Dubai,Kard.Tagle:Ubinadamu wa Yesu ni kwa ajili yetu
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Wafilipino elfu thelathini walihudhuria Misa iliyoongozwa na Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti Mwenza wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji(sehemu ya Uinjilishaji wa Kwanza na Makanisa Mapya Maalum), katika Kanisa la Mtakatifu Maria huko Dubai. Tukio hilo lilifanyika Jumanne tarehe 16 Desemba 2025, katika siku ya pili ya Simbag Gabi, "Misa ya Alfajiri," ambayo inaashiria kipindi cha sala za kabla ya Noeli ambazo zitadumu hadi Siku ya Noeli, ambao ni utamaduni ulioanza wakati wa ukoloni wa Hispania nchini Ufilipino katika karne ya kumi na sita.
Umuhimu wa kuwakaribisha wageni
Akimshukuru Askofu Paolo Martinelli kwa mwaliko wake na kuwasilisha salamu za Papa Leo XIV katika mahubiri yake, Kardinali aliwasihi waamini kukamilisha siku zote tisa za Simbag Gabi (Novena) kwa sababu zinawakilisha "maandalizi ya kuzaliwa kwa Yesu." Kardinali aliongeza zaidi: "Bikira mpendwa alimchukua mtoto Yesu tumboni mwake kwa miezi tisa. Kwa hivyo, kwa siku tisa na usiku tisa, tunaungana na Maria katika kusubiri kuzaliwa kwa Yesu." Akitoa maoni yake kuhusu Injili ya siku hiyo, Mwakilishi wa Baraza la Kimisionari alizingatia umuhimu wa kuwakaribisha na kuwakumbatia, kama Yesu alivyofanya, kuwakubali mababu zake na kurithi "hadhi ya mababu na udhaifu wao, hadhi ya wafalme na kasoro zao, kutokuwa na kitu cha wasiojulikana. Ubinadamu wa Yesu, aliyewapa matumaini waliokata tamaa, unapaswa pia kuwa kwetu.
Tumwige Yesu
Tumwige Yesu," Kardinali aliongeza. Alipofika Emirates kwa ziara iliyoanza jana na itakamilika Desemba 18, Kardinali Antonio Gokim Tagle alikutana na wawakilishi wa jumuiya za parokia za Ufilipino." Anapendwa sana na waumini wa Ufilipino na ana kipawa cha kipekee cha kugusa mioyo ya watu na kuwaunga mkono katika safari yao ya imani," alisema Askofu Martinelli, Askofu Mkuu wa Kusini mwa Arabia, akielezea furaha yake na kumshukuru Bwana kwa neema ya ziara hii, "tamaa ambayo hatimaye imetimia mwaka huu." Misa nyingine imepangwa kufanyika Desemba 18 saa 2:00 usiku huko Abu Dhabi.
Misa huko Dubai kwa wafanyakazi wahamiaji ni fursa
"Kuhudhuria Misa hapa Dubai ni zawadi kwa wafanyakazi wahamiaji kama mimi, kuturuhusu kufanya mazoezi ya imani yetu na kutuunganisha kiroho na kihisia ndani ya jamii ya Ufilipino," alisema Brainard Calub, ambaye anafanya kazi katika usimamizi wa vituo, kwa fahari. "Jana usiku ulikuwa mzuri sana na Kardinali Tagle wetu akimwakilisha Papa Leo, na ilitufanya tujisikie karibu zaidi na Mungu." "Mahubiri ya Kardinali Tagle, yaliyotolewa kwa uchangamfu, unyenyekevu, na ukweli katika Kitagalogi, yaligusa mioyo yetu kweli. Maneno yake yalileta faraja, matumaini, na hisia kubwa ya kuwa sehemu ya jamii, yakitukumbusha uwepo wa Mungu hata tunapokuwa mbali na nyumbani," anasema Emie Mercado, mhasibu ambaye ameishi Emirates tangu 2014. Jumuiya ya Wafilipino wanaoishi katika Falme za Kiarabu ndiyo jumuiya kubwa zaidi ya wahamiaji. Kwa kuwa Ukatoliki ndiyo dini kuu nchini Ufilipino, wengi wao ni Wakatoliki. Pamoja na Wahindi, Waafrika, Wazungu, na wengine, wanaunda Kanisa Katoliki, lenye takriban waumini 850,000.