Tafuta

Tafakari Liturujia ya Neno la Mungu Dominikka ya Nne ya Kipindi cha Majilio: Utii na Unyenyekevu Tafakari Liturujia ya Neno la Mungu Dominikka ya Nne ya Kipindi cha Majilio: Utii na Unyenyekevu 

Tafakari Dominika IV ya Majilio Mwaka A wa Kanisa: Utii na Unyenyekevu

Dominika ya Nne ya Kipindi cha Majilio Mwaka A inakita ujumbe wake kwenye Fumbo la Umwilisho na Bikira Maria kama njia ya Mungu kuleta Ukombozi, ikikumbusha jinsi ambavyo Bikira Maria alivyokubali kutekeleza mpango wa Mungu katika maisha yake. Masomo yanahimiza tumaini, furaha, na maandalizi kwa ajili ya ujio wa Kristo Yesu, Imanueli, yaani Mungu pamoja nasi. Kumbe, kunahitajika: Utii na Unyenyekevu ili kuweza kukubali na kupokea mpango wa Mungu!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya Nne ya Kipindi cha Majilio, Mwaka A wa Kiliturujia katika Kanisa. Ni Dominika ya mwisho katika kipindi cha majilio. Siku ya kushereheke kuzaliwa Yesu Kristo, Krismasi, Noeli, iko mlangoni, inabisha hodi. Ni katika muktadha huu maneno ya wimbo wa mwanzo yanasema: “Dondokeni, enyi mbingu, toka juu, mawingu na yammwage mwenye haki; nchi ifunuke, na kumtoa Mwokozi” (Isa. 45:8). Ujumbe mkuu ni kujivika fadhila ya utii na unyenyekevu, tuweze kumpokea Kristo Yesu Mwokozi katika maisha yetu, ili atuongoze kwenye njia ya uzima wa milele mbinguni. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi; “Tunakuomba, ee Bwana, utie neema yako mioyoni mwetu, ili sisi tuliojua kwa maelezo ya Malaika kwamba, Kristo Mwanao amejifanya mtu: kwa mateso na msalaba wake, tufikishwe kwenye utukufu wa ufufuko.” Somo la kwanza ni la kitabu cha Nabii Isaya (Isa 7:10-14). Ni utabiri na ushauri wa kinabii kwa Ahaz mfalme wa Yuda, ufalme wa kusini, Yerusalemu makao yake makuu, kuwa Mungu ndiye msaada pekee na wa uhakika dhidi ya adui zao. Hivyo wasiwe na hofu wala mashaka na wasiombe wala kufanya mkataba wa kiulinzi na falme zingine, bali wamtumainie Mungu peke yake, naye atawaokoa, maana ana uwezo wote na mwaminifu kwa ahadi zake. Lakini mfalme Ahazi hakuamini, ndipo Nabii Isaya alipomwambia aombe ishara kutoka kwa Mungu kama uthibitisho. Lakini alikataa, na kwa kiburi, akaamua kufanya alichotaka, kuomba msaada wa kibinadamu, akaingia mkataba na mfalme wa Ashuru.

Kristo Yesu ndiye lile Jua la haki
Kristo Yesu ndiye lile Jua la haki   (AFP or licensors)

Ni katika mazingira haya Nabii Isaya anamuonya akimuambia; umeacha kutegemea msaada wa Mungu na umechagua kufuata matakwa yako na kuomba msaada kwa kwa binadamu. Sasa ufalme wako utaangamizwa, na Mungu atakupa ishara uliyoikataa. Na ishara ni hii; “Tazama Bikira atachukua mimba na kuzaa mtoto wa kiume naye ataitwa jina lake Emanueli, yaani Mungu pamoja nasi”. Mababa wa Kanisa wanatufundisha kuwa mwanamke anayetajwa ni Bikira Maria na mtoto wa kiume ndiye Yesu Kristo. Ujumbe kwetu ni huu, tusiweke matumaini yetu yote kwa mamlaka ya kibinadamu, bali tumtegemee Mungu aliye muweza wa yote na mwaminifu kwa ahadi zake. Ni katika muktadha huu zaburi ya wimbo wa katikati inasema; “Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, Dunia na wote wakaao ndani yake. Maana ameiweka misingi yake juu ya bahari, na juu ya mito ya maji aliithibitisha. Ni nani atakayepanda katika mlima wa Bwana? Ni nani atakayesimama katika patakatifu pake? Mtu aliye na mikono safi na moyo mweupe. Asiyeinua nafsi yake kwa ubatili. Atapokea baraka kwa Bwana, na haki kwa Mungu wa wokovu wake. Hiki ndicho kizazi cha wamtafutao, wakutafutao uso wako, Ee Mungu wa Yakobo” (Zab. 24:1-6 (K) 7, 10).

Dominika ya IV ya Kipindi cha Majilio: Unyenyekevu na Utii
Dominika ya IV ya Kipindi cha Majilio: Unyenyekevu na Utii   (ANSA)

Somo la pili ni la waraka Mtume Paulo kwa Warumi (Rm 1:1-7). Katika sehemu hii Mtume Paulo anatueleza kuwa Yesu Kristo, Mwana wa Mungu aliyezaliwa na Bikira Maria katika ukoo wa Daudi, ni Mungu kweli na mtu kweli, lakini hakuwa na dhambi. Ni katika hali hiyo ya kutokuwa na dhambi, anao uwezo wa kutufanya sisi tulio wadhambi tuufikie uzima wa milele. Yeye alizaliwa akafa na kufufuka katika wafu kwa wokovu wetu. Hii ina maana ya kuwa Krismasi na Pasaka ndio msingi wa fumbo la ukombozi wetu. Na hii ndiyo imani tuliyoipokea kutoka kwa mitume, na Kanisa linaendelea kuihubiri kwa nyakati zote, kuwa Kristo peke yake ni Mungu kweli na Mtu kweli, na ni kwa njia yake viumbe vyote viliumbwa na ni katika Yeye tu, sisi tunaweza kuupata uzima wa milele. Injili ni kama ilivyoandikwa na Mathayo (Mt 1:18-25). Sehemu hii ya Injili inaweka wazi kuwa utabiri wa Nabii Isaya umetimia katika kuzaliwa kwake Yesu Kristo na Bikira Maria. Huyu ni Emanueli halisi, Mungu pamoja nasi. Dokezo kwa kazi yake, limebebwa na jina lake ambalo ni “Yesu” yaani “Mungu mkombozi wetu”. Kutimia kwa utabiri huu ni tunda la utii na unyenyekevu wa Maria na Yosefu walivyosikiliza ujumbe wa Mungu, na kuufanyia kazi. Unyenyekevu na utayari wao katika kutimiza mapenzi ya Mungu ulimleta mwokozi duniani, na kwa kupitia Yeye wokovu wa wanadamu umefanyika.

Ujumbe wa Neno la Mungu: Tumtegemee na kumtumainia Mungu
Ujumbe wa Neno la Mungu: Tumtegemee na kumtumainia Mungu   (AFP or licensors)

Kama Bikira Maria tunapaswa tuwe na utii, tuitikie sauti ya Mungu anapotuita katika kumjua, kumpenda, na kumtumikia katika maisha yetu. Kwa Yosefu tunajifunza kuwa wema, wenye haki, na kutokuhukumu wengine. Ikumbukwe kuwa kulingana na sheria za kiyahudi, Yosefu na Maria, ingawa walikuwa bado wachumba, walitambuliwa kama mume na mke, lakini hawakuruhusiwa kukutana kimwili mpaka wafunge ndoa. Katika mazingira hayo, mchumba wa kike akipata mimba kabla ya ndoa, sheria iliamuru apelekwe mahakamani, apewe talaka na adhabu yake ni kupigwa kwa mawe hadi kufa. Yosefu kwa kuwa alikuwa ni mtu wa haki na mcha Mungu, alipotambua kuwa mchumba wake Maria ana mimba aliamua kumuacha kwa siri. Lakini kabla ya kutekeleza maamuzi yake, alipata ujumbe wa Mungu kwa njia ya Malaika katika ndoto, naye bila kusita, aliupokea, akaufanyia kazi, akamchukua Bikira Maria kwake, na akawa tayari kumtunza na kumlea mtoto atakayezaliwa. Ni katika muktadha huu Yosefu amekuwa kielelezo na mfano bora wa kuiga. Nasi tujifunze kutohukumu wengine, wala kufurahia kuangamia kwa makosa yao, tutunze heshima na utu wa wengine, tusaidiane kutimiza mapenzi ya Mungu katika maisha yetu kwa ajili ya uzima wa milele. Tusitafute umaarufu kwa kutangaza makosa ya wengine kwa faida binafsi. Mtakatifu Yosefu atuombee tuwe watu wa kupenda haki na kutunza heshima za wengine, ili Kristo atakapozaliwa atukute tumejiandaa vyema kumpokea kwa kuwatendea haki watu wote bila kujali umri, jinsia au rangi. Kwa kufanya hivyo Kristo Yesu atazaliwa katika maisha yetu, katika nafsi zetu, katika familia zetu na jumuiya zetu, na kutuletea amani na furaha ya kweli.

Kristo  Yesu ni Jua la Haki
Kristo Yesu ni Jua la Haki

Tutambue kuwa Betlehemu ya sasa, hori au pango la sasa ni mioyo yetu ambamo Kristo anataka kujimwilisha. Basi tutumie vizuri muda uliobaki kujiandaa vyema ili tumpokee, naye atupe hadhi ya kuendelea kuitwa wana wapendwa wa Mungu. Hili litawezekana kama tutamruhusu Roho Mtakatifu aingie ndani mwetu na kututakatifuza. Ndiyo maana mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali hivi; “Ee Bwana, Roho yule ambaye kwa uwezo wake Maria mwenye heri alipata mimba, azitakase dhabihu zetu tulizoweka juu ya altare yako, nasi tujaliwe neema kwa hizo dhabihu”. Na katika sala baada ya komunyo anasali hivi; “Ee Mungu Mwenyezi, tumekwisha pokea amana ya ukombozi wa milele. Tunaomba jinsi tunavyoikaribia hiyo sikukuu takatifu, tuzidishe ibada yetu, tupate kuliadhimisha vema fumbo la kuzaliwa kwake Mwanao”. Tukifanya hivyo tutasherehekea Noeli kwa shangwe, nderemo na vigelegele vya furaha. Na hili ndilo tumaini letu. Tumsifu Yesu Kristo!

Dominika IV Majilio
19 Desemba 2025, 08:55