Tafakari Neno la Mungu Dominika ya Huruma ya Mungu: Kiri ya Imani
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya Pili ya Kipindi cha Pasaka. Kadiri ya mapokeo, kilatini dominika hii inaitwa “domenica in albis deponendis,” kwa sababu ni siku ambayo waliobatizwa katika Mkesha wa Pasaka walivuliwa kanzu nyeupe waliyovalishwa walipobatizwa ambayo walipaswa kuivaa katika katika kipindi chote cha Oktava ya Pasaka. Ni katika muktadha huu wimbo wa mwanzo unasema hivi: “Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa, yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu”, Aleluya (1Pet. 2:2). Ni “Dominika ya huruma ya Mungu”, kama ilivyowekwa na Mama Kanisa katika maadhimisho ya Jubilei Kuu mwaka 2000, kufuatia ufunuo alioupokea Mtakatifu Faustina Kowalska kutoka kwa Yesu Kristo mwenyewe. Ni katika Sakramenti ya kitubio huruma ya Mungu inajidhihirisha kwa waliobatizwa, wakaimarishwa kwa Roho Mtakatifu kwa Sakramenti ya Kipaimara na wanapokea Ekaristi Takatifu, Mwili na Damu ya Kristo, chakula cha kiroho. Mama Kanisa katika Katekisimu ya Kanisa Katoliki namba 1426 anafafanua hili fundisho akisema hivi; “Kumwongokea Kristo, kuzaliwa mara ya pili kwa ubatizo, kwa paji la Roho Mtakatifu, na kwa Mwili na Damu Azizi ya Kristo vinavyopokelewa kama malisho, hutufanya watakatifu na bila hatia mbele zake, kama Kanisa lenyewe, Mchumba wa Kristo, tukufu lisilo na hila wala kunyanzi mbele zake. Hata hivyo, maisha mapya yaliyopokewa katika sakramenti za kuingizwa katika Ukristo hayakomeshi udhaifu na ubovu wa hali ya kibinadamu, wala maelekeo kwa dhambi, yaitwayo katika mapokeo tamaa mbaya. Hali hizi zabaki katika mbatizwa, ili kwamba, kwa msaada wa neema ya Kristo waweze kujipima katika mapambano ya maisha ya Kikristo…kwa ajili ya utakatifu na uzima wa milele ambamo Bwana haachi kutuita.” Ni katika tumaini hili katika Sala ya mwanzo anasali hivi akituombea; “Ee Mungu mwenye huruma ya milele, unawasha imani ya taifa lako katika sikukuu hii ya Paska. Uwazidishie hiyo neema uliyowajalia wale waliobatizwa, wapate kuelewa vema kwamba wametakaswa kwa maji, wamepata uzima mpya kwa Roho, na kukombolewa kwa damu.”
Somo la Kwanza kutoka katika Kitabu cha Matendo ya Mitume (Mdo. 2:42-47). Ni simulizi la maisha ya Jumuiya ya kwanza ya Wakristo baada ya Pentekoste, wakiwa chini ya Mitume. Wakristo hawa waliishi maisha ya ushirika: walipendana, walisaidiana, walisali pamoja kuadhimisho fumbo la ukombozi, Pasaka, dominika baada ya dominika na kushiriki Ekaristi Takatifu, naye Bwana mfufuka alidhihirisha uwepo wake kwao popote walipokusanyika kama familia moja kiimani, akifanya miujiza kwa njia ya mitume. Licha ya mateso waliyoyapata, imani kwa Kristo mfufuka iliwapa nguvu ya kuyashinda, na kumshukuru Mungu kwa yote. Ni katika muktadha huu Zaburi ya wimbo wa katikati inasema hivi; “Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, kwa maana fadhili zake ni za milele. Israeli na aseme sasa, ya kwamba fadhili zake ni za milele. Mlango wa Haruni na waseme sasa, ya kwamba fadhili zake ni za milele. Wamchao Bwana na waseme sasa, ya kwamba fadhili zake ni za milele. Walinisukuma ili nianguke; Lakini Bwana akaisaidia. Bwana ni nguvu zangu na wimbo wangu, naye amekuwa wokovu wangu. Sauti ya furaha na wokovu imo hemani mwao wenye haki. Jiwe walilolikataa waashi, limekuwa jiwe kuu la pembeni. Neno hili limetoka kwa Bwana, nalo ni ajabu machoni petu. Siku hii ndiyo aliyoifanya Bwana, tutashangilia na kuifurahia” (Zab. 118: 1-4,13-15, 22-24).
Somo la Pili ni kutoka katika Waraka wa Kwanza wa Mtume Petro Kwa Watu Wote (1Pet. 1:3-9). Ni wosia kwa Wakristo waliokuwa wanadhulumiwa sababu ya Imani yao kwa Kristo. Mtume Petro anawasihi waweke matumaini yao yote kwa Kristo mfufuka, kwa maana ufufuko wake ni msingi wa kupata heri ya milele mbinguni. Hivyo, madhulumu na mateso wanayoyapitia si kitu kama wakiyalinganisha na heri ya milele watakayoipa. Hata sisi tunapaswa kuushuhudia ufufuko wa Kristo hata ikibidi kuteseka, ili mwishoni tukapate heri na utukufu kwa Mungu. Injili ni kama ilivyoandikwa na Yohane (Yn. 20 19-31). Nayo imegawanyika sehemu kuu tatu. Katika sehemu ya kwanza – 20:19-25 – inahusu Yesu mfufuka kuwatokea Mitume na kuweka Sakramenti ya Kitubio, Sakramenti ya Upatanisho, Sakramenti ya ondoleo la dhambi kwa kuwavuvia na kuwaambia; “Pokeeni Roho Mtakatifu. Wowote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wowote mtakaowafungia, wamefungiwa.” Mamlaka hayo wameyapokea Mapadre kutoka kwa mitume. Mama Kanisa akinukuu Maandiko Matakatifu katika Katekismu ya Kanisa Katoliki namba 1420-1421 anaeleza kwanini Yesu ameiweka Sakramenti akisema; “Kwa njia ya sakramenti za kuingizwa katika Ukristo, mtu hupokea uzima mpya wa Kristo. Lakini twauchukua uzima huu katika vyombo vya udongo nao hubaki umefichika pamoja na Kristo. Tumo bado katika makao ya duniani, tukielemewa na hali ya mateso, magonjwa na kifo. Uzima huu mpya wa mtoto wa Mungu waweza kudhoofika na hata kupotezwa kwa dhambi. Bwana Yesu Kristo…alitaka Kanisa lake liendeleze, kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, kazi yake ya uponyaji na ya wokovu... Hilo ndilo lengo la sakramenti za kuponya: Sakramenti ya Kitubio na Sakramenti ya Mpako wa wagonjwa.”
Na katika namba 1422-1424 anatufundisha akisema hivi; “Wanaoijongea Sakramenti ya Kitubio hupokea humo kutoka huruma ya Mungu ondoleo la kosa lililotendwa dhidi yake, na papo hapo hupatanishwa na Kanisa ambalo dhambi yao imelijeruhi, na ambalo kwa mapendo, mfano na sala huhangaikia wongofu wao. Sakramenti hii inaitwa Sakamenti ya wongofu kwa sababu hutekeleza kisakramenti wito wa Yesu wa wongofu, hatua ya kwanza ya kumrudia Baba baada ya kujitenga naye kwa dhambi…. Ni Sakramenti ya Kitubio kwa sababu hutakasa hatua za Mkristo mkosefu binafsi na za Kanisa, mintarafu wongofu, toba na malipizi ya dhambi… Sakramenti ya ungamo kwa sababu kukiri au ungamo la dhambi kwa kuhani ni jambo muhimu la sakramenti hii...yaani kukiri sifa ya utakatifu wa Mungu na huruma yake kwa mwanadamu mdhambi….sakramenti ya msamaha kwa sababu kwa njia ya ondoleo la dhambi kisakramenti atoalo kuhani, Mungu humpa mwenye kutubu msamaha na amani…Sakramenti ya Upatanisho kwa sababu yampa mwenye dhambi upendo wa Mungu anayepatanisha”.Katika sehemu ya pili – 20:26-29 – Yesu Mfufuka aliwatokea Mitume kwa mara ya pili, wiki moja baada kufufuka kwake, ndipo Tomaso alipokiri kiri kuu ya imani akisema; “Bwana wangu na Mungu wangu”. Kiri hii inaweka wazi kuwa Kristo mfufuka ni mtu kweli na ni Mungu kweli. Hii ndiyo kiri ambayo kanisa linaikiri katika Kanuni ya Imani kuwa Yesu Kristo ni Mungu kweli na Mtu kweli. Lakini pia ni katika jumuiya tunakutana na Yesu mfufuka. Tomaso alipokuwa nje ya jumuiya hakuweza kukutana na Kristo mfufuka. Lakini aliporudi ndani ya jumuiya alikutana naye na kuukiri umungu na ubinadamu wa Kristo. Nyakati zetu Kristo Yesu anajidhihirisha kwetu kwa njia ya sakramenti na neno la Mungu. Kwa kuwa Kristo amelikabidhi Kanisa lake sakramenti na Neno lake, vyote ni mali ya Kanisa, yaani Mwili wa Kristo Yesu.
Hivyo basi, tunalihitaji Kanisa na tunahitaji Jumuiya ya Kikristo ili kukutana na Kristo. Kumbe, tunao wajibu wa kuzitunza jumuiya zetu ziendelee kuwa ishara ya uwepo wa Kristo ulimwenguni ili watu wamtambue na kumkiri. Imani yetu kwa Bwana mfufuka inapaswa kutusaidia kujenga jumuiya ya Kikristo ambapo Kristo ndiye kiongozi wake mkuu. Hii ni jumuiya isiyo na ubinafsi, inayomjali kila mmoja, inayozingatia sala. Ni katika jumuiya ya namna hii, Bwana mfufuka anajifunua, na kuwakirimia wanaomwamini baraka na neema zake. Kama kuna shida au changamoto yoyote katika jumuiya, suluhisho si kujitenga, bali kutatua changamoto iliyopo. Kama umejitenga na jumuiya yako kwa sababu yoyote ile, rudi mapema, na ushiriki shughuli zake ili ukutane na Yesu Mfufuka upate neema na baraka tele. Na sehemu ya mwisho ya Injili ni 20:30-31, inatujulisha uwepo wa vyanzo vingine vya mafundisho ya Kanisa navyo ni mapokeo ya mitume, mababa wa kanisa na mitaguso yake. Hivyo hatupaswi kuwa na mashaka juu ya mafundisho ya Kanisa ambayo hayajaandikwa katika Bibilia kwani hayo tunayapata katika hivi vyanzo vingine. Heri yao wanaoyapokea na kuyaishi maana watapa uzima wa milele. Ni katika tumaini hili mama kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali hivi; “Ee Bwana, tunakuomba uzipokee sadaka za taifa lako, ili wote wanaoliungama jina lako na kubatizwa waifikie heri ya milele”. Nahili ndilo tumaini letu.