadamu kwa sura na Mfano wake; tunawajibu wa kuheshimu kazi ya Mungu. Raha ya milele uwape ee Bwana, na Mwanga wa Milele uwaangazie, Wapumzike kwa amani, Amina.
Lengo la pili la Misa hii ni kuwaombea majeruhi. Wapo watu waliojeruhiwa kwenye machafuko ya uchaguzi huu. Majeruhi wengine waliumizwa kwa silaha au mipigo na wengine kwa mazingira walimolazimika kuwemo. Wengine wanateseka kwa sababu wametelekezwa. Tunawaombea majeruhi wote, wapone kwa msaada wa Mungu. Lengo la tatu ni kumuomba Mungu asaidie jitihada za kutafuta watu waliopotea kabla ya Uchaguzi Mkuu na wakati wa uchaguzi mkuu watu kadhaa waliripotiwa kupotea katika mazingira tatanishi. Baadhi wanadhaniwa kutekwa nyara na watu wasiojulikana. Katika Misa hii tunamuomba Mungu aonaye yaliyo sirini, atusaidie tuwapate katika hali yoyote. Kama watakuwa hai tufurahie kupatikana kwao, kama wakiwa wafu tuomboleze, tuwazike kwa heshima za kiutu. Tuwaombee amani ya Mwenyezi Mungu na kisha tuhitimishe msiba. Anayeendelea kuwaficha anatunyima haki hizo za kiutu.
Lengo la nne ni kuwapa pole waliopoteza mali zao kutokana na migogoro hiyo. Katika heka heka za uchaguzi mkuu kumetokea uharibifu na hata upotevu wa mali za Umama. Lengo la tano ni kutoa rai ya kujitathmini kama taifa na kuomba uponyaji na maridhiano kutoka kwa Mungu wetu. Nawasihi wenye mamlaka kunyenyekea. Unyenyekevu sio udhaifu, bali ni utu wa kijasiri na kukiri imani kuwa hakuna mtu ajitwaaliaye wadhifa wa Mwenyezi. Ni Mungu tu muweza wa yote anayestahili kuitwa Mwenyezi. Na lengo la sita, tuungane sote jamii ya Wakristo Wakatoliki Jimbo la Mbeya kumuomba Mungu haya malengo ya misa hii yatimie; wafiwa wafarijike japo ni ngumu kwa uchungu walionao, majeruhi wetu waponywe, waliopotea wapatikane katika hali yoyote ile, na waliopoteza mali wawe na ujasiri, maadamu wana uhai, nafasi ipo bado.