Tafakari Dominika IV Majilio Mwaka A wa Kanisa! Imanueli! Mungu Pamoja Nasi!
Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.
Utangulizi: Wapendwa Taifa la Mungu, leo ni Dominika ya 4 ya Majilio mwaka A wa Kanisa. Ni Dominika ya mwisho ya Majilio kabla ya kuadhimisha Fumbo kubwa la Ukombozi wetu, Fumbo la umwilisho kwa kuzaliwa kwetu Mwokozi wa ulimwengu, Bwana wetu Yesu Kristo. Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika hii inatualika kumtafakari, “Imanueli; Yaani, Mungu pamoja nasi.” Katika dominika ya Nne ya Kipindi cha Majilio, Mshumaa wa Bikira Maria huwashwa. Ni mshumaa wa Upendo. Unatukumbusha Upendo na uaminifu wa Mungu aliyetwaa mwili, akawa sawa na sisi na akakaa kwetu, akitimiza mpango wake wa tangu kale wa kumkomboa tena mwanadamu aliyepotea kwa sababu ya dhambi. Mama Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu kwa Imani, upendo, utii, uaminifu na ukimya wanakubali kushirikishwa huo mpango wa Mungu wa kumkomboa mwanadamu. Tuombe neema ya Mungu, ili daima tuisikie sauti yake katika ukimya akisema na mioyo yetu, tuitambue mipango yake hata pale inapopingana na mipango yetu ya kibinadamu, hata katikati ya hofu, sintofahamu na mashaka katika safari yetu ya maisha. Tuombe pia ya kushiriki mpango wa Mungu kwa ajili ya wokovu wa wengine, kwa njia ya Habari Njema ya Injili.
Somo la Kwanza: Ni kutoka katika kitabu cha Nabii Isaya 7:10-14. Somo la kwanza ni kutoka katika Kitabu cha Nabii Isaya. Ni utabiri wa Nabii Isaya juu ya Ishara ya Imanueli. Utabiri huu unakuja wakati taifa la Yuda yaani ufalme wa Israeli kusini, walikua katika mgogoro mkubwa sana wa kisiasa (Syro-ephramite Crisis 734-732BC). Mataifa ya Aramu (Syria) na Israeli yaani Ufalme wa Kaskazini (Ephraim) waliungana na kutaka kuivamia Yerusalemu na kuuangusha ufalme wa Kusini, yaani Ufalme wa Yuda. Mfalme wa Yuda, Mfalme Ahazi pamoja na watu wake waliingiwa na hofu, mashaka na mahangaiko makubwa sana. Katikati ya hali hii, Mwenyezi Mungu anamtuma Nabii Isaya kumwambia Mfalme Ahazi kwamba, hakupaswa kupanic, hakupaswa kuwa na hofu kwa kuwa Mwenyezi Mungu hatauacha mji wa Yerusalemu kuvamiwa na kuangushwa. Mwenyezi Mungu kupitia Nabii Isaya anamwambia Mfalme Ahazi aombe Ishara yoyote kutoka mbinguni, kama uthibitisho kwamba Mungu yupo pamoja nao. Lakini Ahazi anakataa kuomba Ishara, akisema kwamba, “Sitaitaka wala sitamjaribu Bwana” Mfalme Ahazi alijifanya kwamba hakutaka kumjaribu Bwana lakini kimsingi hakua na Imani, wala hakumtumainia Mungu wa Israeli. Kinyume chake alikwishaanza kuwaza kutafuta msaada kutoka kwa taifa kubwa la Waashuru badala ya kumtegemea na kumtumainia Mungu. Lakini Nabii Isaya anamhakikishia kuwa hata kama yeye alikataa kuomba Ishara, bado Mungu atatoa Ishara. Ni Ishara gani hiyo? Somo hili tulilolisikia ni utabiri juu ya Ishara ya Imanueli. Kwamba Bikira atachukua Mimba, naye atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli, yaani Mungu pamoja nasi. Mungu hawaachi kamwe watu wake, licha ya udhaifu wao, licha ya Imani haba na mashaka, anakuja Katikati yao, anawaletea ukombozi.
Somo la Injili: Ni Injili ya Mt. 1:18-25. Katika somo la Injili takatifu, tunaona utimilifu wa utabiri wa Nabii Isaya unatimia katika kuzaliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristo. Mwinjili Mathayo anatueleza namna kuzaliwa kwake Bwana kulivyokuwa. Katika tamaduni za Wayahudi, uchumba ulikua tayari ni hatua ya kwanza ya ndoa ya kisheria, ambapo ulidumu kwa muda wa takribani mwaka mmoja. Katika hatua hii mwanamume na mwanamke walikua tayari ni Mume na Mke ijapokuwa walikuwa hawaishi pamoja. Endapo kulitokea ukosefu wa uaminifu, uchumba huu ulivunjwa kwa talaka na ilihesabika kama ni uzinzi, na adhabu yake ilikua ni kupigwa mawe mpaka kufa. Ni katika hatua hii ya kwanza kabisa, Yusufu, anagundua kuwa Mariamu alikua tayari na mimba. Ulikua ni wakati mgumu sana kwa Yusufu kwa kuwa kisheria alipaswa kuomba talaka na ndoa ile ivunjwe, na Mariamu angepata adhabu ya kupigwa mawe mpaka kufa. Kwa upande wa Mariamu, ilikua ni ngumu sana kumweleza Mumewe Yusufu jambo lile liliwezakanaje. Yosefu tunaambiwa alikuwa ni “Mtu wa haki” Neno la kigiriki linalotumika hapa ni dikaios, yaani, sio haki tu kwa kufuata sheria kwa ukali, bali huruma, inayoambatana na uaminifu kwa Mungu.
Mtakatifu Yosefu anaamua kumwacha kwa siri, ili Mariamu abaki salama. Ni Katikati ya hofu, mashaka, mkanganyiko huo, Mwenyezi Mungu anatoa jibu, katika ndoto, katika ukimya, anaonesha njia na kuondoa mashaka yote. Na hapa tunaona sababu kwa nini Yosefu anatajwa katika historia ya ukombozi. Kwanza ni ili utabiri utimie, Masiha atazaliwa kutoka katika ukoo wa Daudi kama kama ilivyotabiriwa na Nabii Isaya na manabii wengine katika Agano la kale. Hivyo kwa kumchukua Mariamu na kumpatia mtoto jina, Yesu (Yeoshua) Yusufu anamwingiza Yesu katika ukoo wa Daudi. Pili ni uthibitisho wa wazi kabisa kwamba, kuzaliwa kwake Yesu ilikua ni kwa njia ya Roho Mtakatifu, ulikua ni mpango wa kimungu wala sio kwa nguvu za kibinadamu na Yosefu anakuwa Baba mlishi wa Yesu. Tatu, utii wa Yosefu na Maria katika kupokea mpango wa Mungu, ijapokua ulikua mgumu na usioeleweaka hapo Mwanzo inatuonesha namna Mungu anavyomshirikisha mwanadamu mpango wake wa ukombozi.
Somo la pili: Ni Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi 1:1-7. Mtume Paulo katika Waraka wake kwa Warumi, anajitambulisha kama mtumwa wa Kristo, aliyeitwa na Kristo Yesu mwenyewe kuwa Mtume. Ni wazi kwamba Mtume Paulo hakujichagua mwenyewe, bali ni Mungu mwenyewe alimchagua na kumtuma. Utume wake ulikua ni nini hasa? Anasema aliitwa ili aihubiri Injili ya Mungu, yaani Habari Njema ambayo Mungu aliwaahidi watu wake tangu kale kwa vinywa vya manabii. Hii inatukumbusha kwamba, Habari Njema ya Kristo katika Agano jipya ni mwendelezo na utimilifu wa Ahadi katika Agano la kale, yaani Mpango wa Mungu wa ukombozi utimilifu wa nyakati ulipowadia (Gal 4:4-5). Mtume Paulo anaeleza Injili hii inahusu nini hasa. Ni Habari za Mwanaye. Hapa Mtume Paulo anafundisha ukweli juu ya mambo mawili kuhusu Kristo. Kwanza, Kristo alizaliwa katika ukoo wa Daudi kwa jinsi ya mwili, uthibitisho kwamba Kristo ni mtu kweli, aliyetwaa hali yetu sisi. Pili, kwa jinsi ya roho ya Utakatifu, uthibitisho kwamba ni Mungu kweli, aliyeshinda kifo na mauti katika ufufuko wake. Asili hizi mbili za Kristo zinasimama kama kiini cha Fumbo la Imani yetu sisi Wakristo. Mtume Paulo alipokea neema na utume wa kuwahubiri mataifa yote Habari hii njema, ili waipokee Imani. Kumbe utume wa Warumi nasi sote wabatizwa ni kuudhihirisha uwepo wa Mungu kati ya watu wa mataifa yote kwa njia ya ushuhuda wa Imani yetu.
Ndugu zangu katika masomo yetu yote katika dominika hii ya nne ya Majilio tuna mafundisho yafuatayo ya kujifunza. Kwanza: Mwenyezi Mungu anatuahidia baraka hata pale tunapokuwa dhaifu. Katika somo la kwanza, tunamwona Mfalme Ahazi aliyekuwa katika wakati mgumu, akiwa na hofu na mashaka makubwa kutokana na hatari iliyokua inakabili taifa lake. Nabii Isaya anampa ujumbe wa matumaini kwamba asiogope kwa kuwa Mungu alikua pamoja na watu wake. Lakini Ahazi alikua tayari na mipango yake, aliona tumaini kwa taifa kubwa la Waashuru kuliko kumtegemea Mungu wa Israeli, na licha ya kuambiwa aombe Ishara ya uthibitisho kwamba Mungu angewalinda, bado alikataa pia kuomba Ishara hiyo. Licha ya kukosa kwake Imani, bado Mwenyezi Mungu akatoa Ishara ya Imanueli, utabiri utakaotimia kwa kuzaliwa kwake Yesu. Ndugu mpendwa, katika maisha yetu tunakutana na hofu na mashaka juu ya mambo mengi. Kama Ahazi alivyokuwa na hofu ya kuvamiwa na mji wake kuvunjwa ndivyo nasi tunapata hisia hiyo nyakati fulani za maisha yetu. Kuna nyakati tunaona kabisa, hii biashara yangu inakwenda kufa. Kuna nyakati tunaona hii ndoa hii inaelekea pabaya, kuna nyakati tunaona, hawa watoto kwa mwenendo na style hii ya maisha, hawatafika mbali, kuna nyakati tunaona kabisa kwa mipango hii na hali inayokwenda, hakuna mwanga, hapa siwezi kutoka wala “kutoboa.”
Ni nyakati tunaona kabisa, kwa ugonjwa huu, na kwa afya hii, kwa kweli sitamaliza huu mwaka. Kila mmoja amekua na hofu kwa namna yake. Swali moja la msingi tunalotafakarishwa leo ni kwamba, katika hali hiyo, matumaini na imani yetu tunayaweka wapi? Tunamkumbuka Mungu kwanza au Mungu anakumbukwa baada ya majaribio mbalimbali ya kidunia kutokutoa majibu kwa wakati? Mwenyezi Mungu anatualika nasi pia kuomba ishara, na ishara hiyo si nyingine ni uwepo wa mwanaye ndani mwetu. Ishara tunayoalikwa kuomba ni Imanueli, Njoo Yesu, kaa katika moyo wangu, tawala hofu zangu, ondoa huzuni na mashaka yangu, tawala familia yangu, tawala watoto wangu, tawala ndoa yangu, tawala biashara yangu, nipe nguvu, umenijaribu, umenipima, umejua hata hili naweza kulibeba. Mungu anatuahidi baraka, hata pale tunapokuwa dhaifu. Hatunyimi nguvu ya kufanya kazi kwa kuwa sisi tumekosa imani, hatunyimi afya njema kwa kuwa tumekuwa waregevu, hatunyimi riziki zetu za kila siku kwa kuwa hatujamshukuru, hatunyimi ulinzi dhidi ya maadui wa rohoni na mwilini kwa kuwa sisi tumemkimbia kama Ahazi. Licha ya hayo yote bado anatenda, bado anatuona, bado anatuinua, bado anatubariki. Leo umeamka sio kwa sababu jana ulisali na kushukuru, ila ni kwa sababu Mungu anakupenda, Mungu anakupa nguvu ili uendelee kumtumikia, urekebishe makosa ya jana ili kesho yako ikawe njema, yenye neema na baraka zaidi.
Pili: Mwenyezi Mungu anatimiza ahadi yake kwa muda na wakati wake. Katika somo la pili Mtume Paulo anatuthibitishia kwamba Kristo ni Masiya, Mungu kweli na Mtu kweli, mzao wa Daudi, akitimiza Ahadi ya Mungu kama ilivyotabiriwa na Manabii katika Agano la kale. Ni Ahadi ya Mungu iliyotimia katika wakati wa Mungu. Utabiri wa Nabii Isaya juu ya Masiya unapata utimilifu wake takribani miaka 600 baadaye kwa kuzaliwa Bwana wetu Yesu Kristo. Huu ni ukweli wa Imani yetu kwamba, Kristo ni Mungu kweli na mtu kweli aliyezaliwa na Bikira Maria kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Ndiye Imanueli, Mungu anayekuja, na kutwaa ubinadamu wetu na kukaa kati yetu. Ndugu mpendwa, Mwenyezi Mungu ni mwaminifu kwa Ahadi zake. Alichoahidi kwa Abrahamu na uzao wake anakitimiza kwa kuzaliwa kwake Yesu. Si Mungu aliye mbali tena na watu wake, bali ni Mungu aliye karibu kabisa na watu wake. Ananena nasi sasa kwa njia ya Mwanaye wa pekee. Ndugu mpendwa, Mungu anasema nawe katika wakati wake, anatimiza Ahadi zake kwako katika muda na majira yake. Mara nyingi tunamfikiria Mungu katika vipimo na wakati wetu wa kibinadamu. Tunatamani kumwona Mungu akitenda kazi katika wakati wetu, na kusahau kuwa Mungu wetu hafungwi na wakati, hafungwi na majira. Usisikitike pale unapoona Mungu anachelewa kujibu sala zako, usihuzunike ukiona majibu ya maombi yako yanachelewa. Bali kuwa na tumaini kwamba Mungu ana mpango mkubwa na mzuri zaidi kuliko yale tunayotamani atujibu kwa wakati wetu.
Tatu: Bikira Maria ni Mama wa Mungu. Katika somo la Injili, Malaika Gabrieli anamwambia Yosefu kwamba, Usihofu kumchukua Mariamu Mkeo, maana mimba yake ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana ndiye atakayewaokoa watu na dhambi zao. Utabiri wa Nabii Isaya unatimia kupitia Bikira Maria. Kanisa latufundisha kuwa Yesu ni Mungu, kwa nafsi (Divine person), mwenye asili mbili (two natures) yaani Mungu kweli na mtu kweli. Hivyo katika Mtaguso wa Efeso mwaka 431 AD, Kanisa likatangaza kuwa Bikira Maria ni Mama wa Mungu, kwa sababu alimzaa Yesu nafsi ya pili ya Mungu. Kanisa likatangaza kuwa Bikira Maria ni Mama wa Mungu: “Theotokos” yaani, “Aliyembeba Mungu” (KKK 495). Sherehe hii inaadhimishwa kila mwaka tarehe 01 Januari. Nne: Utii wa Imani kwa Mpango wa Mungu hata kama unakwenda kinyume na mipango yetu. Katika somo la Injili Takatifu tunamwona Mtakatifu Yosefu ambaye alikua tayari na mipango yake. Yosefu alikua na matazamio yake na ndoto zake. Lakini anapojulishwa mpango wa Mungu ambao kimsingi ulikwenda kinyume na logic ya kibidamu, Yosefu anakubali na anapokea huo mpango wa Mungu. Hakubisha, hakukataa, hakulalamika bali aliamini na kutii. Mwenyezi Mungu anahitaji ndiyo ya mwanadamu katika kuutekeleza mpango wake wa kimungu.
Ndugu mpendwa, Mtakatifu Yosefu anakua kwetu kielelezo cha utii kwa Mapenzi ya Mungu. Mapenzi ya Mungu daima si mapenzi yetu, njia zake si njia zetu. Ni katika ukimya, katika ndoto ndipo Yosefu aliweza kuyatambua mapenzi ya Mungu. Aliweza kuelewa na kuuchukua ule kama mpango wa Mungu licha ya kwamba ulikua kinyume na matazamio yake na haukueleweka barabara. Tunapomtafakari Mtakatifu Yosefu, tunaalikwa katika ukimya kumruhusu Mungu aseme na mioyo yetu. Kama tulivyoona katika somo kwanza namna Ahazi alivyojipangia mipango yake na kuukwepa mpango wa Mungu, ndivyo mara kadhaa tunavyoweza kukosa utulivu, ukimya wa ndani kabisa na kuzungumza na Mungu, ili tufahamu anataka nini kwetu, tuisikie sauti yake na kuifuata, tuyapokee mapenzi yake katika hali zote. Mwenyezi Mungu alimwambia Yusufu, usiogope. Anatuambia na sisi hasa pale tunaposhindwa kuyapokea na kuyaelewa mapenzi ya Mungu, usiogope. Anatuambia tusiogope si kwa sababu mambo yote yatakuwa rahisi, bali ni kwa sababu atakuwa nasi, atakwenda nasi katika safari yetu yote ya kutekeleza mpango wake. Njia ya Yosefu haikua rahisi, safari ya kutimiza mpango wa Mungu ilikuwa na vikwazo vingi, lakini alisikia sauti ya Mungu, usiogope. Kristo anazaliwa kati yetu, Yupo daima katikati yetu, sasa na hata milele. Usiogope, kuzungumza naye, usione shaka kumsikiliza anaposema nawe katika sala, katika ukimya.
Sita: Kristo alizaliwa katika familia, anatualika sote katika familia yake. Mwenyezi Mungu aliamua kwamba Kristo azaliwe katika familia ya wanadamu. Anaingia katika historia yetu, katika muda wetu, katika ukoo wa Daudi. Anakuwa katika kila jambo sawa na sisi ili atustahilishe tena kuingia katika familia ya wana wa Mungu. Imanueli anakaa kati ya watu wake, ndiye habari Njema aliyoihubiri Mtume Paulo kwa watu wa mataifa yote, ndiye Kristo anayekaa katika kanisa lake na anaahidi kukaa nasi siku zote mpaka utimilifu wa dahari (Mt. 28:20). Kristo anatualika sote kuingia katika ushirika naye, yeye aliyekubali kukaa katika familia ya wanadamu. Hapa tunaona wajibu wa Maria na Yosefu katika kupokea mpango wa Familia na namna walivyoshirikiana pamoja katika kutunza uhai, kumtunza mtoto Yesu dhidi ya hatari mbalimbali. Je, upo usalama katika familia zetu za sasa? Tunatunza zawadi ya uhai ambao ni mali ya Mungu na zawadi anayotupatia katika familia? Tunaishi kwenye ulimwengu ambapo utoaji wa mimba na uharibifu wa maisha kwa sababu mbalimbali imekua jambo la kawaida kabisa. Tumwombe Mungu msamaha, mara zote tulizoshiriki kuondoa uhai ndani ya familia ya Mungu. Lakini pia tumwombe Kristo aendelee kukaa nasi katika familia zetu, akae ndani ya mioyo yetu na atufanye upya, hata kama tulikwisha shindwa.
Mtakatifu Yosefu alikua tayari kumlinda Maria, hakutaka kumdhalilisha, hakutaka na hivyo akaazimu kumwacha kwa siri. Je, ni mara ngapi tumekuwa warahisi kusema maneno mabaya juu ya wengine na kusambaza habari za uwongo ambazo zimepelekea kuwaumiza mioyo wengine, kuwavua nguo wengine na kuwaaibisha? Tunaalikwa kuinga mfano wa Yosefu ambaye alikua tayari kwa gharama yoyote kumlinda Mariamu ili abaki salama. Tuwe walinzi wa wenzetu kwa kuwasemea mema, kwa kuwatunzia siri pale wanapotuamini na kutushirikisha mambo yao, au hata changamoto zinazowasibu. Tuwe chanzo cha kurejesha furaha na matumaini mapya kwa wale wote wanaopitia changamoto na nyakati ngumu na za maamuzi katika maisha yao. Hitimisho: Katika Dominika ya Nne ya Kipindi cha Majilio Mwaka A wa Kanisa, tumshukuru Mungu kwa zawadi ya Mwanaye Yesu Kristo Mkombozi wetu, tuombe neema ya kupokea furaha, faraja na matumaini mapya yaletwayo na Habari Njema ya Kristo atakayezaliwa kwetu. Imanueli, Mungu pamoja nasi.