Majimbo ya Nigeria yatafanya mkesha wa Pasaka mchana kwa sababu za kiusalama!
Kielce Gussie na Sr. Christine Masivo, CPS – Vatican.
Siku ya Dominika ya Matawi, watu wasiopungua 27 waliuawa katika shambulio dhidi ya Jamii ya Angwan Rukuba katika wilaya ya Jos Kaskazini katikati mwa Nigeria. Baada ya tukio hilo, majimbo mengi ya Kikatoliki nchini kote hayatafanya Misa zao ya Mkesha wa Pasaka usiku. Badala yake, misa hizo zitaadhimishwa mchana kwa sababu za kiusalama zaidi.
Busara za kichungaji
Jimbo la Ondo kwa mfano lilitoa taarifa mnamo Machi 30 likitangaza juu ya uamuzi wa Askofu Jude Ayodeji Arogundade wa kuhamisha Mkesha wa Pasaka hadi saa 11.00, jioni siku ya Jumamosi Takatifu. Ujumbe huo, uliosainiwa na Chansela wa Jimbo, Bruda Michael O. Eniayeju, alielezea sababu ya mabadiliko hayo, akisema ni kutokana na "hali halisi ya wakati wetu, hasa ukosefu wa usalama uliopo katika nchi yetu na Jimbo letu na kwa mwonekano wa busara wa kichungaji," wa askofu. Kulingana na Shirika la Kipapa la habari za Kimisionari Fides, ujumbe huo unawaalika mapadre, watawa na waamini "kubaki imara katika imani ya Kikristo katika ufufuko wa Bwana wetu, ambao Mkesha wa Pasaka unaadhimishwa kwa dhati." Lakini pia unawahimiza kuwa makini kwani "usalama ni jambo la kila mtu." Ujumbe huo unaishia kwa kuelekeza "Parokia na Jumuiya zote kuimarisha mikakati yao ya usalama na kuendelea kuombea amani na ulinzi wa nchi kila mara.
Vurugu zinalaaniwa na wote
Ujumbe kwa majimbo ulikuja siku moja tu baada ya shambulio la Dominuka ya Matawi tarehe 30 Machi 2026. Wahalifu waliishutua jamii ya Angwan Rukuba karibu saa moja na nusu usiku wakati watu wakikamilisha kazi za siku. Hofu ilizuka baada ya risasi kufyatuliwa kwa watu bila kubagua. Viongozi wa madhehebu tofauti ya kidini walilaani shambulio hilo kwa kauli moja. Eneo la Jimbo la Plateau la Jama'atu Nasril Islam (JNI) lilielezea kitendo hicho kama kitendo cha kinyama na kisicho na maana na liliwataka mamlaka kuchunguza shambulio hilo. JNI ni shirika mama la makundi mbalimbali ya Kiislamu nchini Nigeria.
Eneo la Jimbo la Plateau la Jama'atu Nasril Islam (JNI) lilitoa taarifa, iliyosainiwa na katibu wake, ikilaani vikali shambulio hilo, ikiliita "tishio kubwa kwa amani na kuishi pamoja katika Jimbo la Plateau." Inasisitiza umuhimu wa kutetea utakatifu wa maisha ya binadamu, ambao "haupaswi kukiukwa katika hali yoyote." Kwa upande wa Rais wa Chama cha Wakristo cha Nigeria (CAN) ambacho huunganisha madhehebu tofauti ya Kikristo nchini Nigeria pia alitoa tamko, "Tunaomboleza. Lakini lazima pia tuseme ukweli. Tulifikaje hapa? Inakuwaje watu hawawezi tena kujisikia salama katika nyumba zao? Inakuwaje, hata katika siku takatifu, jamii zinaachwa wazi kwa ugaidi kama huo?." Rais wa CAN alisisitiza ukweli wa kutisha kwamba washambuliaji walitumia "sare bandia za kijeshi" kwani "zinashambulia moyo wa imani ya umma na lazima zichunguzwe kwa kina."
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku:Just click here.