Tafuta

Basilika ya Mama Yetu wa Afrika huko Algeris nchini Algeria. Basilika ya Mama Yetu wa Afrika huko Algeris nchini Algeria. 

Kard.Vesco:Kanisa,Algeria limebadilika sana kati ya Uislam-Ukristo na uhai kijamii!

Kwa sasa nchini Algeria inakabiliwa na kipindi nyeti,kilichojaa mabadiliko ya kisiasa na changamoto zinazoendelea za kiuchumi na kijamii.Bado inatafuta usawa mpya,nchi inaendelea kuchukua jukumu muhimu katika mandhari ya Mediterania na Afrika.Haya yamesemwa na Askofu Mkuu wa Algiers,Kardinali Jean-Paul Vesco,katika muktadha wa ziara ya Kitume ya Papa Leo XIV anayewasili nchini mwake Aprili 13.

Na Ferruccio Ferrante – SIR.

Askofu Mkuu wa Algiers nchini Algeria anaelezea nchi inayopitia mabadiliko ya kisiasa, kijamii, na kiuchumi, ambapo jumuiya ndogo ya Kikristo inadumisha uwepo wa siri lakini wenye matokeo chanya. Kanisa la Algiers linahamasisha mazungumzo ya Kiislamu-Kikristo, udugu, usaidizi wa kijamii, na uhusiano na vijana, huku nchi ikitafuta nafasi ya upatanisho katika Mediterania na Afrika. Kwa sasa nchini Algeria inakabiliwa na kipindi nyeti, kilichojaa mabadiliko ya kisiasa na changamoto zinazoendelea za kiuchumi na kijamii. Bado inatafuta usawa mpya, nchi inaendelea kuchukua jukumu muhimu katika mandhari ya Mediterania na Afrika.

Katika muktadha huu, uwepo wa Kikristo ambao ni mdogo kwa idadi lakini muhimu, unajitokeza kwa kujitolea kwake katika mazungumzo na ujenzi wa vifungo vya kidugu. Kardinali Jean-Paul Vesco, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Algiers nchini Algeria katika fursa ya Ziara ya Kitume ya Baba Mtakatifu Leo XIV inayoanza Jumatatu tareh 13 Aprili 2026 , anashuhudia taifa lake na Kanisa lake. Kwa miaka mingi, ameendeleza Kanisa lenye mizizi katika kukutana na kuheshimiana. Yafuatayo ni mahojiano kamili yaliyofanywa na Shirika la Habari Katoliki Italia(SIR.)

Mwadhama hali inayopumuliwa nchini huko ikoje,hata mbele ya migogoro ya kimataifa?

Karibu kama ilivyo Ulaya. Tukiangalia hali halisi kwa ujumla, athari ya mgogoro haionekani kuathiri maisha ya kila siku kwa undani zaidi kuliko huko Roma au katika muktadha mwingine wa Ulaya. Matukio ya kimataifa yanarudiwa, lakini hayabadilishi umakini endelevu au mjadala mkali hasa. Mada hii inazungumziwa katika vyombo vya habari, lakini si kwa nguvu zaidi kuliko kwingineko; vile vile, katika mazungumzo ya kila siku, hakuna ongezeko kubwa la maslahi. Katika baadhi ya matukio, mtu hupata hata hisia ya umbali fulani, kana kwamba ugumu wa picha ya kimataifa ulifanya ushiriki wa moja kwa moja na endelevu kuwa mgumu zaidi.

Je, ni wasiwasi na matumaini yako gani katika suala hili?

Tunapozungumzia wasiwasi na matumaini, lengo kuu haliepukiki zaidi ya mipaka ya kitaifa. Masuala makuu si kuhusu Algeria yenyewe, bali ni kuhusu utulivu wa jumla wa mpangilio wa dunia. Kinachotia wasiwasi ni hisia iliyoenea ya kutofanya kazi vizuri kwa mfumo, ya kudhoofisha mizani, na ya mienendo ya kimataifa ambayo inazidi kuwa vigumu kutafsiri. Katika muktadha huu, matumaini pia yana mtazamo mpana zaidi:  Unahusu uwezekano wa kujenga upya aina imara na za haki za kuishi pamoja kimataifa, zenye uwezo wa kushughulikia mivutano bila kugeuka kuwa migogoro.

Katika muktadha wa Waislamu wengi, jukumu la Jumuiya  ya Wakristo ni lipi?

Katika maisha ya kila siku, mbinu yetu inabaki kuwa yenye msimamo kidete: tunajibu maombi na mahitaji kama yanavyoombwa, bila nia ya kumwelekeza au kumshawishi mzungumzaji. Kwa maana hii, Kanisa lina jukumu sawa na lile la wengine wengi: shughuli ya kichungaji inayolenga Jumuiya ya Wakristo, ikiambatana na hamu ya kutoa uwepo wenye maana na ubora. Uwepo ambao si wa kidini tu, bali pia wa kijamii, ulio wazi na uliojumuishwa katika muundo wa jamii, tayari kusaidia kila mtu.

Kanisa nchini Algeria mara nyingi huelezewa kama "uwepo wa busara." Kwa nini?

Kwa sababu hasa ni mwelekeo wake wa pande mbili, wa kichungaji na kijamii, unaofafanua mojawapo ya sifa muhimu zaidi za kazi yake. Lengo si kuchukua nafasi, bali kuishi katika mahusiano, kwa siri, kwa uwazi, na kwa kujenga. Uwepo ambao haupimwi sana kwa mwonekano bali kwa ubora wa vifungo vinavyozalisha, kwa uwezo wa kusikiliza, na kwa nia ya kushiriki udhaifu na matumaini ya watu. Kanisa nchini Algeria limepitia mabadiliko makubwa: leo limejikita zaidi katika muktadha wa Kiafrika, limeunganishwa katika mienendo ya ndani, na linazingatia upekee wa kiutamaduni wa eneo hilo. Hata hivyo, linadumisha uwepo wake wa busara kama sifa yake tofauti.

Mashahidi wa Algeria walibaki Algeria wakati wa miaka ya giza ya ugaidi, pamoja na watu, wakitoa maisha yao kwa ajili ya upendo. Ni urithi gani wanaouacha kwa Kanisa mahalia  leo?

Urithi unaozidi kumbukumbu ya kihistoria. Ufunguo wa kuelewa wakati uliopo. Uchaguzi wao wa kubaki pamoja na watu wa Algeria wakati wa miaka ya kutisha zaidi ya ugaidi haukuwa kitendo cha ujasiri wa mtu binafsi tu, bali pia ushuhuda wa pamoja wa uaminifu na mshikamano. Katika muktadha uliojaa vurugu na hofu, Kanisa mahalia lilichagua kutoacha eneo hilo, likishiriki kikamilifu hali ya maisha ya watu. Baada ya muda, hii imeunda uhusiano wa kina na jumuiya ya Kiislamu, uliojengwa juu ya uaminifu uliojengwa siku baada ya siku, mara nyingi katika hali mbaya na kwa gharama ya maisha. Zaidi ya miaka thelathini baadaye, ushuhuda huo unaendelea kuwa na ushawishi unaoonekana.

Je, unaweza kutuambia mfano mzuri wa udugu na ushirikiano leo?

Kiutendaji, hii inatafsiriwa kuwa mtandao wa mipango ambayo mara nyingi huwa kimya lakini yenye matokeo. Dada Wadogo, kwa mfano, wanawakilisha sehemu ya marejeo katika vitongoji vilivyo hatarini zaidi. Kazi yao ya kila siku hujitokeza kupitia ishara halisi: kuwakaribisha watoto, kusaidia familia, kupanga shughuli za kielimu, na wakati wa ushirikiano. Kwa zaidi ya miaka ishirini, uzoefu huu umechangia kuunda nafasi za mwingiliano wa kijamii na mshikamano, hasa katika maeneo yaliyotengwa zaidi. Hata katika muktadha wenye uwepo mkubwa wa Waislamu, kazi yao inatambuliwa na kuheshimiwa, hasa kwa sababu inategemea mantiki ya huduma badala ya kujithibitisha.

Je, matarajio ya vijana ni yapi, sehemu ya msingi ya nchi?

Tukitazama vizazi vipya, picha ngumu lakini yenye nguvu hujitokeza. Vijana wanaonesha hitaji kubwa la muunganisho: wanatamani kukutana, kushiriki uzoefu, na kujenga vifungo. Mahitaji haya ya mwingiliano wa kijamii hayapati majibu yaliyopangwa kila wakati, lakini yanabaki kuwa moja ya vipengele muhimu zaidi vya kijamii. Wakati huo huo, kuna hamu kubwa ya uhamaji: vijana wengi hutazama nje ya nchi kama fursa ya ukuaji, ishara ya mvutano kati ya hamu ya kutulia na hitaji la kutafuta fursa kwingine ambazo muktadha wa wenyeji bado unajitahidi kutoa.

Hasa, hali ya wanawake ikoje, katika nyanja za umma na kitaaluma na ndani ya familia?

Jamii ya Algeria inapitia mabadiliko makubwa, hasa kuhusu jukumu la wanawake. Kwa kuongezeka kwa uwepo katika nguvu kazi, hasa katika maeneo ya mijini, wanawake wanasaidia kufafanua upya usawa wa familia na kijamii. Ni mchakato wa taratibu, unaoendelea kwa kasi tofauti kulingana na muktadha na kuishi pamoja na mifumo ya kitamaduni ambayo bado imejikita katika baadhi ya jamii. Uwepo huu wa vipengele vipya na vya kiutamaduni unaonesha taswira ya jamii inayobadilika, iliyojitolea kupata usawa wake kati ya mabadiliko na mwendelezo.

Katika muktadha wa Mediterania, Algeria inaweza kuchukua jukumu gani katika kukuza uhusiano wenye usawa zaidi kati ya watu?

Katika mazingira haya magumu, Algeria inathibitisha nafasi yake kama mchezaji muhimu katika ngazi za kikanda na kimataifa. Mahali pake pa kijiografia na utambulisho wa kiutamaduni huiweka katika kiunganishi kati ya Ulimwengu tofauti: Waarabu-Waislamu na ulimwengu wa Magharibi. Mahali hapa panaifanya kuwa daraja linalowezekana na makosa yanyowezekana. Changamoto ni kubadilisha nafasi hii kuwa fursa, kuimarisha wito wa nchi kwa mazungumzo na upatanishi.

Je, ni matarajio gani kwa ziara ijayo ya Papa Leo nchini Algeria?

Ni katika mwelekeo huu ambapo maono ya Papa yanaelekea, kuiona Algeria kama mahali muhimu pa kukuza njia za kukutana na uelewano wa pande zote mbili. Umakini huu si wa mfano tu; unatafsiriwa kuwa hamu ya kukuza nafasi halisi za mazungumzo, na watu na asasi za kiraia. Wazo la msingi ni kwamba, katika ulimwengu unaojaa mivutano inayoongezeka, uzoefu wa ndani wa kuishi pamoja na kuheshimiana unaweza kutoa maarifa muhimu hata kwa kiwango cha kimataifa.

Ni ujumbe gani ungependa kushirikisha Kanisa nchini Italia na wale walio katika nchi yetu wanaounga mkono kazi ya Kanisa nchini Algeria?

Kwanza kabisa, ningependa kutoa ujumbe wa dhati wa shukrani, unaoambatana na mwaliko mpya wa kuendelea na safari ya pamoja ya usawa. Kwa kujitolea kwa pamoja: hamu, yaani, kukuza kila fursa ya kukutana na mazungumzo kwa uwajibikaji na ufahamu.

Imetafsiriwa na Angella Rwezaula.

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku:Just click here.

 

11 Aprili 2026, 11:36