Tafuta

Tafakari Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya Pili ya Kipindi cha Kwaresima: Utukufu, ukuu na heshima ya Kristo Yesu vimetundikwa juu ya Msalaba Tafakari Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya Pili ya Kipindi cha Kwaresima: Utukufu, ukuu na heshima ya Kristo Yesu vimetundikwa juu ya Msalaba  (ANSA)

Tafakari Dominika ya Pili Kipindi Kwaresima Mwaka A: Kashfa ya Fumbo la Msalaba!

Hii ni changamoto kwa kila mwamini kuhakikisha kwamba, anatoa nafasi kwa mwanga wa imani, matumaini na mapendo, ili uweze kumletea mabadiliko ya dhati katika maisha, kwa kuifia dhambi na nafasi zake, ili kutoa fursa ya kuishi katika utu mpya unaofikia hatima yake katika Fumbo la Msalaba wa Kristo Yesu ambaye kimsingi ni utimilifu wa Sheria na Unabii; Masiha wa Bwana anayeshuhudiwa na Mungu Baba.; mwaliko wa kumsikiliza na kutekeleza ujumbe wake!

Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.

Utangulizi: Wapendwa Taifa la Mungu, leo ni Dominika ya Pili ya Kwaresima, mwaka A wa Kanisa. Mama Kanisa katika tukio la Kristo Yesu kung’ara Uso mbele ya Mitume wake anaungama kwa dhati kabisa kuhusu: Ubinadamu na Umungu wa Kristo; Kuzaliwa kwa Mwana wa Mungu na Mkombozi wa dunia sanjari na kuzaliwa kwa Kanisa Sakramenti ya wokovu kwa binadamu! Tukio hili inagusa kwa namna ya pekee, umuhimu wa Kanisa kusimama kidete kulinda na kutunza kazi ya uumbaji kama anavyokaza kusema Mtakatifu Damascene.  Kristo Yesu anaufunua Umungu wake kwa njia ya mwili uliotukuka, ndiyo maana Kanisa linamwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa, shukrani na utukufu kwani ukuu una Yeye milele hata na milele! Hii ni changamoto kwa kila mwamini kuhakikisha kwamba, anatoa nafasi kwa mwanga wa imani, matumaini na mapendo, ili uweze kumletea mabadiliko ya dhati katika maisha, kwa kuifia dhambi na nafasi zake, ili kutoa fursa ya kuishi katika utu mpya unaofikia hatima yake katika Fumbo la Msalaba wa Kristo Yesu ambaye kimsingi ni utimilifu wa Sheria na Unabii; Masiha wa Bwana anayeshuhudiwa na Mungu Baba. Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika ya Pili ya Kipindi cha Kwaresima inatutafakarisha juu ya, “Safari ya mabadiliko kwa njia ya imani: kutoka ahadi hadi utimilifu.” Ukombozi wa wanadamu baada ya anguko ni mpango ambao Mungu mwenyewe aliuanzisha tena upya kwa kumwita Abrahamu. Ahadi hii inatimizwa hatua kwa hatua katika historia, na kufikia utimilifu wake katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Tumshukuru Mungu kwa uaminifu wa Ahadi yake na tuombe neema ya kupokea mabadiliko ya ndani, ili tustahilishwe kushiriki utukufu wa ufufuko pamoja na Kristo Yesu.

Waamini wanakutana na Kristo Yesu katika Neno lake
Waamini wanakutana na Kristo Yesu katika Neno lake   (@Vatican Media)

Somo la Kwanza: Ni kutoka katika Kitabu cha Mwanzo 12:1-4a. Somo la kwanza kutoka katika kitabu hiki cha Mwanzo, Mwenyezi Mungu anamwita Abramu. Katika somo hili tutatafakari mambo makubwa manne muhimu; kwanza, Wito ni mpango wa upendelo wa Mungu, unaopokelewa kwa imani, Pili, Wito huu wa Mungu unahitaji mabadiliko, yanayohusisha utii na sadaka. Tatu, Imani inatusukuma kutembea katika Ahadi za Mungu hata kabla hazijatimia na nne, Wito wetu unatusukuma kwenye utume, kuwa lango la baraka kwa wengine. Tutatafakari haya tukitazama wito wa Abramu Baba yetu wa Imani. Jambo la kwanza: Wito kama mpango na Upendeleo wa Kimungu. Katika simulizi hili la wito wa Abramu tunaweza kujiuliza swali moja muhimu sana; Kwa nini Mungu alimchagua na kumwita Abramu? Je, Abramu alimtafuta Mungu kwanza, au ni Mungu alimtafuta Abramu? Mungu alimchagua Abramu kwa sababu alipenda yeye mwenyewe kwa uhuru wake. Ni tendo upendeleo wa kimungu (It is an act of God’s favor and sovereign freedom). Mungu ndiye anayezungumza kwanza. Ni Mungu anayemtafuta Mwanadamu aliyepotea, aliyekosa utii na kuanguka katika dhambi. Ndugu mpendwa, hii yatukumbusha ni kwa jinsi gani Mungu alivyoupenda hivi ulimwengu. Mungu aliyemwumba Mtu kwa upendo huo hakutaka mwanadamu abaki katika dhambi hivyo anaamua tena yeye kwa mpango na upendeleo wake kumtafuta na kuanzisha upya tena safari ya ukombozi. Ndugu mpendwa, kwa Mungu hatupaswi kukata tamaa kwamba hapo ndio mwisho wa hadithi yetu. Mungu alitupenda sisi kwanza, hatukustahili ila alitustahilisha. Hapo ulipo ndugu mpendwa sio kwa sababu tu ya juhudi yako, wito ulio nao, kazi uliyo nayo, familia uliyo nayo, Watoto, mafanikio yako, sio tu matunda ya juhudi yetu, bali ni Mungu ndiye anayepanga kila jambo. Kuna nyakati twaweza kujiuliza, hivi mimi ni nani hata Mungu amenileta mpaka hapa? Mimi ni nani hata Mungu amenilinda mpaka leo? Mimi ni nani hata Mungu ameniita, akanishirikikisha zawadi ya ukombozi, bure bila hata mastahili yangu. Mshukuru Daima Mungu ambaye alitupenda sisi kwanza, aliyetutafuta kabla sisi hatujamtafuta bado.

Waamini wajifunze utamaduni wa kusikiliza kwa makini
Waamini wajifunze utamaduni wa kusikiliza kwa makini   (@Vatican Media)

Jambo la pili: Wito huu wa Mungu unahitaji mabadiliko, yanayohusisha utii na sadaka. Mwenyezi Mungu anavyomwita Abramu anamwambia, “Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya Baba yako na uende mpaka nchi nitakayokuonesha” Mambo haya matatu anayopaswa Abramu kuyaacha yaani, Nchi yake (Land), jamaa zake (Family) na nyumba ya Baba yake (Ancestors) yalikua ni alama ya utambulisho, usalama na urithi wa mtu katika ulimwengu wa wakati ule. Hii ina maana kuwa, Abramu alipaswa kujikata kabisa kutoka katika utambulisho wake wa kale (social death) na kuanza safari mpya kabisa ya maisha. Halikuwa jambo rahisi, lakini kwa Imani na utii Abramu anaondoka. Habishi wala hapingi, aliamini kwa asilimia mia moja. Ndugu mpendwa, sisi pia kama ilivyokuwa kwa Abramu, tumeitwa na Mungu kwanza kabisa katika Imani kwa njia ya ubatizo wetu. Kwa ubatizo, Mwenyezi Mungu anaanzisha safari mpya ya maisha ndani mwetu kama ilivyokuwa kwa taifa lake teule. Utambulisho wetu huu mpya unatudai utii na sadaka kubwa. Utii kwa Mungu, sisi kama watoto wake wapendwa, na uaminifu katika kuishi huo wito wetu kama taifa jipya la Mungu tulio safarini kuelekea utimilifu wa Ahadi zake, yaani uzima wa milele. Kila mara tunakumbushwa juu wa wajibu wetu huu msingi wa kuishi kweli wito wetu kama Wakristo na kila mmoja wito wake kadiri ya hali yake. Kwaresima hii inatualika kujikata kutoka katika maisha yetu ya zamani, mahusiano ya zamani, maelekeo ya zamani. Tunaalikwa kuacha na mambo ambayo pengine tunaona ndipo ulipo ulinzi na utambulisho wetu, mali, vyeo, marafiki, umaarufu, anasa, starehe, na mizizi yote ya dhambi, na kuukumbatia wito wetu kiaminifu kama watoto wa Nuru. Je, nini kinanizuia bado kufanya mabadiliko ya kweli? Ni jambo gani linanishinda bado kuachana nalo, nimejishikamanisha na nini ambacho inakuwa vigumu sana kuitikia wito na mwaliko wa Mungu wa kuanza maisha mapya. Toka sasa hapo ulipo, ondoka, nenda kule Mungu anataka uwe. Huenda upo katika shimo la huzuni na hofu, toka. Huenda upo katika hali ya kukata tamaa kila wakati, toka. Huenda umeshikilia mambo mengi ya dunia na hayo yanakupa nguvu na ujasiri kwamba ndio kilele cha maisha, toka. Acha yote, kwa msaada wa Mungu, nenda kule Mungu anataka uwe, kule alikokutayarishia kwa gharama kubwa, bora zaidi ya hapo ulipo sasa. Hii inahitaji neema ya pekee. Kesho yetu na Mungu ni bora sana kuliko leo yetu tunayoihangaikia kwa nguvu zetu wenyewe.

Kristo Yesu anakutana na waja wake Neno la Mungu linaposomwa
Kristo Yesu anakutana na waja wake Neno la Mungu linaposomwa   (@VATICAN MEDIA)

Jambo la Tatu: Imani inatusukuma kutembea katika tumaini la Ahadi za Mungu hata kabla hazijatimia. Abrahamu alivyoitwa na Mungu hakuhoji maswali wala hajiuliza mara mbili, hakubisha wala hakupinga. Mungu anampa uhakika wa maisha mapya kwa njia ya Ahadi alizomtamkia ambazo kusema ukweli kibinadamu zilikuwa hazitekelezeki. Ijapokuwa Abramu alijua ugumu wa utimilifu wa Ahadi hizo, bado aliamini. Aliahidiwa kuwa taifa kubwa (descendants), lakini mkewe Sarai alikua tasa, aliahidiwa ardhi (land) lakini kule alikokwenda ardhi ilikua mali ya watu wengine, aliahidiwa baraka (Blessings), lakini kutokuwa na mtoto au uzao ilikua ni kinyume cha ishara ya baraka. Hata hivyo, Abramu anaamini na anatii. Hakuna hata moja ya Ahadi aliyoiona kwa macho yake wakati anaitwa. Tunaambiwa, “Akaenda kama Bwana alivyomwamuru” Ndugu mpendwa Imani ya Ibrahimu kama Baba wa Imani unatualika nasi kuomba fadhila hii ya Imani wakati wote. Safari yetu ya maisha na Imani sio rahisi. Imani inatusaidia kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo. Imani inatusaidia daima kutembea katika Neno la Mungu, kuamini daima katika utimilifu wa lile alilotuahida kwa kuwa yeye ni Mungu mwaminifu. Huenda tumekua tukijiuliza uliza maswali mengi, kwamba nikiitika wito huu wa Mungu maisha yangu huko mbeleni yatakuwaje, je mambo yote ninayopaswa kuacha nitayapata tena? Mitume wa Yesu pia walimwuliza Yesu swali hili kwamba, Bwana tumeacha yote tukakufuata, tutapata nini zaidi? Yesu anawaahidi kwamba watapata mara mia zaidi na kubwa zaidi uzima wa milele. Ahadi kubwa Mungu anayotuahidi ni kuishi naye milele, na amekwisha tufungulia njia kwa kumtuma kwetu mwanaye wa pekee. Ni Ahadi ya kung’ara na kushirikishwa utukufu wake, licha ya mateso na msalaba wa maisha haya.

Waamini wanaitwa na kutumwa kuwa ni mashuhuda wa huruma ya Mungu
Waamini wanaitwa na kutumwa kuwa ni mashuhuda wa huruma ya Mungu   (@Vatican Media)

Jambo la nne: Wito wetu unatusukuma kwenye utume, kuwa lango la baraka kwa wengine. Mwenyezi moja kati ya Ahadi alizompa Abramu ni kwamba, “Nami nitakufanya wewe kuwa Taifa kubwa, na kukubariki na kulikuza jina lako, nawe uwe baraka…” Abramu hakuchaguliwa kwa ajili yake mwenyewe bali alichaguliwa ili kupitia yeye Mwenyezi Mungu ayabariki mataifa yote ya ulimwengu. Ndugu mpendwa, Mungu anapotuita na kutuinua kwa wajibu wowote ule, anatutuma. Hatuinui kwa ajili yetu sisi bali ili kupitia sisi baraka zake ziwaendee watu wengine. Kwaresma hii itukumbushe wajibu wetu wa kuwa kweli baraka kwa wengine kwa kuwatendea wengine mambo mema, kuwawazia wengine Mawazo ya amani, kuwaonea huruma wenye shida, kuwa tayari kutoa na kupokea msamaha, kutokuwa chanzo cha maumivu na vilio kwa wengine. Wewe u baraka, u lango la neema na baraka za Mungu. Wewe u mwana wa Mfalme, toa katika hazina yako yale yaliyo mema, sambaza neema za Mungu, sambaza upendo wa Mungu, sambaza Msamaha, sambaza wema na huruma ya Mungu, sambaza ukarimu, sambaza sadaka yako kujibakisha na bila kikomo na masharti. Kristo atusaidie ili daima tujitoe bila kuibakiza kumdhihirisha kwa watu wote. Kristo, ajulikane na kupendwa. Je, ninatoa baraka? Nimekua mkondo, au lango la baraka za Mungu?

Hata leo hii Mungu bado anawaita na kuwatuma waja wake
Hata leo hii Mungu bado anawaita na kuwatuma waja wake   (@Vatican Media)

Somo la Injili ni kama ilivyoandikwa na Mwinjili Mathayo 17:1-9. Somo la Injili Takatifu kutoka katika Injili ya Mathayo, latueleza tukio la Bwana wetu Yesu Kristo kugeuka sura. Katika somo hili tuna mambo yafuatayo ya kutafakari. Kwanza, kwa nini Kristo aliwachukua Mitume watatu kati ya wote? Pili, kwa nini Kristo aligeuka sura mlimani? Tatu, uwepo wa Musa na Eliya maana yake ni nini? Nne, sisi tunajifunza nini hasa katika tukio hilo tunapoelekea kuadhimisha fumbo Takatifu la Pasaka? Tuanze kujadili mambo haya kwa kina. Jambo la kwanza: Kwa nini Kristo aliwachukua Mitume hawa watatu kati ya Mitume wote kumi na wawili? Katika Dominika ya pili ya Kwaresma kila mwaka tunasikia simulizi hili la Bwana wetu Yesu Kristo kugeuka sura. Sehemu inayotangulia tukio hili, ni utabiri wa Kristo juu ya kuteswa, kufa na kufufuka kwake (Mt. 16:21-28), akiwasisitizia Mitume wake kwamba hakuna utukufu bila Msalaba na kifo. Ndugu mpendwa Yesu anawachukua Mitume hawa watatu (inner circle), Petro, Yohane na Yakobo kwanza ili kuwakumbusha kuwa safari ya kuelekea utukufu si safari rahisi. Anawaonesha na kuwashirikisha tu sehemu ya utukufu huo ili kuwaimarisha ili nao wakawaimarishe mitume wengine hasa nyakati watakapopitia pia katika mateso na kifo. Petro atakuja kuwa kiongozi wa Mitume wote, Yakobo atakuwa wa kwanza kufa kifo dini na Yohane atakuwa mtume wa mwisho kabisa kufa kati ya Mitume wote. Hivyo lengo kubwa hapa la Yesu ni kuwaimarisha hawa Mitume na kuwatia moyo ili wasikate tamaa kuishuhudia Imani yao hata ikiwapasa kuteseka na kufa. Katika tamaduni za Wayahudi, ushahidi wa watu watatu ulichukuliwa kuwa ni ushahidi wa kweli juu ya tukio lililotokea. Kwa kuwachukua Mitume hawa watatu Yesu alitaka kuthibitisha kwamba tukio lile ni tukio la kweli na Mtume Petro anaeleza hili katika (2 Pet 1:16-19). Tukio hii liliwaimarisha Mitume baadaye katika jumuiya ya Wakristo wa kwanza.

Waamini wanakutana na Kristo Yesu katika Sakramenti za Kanisa
Waamini wanakutana na Kristo Yesu katika Sakramenti za Kanisa   (@Vatican Media)

Jambo la pili: Kwa nini Kristo alibadilika sura Mlimani? Tukio hili la kugeuka sura linatokea siku sita baada ya Kristo kutoa utabiri juu ya mateso kifo na ufufuko wake. Aya ya mwisho katika sura iliyotangulia sehemu hii, Kristo anawaahidi kuushuhudia utukufu huo anaposema, “Amini nawaambieni, pana watu katika hawa wasimamao hapa, ambao hawataonja mauti kabisa hata watakapomwona mwana wa Adamu akija katika ufalme wake” (Mt 16:28). Siku sita baadaye Kristo anabadilika sura akiwa na baadhi ya wanafunzi wake. Namba sita hapa katika Injili hii ya Mathayo yaturudisha katika kitabu cha kutoka 24:16, ambapo Musa alipopanda Mlimani Sinai, na akiwa huko utukufu wa Mungu uliufunika huo mlima na kukaa juu yake, wingu likaufunikiza huo mlima siku sita na siku ya saba Mungu akamwita Musa toka katika lile wingu. Kumbe ni katika muktadha huo huo Mwinjili Mathayo anamtambulisha kwetu Kristo kama Musa mpya anayeratibisha tena Agano jipya na la milele kati ya Mungu na taifa lake jipya na kuudhirisha kwetu katika utimilifu wake utukufu wa Mungu. Mwenyezi Mungu anamtambulisha Kristo Yesu, “Huyu ni mwanangu mpendwa, ninayependezwa naye, msikieni yeye” Kristo anatambulishwa na kufunuliwa kwetu kwa mara nyingine tena kama Masiya, Mwana wa Mungu na wajibu wetu sisi ni kumsikiliza Yeye ambaye kwa njia yake tumepata ukombozi wa milele. Kumbe tukio hili ni tendo la ufunuo wa Mungu kwa njia ya Mwanaye Yesu Kristo.

Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa
Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa   (ANSA)

Jambo la tatu: Uwepo wa Musa na Eliya katika tukio hili maana yake ni nini? Katika tukio hili la kugeuka sura Bwana wetu Yesu Kristo, walitokea Musa na Eliya wakizungumza na Yesu. Musa anawakilisha Torati na Eliya anawakilisha Manabii. Ni kusema kwamba Kristo, kwa ujio wake ulimwenguni anakamilisha Agano zima la Kale. Musa alipewa Torati ambayo kimsingi ililenga kuwaelekeza Taifa la Mungu kufikia utimilifu wa Ahadi zile Mwenyezi Mungu alizonena na Abrahamu alipomwita na kuanzisha upya mpango wa ukombozi wa wanadamu wote. Eliya anawakilisha manabii wote ambao waliwakumbusha watu wajibu wao wa kulishika Agano, lakini pia waliotabiri utimilifu wa ahadi hizi za Mungu. Kristo sasa anatimiza yote aliyonena Mungu kwa watu wake. Tunaona jinsi Mungu alivyo mwaminifu kwa Ahadi zake, alichomwahidi Abramu sasa kinatimia katika Kristo kwa Fumbo Takatifu la Pasaka.

Yesu anakutana na waja wake katika Ibada mbalimbali za Kanisa
Yesu anakutana na waja wake katika Ibada mbalimbali za Kanisa

Jambo la nne: Sisi tunajifunza nini hasa katika tukio hilo tunapoelekea kuadhimisha fumbo Takatifu la Pasaka? Tukio hili la kugeuka sura Bwana wetu Yesu Kristo lilitokea majuma kadhaa kabla ya kuingia katika mateso yake. Lengo hapa kama nilivyotangulia kusema ni kutuonesha muungano wa pekee uliopo kati ya utukufu na msalaba. Kristo anawafunulia Mitume wake kwa muda tu utukufu wake, lakini ni utukufu usiotenganishwa kamwe na mateso na msalaba. Kwanza: Kugeuka sura kwa Bwana wetu Yesu Kristo kunatupa nguvu na matumaini ya kuchukua misalaba yetu. Yesu aligeuka sura ili kuwaimarisha Mitume wake alipokuwa anakaribia mateso, kifo na ufufuko wake, ili wawe imara katika Imani matumaini na mapendo. Katika nyakati ngumu katika safari yetu ya maisha, hasa tunapochukua misalaba Yetu, kugeuka sura kwa Bwana wetu Yesu Kristo kunatupa nguvu ya kusonga mbele katika kubeba misalaba yetu kwa matumaini kwamba ni kwa njia ya msalaba tutapata neema ya kuishi pamoja na Kristo katika uzima wa milele. Msalaba wangu ndio ngazi yangu ya kwenda mbinguni, sina budi kuukumbatia, kuupenda na kuubeba kwa Imani na matumaini. Hakuna utukufu bila mateso na kufa, ndipo tufufuke pamoja na Yesu katika uzima wa milele. Pili: Kila mara nasi tunapokutana na Kristo, tunabadilishwa. Kristo Yesu anakutana nasi katika nyakati mbalimbali za maisha yetu. Anakutana nasi katika Neno lake, kumbe tulisikiapo Neno lake, Neno la faraja linatubadilisha, nyakati tulipokata tamaa, tulipokosa matumaini Neno lake linasema ndani mwetu na kutuinua tena. Kumbe, wajibu wetu hapa ni kumsikiliza yeye Mwana pekee wa Mungu aliyekuja ulimwenguni ili kutuletea ukombozi. Ni wajibu tunaopewa na Mungu Baba wa kumsikiliza Mwanaye aliyemtuma kwetu.

Kuzeni na kudumisha Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu
Kuzeni na kudumisha Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu

Anakutana nasi katika Ekaristi Takatifu, mkate unabidilishwa kuwa mwili na Divai kuwa Damu yake Takatifu katika ibada ya Misa Takatifu. Nasi tunapopokea Ekaristi Takatifu tunabadilishwa, Kristo anayebadili Mkate kuwa Mwili wake kweli na Divai kuwa Damu yake kweli anabadili pia hali zetu. Anabadili unyonge wetu kuwa ushindi, anabadili huzuni yetu kuwa furaha, anabadili hofu zetu kuwa ujasiri, anatulisha na kutushibisha roho zetu. Tunatoka wapya kabisa, tunatoka tumebadilishwa kabisa. Kristo anakutana nasi katika Sakramenti ya Kitubio, anatupatanisha naye, dhambi zetu zijapokua nyekundu kama Damu anatufanya kuwa weupe kama sufu. Katika sakramenti ya kitubio tunang’arishwa na Kristo mwenyewe. Mahusiano yetu ya Mungu yanasafishwa, mahusiano yetu na ndugu zetu yanaponywa, fikra zetu zinatakaswa, dhambi zetu zinaondolewa. Katika Sakramenti zote za Kanisa, Kristo anaanzisha safari mpya kabisa ndani mwetu, hatubaki tulivyokuwa, anatubadili utu wetu wa ndani nasi tungang’aa. Kristo anakutana nasi katika nafsi za wanaoteseka, maskini, wagonjwa, wafungwa magerezani, watoto yatima, watoto wa mitaani, watu waliokataliwa na wanaonyanyaswa. Na kila anayenyoosha mkono kuwasadia hawa walio wadogo, Kristo anatuhakikishia kwamba tunakutana naye na tumemtendea yeye. Thawabu yetu ni kushirikishwa utukufu tuliowekewa tayari tangu kuumbwa kwa ulimwengu. Huku ndiko kuwashirikisha wengine utukufu wa Mungu. Petro alitaka kujenga vibanda vitatu, ili waendelee wao tu kuufurahia utukufu wa uwepo wa Mungu kati yao. Kama Ilivyokuwa kwa Abramu, tuwashirikishe wengine utukufu wa Mungu, maisha yetu yawasaidie wengine kuhisi uwepo wa Mungu anayefanya kazi kupitia sisi. Huenda mara nyingi tunajenga vibanda na kusahau kuwashirikisha wengine utukufu wa Mungu. Kwaresma inatualika kutenda matendo ya huruma na kutoa sadaka.

Utukufu wa Kristo Yesu Umetundikwa Msalabani
Utukufu wa Kristo Yesu Umetundikwa Msalabani   (@Vatican Media)

Kristo anakutana nasi tunapopanda Mlimani kusali. Kristo alipanda mlimani na wanafunzi wake kusali na huko aligeuka sura. Sisi nasi tunapanda mlimani kila wakati, yaani tunapata wasaa wa kusali na kuongea na Mungu. Tunaalikwa kuwa na muda kwa ajili ya kusali. Tunakutana na Mungu kama nilivyosema katika Adhimisho la Ibada ya Misa Takatifu, hapo ndipo mlima wetu, tunaposali sala zetu binafsi, hapo ndipo mlima wetu, katika kuabudu Ekaristi Takatifu, hapo ndipo mlimani kwetu. Matokeo yake ni kung’ara. Sala ilikiwa kipaumbele cha maisha yetu, tutaungana kabisa na Mungu, nyoyo zetu zitang’aa na utukufu huo utadhihirika nje. Familia zetu zitang’aa, ndoa zetu zitang’aa, jumuiya zetu zitang’aa, makazini kwetu kutan’gaa na popote tutakapokuwa patafunikwa na utukufu wa Mungu. Somo la pili: Ni Waraka 2 Timotheo 1:8b-10. Katika somo hili la pili, Mtume Paulo anamwandikia Timotheo mshirika wake katika kuitangaza Injili, kwamba, sisi sote tumeitwa na Mungu tangu milele sio kwa mastahili yetu bali ni kwa upendeleo, kama tulivyoona mpango wa Mungu namna ulivyoanzishwa kwa Abramu. Sisi wajibu wetu ni kumwungama Kristo kwa Imani, na kuvumilia katika mateso kwa ajili ya Injili. Sisi tulio wafuasi wa Kristo hakuna namna tunaweza kuitikia wito wa kuwa wafuasi kwa kukwepa msalaba na mateso. Lakini Paulo anamtia Moyo Timotheo kwamba, Msalaba na mateso sio bure, bali tunashiriki mateso ya Kristo kwa njia ya nguvu waliyoipokea kutoka kwa Mungu. Ni kwa njia hiyo Kristo amebatili mauti na kuufunua uzima na kutokuharibika kwa ile Injili. Hitimisho: Katika Dominika ya leo, tumshukuru Mungu ambaye ameanzisha na kukamilisha safari mpya ya ukombozi wa milele wa wanadamu wote. Tuombe neema ya kusikia sauti ya Mungu kila siku na kuwa tayari kukumbatia upya wa maisha ili nasi tustahilishwa kuupata uzima wa milele.

Tafakari Dominika 2 Kwaresima
27 Februari 2026, 15:21