Tafuta

Ujumbe wa Papa Leo XIV unanogeshwa na kauli mbiu: “Kusikiliza na Kufunga. Kwaresima kipindi cha wongofu.” Ujumbe wa Papa Leo XIV unanogeshwa na kauli mbiu: “Kusikiliza na Kufunga. Kwaresima kipindi cha wongofu.”   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Jumatano Ya Majivu: Kusikiliza, Kufunga na Kutenda Mema Bila Kuchoka!

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV kwa Kwaresima ya mwaka huu 2026, una kichwa cha habari: “Kusikiliza na Kufunga. Kwaresima kipindi cha wongofu.” Baba Mtakatifu anasema kuwa kuongoka ni mchakato unaoanza kwa kukubali kufikiwa na Neno na kulipokea kwa moyo wa unyeyekevu na usikivu. Kukubali kusikiliza ni alama na hatua ya kwanza ya kuonyesha hamu ya kuingia katika mahusiano mema na mwingine: Sala, Neno la Mungu, Sakramenti na Matendo!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumatano ya majivu, siku ya kwanza ya kipidi cha Kwaresima mwaka A wa kiliturujia katika Kanisa, 2026. Ni Kwaresima ya kipekee, yenye neema na baraka za kijubilei ya miaka 2025 ya wokovu wetu, Mahujaji wa matumaini. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV kwa Kwaresima ya mwaka huu 2026, una kichwa cha habari: “Kusikiliza na Kufunga. Kwaresima kipindi cha wongofu.” Baba Mtakatifu anasema kuwa kuongoka ni mchakato unaoanza kwa kukubali kufikiwa na Neno na kulipokea kwa moyo wa unyeyekevu na usikivu. Kwani kukubali kusikiliza ni alama na hatua ya kwanza ya kuonyesha hamu ya kuingia katika mahusiano mema na mwingine. Hata Mungu alipomtokea Musa alijidhihirisha kuwa Yeye daima anasikiliza kilio cha wanaoteswa na kuthulumiwa (rej. Kut. 3:7). Baba Mtakatifu Leo XIV anasisitiza kuwa ili mfungo wetu uwe wa kweli na wenye manufaa ya kiroho lazima kufuata mashauri ya kiinjili, tukiongozwa na imani na unyenyekevu katika kulisikiliza na kulisoma Neno la Mungu. Kisha anatualika kuangalia namna yetu ya kuongea, kulinda ndimi zetu dhidi ya maneno mabaya na machafu yanayoweza kuumiza wengine, maneno yaliyo kama upanga, maneno ya kuhukumu, kusema vibaya wengine wasio na uwezo wa kujitetea. Namna yetu ya kuongea iwe ni ya staha katika kila nyanja ya maisha – katika familia, jumuiya, kazi na siasa, ili kuleta amani ya kweli na matumaini katika maisha.

JUmatano ya Majivu: Toba na Wongofu wa ndani
JUmatano ya Majivu: Toba na Wongofu wa ndani   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Nalo Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC katika ujumbe wake wa Kwaresima kwa Mwaka 2026, linatuasa likisema; “Ndugu, msichoke kutenda mema” (2The 3:13), ili watu wanapoona matendo yetu mema waweze kumtukuza Mungu Baba yetu aliye mbinguni (rej. Mt 5:16), aliye asili na chemchemi ya wema na utakatifu wote. Huu ni mwaliko wa kutenda mema bila kuchoka katika mazingira na hali yoyote ile, bila ubaguzi wowote ule, kuishi kadiri ya mapenzi ya Mungu. Ni mwaliko wa kuwa watu wema, watakatifu, kama alivyo Mungu aliyetuumba kwa sura na mfano wake (rej. Mwa 1:26-27). Hivyo hatupaswi kutendeana mabaya, kwa kuwa kule kuumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, sisi sote ni ndungu, kaka na dada wa Baba mmoja, Mungu wetu wa mbinguni (rej. KKK 361). Kwa msingi huu wa undugu, tunaalikwa tusichoke kutendeana mema, huku tukijiepusha na tabia na vitendo vyovyote vile vyenye kuumizana na kukatishana tamaa, kwa kutenda na kutendeana maovu, kwa kuwa hiyo ni kazi ya Shetani. Maaskofu Katoliki Tanzania wanasisitiza kuwa tukijikuta katika maelekeo binafsi ya kutenda uovu, kutenda mabaya, kutenda dhambi, au kuishi katika mazingira ya kutushawishi kutenda dhambi kama vile kuishi kati ya watu wenye midomo michafu, watu waovu na wabaya (rej. Is 6:5), au jamii iliyojaa uchafu wa lugha, isiyothamini utu wa wengine na maumbile yake, jamii isiyoheshimu amri za Mungu, sheria na miongozo yake mizuri, jamii ambayo dhambi, uovu na ubaya ndio ni mtindo wake wa maisha. Sisi tuchague kumpendeza Mungu na sio wanadamu, tudumu katika kutenda mema, kwa kuwa kutenda wema ni wito endelevu unaodai sadaka, ili kukuza upatikanaji na utoaji wa haki sawa kwa wote bila upendeleo wala ubaguzi.

Ndugu Msichoke Kutenda Mema
Ndugu Msichoke Kutenda Mema

Kipindi hiki cha Kwaresima kinatuongoza kuvipiga vita vizuri vya kiroho ili tujiweka sawa katika kuyatekeleza haya. Ndiyo maana Mama Kanisa katika sala ya mwanzo anatuombea akisali; “Ee Bwana, utujalie sisi waamini wako tuanze vita vya kiroho kwa mfungo mtakatifu. Nasi tulio tayari kupigana na pepo wabaya tujipatie nguvu kwa sababu ya kufunga”. Silaha za vita hivi ni kufunga na kusali kwa bidii, kulisoma na kulitafakari Neno la Mungu, na kusaidiana sisi kwa sisi kwa kutendeana matendo ya huruma tukiongozwa na amri kuu ya mapendo, kumwilisha ndani mwetu utamaduni wa upendo, kusameheana na kujipatanisha na ndugu, jamaa na marafiki, kufanya toba na kuzipatanisha nafsi zetu na Mungu Baba yetu mwema anayetupenda kwa upendo usio na kifani kama wimbo wa mwanzo unavyosema; “Ee Bwana, wewe wavipenda vitu vyote vilivyopo, wala hukichukii kitu chochote ulichokiumba. Unawasamehe watu dhambi zao kwa ajili ya kufanya kitubio, na kuwahurumia kwa kuwa ndiwe Bwana Mungu wetu” (Hek. 11:24-25, 27). Ni katika muktadha huu, Kwaresima inakuwa ni hija ya kiroho, kilele chake ni adhimisho la fumbo la ukombozi wetu - mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo – Pasaka.  Ndiyo maana Mama Kanisa katika sala ya kubariki majivu tunayopakwa kama alama na ishara ya kukubali kuwa tu wadhambi tunaohitaji kufanya toba anatuombea akisali hivi; “Ee Mungu, unayependezwa na unyenyekevu na kutulizwa na kitubio chetu, usikilize kwa wema sala zetu. Uwashushie kwa rehema baraka yako watumishi wako watakaopakwa majivu haya; ili baada ya kutimiza wajibu wa Kwaresima, waje waliadhimishe fumbo la Pasaka la Mwanao, wakiwa wametakata rohoni”. Na katika sala ya kuombea dhabihu anasali; “Ee Bwana, tunatoa sadaka hii ya kuanzia Kwaresima, na kukuomba tuzishinde tamaa mbaya kwa matendo ya kitubio na mapendo. Nasi tukisha takaswa dhambi, tuwe na ibada ya kuadhimisha mateso yake Mwanao.”

Msichoke kutendeana mema katika maisha
Msichoke kutendeana mema katika maisha   (AFP or licensors)

Somo la kwanza ni la kitabu cha Nabii Yoeli (2:12-18). Ujumbe wake ni mwaliko wa Mungu akituita sisi wanae tumrudie Yeye kwa mioyo yetu yote, kwa kufunga na kwa kulia na kwa kuomboleza, tukiirarua mioyo yetu, na siyo mavazi, ishara ya toba ya kweli, toba ya mtu mmoja mmoja, toba ya pamoja kama jumuiya ya waamini, toba ya watu wote; wazee, vijana na watoto, na toba ya taifa zima, ili haki itawale, kurudisha amani na matumaini kwa wote. Somo la pili ni la Waraka wa pili wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (2Kor 5:20-6:2). Ujumbe wake ni kuwa tukubali kupatanishwa na Mungu kwa njia ya Kristo Mwanae wa pekee ambaye Mungu mwenyewe alimtuma aje kutukomboa kutoka utumwa wa dhambi. Kwa maana Mungu asiyejua dhambi alimfanya Mwanae Yesu Kristo kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki yake katika Yeye. Hili linawezekana tukijivika moyo wa toba kwa unyenyekevu, kujikabidhi kwake na kuitumainia huruma yake kuu. Injili ni ilivyoandikwa na Mathayo (Mt 6:1-6;16-18). Ujumbe wake umejikita katika namna sisi tunavyopaswa kukiishi kipindi hiki cha Kwaresima: Tusiwe wanafiki, tusifunge, tusisali wala tusifanye matendo mema ili tuonekane machoni pa watu. Kwani kwa kufanya hivyo tutakuwa tumepokea thawabu yetu kwa njia ya watu wanaotutazama, kutustaajabia, na kutusifia. Kufunga kwetu, kusali kwetu na matendo yetu ya huruma kwa wengine, yawe ni mawasiliano binafsi kati yetu na Mungu, yakilenga kujenga muungano na Mungu wetu aliyemtakatifu, ili Yeye atukuzwe, nasi tuweze kutakatifuzwa na kuwa watakatifu.

Msichoke kutendeana mema, maisha ya hapa duniani ni mafupi!
Msichoke kutendeana mema, maisha ya hapa duniani ni mafupi!

Ni katika muktadha huu siku ya kwanza ya Kwaresima inapambwa na tendo la kiroho la kupakwa majivu katika paji la uso, ishara ya kukubali kuwa tu wa dhambi, tunahitaji kufanya toba ili tusamehewe. “Tukisema kwamba hatuna dhambi twajidanganya wenyewe na wala kweli haimo ndani mwetu. Lakini tukiziungama dhambi zetu, Mungu ni mwaminifu, tena mwadilifu na wa haki, hata atatusamehe na kututakasa na kutusafisha na udhalimu wote” (1Yn 1:8-10). Majivu yanatukumbusha kuwa sisi ni viumbe duni na dhaifu na kwamba maisha yetu hapa duniani ni mafupi, yanapita mbio, kuelekea mbinguni, aliko Mungu Baba yetu. Tahadhani. Kuna uwezekano wa kufikiri na kudhani kuwa hakuna jipya katika kipindi cha kwaresima cha mwaka huu na cha mwaka uliopita. Tukumbuke kuwa kila adhimisho la kiliturujia katika historia ya wokovu wetu katika mzunguko wa mwaka wa kiliturujia katika Kanisa, lina hali mbili. Kwanza ni kutukumbusha mambo ya kihistoria ya fumbo la ukombozi wetu. Na pili ni kuhuisha na kupyaisha maisha yetu ya kiroho kwa kuwa yanafanya sehemu ya maisha yetu na kutuonjesha upendo wa Mungu. Hivyo kila kipindi cha mwaka wa kiliturujia ni kipya na cha pekee, hakifanani na kingine. Maana kila kipindi kinapyaisha na kuhuisha maisha yetu ya kiroho na hivyo kutuleta karibu zaidi kwa Mungu. Basi kwa unyenyekevu, tufungue mioyo yetu tuweze kujichotea neema na baraka zitokanazo na kipindi hiki kitakatifu, kwa kuachana na maisha ya kale – maisha ya dhambi na kuanza maisha mapya ya kiroho kwa kusali kwa bidii, kufanya toba na malipizi, kujikatalia furaha za kimwili, kuwasaidia na kuwatendea kwa ukarimu na upendo wengine. Nawasihi tukiingie kipindi hiki kama vile ni cha kwanza na cha mwisho. Tuitumie vyema Kwaresima hii kana kwamba hakuna nyingine. Kwa hakika, hakuna mwenye uhakika wa kuiona Kwaresima nyingine. Kumbe wakati uliokubalika ndio huu, siku ya wokovu ndiyo sasa. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala baada ya Komunyo anasali hivi akituombea; “Ee Bwana, Sakramenti tulizopokea zituletee shime yako, ili kufunga kwetu kukupendeze, kutupatie nasi dawa ya kutuponya”. Nawatakieni mwanzo mwema wa kipindi cha Kwaresima. Tumsifu Yesu Kristo!

Jumatano Majivu
17 Februari 2026, 15:58