Tafuta

Usiku huu wa Pasaka ni usiku Mtakatifu inapopigwa mbiu ya kutujulisha ushindi dhidi ya dhambi na mauti, Yesu Kristo ametoka kuzimu, ametoka mautini, ni mzima. Usiku huu wa Pasaka ni usiku Mtakatifu inapopigwa mbiu ya kutujulisha ushindi dhidi ya dhambi na mauti, Yesu Kristo ametoka kuzimu, ametoka mautini, ni mzima.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Tafakari Jumamosi Kuu: Kesha la Pasaka: Ukuu wa Fumbo la Wokovu

Ufufuko wa Kristo Yesu ni kilele cha ukweli wa imani ya Kikristo, ambayo jamii ya kwanza ya wakristo iliusadiki na kuuishi kama kiini cha ukweli; waliiendeleza kama msingi kwa njia ya Mapokeo; waliithibitisha kwa njia ya Maandiko ya Agano Jipya; na wakaihubiri kama sehemu muhimu sana ya Fumbo la Pasaka yaani: mateso na kifo cha Kristo Msalabani. Kristo amefufuka kwa wafu, kwa kifo chake alishinda dhambi na mauti na amewakirimia wafu uzima wa milele!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Fumbo la Wokovu wetu katika Kesha la Pasaka. Katekismu ya Kanisa Katoliki namba 1169 inatufudhisha kuwa; Pasaka ni sikukuu ya sikukuu, sherehe ya sherehe, kama Ekaristi ilivyo Sakramenti ya Sakramenti – sakramenti Kuu. Mtakatifu Athanasi anaiita Pasaka “Dominika Kuu”, kama Juma Takatifu linavyoitwa “Juma Kuu.” Na katika namba 1163 inasema hivi; “Mama Kanisa katika siku aliyoiita “Siku ya Bwana”, anaadhimisha kumbukumbu ya ufufuko wa Bwana pamoja na mateso yake yenye heri mara moja kwa mwaka katika sikukuu ya Pasaka iliyo kubwa kuliko zote. Anapoadhimisha namna hii mafumbo ya ukombozi huwafungulia waamini utajiri wa nguvu na mastahili ya Bwana wake. Kwa njia hii, uwepo wa mafumbo haya unakuwako kwa nyakati zote, ili kutoka humo waamini waweze kuchota na kujazwa neema ya wokovu.” Mkesha huu unatupa sababu ya Pasaka kuwa Sikukuu ya sikukuu, kuwa Dominika Kuu, kuwa ni Siku ya Bwana. Usiku huu wa Pasaka ni usiku Mtakatifu inapopigwa mbiu ya kutujulisha ushindi dhidi ya dhambi na mauti, Yesu Kristo ametoka kuzimu, ametoka mautini, ni mzima. Hivyo, mama Kanisa anatueleza maana ya usiku huu kwamba ni usiku wa kutoka katika hali ya upotevu na kuingia katika hali ya uzima wa Kimungu, na anatualika wanawe wote popote duniani, kukesha na kusali pamoja, kuyaadhimisha na kuyatukuza mafumbo yake, katika kesha hili katika sehemu kuu nne.

Mkesha wa Sherehe ya Pasaka ni Mama ya Mikesha Yote ya Kanisa
Mkesha wa Sherehe ya Pasaka ni Mama ya Mikesha Yote ya Kanisa   (Vatican Media)

Sehemu ya kwanza ya ni Liturujia ya Mwanga. Katika Liturujia hii, Kanisa linatafakari maajabu aliyolifanyia Mungu taifa lake tangu mwanzo kwa kubariki moto na kuutayarisha mshumaa wa Pasaka, tukimwomba Mungu atutie moto wa upendo wake kwa njia ya Mwanae, atujalie tuwake tamaa ya kwenda mbinguni, ili tuweze kuzifikia raha za heri yake ya milele kwa mioyo iliyotakata. Katika matayarisho ya mshumaa, Padre anauchora ishara ya msalaba kwa kalamu ya chuma. Kisha anauchora herufi za Kigiriki: Alfa - juu ya Msalaba, Omega - chini yake, kati ya mikono ya msalaba anachora tarakimu nne za mwaka husika akisema: “Kristo jana na leo, Mwanzo na Mwisho, Alfa na Omega, nyakati ni zake na karne pia, utukufu ni wake na enzi pia, daima na milele.” Baada ya kuuchora alama hizo, anauchomeka chembe tano za ubani kwa kuzipanga mfano wa msalaba, akisema: “Kwa majeraha yake matakatifu, na matukufu, Kristo Bwana wetu, utulinde na kutuweke salama.” Hii ni kuonyesha na kukiri ukuu na utakatifu wa msalaba ambao kwao wokovu wetu, Yesu Kristo alitundikwa juu yake, akafa, akazikwa na sasa amefufuka yu mzima ameshinda dhambi na mauti, ametuweka huru kutoka utumwa wa dhambi na mauti. Ishara ya ushindi wetu, ni mshumaa wa Pasaka, mwanga wa Kristo, uondoao giza la usiku, dhambi na mauti. Ndiyo maana mama Kanisa katika adhimisho hili, anausalimu na kuuheshimu Mshumaa huu ishara ya Kristo mfufuka, mleta uzima. Ni katika Mshumaa huu, inawashwa mishumaa ya wanaobatizwa kwa maji na Roho Mtakatifu, na katika mazishi, Mshumaa huu unaweka kando ya mwili wa marehemu katika jeneza, kuashiria kuwa Yesu Kristo ni uzima na ufufuo wa wafu.

Sehemu ya Kwanza ni Liturujia ya Mwanga
Sehemu ya Kwanza ni Liturujia ya Mwanga   (Vatican Media)

Sehemu ya Pili ni Liturujia ya Neno. Katika kesha hili, ambalo ni Mama ya mikesha yote Mama Kanisa ametuwekea Masomo kenda yakututafakarisha kuhusu Fumbo la Ukombozi wetu; saba ya Agano la Kale na mawili ya Agano Jipya – Waraka na Injili. Baada ya kupigwa mbiu takatifu, kutangaza ushindi, Padre anawaalika waamini kulisikiliza Neno la Mungu kwa makini ili kulijua vyema fumbo la ukombozi wetu tangu matayarisho yake katika Agano la kale na utimilifu wake katika Agano jipya na la milele akisema; “Tumeingia katika Kesha la Pasaka, sasa tusikilize neno la Mungu kwa moyo mtulivu. Tuwaze jinsi Mungu alivyolikomboa taifa lake wakati ulipowadia, na mwishowe akamtuma kwetu Mwanawe awe Mkombozi. Tumwombe Mungu wetu aifanikishe hii kazi ya wokovu wakati huu wa Pasaka, ili nasi tupate ukombozi kamili”. Masomo haya ni ya kusikiliza yote, ili kutambua historia ya fumbo hili la ukombozi kutoka Agano la Kale mpaka sasa katika Agano jipya, na kuliishi vyema. Ni katika muktadha huu Katekisimu ya Kanisa Katoliki namba 1096 na 1164 inatufundisha hivi; Liturujia ya Neno katika muundo wake ina asili yake katika sala ya Kiyahudi. Sala za Ekaristi zinachota pia uvuvio kutoka muundo wa mapokeo ya Kiyahudi. Wakristo na Wayahudi huadhimisha Pasaka; Pasaka ya historia huelekea mambo yajayo kwa Wayahudi; kwa Wakristo ni Pasaka iliyotimilizwa kwa kifo na ufufuko wa Kristo, ingawa daima ni katika kungoja utimilifu halisi. Katika liturujia ya Agano Jipya, kila tendo la kiliturujia, hasa adhimisho la Ekaristi na Sakramenti, ni mkutano kati ya Kristo na Kanisa. Kusanyiko la kiliturujia hupata umoja wake kutoka umoja wa Roho Mtakatifu anayewakusanya watoto wa Mungu katika Mwili mmoja wa Kristo. Zaidi sana, Taifa la Mungu, tokea Sheria ya Musa, lilijua sikukuu zisizobadilika kuanzia Pasaka, kwa ajili ya kukumbuka matendo mastaajabivu ya Mungu Mwokozi, kumshukuru na kudumisha kumbukumbu na kufundisha vizazi vipya ili mwenendo wao ulingane nazo. Nyakati za Kanisa, kati ya Pasaka ya Kristo Yesu iliyotekelezwa mara moja kwa nyakati zote na utimilifu wake katika ufalme wa Mungu, liturujia inayoadhimishwa katika siku zisizobadilika imejazwa kabisa upya wa fumbo la Kristo.

Sehemu ya Pili ni Liturujia ya Neno: Kusikiliza kwa makini Neno la Mungu
Sehemu ya Pili ni Liturujia ya Neno: Kusikiliza kwa makini Neno la Mungu   (@Vatican Media)

Sehemu ya Tatu ni Liturujia ya Ubatizo wa Wakatekumeni walioandaliwa wakati wa Kipindi cha Kwaresima. Kwa Sakramenti ya Ubatizo, wanazaliwa upya kwa Maji na Roho Makatifu, wanakufa kuhusu dhambi na kufufuka pamoja na Kristo ndiyo maana kabla ya adhimisho la Sakramenti hii Padre anawaalika waamini akisema; “Ndugu zangu, tuwasaidie kwa sala zetu hawa ndugu zetu wawe na matumaini ya wokovu. Na hapo watakapoijongea chemchemi ya uzima mpya, Baba Mwenyezi azidi kuwasaidia kwa huruma yake.” Kumbe ufufuko wetu huonekana na kudhihirishwa katika sherehe ya ubatizo. Wanaobatizwa huzaliwa upya katika Kristo, lakini hata tuliokwisha batizwa, tunashirikishwa huko kuzaliwa upya, kwa kurudia tena ahadi zetu za ubatizo. Kwa tendo hilo, umoja wetu na Kristo mfufuka huimarishwa. Mama Kanisa anapofafanua uhusiano uliopo kati ya Pasaka, Ufufuko wa Kristo Yesu na Sakramenti ya Ubatizo katika Katekisimu namba 1225 anasema hivi; Katika Pasaka yake, Kristo amewafungulia watu wote chemchemi ya ubatizo. Kwa kweli alikwisha ongea juu ya mateso yake ambayo angeteswa Yerusalemu kama ni “ubatizo” ambao yeye alipaswa kubatizwa nao. Damu na maji vilivyotoka ubavuni mwa Yesu aliyesulubiwa ni mifano ya Ubatizo na Ekaristi, sakramenti za uzima mpya: kutoka hapo inawezekana “kuzaliwa kwa maji na Roho ili kuingia katika Ufalme wa Mungu. Fundisho hili ndilo linalotuingiza katika sehemu ya nne na ya mwisho katika mkesha wa vijilia vya Pasaka, adhimisho la Ekaristi Takatifu.

Sehemu ya Tatu ni Liturujia ya Ubatizo
Sehemu ya Tatu ni Liturujia ya Ubatizo   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Sehemu ya Nnne: Liturujia ya Ekaristi Takatifu ambayo ni kilele na kiini cha adhimisho la fumbo la ukombozi wetu. Katekismu ya Kanisa Katoliki namba 1323, inafafanua fundhisho hili ikisema; “Mwokozi wetu, katika Karamu ya mwisho, usiku alipotolewa, aliweka sadaka ya Ekaristi ya Mwili wake na Damu yake. Alifanya hivyo ili kuendeleza sadaka ya msalaba siku zote mpaka atakaporudi, kusudi amwachie Bibi Arusi mpendwa, yaani Kanisa, ukumbusho wa kifo chake na ufufuko wake: sakramenti ya upendo, umoja, kifungo cha mapendo, karamu ya Pasaka ambamo Kristo huliwa, na roho hujazwa neema, na ambamo tunapewa amana ya uzima wa milele”. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali hivi; “Ee Bwana, tunakuomba uzipokee sala na dhabihu za taifa lako, ili hayo tuliyoanza kutenda katika mafumbo tupate uzima wa milele. Nayo sala ya utangulizi inalielezea ikisema; “Kristo ametolewa Pasaka yetu. Yeye ndiye Mwana kondoo wa kweli aliyeondoa dhambi za dunia, alishinda mauti yetu kwa kufa kwake, akaturudishia uzima wetu kwa kufufuka kwake. Na kwa sababu hiyo, watu wote wanaitukuza sikukuu ya Pasaka kwa furaha kubwa popote duniani”. Ni furaha kweli kweli, kwani “Kristo Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka”, “basi na tuifanye karamu kwa yasiyo chachika, ndio weupe wa moyo na kweli.” Huu ndio usiku tuliokombolewa kutoka utumwa wa dhambi. Ni usiku Mtakatifu. Ni usiku wa kuutangazia ulimwengu kuwa Kristo amefufuka yu hai. Ni usiku wa kuepuka nafasi za dhambi. Ni usiku wa amani, ni usiku wa kwenda mbio kuutangazia ulimwengu kuwa Bwana amefufuka. Ni usiku wa kutanga habari za kaburi kuwa wazi, Kristo amefufuka, yu mzima nasi tunamtambua katika kuumega mkate. Herini kwa Sherehe ya Pasaka.Tumsifu Yesu Kristo!

Kesha kuu la Pasaka 2026
03 Aprili 2026, 11:26