Tafuta

Dominika ya Tatu ya Kipindi cha Majilio: Baba Mtakatifu Francisko anasema, Furaha ya Injili huijaza mioyo na maisha ya wote wanaokutana na Kristo Yesu. Dominika ya Tatu ya Kipindi cha Majilio: Baba Mtakatifu Francisko anasema, Furaha ya Injili huijaza mioyo na maisha ya wote wanaokutana na Kristo Yesu.   (ANSA)

Tafakari Dominika ya Tatu ya Majilio Mwaka A wa Kanisa: Furaha Katika Bwana

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Furaha ya Injili huijaza mioyo na maisha ya wote wanaokutana na Kristo Yesu. Wale wanaokubali zawadi yake ya ukombozi wanawekwa huru kuondokana na dhambi, uchungu, utupu wa ndani na upweke. Pamoja na Kristo Yesu, daima furaha inazaliwa upya na huo unakuwa ni mwanzo wa uinjilishaji mpya unaosimikwa kwa Kristo Mfufuka. Rej Evangelii gaudium, 1. Kanisa linaadhimisha pia Jubilei ya wafungwa pamoja na askari magereza.

Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., - Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.

Utangulizi: Wapendwa Taifa la Mungu, leo ni Dominika ya 3 ya Kipindi cha Majilio Mwaka A wa Kanisa. Ni nusu ya safari yetu ya Majilio, ambapo tunapewa ujumbe wa matumaini kwamba, “FURAHINI au GAUDETE” Kwa nini tunaalikwa kufurahi? Baba Mtakatifu Francisko anasema, Furaha ya Injili huijaza mioyo na maisha ya wote wanaokutana na Kristo Yesu. Wale wanaokubali zawadi yake ya ukombozi wanawekwa huru kuondokana na dhambi, uchungu, utupu wa ndani na upweke. Pamoja na Kristo Yesu, daima furaha inazaliwa upya na huo unakuwa ni mwanzo wa uinjilishaji mpya unaosimikwa kwa Kristo Mfufuka. Rej Evangelii gaudium, 1. Mtume Paulo katika waraka wake kwa Wafilipi 4:4-5 anatupa sababu kwa nini tunapaswa kufurahi. Tumeimba katika antifona ya mwanzo maneno haya ya Mtakatifu Paulo kwamba, “Furahini katika Bwana siku zote, tena nasema furahini. Bwana yu karibu” Hatufurahi kwa sababu tunaondolewa shida, matatizo na misalaba yetu, la hasha, tunafurahi kwa kuwa hata katika shida na mahangaiko yetu, Mungu yupo katikati yetu, akituahidia mwanzo mpya na utimilifu wa Ahadi zake. Ndio maana katika Dominika ya leo, Liturujia inabadilika. Mshumaa wa tatu, mshumaa wa Mtakatifu Yosefu, pamoja na mavazi ya ibada ni rangi ya waridi tofauti na mishumaa na mavazi ya dominika zingine, Ishara ya furaha tunayokaribia kuipokea, furaha tuliyoipoteza sababu ya dhambi, inayorejeshwa kwa kuzaliwa Mwokozi wa ulimwengu. Masomo yetu yote katika Dominika hii yanatupa sababu kwa nini tunaalikwa kufurahi.

Furahini katika Bwana, tena nasema furahini
Furahini katika Bwana, tena nasema furahini   (ANSA)

Somo la 1: Ni kitabu cha Nabii Isaya 35:1-6, 10: Somo la kwanza ni kutoka kitabu cha Nabii Isaya. Ni utabiri wa Nabii Isaya juu ya taifa la Mungu waliokaa utumwani Babeli kwa muda wa miaka 70. Wataalamu wa Maandiko Matakatifu wanatueleza kuwa, sura hii ya 35 inasimama kama daraja kati ya nyakati mbili za maisha ya Taifa la Mungu, yaani nyakati za Mateso na hofu na nyakati za Furaha na matumaini mapya. Taifa hili la Mungu kwa kupelekwa utumwani Babeli walipoteza nchi yao na kuwa watumwa, walipoteza uhuru wao, walipoteza hekalu ambapo walimwabudu Mungu, walipoteza utambulisho wao, kutoka kuitwa taifa la Mungu hadi kuwa watumwa na mateka, walipoteza familia, ndugu, na jamaa zao. Ni watu waliokuwa wamejikatia tamaa kabisa. Kwao, maisha yalikua ni jangwa tupu litishalo, maisha yalikua ni nchi kame isiyo na chakula wala maji, maisha yalikua ni usiku wenye kiza kinene, maisha yalikua ni ukiwa. Matumaini yalififia, furaha ilipotea, huzuni, hofu na mateso vilitawala. Katika hali hiyo Mwenyezi Mungu ananena na mioyo yao kupitia kinywa cha Nabii Isaya akisema, “Nyika na mahali palipo na ukiwa patafurahi; jangwa litashangilia na kuchanua maua kama waridi. Itieni nguvu mikono iliyo dhaifu, yafanyeni imara magoti yaliyolegea. Waambieni walio na moyo wa hofu, jipeni moyo msiogope.  Kwa nini wasiogope? Kwa kuwa Mungu wenu atakuja kuwaokoa ninyi” Ni Mungu ambaye katika utimilifu wa wakati, anatwaa mwili na kuja kati ya watu wake, anawaletea ukombozi wa milele, kutoka utumwa wa dhambi na mauti. Vipofu wataona, viziwi watasikia, vilema watarukaruka. Utabiri huu unatimia katika maisha na utume wa Bwana wetu Yesu Kristo.

Furahini kwani Bwana Yu Karibu
Furahini kwani Bwana Yu Karibu   (ANSA)

Somo la Injili: Ni Injili ya Mt. 11:2-11. Katika somo la Injili takatifu, Yohane Mbatizaji akiwa gerezani. Tukumbuke katika dominika iliyopita ile sura ya 3:1-12, Yohane anatangaza ujio wa masiya, na anataalika watu kujiandaa kwa ujio wake, akitangaza pia ujio wa hukumu akisema, shoka limekwishawekwa penye shina, basi kila mti usiozaa matunda mazuri utakatwa (Mt. 3:10). Akaongezea kusema, anakuja yeye ambaye pepeto lake li mkononi mwake, naye atausafisha sana uwanda wake na kuikusanya ngano yake ghalani, bali makapi atayateketeza kwa moto usiozimika (Mt. 3:12). Kumbe Yohane alitegemea Masiha atakapokuja, atatoa hukumu mara moja kwa wale waliokuwa wakiwatesa na kuwaumiza taifa   Mungu, yaani dola dhalimu ya warumi, akiwaondoa watawala dhalimu kama Herodi aliyekua mtawala wakati huo. Matokeo yake, Yesu anatangaza habari Njema ya Ufalme mpya wa Mungu, anatangaza msamaha, anakula pamoja na wenye dhambi, anafufua wafu, anaponya wagonjwa, hakupambana kisiasa kuiangusha dola ya Mrumi na mbaya zaidi, Yohane aliendelea kubaki gerezani mpaka atakapokatwa kichwa. Hivyo Yohane anapata wasiwasi, kwamba, hivi ni wewe tuliyekutegemea au tusubiri mwingine? Mbona mambo siyo kabisa kama tulivyotegemea? Kama ni wewe tuliyekutegemea, kwa nini bado shida zipo, mbona mateso ni yale yale tu, kwa nini bado maumivu, dhuluma, unyanyasaji na maovu yapo? Jibu la Yesu ni fupi na linaturejesha tena katika somo la kwanza tulilosikia kutoka kwa Nabii isaya. Anasema, “Nendeni mkamweleze Yohane mnayoyaona na kuyasikia, vipofu wanaona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa na maskini wanahubiriwa Habari Njema. Kumbe utabiri ule wa Nabii Isaya sura ile ya 35 unatimia kwa kuja kwake Masiya. Yohane Mbatizaji anakua mtangulizi wa huyo Masiha.

Msiogope Mungu wenu anakuja kuwaokoa
Msiogope Mungu wenu anakuja kuwaokoa   (ANSA)

Somo la pili: Ni waraka wa Mtume Yakobo kwa watu wote 5:7-10. Mtume Yakobo aliandika waraka huu kwa Wakristo walikua wakiishi nje ya Palestina, waliotawanyika (diaspora) katika dola ya Kirumi. Kama ilivyokuwa kwa Wakristo wengi wa mwanzo, Wakristo hawa walishika mafundisho ya mitume juu ya ujio wa pili wa Bwana (parousia), lakini waliamini kwamba angekuja mara, asingekawia. Kwa nini Mtume Yakobo anawaandikia? Katika karne ya kwanza, Wakristo wengi walikua wakipitia katika mateso mengi kwa sababu ya imani yao. Kijamii, Walinyimwa haki zao nyingi za msingi. Hakuwa na haki ya kumiliki ardhi, walifanya kazi kwa matajiri lakini hawakulipwa mishahara yao kwa wakati, hawakupata haki mahakamani, waliishi maisha ya shida, tabaka la chini lisilo na nguvu, walinyanyapaliwa na kutengwa na wale ambao hawakua wakristo. Kiimani walikuwa chini pia, wengi walianza kurejea kwenye dini zao za kipagani na kuwa baridi kiimani. Wakajiuliza maswali kwamba, Kwa nini Kristo anachelewa kurudi, kutuletea haki na kututoa katika mateso na changamoto hizi? Kwa nini anachelewa kujibu sala zetu? Je Mungu haoni mateso tunayopitia? Kwa nini Mungu anaruhusu watu wake wema na waaminifu wateseke ilihali wabaya na waovu wanastawi? Mtume Yakobo anawapa moyo, kwamba, walipaswa kuvumilia katika kumngoja Bwana, sio kwa kulala na kuwa baridi bali kwa imani na matumaini hai kama mkulima. Mkulima hupanda mbegu, huweka mbolea, huondoa magugu, hufuata ratiba za majira, kisha husubiri mavuno, akimwachia Mungu kazi yake. Kumbe anawaalika kuvumilia kwa saburi.

Liturujia ya Neno la Mungu inakita ujumbe wake katika furaha
Liturujia ya Neno la Mungu inakita ujumbe wake katika furaha   (@Vatican Media)

Katika kusubiri hawakupaswa kunung’unika wala kulaumiana, wasije wakahukumiwa siku ya Bwana. Anawatahadharisha ya kwamba, hukumu haipo mbali, Kristo yu tayari karibu. Anawasihi pia watazame maisha ya manabii waliopitia mateso kama wao na wakahesabiwa haki. Ndugu zangu katika masomo yetu yote katika dominika hii ya tatu ya Kipindi cha Majilio tunaalikwa kufurahi. Kwa nini tunaalikwa kufurahi? Je kati ulimwengu huu wenye kila aina ya chagamoto, kwa nini furaha? Kwanza: Bwana yu karibu, na atafanya kila kitu kuwa kipya. Katika somo la kwanza, Mwenyezi Mungu anasema na taifa lake kwa kinywa cha Nabii Isaya, waliokua utumwani, waliokuwa wamevunjika mioyo. Maisha yao yalikua kama jangwa lenye ukiwa, hawakuona matumaini yoyote mbele. Nabii anasema, jangwa litachanua maua kama waridi, vipofu wataona, walio dhaifu watatiwa nguvu, viziwi watasikia, vilema watatembea. Anasema waambieni, hao walio na moyo wa woga, moyo wa hofu, jipeni moyo, msiogope. Bwana anakuja, na atafanya yote kuwa mapya. Ndugu mpendwa, katika maisha yetu tunapitia katika nyakati kama hizi hizi ambazo walipitia taifa la Mungu. Kuna nyakati tunapitia katika majangwa. Jangwa la huzuni, jangwa la hofu, upweke, msongo wa mawazo, kukata tamaa, kukosa mwelekeo, kukosa amani katika familia, misiba, ukavu rohoni nk. Katika hali hii hatuoni mbele, tunaona kila kitu kimekauka, hakuna uhai tena, hakuna dalili ya matumaini ya mbele, hakuna furaha tena. Tunadiriki wakati mwingine kuhisi kama vile Mungu hayupo, au Mungu ametusahau, kama Mungu hatuoni, au ametuacha kabisa.

Kristo Yesu ni chemchemi ya imani na nuru ya Mataifa
Kristo Yesu ni chemchemi ya imani na nuru ya Mataifa   (@Vatican Media)

Ndugu mpendwa, Mungu anakupa matumaini mapya, anakupa Neno la Baraka. Anaipa nguvu miguu yetu iliyo dhaifu, anasema, ewe uliye na moyo wa hofu, jipe moyo, usiogope. Katika Majilio hii, na kwa namna ya pekee mwaka huu mpya, Mwenyezi Mungu akafanye kila kitu upya ndani mwako. Akachipushe upya jangwa la maisha yako. Ewe uliyetikiswa kwa magonjwa, uliyechoka kwa hali mbaya ya uchumi, uliye kwenye familia yenye mgogoro, iliyosambaratika, uliyelia kwa misiba, unayejiona usiye na bahati maishani, jipe moyo, usiogope. Hakuna lisilowezekana kwa Mungu. Mungu akaipe nguvu miguu yako, ukasimame na kutoa ushuhuda kwamba Mungu ana nguvu, Mungu aliye katikati yetu ni mkuu mwenye uweza wote. Pili: Tunafurahi kwa sababu Mungu hachelewi, anatenda kwa wakati wake. Katika somo la Pili, mtume Yakobo anaongea na Wakristo waliokuwa wakiteswa na kunyanyaswa sana kwa sababu ya imani yao. Katika hali hiyo, wakiwa na imani juu ya Ujio wa Pili wa Bwana, wanaona kama anachelewa. Lakini wanajiuliza maswali mengi, kwa nini mateso yanaendelea ilihali masiya alikuja kutuletea haki? Kwa nini hali yetu haibadiliki? Mungu atatujibu lini? Atakuja lini basi? Yakobo anawaambia, “Muwe na subira kama mkulima angojavyo matunda ya kazi ya mikono yake “mkulima akiisha kuotesha mbegu huondoka kwa matumaini kwamba, Mungu atatenda iliyobakia. Hafukui shimo na kutazama shina kila kukicha kuangalia kama imeota, bali anajua na kwa matumaini anaamini kwamba, Mungu kwa wakati wake ataikuza mbegu, na kwa muda wake atapata mavuno. Ndugu mpendwa, ukristo wetu ni tunda la imani iliyojengwa juu ya matumaini yetu kwa Kristo, matumaini ambayo hayatutahayarishi, hayatudanganyi. Dominika ya leo inatukumbusha kuwa, Mungu hafanyi haraka, lakini pia hachelewi. Mungu hatendi kwa mipango na ratiba zetu bali kwa wakati wake mkamilifu. Yamkini umesali, hujaona majibu, umeomba kwa nia zako mbalimbali, utembea na bahasha tangu januari mpaka disemba kutafuta ajira, uponyaji wa wa maradhi, amani, mafanikio, nafuu katika ugumu wa maisha, biashara, umeombea watoto, umeomba mwenza wa ndoa, lakini pengine majibu ya sala zako usiyaone kwa haraka. Mbegu haikuwi kwa usiku mmoja, mbegu lazima ifukiwe, lazima ife ndipo itoboe tena ardhi na kukua upya. Usife moyo uwapo ardhini, usife moyo mbegu ya hatima yako inapopaswa kuoza na kupasuka. "Trust the process, because God is in control."

Mwenyezi Mungu ni utimilifu wa nyakati
Mwenyezi Mungu ni utimilifu wa nyakati   (@Vatican Media)

Tatu: Tunafurahi kwa sababu Ufalme wa Mungu tayari upo katikati yetu. Katika somo la Injili Takatifu, Yohane Mbatizaji naye akiwa gerezani anatuma watu kumwuliza Yesu swali la msingi sana, kwamba, Je, ni wewe atakayekuja au tumsubirie mwingine? Jibu la Yesu ni fupi tu, nenda kamwambie Yohane, vipofu wanaona, viziwi wanasikia, maskini wanahubiriwa Habari Njema. Hizi ni alama za uwepo wa ufalme wa Mungu kati ya watu wake. Ufalme wa Mungu haonekani kwa maneno bali katika matendo. Ndugu mpendwa, katika dominika ya leo kila mmoja ajiulize swali hili la msingi kwamba je, ufalme wa Mungu unadhihirikaje katika maisha yangu ya kila siku? Ufalme wa Mungu haupo katika mambo makubwa, wala hautudai kufanya mambo makubwa sana. Yohane mbatizaji alitegemea kuona mambo makubwa kama uthibitisho wa uwepo wa Masiya kati ya watu wake. Mungu yupo kati yetu katika mambo ya kawaida kabisa. Tunaposamehe na kuachilia, tunaleta uponyaji rohoni, tunawafungulia na kuwaweka huru wale wote tuliowafungia katika gereza ndani ya mioyo yetu. Tunaponya majeraha tuliyosababishiwa na wengine au tuliyowasababishia wengine. Tunapokuwa wanyenyekevu, tunaponya upofu ndani mwetu, upofu unaotuzuia kuona na kukubali mema na mazuri ya wengine. Upofu unatuzuia kuona madhaifu yetu na kuwanyooshea tu wengine vidole, na kuwalaumu kila mara.  Tunapowasaidia maskini, tunawaimarisha na kuwatia nguvu. Tunapotafuta upatanisho ndani ya ndoa na familia zetu, tunaziponya familia zetu, tunaponya mahusiaono yetu. Tunapotenda haki, kusema ukweli, kukemea maovu, kutetea wanyonge, hizi ndizo ishara za uwepo wa ufalme wa Mungu kati yetu. Tunapowasaidia watu katika mahangaiko yao, kwa maneno yanayoponya, yanayotia faraja, hizi zote ni ishara za uwepo wa Kristo na ufalme wake katikati yetu. Ufalme wa Mungu unadhihirika kupitia matendo makuu ya Mungu kwa wengine. Kristo anasema tazameni Ishara. Tazama anayotenda kwa wengine. Ndugu mpendwa Mungu anatenda kazi ndani ya wengine ili kudhihirisha uwepo wake kati yetu. Matendo makuu ya Mungu kwa wengine yanatuinua na kuwa sababu ya furaha na matumaini yetu mapya.

Kristo Yesu ni chemchemi ya matumaini mapya
Kristo Yesu ni chemchemi ya matumaini mapya

Nne: Tunafurahi kwa sababu tunashiriki kazi ya Mungu. Kristo katika somo la Injli takatifu anamsifu Yohane Mbatizaji, kwa kuwa maisha na utume wake wote ulilenga katika kuiandaa njia kwa ajili ya Masiha. Mwaliko wake ulilenga katika kuwaandaa watu kumpokea yule aliyetabiriwa na Manabii. Ndugu mpendwa, sisi kila mmoja wetu ni mtangulizi wa Bwana. Kama nilivyoeleza hapo mwanzo, tunamtambulisha Kristo kwa njia ya maisha yetu. Mtume Yakobo amekwisha tufundisha kuvumilia katika saburi, kutolipiza kisasi, na kufurahi hata katika mateso, kwa kuwa mateso sio mwisho wa safari yetu, bali ni seheme ya safari ya ukombozi wetu. Ni ushiriki wa kazi ya ukombozi wetu na ukombozi wa wengine. Mtakatifu Agustino anatufundisha kuwa, Mungu aliyetuumba sisi bila sisi, hawezi kutukomboa sis bila sisi kutaka, kuwa tayari na kushiriki. Furaha yetu kumbe sio kwa sababu tunaondolewa mateso, bali kwa sababu ya uwepo wa Mungu hata katika mateso yetu. Kuna nyakati tunaweza kulalamika kwa Mungu pendine kuhusu hali zetu, au afya, au changamoto nyingine yoyote, ila tunapokutana na waliokua na changamoto kubwa kuliko sisi, na bado wana imani na matumaini, tunaona Mungu anayetenda kazi ndani ya wengine. Tunapofikiri kumkatia Mungu tamaa lakini tukaona wenye changamoto kuliko sisi bado wana tumaini, bado wana imani, tunapata nguvu ya kusonga mbele. Tunapopigwa na misukosuko lakini bado tukawaona wengine walio na misuko suko kuliko sisi watatupa uso wa tabasamu, tunauona mkono wa Mungu ukitenda kazi ndani yao. Shiriki kazi ya Mungu ya kufufua matumaini kwa waliokata tamaa, rejesha tabasamu kwa waliopoteza furaha, ponya mioyo iliyovunjika kwa maneno ya faraja na ya kutia moyo, tembelea wagonjwa, fariji wajane na yatima, saidia wenye njaa na fukara. Kwa njia hiyo tutaudhihirisha uso wa Baba mwenye huruma kwa wengine, kama alivyofanya Yohane Mbatizaji. Hitimisho: Katika Dominika ya leo, tumshukuru Mungu kwa zawadi ya Mwanaye Yesu Kristo Mkombozi wetu, tuombe neema ya kupokea furaha, faraja na matumaini mapya yaletwayo na Habari Njema ya Kristo atakayezaliwa kwetu na tuwe tayari kuwa chanzo na chemchemi ya faraha ya Injili ya Kristo kwa wengine.

13 Desemba 2025, 16:41