Tafuta

Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya Kwanza ya Kipindi cha Kwaresima: Mwaliko kwa waamini wawe ni watii kwa sauti ya Mungu na wasikivu kwa Neno la Mungu, dira na mwongozo wa maisha. Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya Kwanza ya Kipindi cha Kwaresima: Mwaliko kwa waamini wawe ni watii kwa sauti ya Mungu na wasikivu kwa Neno la Mungu, dira na mwongozo wa maisha.  (@Vatican Media)

Tafakari Dominika ya Kwanza Kwaresima Mwaka A: Watii Kwa Sauti Ya Mungu; Wasikivu Wa Neno!

Jangwa ni mahali ambapo Mwenyezi Mungu anazungumza kutoka katika undani wa mtu mwenyewe, yaani dhamiri nyofu. Hii ni chemchemi ya majibu ya Mungu katika sala. Ni mahali pa majaribu na kishwawishi kikubwa! Kumbe, jangwa, katika Biblia, ni mahala ambapo mtu anajitambua kuwa “ni nani” mbele ya watu na mbele ya Mungu. Kwaresima ni muda uliokubalika wa kuingia katika jangwa la maisha ya kiroho, yaani upweke, ili kusikiliza kile kinachotoka moyoni!

Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.

Utangulizi: Wapendwa Taifa la Mungu, leo ni Dominika ya 1 ya Kwaresima Mwaka A wa Kanisa. Tumeanza rasmi kipindi cha Kwaresima. Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka huu 2026 kinanogeshwa na ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV kwa kauli mbiu: “Kusikiliza na kufunga: Kwaresima kama Kipindi cha Wongofu wa ndani.” Kwaresima ni kipindi ambacho Kanisa kama Mama na Mwalimu, anawaalika watoto wake kutoa kipaumbele cha pekee kwa Fumbo la Mungu katikati ya maisha yao, ili imani ipate tena nguvu na mioyo ya waamini isipotee katikati ya mahangaiko na bughudha za maisha ya kila siku. Kila safari ya wongofu wa ndani huanza pale waamini wanaporuhusu Neno la Mungu liwafikie na kulikaribisha kwa moyo wa unyenyekevu. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, kuna uhusiano kati ya karama ya Neno la Mungu, Nafasi ya Ukarimu na mabadiliko ambayo Neno hili linaleta. Kwa sababu hiyo, safari ya Kwaresima inakuwa ni fursa muafaka ya kusikiliza sauti ya Mungu na hivyo kupyaisha tena maamuzi ya kumfuasa Kristo Yesu, kwa kutembea katika njia ile iendayo Yerusalemu ambako Fumbo la Pasaka yaani: Mateso, kifo na ufufuko vinapata utimilifu wake. Jangwa ni mahali ambapo Mwenyezi Mungu anazungumza kutoka katika undani wa mtu mwenyewe, yaani dhamiri nyofu. Hii ni chemchemi ya majibu ya Mungu katika sala. Ni mahali pa majaribu na kishwawishi kikubwa! Kumbe, jangwa, katika Biblia, ni mahala ambapo mtu anajitambua kuwa “ni nani” mbele ya watu na mbele ya Mungu. Kwaresima ni muda uliokubalika wa kuingia katika jangwa la maisha ya kiroho, yaani upweke, ili kusikiliza kile kinachotoka moyoni, ili hatimaye kukutana na ukweli wa maisha.

Jangwa ni mahali pa mapambano ya maisha ya kiroho
Jangwa ni mahali pa mapambano ya maisha ya kiroho

Katika kipindi hiki tunaalikwa kuhuisha maisha yetu ya kiroho ili tuweze kuadhimisha Fumbo Takatifu la Pasaka pamoja na Bwana wetu Yesu Kristo Mfufuka, aliyeshinda dhambi na mauti kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake. Liturjia ya Neno la Mungu inatutafakarisha kwamba, “Utii kwa Neno la Mungu unatusaidia kushinda vishawishi na dhambi” Katika safari yetu ya maisha, hapa duniani tunajaribiwa kwa namna nyingi. Peke yetu hatuwezi kushinda majaribu na vishawishi, tunahitaji neema na msaada wa Mungu.  Katika Dominika hii tuombe neema ya kuwa watii wa Neno la Mungu ili tuweze kushinda vishawishi na dhambi. Somo la 1: Ni kutoka katika Kitabu cha Mwanzo 2:7-9, 3:1-7. Somo la kwanza ni kutoka katika kitabu cha Mwanzo. Somo hili latupatia simulizi namna dhambi ilivyoingia katika historia ya mwanadamu. Mara kadhaa tumekua tukijiuliza swali hili, “Kama Mwenyezi Mungu baada ya kuumba (Mwa 1:31) na akaona kila kitu alichokifanya kuwa ni chema sana, je dhambi, uovu, mateso, maumivu, uadui na kifo vilitoka wapi?” Fundisho la kwanza: Kwa nini dhambi iliingia katika historia ya mwanadamu? Mwenyezi Mungu alimwumba mtu mzima, mwili na roho akampa maisha ya heri na amani bila kufa ndani ya Bustani ya Edeni (2:7-8). Sehemu ya kwanza ya somo la kwanza yaani 2:7-9 ni simulizi la pili la uumbaji ambalo linaanzia kimsingi ile sura hii ya 2:4-25. “Edeni” maana yake ni mahali pa furaha, Edeni ni bustani ya paradiso iliyopandwa na Mungu, ambamo Adamu na Hawa waliishi kama viumbe wa kwanza, ikiwakilisha mahali pa amani kamilifu, ulinzi, na uasilia usiolimwa na binadamu. Katika Bustani hii hawakupungukiwa kitu kama tunavyoelezwa katika somo hili, kwa kuwa, “Mungu alichipusha katika ardhi kila mti unaotamanika kwa macho na kufaa kwa kuliwa” (2:9). Kumbe Mungu hakutuumba ili tuteseke, hakutuumba ili tuumie, hakutuumba ili tufe bali tuishi naye milele yote katika enzi na utukufu.

Kwaresima ni muda muafaka wa sala, toba na wongofu wa ndani
Kwaresima ni muda muafaka wa sala, toba na wongofu wa ndani   (@Vatican Media)

Mwanadamu amepewa uhuru wa kuchagua. Pamoja na miti mingine iiyokuwemo ndani ya Bustani, Mwenyezi Mungu alichipusha pia mti wa uzima katikati ya Bustani, na mti wa ujuzi wa mema na mabaya (aya ya 9). Miti hiyo, ikiwa imewekwa katikati, inawakilisha uwezo wa mwanadamu wa kuchagua. Uwepo wake unaonyesha kuwa Mungu hakumuumba mwanadamu kama roboti, bali kiumbe mwenye uwezo wa kufanya maamuzi ya kufuata njia ya uzima (kumtii Mungu) au njia ya mauti (kujitegemea). Tukumbuke baada ya hapo Mwenyezi Mungu alimpa Adamu Amri moja, kwamba, “Matunda ya kila mti wa Bustani waweza kula, walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo, hakika utakufa (Mwa 2:17). Kumbe ulikua ni uhuru wenye ukomo. Hii inatupeleka kwenye sehemu ya pili ya somo hili yaani 3:1-7 inayotupa jibu la swali letu sasa, kwa nini dhambi, kwa nini maumivu, kwa nini kifo? Mwanadamu aliyeumbwa kwa uhuru kamili, aliamua kutokumtii Mungu. Ni kama mtoto aambiwaye na Baba yake, “Usishike moto utakuunguza mwanangu” lakini yeye kwa uhuru wake ananyoosha mkono na kushika moto. Kumbe moto sio mbaya bali maamuzi ya mtoto kutokutii sauti ya Babaye ndipo ubaya unapoanzia. Eva anaruhusu mazungumzo na nyoka, nyoka anayewakilisha hapa kishawishi (temptation) kinachotupeleka kwenye dhambi na udanganyifu wa kututoa katika utii kwa Mungu, na kutafuta uhuru kamili bila Mungu. Matokeo yake wanapoteza neema ya utakaso, yaani uzima wa kimungu ndani mwao. Wanafukuzwa katika Bustani ya Edeni ambapo Mungu aliwaandalia waishi humo katika utulivu na amani. Chuki, dhambi (ambayo na sisi sote tumeirithi), mateso, mahangaiko, maumivu na kifo vinaingia katika historia ya Mwanadamu. Licha ya hayo, Mungu hamwachi mwanadamu apotee katika dhambi. Mpango wa ukombozi wa mwanadamu unaanza na utakamilishwa kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo, Adamu mpya aliyekuwa mtii kwa Imani katika kutimiza mapenzi ya Mungu.

Maisha ya sala ni muhimu sana
Maisha ya sala ni muhimu sana   (@Vatican Media)

Fundisho la pili: Kwa nini nasi wanadamu tunaanguka kila mara katika dhambi? Somo letu la kwanza limetueleza sababu kuu mbili ambazo zilipelekea Adamu na Eva kuanguka katika dhambi ambazo kwa ufupi twaweza kuzitaja kuwa ni, kwanza, kutokuridhika na wema na uzuri wa Mungu (hawakutosheka na Maisha ndani ya Bustani ya Edeni), pili ni kutumia vibaya uhuru waliopewa na Mungu kwa kuruhusu majivuno na mazungumzo na Shetani. Mambo haya yanatuhusu sisi pia kama ifuatavyo. Kwanza: Kushindwa kuona, kukiri na kuridhika na uzuri wa Mungu ndani mwetu. Mwenyezi Mungu ametuumba kwa sura na mfano wake ili tumjue, tumpende, tumtumikie na mwisho turejee tena kwake mbinguni. Ametukomboa kwa gharama kubwa ya mateso kifo na ufufuko wa Mwanaye ili aturejeshe nyumbani kwetu pa awali katika Bustani ya Edeni, Paradiso yaani mbinguni. Mungu atupe nini tena sisi watoto wake? Ametupa kila kitu tunachohitaji ili tuishi maisha ya furaha, amani, na utulivu wa moyo ndani ya uwepo wake. Ametupa Kanisa, ametupa Sakramenti mbalimbali, ametupa Neno lake Takatifu na yeye Mwenyewe amejitoa kama chakula, Ekaristi Takatifu kwa ajili ya uzima wetu. Tunahitaji nini zaidi sisi kutoka kwa Mungu?  Mungu atupe nini zaidi ili tutambue kuwa anatupenda upeo? Mara nyingi tunaposhindwa kutambua thamani hii kubwa ya ukombozi wetu, tunaposhindwa kushikamana na Mungu na kuitunza na kuithamini ile sura na mfano wake ndani mwetu ndio mwanzo wa kuwa na majivuno na kuanguka katika dhambi.

Neno la Mungu ni dira na mwongozo wa maisha
Neno la Mungu ni dira na mwongozo wa maisha   (@VATICAN MEDIA)

Pili: Kutumia vibaya uhuru wetu kwa kuruhusu mazungumzo na nyoka kila mara, yaani kuruhusu nafasi ya vishawishi. Eva aliruhusu mazungumzo na nyoka. Nyoka hapa kama nilivyosema hatajwi kuwa ni shetani bali anasimama kama ishara ya vishawishi na udanganyifu ambayo vinatutoa katika utii na Imani kwa Mungu, yaweza kuwa watu na zaweza kuwa hali na mazingira mbalimbali pia. Maandiko matakatifu baadaye yanamtaja huyu nyoka kama ibilisi (rejea Ufunuo 12:9). Somo hili latuambia kuwa nyoka alikuwa mwerevu kuliko Wanyama wote wa mwitu aliowafanya bwana Mungu. Sote twafahamu sifa za nyoka. Nyoka huwa anakuja kwa ukimya, si rahisi sana kumwona na kumtambua, hapigi kelele, lakini sumu yake na madhara yake ni makubwa. Ndugu mpendwa ndivyo vilivyo vishawishi katika maisha yetu ya kila siku. Nyoka yupo katikati yetu katika namna mbalimbali na hizi ndizo kazi za shetani. Mabadiliko mbalimbali tunayoyashuhudia katika dunia yetu ya sasa, katika jamii yetu, katika familia zetu, katika mifumo ya elimu katika shule zetu, katika kanisa ni matokeo ya nyoka anayesambaza sumu ya kufisha taratibu, kimya kimya nyuma ya pazia, sisi tunashuhudia tu matokeo yake. Tufungue Macho na kuchukua daima hatua. Tusipokuwa na jicho la kutazama na weledi wa kutambua hila na mitego ya nyoka tutashuhudia uharibifu mwingi katikati yetu. Wakati mwingine tunaweza kuwa na uwezo wa kutazama na kutambua hila na mitego hii ya adui mwovu lakini tukafumba macho na kukaa kimya, tukasema haituhusu. Tunaweza kuona uovu ukiendelea katika jamii yetu, lakini kwa sababu ya kulinda maslahi yetu tukaendeleza mazungumzo na nyoka kushuhudia akiendelea kuleta uhairibifu katikati yetu. Hakuna atakayebaki salama. Madhara ya dhambi si ya mtu binafsi bali yanaathiri jamii nzima, yanaangamizia familia nzima, yanaangamiza taifa zima.

Kkwaresima ni safari ya maisha ya kiroho
Kkwaresima ni safari ya maisha ya kiroho

Kipindi cha Kwaresima hii tunataka kuweka nia ya dhati ya kushikamana daima na Mungu, kuepuka mazingira, watu na vitu vinavyoweza kutupeleka dhambini tena na tena. Tuseme hapana mapema, kabla hatujachelewa na kugundua kuwa tu uchi tayari. Katika malezi ya watoto wetu, tutambue mapema tabia na mienendo isiyofaa na kukemea. Katika kanisa, tusimame imara kutengeneza jamii inayotambua na kutofautisha mema na mabaya. Tujenge Jamii inayoendenenda katika misingi ya uadilifu na ukweli. Tunaishi katika ulimwengu uliopotoka katika nyanja mbalimbali na bado unaendelea kupotoka zaidi. Tulinde familia zetu, tulinde watoto na vijana wetu, tulindane sote dhidi ya uharibifu wa maadili, uregevu wa imani na uadilifu wa kweli. Tuchukue hatua za haraka na za lazima kabla hatujagundua kuwa tu uchi, kabla hatujachelewa. Ibilisi yupo kazini, tuseme pamoja na Kristo kwamba tunataka na tunatamani kila wakati kuyatenda daima mapenzi ya Mungu kama tunavyomwona yeye katika somo la Injili Takatifu.

Kwaresima ni safari ya toba na wongofu wa ndani
Kwaresima ni safari ya toba na wongofu wa ndani

Somo la Injili: Ni Injili kama ilivyoandikwa na Mathayo 4:1-11. Katika somo la Injili Takatifu tunamwona Bwana wetu Yesu Kristo baada ya ubatizo wake anaongozwa na Roho kwenda nyikani na huko alifunga siku arobaini mchana na usiku. 40 katika maandiko matakatifu ni muda wa kutosha, ni kipindi cha maandalizi. Bwana wetu Yesu Kristo alikua akijiandaa na nini? Alikuwa anajiandaa kuanza rasmi utume wake wa wazi, utume wa kumkomboa mwanadamu aliyeanguka katika dhambi. Maandalizi ya safari ya ukombozi kuanzia utume wake wa wazi mpaka pale juu ya Msalaba. Sisi kwa kufunga tunajiandaa na nini hasa? Sisi nasi kwa kuadhimisha jumatano ya majivu tulianza nasi rasmi safari yetu ya siku 40, ni muda wa maandalizi na tunasafiri mpaka Ijumaa kuu pale juu ya msalaba wa Kristo, na kuendelea mpaka kushangilia ushindi wa Kristo katika ufufuko wake kwa fumbo la Pasaka. Ni safari ya kiroho inayoeleza uhalisi wa safari yetu ya maisha ya yote ya hapa duniani. Tunasafiri kuelekea nchi yetu ya Ahadi mbinguni, yalipo makazi yetu ya kudumu tangu kuumbwa kwetu. Ni safari inayotudai nguvu za kiroho na ndio sababu kama Kristo nasi tunafunga. Kristo ni Musa mpya anayewatoa taifa jipya la Mungu kutoka katika utumwa wa dhambi kwenda kwenye uhuru kamili wa wana wa Mungu, nchi mpya ya Ahadi, yaani mbinguni. Kwa miaka 40 taifa la Israeli walikuwa jangwani, ambapo walijaribiwa kwa namna nyingi. Waliweza kushinda vishawishi hivyo kwa kuwa wasikivu kwa na watii kwa Neno la Mungu. Mwinjili Mathayo, kwa simulizi hili la kwenda Yesu Jangwani anataka kumwonesha Kristo kama Israeli mpya ambaye anakwenda njia ile ile kama Musa alivyowaongoza taifa la Mungu kwenda kwenye ncihi ya Ahadi. Katika safari hii Kristo alikutana na vishawishi vingi kutoka kwa ibilisi. Kristo anatufundisha kwamba njia pekee ya kumshinda shetani ni kuwa watii kwa sauti ya Mungu, kuwa wasikivu kwa Neno la Mungu. Nasi katika safari yetu ya maisha, tutapitia majaribu kama haya haya waliyopitia taifa la Israeli, lakini tukitii kama Kristo tutashinda. Kristo alijaribiwa katika mambo yale yale kama waliyojaribiwa wana wa Israeli na wakashindwa na kuanguka kila mara dhambini, mambo ambayo hata sisi yanatuangusha kila mara katika dhambi.

Jumatano ya Majivu ni mwanzo wa Kipindi cha Kwaresima
Jumatano ya Majivu ni mwanzo wa Kipindi cha Kwaresima   (AFP or licensors)

Kwanza: Kishawishi cha Chakula. Yesu alikua na njaa, siku arobaini alifunga. Ibilisi alijua ya hitaji lake. Lengo la jaribu hili ni kutaka kumshawishi Yesu atumie karama/nguvu zake za kimungu kwa ajili ya maslahi binafsi badala ya kusudi la Mungu. Ni jaribu la kutaka “kuridhika sasa hivi”. Hili ni jaribu la kutosheleza tamaa za mwili kwa njia zisizo halali au nje ya wakati na mpango wa Mungu. Mara kadhaa mahitaji ya kimwili na kidunia yanatushika kupita kiasi na kutusahaulisha hitaji letu la muhimu na la kwanza. Pengine kila wakati nawaza kazi, biashara, utajiri na mali, kama hayo ndiyo yanayoweza kuleta furaha ya kweli. Je mara ngapi nimewazia roho yangu kama ninavyowazia mahitaji mengine ya mwili? Kipaumbele change cha kwanza ni nini. Jibu la Yesu (“Mtu haishi kwa mkate tu ila kwa kila Neno litokalo katika kinywa cha Mungu Kumb 8:3”) linatukumbusha kuwa roho yetu inahitaji chakula (Neno) zaidi ya mwili unavyohitaji chakula. Pili: Kujirusha toka kilele cha Hekalu (Kiburi cha Uzima). Shetani ananukuu maandiko (Zaburi 91:12) akisema malaika watamlinda. Shetani anatumia Neno la Mungu ili kumshawishi Yesu. Lengo la Jaribu ni jaribu la kutafuta umaarufu na sifa (Identity). Shetani alitaka Yesu athibitishe kuwa yeye ni Mwana wa Mungu kwa njia ya miujiza ya kustaajabisha badala ya imani na unyenyekevu. Hili linatokea tunapotaka kutumia dini au mahusiano yetu na Mungu ili tujikweze na kujitafutia faida binafsi. Maandiko Matakatifu yaweza kutumika pia katika kupotosha. Shetani alitaka Yesu amlazimishe Mungu kufanya muujiza ili kuthibitisha upendo wake. Yesu anafundisha kuwa imani ya kweli ni kumtumaini Mungu bila kuhitaji kumuweka katika majaribio au mtego ili athibitishe uwezo wake. 

Kishawishi cha tatu ni tamaa ya macho
Kishawishi cha tatu ni tamaa ya macho

Tatu: Katika kishawishi cha tatu, ambacho ni jaribu la madaraka na utajiri wa dunia (Tamaa ya Macho), Shetani anampa Yesu ofa ya kumilikishwa falme zote za ulimwengu kwa sharti moja tu: “Ukianguka kunisujudia.” Yesu anajibu kwa mamlaka makubwa akitumia neno kutoka Kumbukumbu la Torati 6:13: "Nenda zako, Shetani; kwa maana imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake. Shetani alikuwa anampa Yesu ufalme bila msalaba. Yesu alijua kuwa njia ya kuikomboa dunia ni kupitia mateso na utii kwa Baba, si kwa kufanya mapatano na uovu ili kupata mafanikio ya haraka. Siku hizi zipo Injili nyingi, Injili ya mafanikio, Injili ya miujiza, Injili ya uponyaji, lakini wachache wanaohubiri ukweli wa mateso na msalaba, wanaokemea maovu katika jamii, wanaohubiri utii na unyenyekevu kwa Mungu. Sio kweli kwamba anayemwamini Mungu hateseki na kufa, si kweli kweli kwamba anayemwamini Kristo atakua na maisha rahisi. Kristo mwenyewe alitupa mfano, kwa kuteseka na kufa, Ishara kwamba hakuna pasaka bila mateso.Somo la Pili: Ni kutoka Katika Waraka Mtume Paulo kwa Rum 5:12-19. Katika somo la pili Mtume Paulo anatueleza kuwa Adamu wa kwanza, kama tulivyosikia katika somo la kwanza alikosa utii na kwa njia yake dhambi ikaingia katika historia ya Mwanadamu.

Hakuna Pasaka Pasi na Ijumaa kuu
Hakuna Pasaka Pasi na Ijumaa kuu

Lakini Kristo, Adamu mpya alikua mtii kwa Mungu na kwa njia yake Mwanadamu aliyeanguka katika dhambi akapata tena neema inayoshinda dhambi ya mauti, ndio neema ya utakaso, uzima wa kimungu tulioupoteza kwa sababu ya dhambi. Kristo aliturejeshea tena uhusiano mwema na Mungu ambao Paulo anauita kuhesabiwa haki (Justification), ambayo inatujia kama neema tusiyostahili. Mti katika simulizi la anguko la mwanadamu ulikuwa mahali ambapo mwanadamu alijaribiwa na kushindwa kwa sababu ya kutaka kuwa kama Mungu kupitia majivuno na uasi. Huu unaitwa mti wa laana kwa sababu ulileta mauti. Katika Msalaba Kristo (Adamu wa Pili) anachukua nafasi ya Adamu juu ya "mti" (msalaba). Hapa, ushindi unapatikana si kwa kujitwalia madaraka, bali kwa utii kamili kwa Mungu. Kumbe msalaba ni mti wa uzima uliorejeshwa. Hitimisho: Katika Dominika hii tumshukuru Mungu ambaye licha ya dhambi na udhaifu wa Mwanadamu hakumwacha apotee, bali kwa Upendo na huruma kuu alianzisha mpango mpya wa ukombozi.

Tafakari D Kwaresima
21 Februari 2026, 16:24