Tafuta

Askofu Mkuu  Saúre, wa Jimbo Kuu la Nampula, Msumbiji. Askofu Mkuu Saúre, wa Jimbo Kuu la Nampula, Msumbiji. 

Msumbiji:Kanisa Katoliki dhidi ya vurugu na ukosefu wa usalama

Kaskazini mwa Msumbiji inaendelea kukabiliwa na uasi wa muda mrefu na unaobadilika unaosababishwa kwa kiasi kikubwa na ukosefu wa usawa, kutengwa,na ushindani dhidi ya maliasili.Askofu Mkuu Inácio Saure katika mkutano wake wa hivi karibuni katika Bunge la Ulaya huko Brussels,aLIsisitiza kwamba ingawa Wakristo wanalengwa,mizizi ya mgogoro huo ni ya kiuchumi na kijamii si ya kidini tu.

Sr Christine Masivo, CPS – Vatican.

Askofu Mkuu wa Nampula, Inácio Saure alihutubia viongozi katika Bunge la Ulaya, huku akieleza ukweli wenye uchungu unaojitokeza Kaskazini mwa Msumbiji. Haya yalithibitishwa na Shirika la Kipapa la habari za Kimisionari Fides kwamba, “Nchini Msumbiji, msalaba si ishara ya imani tu, umekuwa sababu ya mateso kwa wale wanaoubeba," alisema, akilenga mashambulizi dhidi ya misheni za Wakatoliki na ubadilishaji wa kulazimishwa unaofanywa na waasi wanaofanya kazi chini ya bendera ya Dola ya Kiislamu tangu 2021. Hata hivyo, Askofu Mkuu alisisitiza kwamba dini pekee haielezei mgogoro huo. Ingawa Wakristo wamekuwa ndio wanaolengwa, chanzo kikuu cha mgogoro uko mahali pengine, na kufanya hali hiyo kuwa ngumu zaidi kuliko vita vya kidini tu.

Rasilimali, ukosefu wa usawa na kutengwa kwa vijana

Katika jimbo la Cabo Delgado, Askofu Mkuu Saure aliakisi jukumu muhimu la maliasili katika kuchochea vurugu. Utajiri mkubwa wa gesi na madini katika eneo hilo umevutia mashirika ya kimataifa, lakini jamii za wenyeji mara nyingi hawafaidiki sana, na hivyo kuunda mazingira mazuri ya kutokuwa na utulivu. Umaskini, ukosefu wa ajira, na kutengwa hasa miongoni mwa vijana kumewafanya wawe katika hatari ya kuathiriwa na itikadi kali na kuajiriwa na vikundi vyenye silaha. Alitoa wito kwa Umoja wa Ulaya kuweka shinikizo kwa Serikali ya Msumbiji ili kuhakikisha uwazi, kupambana na ufisadi, na kuhakikisha kwamba misaada inawafikia wale walioathiriwa zaidi. Aliongeza kuwa msaada wa kijeshi unapaswa kuzingatia mafunzo badala ya kusambaza silaha tu.

Vita bado viko katikati yetu

Ingawa havionekani sana katika vichwa vya habari vya kimataifa, mgogoro ulioanza Oktoba 2017 bado haujaisha. Kulingana na Askofu Mkuu Saure, umebadilika tu katika hali yake. Miji mikubwa huko Cabo Delgado inaweza kuonekana kuwa salama kiasi, lakini hii imesababisha msongamano mkubwa wa watu huku wakimbizi wakifurika maeneo ya mijini wakitafuta usalama. Wakati huo huo, maeneo ya vijijini na vichaka yanabaki kuwa maeneo yenye migogoro yaliyo na vurugu na "vifo visivyo vya kibinadamu."

Kiwango cha mgogoro wa kibinadamu ni kikubwa na zaidi ya watu 6,000 wameuawa, na mamilioni wamehama makazi yao. Askofu Mkuu alisisitiza kwamba takriban 80% ya watu waliohamishwa ni wanawake na watoto. Maelfu ya watu waliohamia Nampula wanakumbwa na umaskini mkubwa. Wahamiaji wengi wanaishi na familia nyingine na kuifanya hali hiyo kuwa ngumu na hata kushindwa kujikimu kama familia.  Askofu Mkuu alikumbuka shambulio la 2022 huko Chipene, ambapo mtawa wa Italia Maria De Coppi aliuawa, tukio ambalo lilisisitiza kuenea kwa vurugu.

Kuhama, Magonjwa, na Kizazi Kilichopotea

Askofu Mkuu Saure alikosoa majibu kwa wahamiaji, akisema kwamba vituo vya makazi havijafanikiwa. Badala yake, alitetea suluhisho za makazi ya kudumu zilizojumuishwa ndani ya jamii za wenyeji. Msongamano na usafi duni katika maeneo yaliyoathiriwa vimesababisha milipuko ya mara kwa mara ya kipindupindu, haswa huko Nampula. Labda kinachotisha zaidi ni athari ya muda mrefu kwa watoto. Maelfu ya watoto waliokimbia makazi yao hawana hati za utambulisho na upatikanaji wa elimu. Bila shule au ulinzi, wanakuwa shabaha rahisi za kuajiriwa na makundi yenye msimamo mkali, na kuzua hofu ya "kizazi kilichopotea."

Kanisa, tumaini la utu wa binadamu

Katikati ya mgogoro huu, Kanisa Katoliki linaendelea kuchukua jukumu muhimu na mara nyingi halitambuliwi. Katika Cabo Delgado na Nampula, parokia zimekuwa vituo vya kimbilio vinavyotoa makazi bila ulinzi wa silaha, na utunzaji bila ubaguzi. Mwitikio wa Kanisa unaenea zaidi ya unafuu wa haraka. Linatoa msaada wa kisaikolojia kwa waathiriwa wa kiwewe, linasambaza misaada ya kibinadamu, na linafanya kazi ya kujenga upya uaminifu na mshikamano wa kijamii ndani ya jamii zilizovunjika.

Askofu Mkuu Saure alielezea dhamira hii kama yenye mizizi katika maadili ya Injili ya msamaha, huduma, na upendo mbele ya vurugu. "Jibu letu si chuki," alithibitisha, "bali msamaha, huduma na upendo." Pia aliangazia juhudi za mshikamano wa kimataifa kama vile mpango wa Hungary Helps, akizielezea kama "nuru" na "mwanga wa matumaini" kwa watu waliokimbia makazi yao. Hatimaye, ujumbe wa Askofu Mkuu ulikuwa wazi kwamba mgogoro kaskazini mwa Msumbiji hauwezi kutatuliwa kwa njia za kijeshi pekee. Amani ya kudumu inahitaji mbinu jumuishi inayoshughulikia dhuluma za kiuchumi, kuimarisha utu wa binadamu, na kuhakikisha kwamba maendeleo yanafikia hata waliotengwa zaidi.

Nigeria

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku:Just click here.

01 Aprili 2026, 15:46