Tafuta

2026.02.20 Marais wa Mabaraza ya Maaskofu wa Marekani, Canada,Amerika Kusini na Visiwa vya Carribiea 2026.02.20 Marais wa Mabaraza ya Maaskofu wa Marekani, Canada,Amerika Kusini na Visiwa vya Carribiea  

Maaskofu wa Amerika:"Hakuna mhamiaji mgeni katika Kanisa"

Februari 19,ulihimitishwa Mkutano wa kila baada ya miaka miwili wa Maaskofu wa bara lote la Amerika huko Tampa,Florida,kwa wito wa kuendeleza majibu ya pamoja kwa changamoto zinazokabili bara hilo.Na walitoa wito wa kuwatambua wale wanaoacha nyumba zao wakitafuta usalama kuwa ni kama "uso wa Kristo unaosonga mbele."

Vatican News

"Hakuna mhamiaji mgeni katika Kanisa," hii ni imani thabiti ya Marais na wawakilishi wa Mabaraza ya Maaskofu wa Amerika, waliokutana katika siku za hivi karibuni, hadi, Alhamisi, tarehe 19 Februari 2026, huko Tampa, Florida (Marekani), kuimarisha ushirika wa kikanisa na kupanga majibu ya pamoja kwa changamoto zinazokabili bara hilo. "Katika kila mtu anayeondoka nchini mwake kutafuta usalama, fursa, au heshima, tunamtambua kaka, dada; tunatambua uso wa Kristo katika safari" inasomeka taarifa ya pamoja

Mkutano huo ulihudhuriwa na Marais wa Mabaraza ya Maaskofu Wakatoliki wa Marekani (USCCB), Mabaraza ya  Maaskofu Katoliki wa Canada (CCCB), na Mabaraza ya Maaskofu wa Amerika Kusini na Caribbean (CELAM), wakiendeleza utamaduni wa mazungumzo ya kiaskofu yaliyoanza mwaka 1959 na sasa yanaelekea kwenye upeo wa kisinodi. Askofu Mkuu wa Porto Alegre, Rais wa Baraza la Maaskofu wa Brazil,  na wa CELAM, Kardinali Jaime Spengler, alisisitiza thamani ya kikanisa ya nafasi ya pamoja: "Sisi katika CELAM, pamoja na Urais wa Mabaraza ya  Maaskofu Wakatoliki wa Marekani na Canada, tumekusanyika hapa ili kufahamiana vyema, kusali pamoja, na kutafakari masuala yanayoathiri uhalisia wa Makanisa yetu."

Uhamiaji na Sinodi

Miongoni mwa mambo yaliyozungumziwa wakati wa mkutano huo ni mada ya uhamiaji, inayochukuliwa na maaskofu kuwa "muhimu kwetu sote," pamoja na mada ya sinodi, "safari iliyoanzishwa na Papa Francisko na ambayo lazima tufanye maendeleo, baada ya muda na katika hali halisi za kanisa za ndani." Kisha ikaja mada ya mgawanyiko, ambayo "ni kitu kinachotugawanya, na tumeitwa kujenga ushirika, na  umoja." Wakati wa hotuba yake, Askofu Pierre Goudreault, Askofu wa Sainte-Anne-de-la-Pocatière na Rais wa Baraza la Maaskofu Canada(CCCB), alirejea asili ya sinodi ya mkutano wa bara, akielezea kwamba tukio hilo lilitoa "wakati muhimu kwetu sisi maaskofu." Miongoni mwa mada zilizojadiliwa, alitaja "uhamiaji na changamoto zake, mgawanyiko, na mchakato wa kutekeleza sinodi katika Makanisa yetu ya mahali."

Rais wa USCCB:Mkutano ni uzoefu wa kipekee  katika huduma yetu

Kwa upande wake, Askofu Mkuu Paul Stagg Coakley wa  Jiji la Oklahoma na rais wa USCCB, alisifu mkutano huo kama uzoefu wa kipekee katika huduma yake: "Ni wakati mzuri wa kuwajua ndugu zangu maaskofu kutoka kila pembe ya Amerika. Kwa sababu hii, ninashukuru kwa fursa ya kuungana, kujifunza kutoka kwa kila mmoja, kusikilizana, na kusaidiana." Katika taarifa zao za pamoja, walionesha hamu yao ya kujibu kwa kina zaidi mateso ya watu wa Mungu, hasa katika kukabiliana na unyanyapaa wa wahamiaji, umaskini unaozidi kuwa mbaya, mvutano wa kisiasa, na ukosefu wa usalama wa kijamii. Kutokana na mkutano huo, maaskofu walionesha azimio lao la kuimarisha ushirikiano wa kichungaji wa sinodi kote barani na wakathibitisha tena kwamba "uhamaji wa binadamu hauwezi kupunguzwa kuwa suala la kisiasa au kiuchumi tu; ni ukweli wa kibinadamu unaotilia changamoto dhamiri yetu ya Kikristo na wajibu wa kimaadili wa mataifa."

MAASKOFU WA AMERIKA

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku. Just click here

21 Februari 2026, 10:43