Tafuta

Fadhila ya unyenyekevu ni msingi wa tafakari kuhusu Fumbo la Umwilisho. Fadhila ya unyenyekevu ni msingi wa tafakari kuhusu Fumbo la Umwilisho.  (ANSA)

Tafakari Dominika IV Majilio: Chemchemi ya: Tumaini, Haki na Amani

Fadhila ya unyenyekevu ni msingi wa tafakari kuhusu Fumbo la Umwilisho.: "Bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba”. Flp. 2:7-8. Mwenyezi Mungu ni upendo na kielelezo cha hali ya juu kabisa cha unyenyekevu, mwaliko ni kumjifunza Kristo Yesu kwani Yeye ni mpole na mnyenyekevu.."

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

UTANGULIZI. Karibu mpenzi msikilizaji na msomaji wa tafakari ya neno la Mungu kutoka hapa Radio Vatican Tumefika katika hatua ya mwisho ya safari ya Kipindi cha Majilio. Sherehe ya Noeli ni kielelezo cha unyenyekevu wa Mungu, ni Sakramenti ya ufukara wa Kristo Yesu anayeteseka kati ya waja wake, lakini zaidi kati ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Mama Kanisa anawaalika watoto wake kumwendea Kristo Yesu ili aweze kufanya makazi yake kati yao. Fadhila ya unyenyekevu ni msingi wa tafakari kuhusu Fumbo la Umwilisho. “Hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba”. Flp. 2:7-8. Mwenyezi Mungu ni upendo na kielelezo cha hali ya juu kabisa cha unyenyekevu, mwaliko ni kumjifunza Kristo Yesu kwani Yeye ni mpole na mnyenyekevu wa moyo! Kumbe, Sherehe ya Noeli ni kielelezo cha unyenyekevu wa Mungu, mwaliko kwa waamini kujishusha na kumwabudu. Tumaini lililopandwa katika wiki ya kwanza sasa limekaribia kuchanua katika ujio wa Mkombozi. Leo, tunakumbushwa kuhusu tumaini na wokovu wa Mungu. Kristo Yesu anakuja ulimwenguni kuleta amani na haki. Katika hali ya maisha ya leo, dunia inakabiliwa na migawanyiko, vita, umasikini, na changamoto za familia na jamii. Masomo ya leo yanatufundisha kushikamana na Mungu, kuishi kwa haki, na kuwa mashahidi wa amani.

Kristo Yesu ni jua la haki
Kristo Yesu ni jua la haki

Dominika hii inatufundisha jambo kuu: matumaini ya kweli hupata mwili katika Kristo Yesu. Ndiyo maana Kanisa leo linatupatia jina hili la ajabuImanueli, yaani Mungu pamoja nasi. Katika mwaka huu wa Jubilei ya Tumaini, tunatazama si tu tukio la kuzaliwa kwa Yesu, bali maana yake ya kudumu: Mungu hakubaki mbinguni, alishuka kuwa nasi, kutembea katika historia yetu, kubeba udhaifu wetu, na kutupa tumaini jipya. Uzazi wa Mwana pekee wa Mungu ni zao la utii na heshima kwa mpango wa Mungu kumkomboa mwanadamu. Maria na Yosefu kila mmoja kwa nafasi yake wanaridhia nia ya Mungu kwa viumbe wake, wanatii na kutufundisha sisi pia kuwa watii kwa Mungu na kwa Kanisa lake. Somo la Kwanza: Isaya 7:10-14 Mungu anatoa ishara Mwana atazaliwa, aitwe Immanuel, “Mungu pamoja nasi”.Leo, bado tunahitaji ishara ya tumaini pale tunapokosa amani na usalama. Kristo ni mwanga katika giza. Je, ninaweka imani yangu kwa Mungu hata pale changamoto zinapokuwa kubwa? Ujauzito ambao ameelezwa kuwa nao Bikira Maria katika Injili ya leo (Mt 1:18-25) ni zao la ukubali wake kwa ujumbe wa Gabriel  Malaika wa Mungu wa  kutaka kwa njia yake azaliwe Mwana atakayeikomboa dunia (Lk 1:28-35)... Yosefu na Maria walikuwa wachumba, halafu bila kutazamia Yosefu akaona mwenzake mjamzito, akajiuliza mambo haya maana yake nini? Iwaje ampe jina, amlee na kumtunza mwana asiye wake? Yosefu anadhamiria kuachana na Maria kistaarabu. Yosefu aliwaza hayo sababu alikuwa mcha Mungu akishika sheria ya Musa na sheria ya Upendo… la sivyo angemwaibisha hadharani na zaidi angefurahia kuona hukumu yake ya kifo cha mawe mbele ya mlango wa baba yake kadiri ya sheria yao nyakati zile (Kumb 22:22 -23).

Fumbo la Umwilisho ni ushuhuda wa uwepo endelevu wa Mungu.
Fumbo la Umwilisho ni ushuhuda wa uwepo endelevu wa Mungu.   (@Vatican Media)

UFAFANUZI: Inawezekana Maria alimtaarifu Yosefu juu ya ujumbe wa Gabrieli, hakuwa na sababu ya kumficha. Hivi kubabaika kwa Yosefu haikuwa sababu hasa ya kukosa uaminifu kwa Maria ila alijitafakari mwenyewe na kujiuliza yeye Yosefu katika ule mchakato mzima ana nafasi gani? Isije kuwa kwa kuendelea kuambatana na yule binti Sayuni akawa anaingilia mpango wa Mungu, akaamua kusubiri. Daima Mwenyezi Mungu huwakirimia busara na hekima wachamungu wake na ndiyo maana busara za Yosefu za kutochukua hatua mapema zinatoa nafasi ya mafunuo kwa njia ya Malaika juu ya mradi mzima. Paulo anatufundisha juu ya wito wa kuwa watumishi wa Injili. Hii inatufundisha kwamba kila mmoja wetu ana jukumu la kueneza upendo na haki katika familia na jamii. Ni kutokana na utii, heshima na ukubali wa Maria na utayari wa Yosefu kumtwaa Maria kama mke wake ndio kunapelekea unabii wa Isaya katika somo I (7:10-14) kuzaliwa Emmanuel kwa njia ya Bikira unatimia, Mungu anazaliwa kutoka ukoo wa Daudi kwa jinsi ya mwili na kudhihirishwa kwa uweza kuwa Mwana wa Mungu kwa jinsi ya roho ya utakatifu (somo II: Rum 1:1-7)na kukaa nasi ili ubinadamu wetu uzaliwe upya nasi tustahili tena kuitwa wana wapenzi wa Baba. Mara nyingi na kwa namna mbalimbali Mungu hutupatia maagizo ili tuishi vema na kuung`arisha ufalme wake, bila bahati hatujawa watii kutosha, ndicho kiburi kilichopelekea wazee wetu kufukuzwa bustanini na kuadhibiwa... tutamani na kuiga utii wa Bikira Maria na Yosefu kwa mpango wa Mungu.

Bikira maria na Mtakatifu Yosefu ni Mashuhuda amini wa Fumbo la Umwilisho
Bikira maria na Mtakatifu Yosefu ni Mashuhuda amini wa Fumbo la Umwilisho   (@Vatican Media)

Utii huleta utaratibu na nidhamu katika jamii na taasisi, kwenye utii hakuna fujo wala malumbano, utii huleta maendeleo sababu sote tunakuwa tunazungumza lugha moja na kusikiliza sauti moja. Tujifunze kumwamini Mungu, kuisikia sauti yake na kuwa waaminifu kama Yosefu na Maria.Yosefu aliamua kumchukua Maria kuwa mke wake licha ya hali isiyo ya kawaida. Hii ni ishara ya imani, usaliti wa kweli, na uaminifu.  Je, katika maisha yangu, ninaonyesha uaminifu na upendo kwa familia na jirani hata wakati ni vigumu? Yosefu katika utii na uchamungu wake hakutaka kumwaibisha Maria kwa ujauzito kabla ya ndoa. Huenda sisi huwa tunafurahi kuaibishwa kwa wengine? Mfano katika familia, tunaaibishana sana, yaani mfano baba na mama kupelekana kwa balozi, kwa kitongoji, polisi nk kwa ajili ya changamoto za kinyumbani. Tujifunze kwa Yosefu mwenyeheri ambaye hakutaka kumwaibisha Maria. Kila mmoja wetu Dominika hii ya mwisho kuelekea sherehe ya Noeli aweke lengo la heshima na utii akisema ‘mimi ni mjakazi wa Bwana na iwe kwangu kama ulivyosema` hasa pale Mungu anapotutaka tumtumikie kwa namna ya pekee jinsi ile Bikira Maria alivyoridhia.

Kristo Yesu ni mwanga wa imani, haki na matumaini.
Kristo Yesu ni mwanga wa imani, haki na matumaini.   (@Vatican Media)

Yesu ni mwanga na wokovu wa dunia. Hata giza kubwa linaweza kuondolewa kwa imani na tendo la wema.  Haki na Amani: Tushirikiane na wengine, tuwe waaminifu, tuwe na huruma kwa wagonjwa na walio na changamoto. Matendo ya Kila Siku Tukumbuke kuomba kwa ajili ya familia na jamii yetu. Tukumbuke kuwasaidia wagonjwa na maskini. Tuwe mashahidi wa amani, tukionyesha mshikamano na upendo. Na kama Yosefu,  tusiwe wepesi wala tusiwe na papara ya kuamua na kuhukumu na kwa kuwa tumebakiza siku chache kumpokea Masiha ni vema ambao bado kufukia mabonde ndani ya mioyo yetu tufanye hima kwa kitubio ili siku hiyo ipate kuwa ya maana zaidi... Ili kuwa watii kweli kwa Mungu tusali tukiomba nguvu ya kutenda mema kwa maendeleo ya roho na mwili… kustawisha roho ya ukarimu, kusamehe kwa hiyari, kazi kwa bidii, kutowaza visasi, kauli njema, kutambua yaliyo ya muhimu zaidi, kuishi kwa viwango vya kimungu na kuuishi upendo usio na ubinafsi … “Ee Bwana, tufundishe kuishi kwa haki, kuwa na mshikamano, na kuwa chanzo cha tumaini kwa wengine. Amina.

Tafakari D4 Majilio
19 Desemba 2025, 11:09