Tafuta

Msalaba wa Kristo Yesu ni chombo cha wokovu na utukufu wa Mungu. Msalaba wa Kristo Yesu ni chombo cha wokovu na utukufu wa Mungu.   (Vatican Media)

Tafakari ya Neno la Mungu: Ijumaa Kuu: Msalaba Ishara ya Wokovu

Badala ya kashfa na utupu, Msalaba unakua ni chombo cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu! Ni ishara ya mapendo, neema, sala, msamaha, upatanisho na matumaini. Ni kutokana na maana hii mpya, Mama Kanisa anaona fahari kuu kuutangaza utukufu na kuimba sifa kuu za Msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Msalaba unaendelea kumfunza mwamini kwamba, hakuna mapendo kamili yasiyokuwa na mateso na matumaini ya uzima wa milele!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Msalaba wa Kristo Yesu ni chombo cha wokovu na utukufu wa Mungu. Badala ya kashfa na utupu, Msalaba unakua ni chombo cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu! Ni ishara ya mapendo, neema, sala, msamaha, upatanisho na matumaini. Ni kutokana na maana hii mpya, Mama Kanisa anaona fahari kuu kuutangaza utukufu na kuimba sifa kuu za Msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Msalaba unaendelea kumfunza mwamini kwamba, hakuna mapendo kamili yasiyokuwa na mateso na matumaini ya uzima wa milele. Changamoto kwa waamini katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo ni kuuangalia, kuutafakari, kuushangaaa, kuusikiliza, kuuheshimu, kuutukuza na kuuabudu kwa imani, matumaini na mapendo, kwani ni kielelezo ambacho wokovu wa dunia umetundikwa juu yake! Fumbo la Msalaba wa Kristo Yesu yaani: Mateso, kifo na ufufuko wake ni kilele cha ufunuo wa: huruma, upendo, ukuu, utukufu na utakatifu wake, changamoto kwa Wakristo ni kushikamana pamoja na Kristo katika mapambano, ili siku moja waweze kushinda pamoja naye! Huu ndio ujumbe wa matumaini unaofumbatwa kwa namna ya pekee katika Fumbo la Msalaba, mwaliko kwa waamini kumtafakari Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kuwa ni kiini cha imani ya Kikristo. Fumbo la Msalaba ni alama ya upendo wa Mungu kwa binadamu; kielelezo cha sadaka ya hali ya juu kabisa ya Kristo Yesu dhidi ya ukosefu wa haki msingi za binadamu; ubinafsi, dhuluma na nyanyaso. Msalaba ni alama ya ushindi dhidi ya dhambi na kifo. Msalaba ni kielelezo cha mateso, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo wanaouwawa kikatili kwa kuchomwa moto wangali hai; na wakati mwingine nyanyaso na dhuluma hizi zinatendwa katika hali ya kimya kikuu.

Wokovu wetu umetundikwa juu ya Msalaba
Wokovu wetu umetundikwa juu ya Msalaba   (Vatican Media)

Tafakari ya Neno la Mungu, Ijumaa Kuu. Hii ni siku ambayo Kanisa haliadhimishi Sadaka ya Misa Takatifu, kwa sababu ni siku ambayo Yesu mwenyewe alijitoa Sadaka Msalabani, sadaka ya Agano jipya na la milele. Ibada ya siku hii imegawanyika katika sehemu kuu tatu. Sehemu ya kwanza ni liturujia ya Neno, kiini chake kikiwa ni simulizi la mateso na kifo cha Yesu Kristo, ambayo kwayo sisi tumepata wokovu kutoka utumwa wa dhambi. Ndiyo maana mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi; “Ee Mungu, kwa mateso ya Kristo Mwanao Bwana wetu, umetuondolea mauti tuliyorithi sisi binadamu kwa dhambi ya kale. Utujalie sisi tuliozaliwa na hali ya kibinadamu kwa maumbile, vivyo hivyo tuzaliwe na hali ya kimungu, kwa kutakaswa na neema yake.”  Sehemu ya Pili ni Kuuabudu Wokovu wa dunia uliotundikwa Msalabani, ndiye Yesu Kristo. Na sehemu ya tatu na ya mwisho ni Ibada ya Komunyo Takatifu. Somo la kwanza ni kutoka katika Kitabu cha Nabii Isaya (Isa. 52:13-53:12). Ni tafakari ya wasifu wa mtumishi wa Mungu aliyeteswa mateso mengi; uso wake uliharibiwa, hakuwa na umbo wala uzuri wa kumtamani, alidharauliwa na kukataliwa na watu wake, mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko, na hakuhesabiwa kuwa kitu. Yeye aliyachukua masikitiko yetu, akajitwika huzuni zetu, akajeruhiwa kwa makosa yetu, akachubuliwa kwa maovu yetu, adhabu yetu ikawa juu yake, na kwa kupigwa kwake sisi tumepona. Bwana aliweka juu yake maovu yetu yote. Alipoonewa, alinyenyekea, hakufunua kinywa chake mbele ya watesi wake. Alihukumiwa, akapigwa kwa sababu ya makosa yetu, na akafanyiwa kaburi pamoja na wabaya. Ingawa hakutenda jeuri, wala hapakuwa na hila kinywani mwake. Bwana aliridhia kumchukua amehuzunisha, akaifanya nafsi yake kuwa dhabihu kwa dhambi zetu. Kwa haki yake akawafanya wengi kuwa wenye haki, kwa kuyachukua maovu yetu kwa kumwaga nafsi yake, hata akafa ili sisi wakosaji tukombolewa kutoka utumwa wa dhambi na mauti. Mtumishi huyu aliweka tumaini lake lote kwa Mungu, naye akamwokoa na kila uovu na ubaya.

Ijumaa Kuu: Liturujia ya Neno, Kuabudu Msalaba na Komunyo Takatifu
Ijumaa Kuu: Liturujia ya Neno, Kuabudu Msalaba na Komunyo Takatifu   (Vatican Media)

Ni katika tumaini hili wimbo wa katikati unasema hivi; “Nimekukimbilia Wewe Bwana, nisiaibike milele, kwa haki yako uniponye, mikononi mwako naiweka roho yangu. Umenikomboa, Ee Bwana Mungu wa kweli. Kwa sababu ya watesi wangu nimekuwa laumu; Naam, hasa kwa jirani zangu. Na kitu cha kutisha kwa rafiki zangu; walioniona njiani walinikimbia. Nimesahauliwa kama mfu asiyekumbukwa; Nimekuwa kama chombo kilichovunjika. Maana nasikia masingizio ya wengi, hofu ziko pande zote. Lakini mimi nakutumaini Wewe, Bwana, nimesema, Wewe ndiwe Mungu wangu. Nyakati zangu zimo mikononi mwako, uniponye na adui zangu, nao wanaonifuatia. Umwangaze mtumishi wako kwa nuru ya uso wako; Uniokoe kwa ajili ya fadhili zako. Iweni hodari, mpige moyo konde, ninyi nyote mnaomngoja Bwana” (Zab. 31 :1, 5, 11-13a, 14-16, 24).Somo la Pili ni kutoka katika Waraka kwa Waebrania (Ebr 4:14-16; 5:7-9). Ni mausia ya kumwamini Yesu Kristo kuhani wetu mkuu aliyeonja na kuvumilia taabu na mateso kwa ajili yetu. Maana yeye anayefahamu taabu na matatizo yetu, daima yupo tayari kutuombea kwa Baba. Sharti ni hili; kuyashika maangano yetu tuliyofanya naye kwa njia ya ubatizo. Basi na tukikaribie kiti cha neema zake kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji yetu kwa njia yake yeye aliye Wokovu wetu. Injili ni kama ilivyoandikwa na Yohane (Yn. 18:1-19: 42). Ni simulizi la mateso na kifo cha Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyosalitiwa na Yuda, na kukamatwa kwake, na jinsi kesi yake ilivyoendeshwa kihuni na kwa uonevu mkubwa, kwa kuvunjwa kwa sheria nyingi, na hivyo kukandamizwa kwa mwenye haki na kuhukumiwa bila haki, adhabu ya kifo cha aibu kwa kusubuliwa msalabani, kwa sababu ya dhambi zetu.

Fumbo la Msalaba ni Ufunuo wa: Huruma, Upendo na Msamaha
Fumbo la Msalaba ni Ufunuo wa: Huruma, Upendo na Msamaha   (Vatican Media)

Ndiyo maana Katekismu ya Kanisa Katoliki namba 598 inasema hivi; “Kila mmoja mwenye dhambi ni sababu na chombo cha mateso ya Mkombozi wetu.” Lakini kifo chake – kama inavyofundisha Katekisimu ya Kanisa Katoliki (KKK 613-614) kikawa ni sadaka ya Pasaka kwa ukombozi halisi wa watu, maana Yeye ni Mwana kondoo aichukuaye dhambi ya ulimwengu, na sadaka ya Agano Jipya inayomweka mtu tena katika ushirika na Mungu, ikimpatanisha naye kwa njia ya damu yake iliyomwagika kwa ajili ya ondoleo la dhambi. Sadaka hii ya Kristo ni ya pekee, inatimiliza na kupita sadaka zote. Juu ya yote hii ni zawadi ya Mungu Baba mwenyewe aliyompa Mwanae kwa ajili ya kutupatanisha naye. Wakati huo huo ni sadaka ya Mwana wa Mungu aliyefanyika mtu, aliyetoa maisha yake mwenyewe, kwa hiari na mapendo kwa Baba katika Roho, kwa ajili ya kulipa kutotii kwetu. Hivyo hatuna budi kuutazama msalaba kwa moyo wa toba na majuto, kuomba msamaha na kuanza maisha mapya ya kumpendeza Mungu.

Sehemu ya Pili ni Kuabudu Msalaba Mtakatifu
Sehemu ya Pili ni Kuabudu Msalaba Mtakatifu   (Vatican Media)

Ni katika muktadha huu, sehemu ya Pili ya Liturujia ya Ijumaa Kuu ni Ibada ya Kuabudu Msalaba; Kuuabudu wokovu wetu, Yesu Kristo aliyetundikwa juu yake. Mama Kanisa katika Katekisimu namba 616 na 618, akinukuu Maandiko Matakatifu anatueleza kuwa sisi tunafanya tendo hili la kiibada kwa kuwa kwetu sisi msalaba wa Kristo ni alama ya wokovu, bendera na bango la ushindi dhidi ya dhambi na mauti. Msalaba wa Kristo ni sadaka yake, na zao la upendo wake kwetu sisi. Ni upendo usio na upeo, uliyoipa sadaka hii thamani ya ukombozi, malipo, fidia na kipatanisho. Msalaba ni sadaka ya pekee ya Kristo ambaye peke yake ni “mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu. Hivyo ni kwa njia ya msalaba sisi tumekombolewa. Ndiyo maana Mababa wa mtaguso wa Trento wanakiri na kusema; “Mateso yake matakatifu sana katika mti wa msalaba yametustahilia kuwa wenye haki” (KKK 617). Mtakatifu Yohane Paulo II anasema; “Msalaba siyo ishara ya kifo, bali uzima; siyo jambo la kutuvunja moyo, bali matumaini; siyo ishara ya kushindwa, bali ya ushindi”. Jogoo amekwisha wika mara ya tatu, tunaalikwa kujiweka chini ya msalaba pale tulipokosea, tufanye toba ya kweli na kuomba msamaha, kwani hatuna tumaini lingine, japo kwao wanaopotea msalaba ni kikwazo na upuuzi, kwetu sisi ni wokovu kama tukiutazama kwa imani na moyo wa toba.

Fumbo la Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu
Fumbo la Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu

Sehemu ya Tatu na ya Mwisho inayohitimisha maadhimisho ya Ijumaa Kuu ni Ibada ya Komunio Takatifu, tunda la mateso, kifo na ufufuko wake Kristo Yesu kama sala baada ya Komunio inavyosema; “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, wewe umetukomboa kwa kufa na kufufuka kwake Kristo Mwanao. Dumisha ndani yetu hiyo kazi ya huruma yako, ili tunaposhiriki fumbo hili, tuishi katika uchaji siku zote”. Kisha Kukomunika Mama Kanisa anahitimisha maadhimisho haya kwa sala ya kuwaombea watu akisali hivi; “Tunakuomba, ee Bwana, baraka zako nyingi ziwashukie watu wako, ambao wamekumbuka kufa kwake Mwanao na kutazamia kufufuka kwao. Wapate rehema, wajaliwe kitulizo, waongezewe imani takatifu, wathibitishiwe ukombozi wa milele.” Baada ya sala hizi waamini wote wanaondoka kimya kimya wakiyatafakari na kuyawaza-waza Mateso na kifo chake Yesu Kristo, mpaka siku ya Jumamosi Kuu, zitakapoanza sherehe za vijilia vya Pasaka. Hapo tena sherehe za kipasaka zitaendelea muda wa siku hamsini, mpaka Sherehe ya Pentekoste. Tumsifu Yesu Kristo!

tAFAKARI iJUMAA kUU 2026 ok

 

02 Aprili 2026, 16:12