Tafuta

Mchoro wa picha inayoonesha wakati wa kifo cha Mtakatifu Francis wa Assisi Mchoro wa picha inayoonesha wakati wa kifo cha Mtakatifu Francis wa Assisi 

Masalia ya Mtakatifu Francis kuwekwa wazi kwa ajili ya Heshima huko Assisi

Padre Giulio Cesareo,Mkurugenzi wa Ofisi ya Mawasiliano wa Konventi Takatifu ya Assisi, alizungumza na Vatican News,na kueleza umuhimu wa kuweka wazi masalia ya Mtakatifu Francis wa Assisi na ujumbe unaoenezwa hadi leo hii kwa ulimwengu.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Kuanzia Dominika tarehe 22 Februari hadi 22 Marchi 2026, katika Kanisa la chini,  ndani ya Basilika ya Mtakatifu Francis wa Assisi, Mahujaji wataruhusiwa kwa mara ya kwanza kusali mbele ya masalia  ya Mtakatifu huyo, kwa ajili ya  kuadhimisha miaka 800 tangu kifo chake mwaka huu 2026.

Katika nyakati zinazogubikwa na hali ya kutokuwa na uhakika, mvutano wa kijamii na utafutaji wa maana halisi ya maisha, kuonyeshwa kwa masalia ya Mtakatifu Francis ni tukio linalozidi ibada ya kawaida. Kwa wakatoliki, ni wito wenye nguvu wa kiroho, na kwa waamini ni fursa ya kukutana kwa namna ya pekee wa halisi na kumbukizi hai ya mmoja wa watakatifu wanaopendwa na kuheshimiwa zaidi ulimwenguni.

La cappella delle reliquie di san Francesco ad Assisi

Kikanisa chenye baadhi ya masalia aliyotumia Mtakatifu Francis wa Assisi

Katika mji wa Assisi, kuonyeshwa tena kwa masalia haya, kunauhuisha tena uhusiano wa kina kati ya historia, imani na jamii na kuendeleza upya ujumbe wa Mtakatifu Francis wa amani, udugu, unyenyekevu ambao unaendelea kuzungumza na ulimwengu wa leo. Kwa heshima ya Mtakatifu huyo, inakadiriwa kuwa kati ya watu 15,000 hadi 18,000, wanatarajiwa kufika kila siku kuona na kusali mbele ya masalia hayo, hivyo, takribani wageni 370,000 watafika Assisi. Katika Mahojiano na Vatican News, Padre Giulio Cesareo Mkurugenzi wa Ofisi ya Mawasiliano wa Konventi Takatifu ya  Assisi alifafanua kwa kina juu ya maana ya tendo hili la kale kwa jamii ya leo.

Kuna maana gani ya kiroho na kichungaji katika kuweka wazi masalia ya Mtakatifu Francis kwa Kanisa Katoliki leo hii?

Wakristo daima wamekuwa wakiheshimu masalia ya Watakatifu, hasa wafiadini, wale waliothibitisha kwa njia ya maisha yao kuwa upendo wa Mungu uliowakumbatia kikamilifu, na upendo wa Mungu siyo jambo la nadharia, kwani unahusisha mwili. Watakatifu hawa waliwahudumia maskini, walisali, walifunga, waliwapenda wengine na waliruhusu wao wenyewe kumilikiwa na Upendo wa Kristo. Wakristo daima wamekuwa wakiheshimu maisha ya watakatifu kwani ndani yao wanaona tendo la Roho Mtakatifu likijaza miili yao upendo huu. Huu ndio muktadha wa kuheshimu masalia ya Mtakatifu Francis. Tumechagua Injili ya Yohane 12:24, kama ufunuo wa tafsiri hii. Ndani yake Yesu, akizungumza juu yake mwenyewe, anasema kwamba “mbegu ya ngano isipoanguka ardhini na kufa, hubaki peke yake, lakini ikifa, huzaa matunda mengi.” Mtakatifu Francis kweli ni mbegu hii ambaye kwa namna ya Yesu, kwa njia ya Watakatifu, mashahidi na ya watu wote wenye mapenzi mema, hujitoa katika maisha ya kila siku. Anayejitoa humegwa na kuisha, na hakuna namna nyingine lakini baadaye huzaa matunda.

Kuoneshwa kwa masalia, kunaimarishaje maisha ya jumuiya na ushirika miongoni mwa waamini, katika eneo la Assisi na Ulimwenguni kote?

Tendo hili huimarisha Imani. Imani yetu siyo wazo lililokuwepo kabla, bali ni uhusiano na Bwana ambaye ni upendo. Kuwa na Imani hakutenganishwi na uzoefu wa kuwa wamoja, tukiunganishwa katika upendo. Kwa mantiki hii kuheshimu masalia ya Mtakatifu Fransisko kunamaanisha kutiwa nguvu. Kuna maana ya kupokea neema ya kuthibitishwa tena katika hakika hii: kwamba anayependa, huku akijitoa na kuishi, kiukweli anaishi vifungo vya umoja vya Kanisa, vya upendo wa huruma. Kadiri tunavyoishi katika upendo na kujitoa, ndivyo ubinadamu wetu unavyokuwa kiini cha utu wetu. Kile kinachotuunganisha na wengine si mawazo, bali ni upendo tunaotoa katika mahusiano yetu. Kwa kumheshimu Mtakatifu Francis kunadhihirisha jinsi upendo wa kweli unavyozaa matunda kwa vizazi vyote, kiasi kwamba hata baada ya miaka 800 ya kifo chake, bado anakumbukwa.

Tukio hili lina matokeo gani kwa watu wa Assisi na Mahujaji wataokafika kwenye Basilika hapo Assisi?

Kwa hakika kwa mwezi huu, Assisi na maeneo jirani wataishi kwa tukio hili. Malazi yamejaa kwa miezi kadhaa, hoteli na nyumba za wageni tayari zimejaa.Tunaamini huu utakuwa wakati wa neema, kwa kuwa jamii inayotuzunguka daima hutuambia kwamba: “Jifikirie mwenyewe. Usijitoe. Usijali wengine. Jifikirie na kujijali wewe kwanza.” Wakati huu, Mtakatifu Francis  anasema kinyume kabisa, na mifupa yake inashuhudia hilo. Hii ni mifupa ya mtu aliyejitoa, aliyeishi nguvu zake kwa kutembea, kupiga magoti na kuishi mapangoni. Anatuambia moyoni mwetu: “Usiogope kujitoa, kwa sababu kwa kufanya hivyo unazaa matunda.” Nafikiri hili ni jambo zuri na lenye manufaa makubwa kwa watu wote.

Kwa nini mwili wa Mtakatifu Francis unaendelea kuzungumza na vijana na hata wasioamini kupitia ishara wazi kwa njia ya masalia yake?

Naamini ni Mtakatifu Francis mwenyewe anayezungumza. Masalia ni sehemu ya mwili wake halisi. Ni kama unavyoweza kunisikia mimi ninazungumza hivyo, nina mwili, kama nisingekuwa na mwili, nisingekuwa na sauti. Katika miili yetu ndipo mahusiano huanzia. Vivyo hivyo, masalia ya Mtakatifu Francis ni kama ganda la mbegu ya Mtakatifu Francis iliyochipuka, na ganda hili linatuambia habari zake. Kwa nini watu wanamtafuta? Naamini wanamtafuta kwa sababu yeye ni Injili iliyo hai. Ndani yake tunaona kuwa Injili inavyokubaliwa, ni  habari njema kwa ulimwengu, kwa mtu binafsi na kwa jamii. Hiki ndicho kinachowavutia watu kuja kuhiji. Tangu awali, Francis aliitwa alter Christus,  siyo kwa maana ya Kristo mwingine, bali kama mfano wa Kristo, sura inayofanana na Kristo.

Je, kuonyeshwa huku ni tukio la Ibada muhimu kwa watu, au ni tendo la kikanisa lenye maana kubwa katika Taalimungu na kiutamaduni?

Tumetoa ufafanuzi wa kutosha kupitia Ukura wetu wa Mtandao(website) na kwenye mitandao yetu ya kijamii kama vile  Facebook na Instagram. Tunatamani kuhamasisha Ibada, upendo wetu kupitia uzoefu wa kikanisa uliowekwa juu ya msingi wa taalimungu, lakini si lazima uwe mgumu. Taalimungu haikuzaliwa kuwa ngumu, bali ilizaliwa kueleza kwa maneno maisha yanayoishi ndani mwetu. Kwa maana hii, tunaona katika Mtakatifu Francis,  ganda la mbegu inayochipuka katika upendo na huruma ikivuka muda na nafasi. Huu ni mwaliko kwetu sote kuishi maisha ya kila siku kwa upendo. Huo ndio mwaliko anaotupatia Mtakatifu Francis leo hii.

Katika nyakati zinazogubikwa na migogoro ya kijamii na mivutano, ni ujumbe gani ambao Mtakatifu Francis anaweza kuutoa kwa waamini ulimwenguni kote?

Mtakatifu Francis hakuishi nyakati bora zaidi ya nyakati zetu. Kulikuwa na vita vya kidini, migogoro ya ndani, mabishano makubwa, uhasama ndani ya familia na kukosekana haki. Hakuishi katika nyakati bora za kihistoria. Lakini bado ujumbe wake ni mzuri: kama kweli mtu atakumbatia Injili, anatengeneza historia tofauti katika maisha yake, na kuunda mahusiano mapya. Wakati mwingine tunaweza kusikia sauti ikituambia “huwezi kufanya kitu, upo peke yako, huna maana, wenye nguvu wanatawala. Hatuwezi kufanya chochote.” Lakini Mtakatifu Francis anashuhudia kwetu kuwa sauti hizo ni uongo, kwa sababu  mtu mmoja aliyekumbatia Injili huenda asiweze kuubadili ulimwengu mzima, lakini anaweza kubadili mambo yanayomzunguka. Kwa miaka hii 800 ya Mtakatifu Francis ameendelea kugusa mioyo ya watu. Naamini ujumbe mzuri ni huu kwamba: “hatuwezi kutatua kila tatizo, lakini kila mmoja akichukua hatua, hatua hiyo huacha alama na matokeo chanya. Na siyo sahihi kusema kwamba hatuwezi kufanya chochote.”

Masalia ya Mtakatifu Francis

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku. Just click here

18 Februari 2026, 13:30