Tafuta

Mtakatifu Rita wa Cascia Mama.mjane na mtawa Mwombezi. Mtakatifu Rita wa Cascia Mama.mjane na mtawa Mwombezi.  (ANSA)

Kard.Dziwisz,Cascia:Rita ni lulu ya thamani ya Umbria,karne nyingi imewavutia mahujaji

Katika kumbukizi ya Mtakatifu Rita wa Cascia,Mei 22,Kardinali Dziwisz alisema:Ingawa Rita aliishi karne sita zilizopita,ushuhuda wa maisha yake na utakatifu wake hauzeeki kamwe ulimwenguni kote.Askofu Mkuu wa Spoleto-Norcia,Jimbo Kuu linalojumuisha pia Cascia na Madhabahu ya Roccaporena,alikozaliwa Rita alikumbuka wakati wa sala na salia iliyotumiwa na wafungwa wa gereza la Spoleto 2025.

Angella Rwezaula na Roberta Barbi – Vatican.

Kila ifikapo tarehe 22 ya kila mwaka, Mama Kanisa anaadhimisha Mtakatifu Rita wa Cascia, mwombezi wa mambo yasiyowezekana, ambaye ulimwenguni kote anajulikana sana. Ni katika muktadha huo ambapo mji wa Cascia wa Umbria kama kila mwaka umekuwa na wakati mzuri wa kiroho katika kuadhimisha Mtakatifu Rita, ambapo katika madhabahu yake iliwakaribisha umati wa waamini waliofika kumsheherekea Mtakatifu wa Cascia, mwanamke, mama, mjane, na mtawa wa Kiagostiniani. Misa Takatifu iliongozwa na Kardinali Stanisław Jan Dziwisz,  Askofu Mkuu Mstaafu wa Krakow, Poland na aliyekuwa Katibu binafsi wa muda mrefu wa Mtakatifu Yohane Paulo II, lakini pia akishirikiana na Askofu Mkuu Renato Boccardo wa Jimbo Kuu la Spoleto-Norcia, Padre Joseph Farrell, Mkuu wa Shirika la Mtakatifu Agostino, na mapadre kadhaa waliofika kwa ajili ya hafla hiyo, watawa wengi wa Kiagostiniani, mamlaka za kiraia na kijeshi mahalia na waamini watu wa Mungu.

Kardinali Dziwisz

Kardinali Dziwisz

Kabla ya kuanza maadhimisho hayo aliyetoa utangulizi alikuwa Askofu Mkuu wa Jimbo hilo Boccardo ambaye alitoa salamu za dhati kwa Kardinali Dziwisz, akikumbusha huduma yake ndefu na ya uaminifu pamoja na Mtakatifu Yohane Paulo II. "Tunaomba uweke nia hizi zote madhabahuni na uzikabidhi, kwa niaba ya wote, kwa Mtakatifu Rita na Mtakatifu Yohane Paulo II," alisema Askofu Mkuu Boccardo, akisisitiza uhusiano wa kiroho unaounganisha Kardinali wa Poland na sura ya Papa Mtakatifu.

Ushuhuda wa maisha yake na utakatifu wa Mtakatifu Rita, hauzeeki

Katika mahubiri yake, Kardinali Dziwisz alitoa shukrani zake kwa Askofu Mkuu Boccardo kwa mwaliko huo, huku akikumbuka vifungo vya urafiki vilivyowaunganisha "tangu wakati Askofu Mkuu Renato alikuwa mshirika wa karibu wa Mtakatifu Yohane Paulo II, miongoni mwa mambo mengine kama mratibu wa Siku za Vijana Duniani na ziara za Kitume za Papa." Kardinali aliwapatia  huko Cascia, zawadi ya sala kutoka Krakow, huku akikumbuka jinsi hasa katika jiji hilo, mahali pa kuzaliwa kwa Yohane Paulo II na Mtakatifu Faustina Kowalska, sala zinatolewa kila mara kwa ajili ya nia ya Kanisa la ulimwengu na kwa ulimwengu ulio na matatizo katika nyakati zetu, ulioguswa na mikasa ya vita vya mauaji ya ndugu." Ingawa Rita aliishi karne sita zilizopita, Kardinali alisema, "ushuhuda wa maisha yake na utakatifu wake hauzeeki kamwe na unaendelea kuzungumza na mioyo yetu." Utakatifu unaotambuliwa na watu wa Mungu  ulimwenguni kote, ikiwa ni pamoja na Poland, ambao wakiongozwa na imani ya kimungu wanasadikishwa na maombezi ya ajabu na yenye ufanisi ya Mtakatifu Rita mbele ya kiti cha enzi cha Mungu.

Madhabahu ya Mtakatifu Rita

Madhabahu ya Mtakatifu Rita   (ANSA)

Kumweka Mungu katikati:“Tulitoka kwa Mungu na tunaenda kwa Mungu"

Akidadavua  kuhusu kifungu kutoka Kitabu cha Mithali, katika somo lilosomwa, Kardinali Dziwisz alielekeza kwenye hekima ya kweli ya kumweka Mungu katikati ya maisha kwamba: “Tulitoka kwa Mungu, na tunakenda kwa Mungu. Tunaweza na lazima tusikilize sauti Yake, tuzishike amri Zake, ili tusipoteze njia yetu na kufuata njia iliyonyooka kuelekea kukutana Naye katika ufalme Wake wa uzima na upendo.” Mojawapo ya vifungu vya mahubiri vyenye kugusa moyo zaidi vilihusu uwezo wa “Rita kuishi amri ya upendo hata katika hali zenye uchungu zaidi: kuelekea mume mwenye tabia ngumu, na hata kuelekea wale waliomtoa maisha na baadaye kutishia familia yake. "Hakukuwa na nafasi moyoni mwa Rita ya chuki na hamu ya kulipiza kisasi," Kardinali alisisitiza  huku akikumbuka maneno ya Mtakatifu Paulo kwa Warumi: "Msishindwe na uovu, bali shindeni ubaya kwa wema." Kardinali Dziwisz kisha akakumbuka mateso ya Rita kwa kifo cha watoto wake wawili, mateso "kama mama pekee anavyoweza kuyapata", huku akisisitiza jinsi mtakatifu hakujiruhusu kukata tamaa kwa sababu "aliunganisha mateso yake na mateso na Kalvari ya Yesu Kristo." Kwa njia hiyo, baada ya kupoteza familia yake yote, alichagua maisha ya wakfu kulingana na Kanuni ya Mtakatifu Agostino.

Waamini katika Madhabahu ya Mtakatifu Rita

Waamini katika Madhabahu ya Mtakatifu Rita

Siri ya Mt. Rita:alijenga maisha yake juu ya Mwamba Yesu Kristo

Kwa kutazama taswira ya kiinjili ya mzabibu na matawi, Kardinali alielezea siri ya maisha ya Mtakatifu Rita kuwa: “Alijenga nyumba ya maisha yake juu ya mwamba ambao ni Yesu Kristo. Aliishi kwa umoja wa karibu naye. Na akaongeza: "Bila Yeye, tunanyauka, kama tawi lililokatwa kutoka kwenye mzabibu. Bila Yeye, bila Yesu, hatujui tunaishi kwa ajili gani au tunaelekea wapi." Kifungu kilichowekwa wakfu kwa mafundisho ya Mtakatifu Yohane Paulo II kuhusu Mtakatifu Rita kilikuwa cha kugusa moyo sana. Kardinali alikumbuka barua ambayo Papa wa Poland aliandika mwaka 1982, wakati wa kuadhimisha miaka mia sita ya kuzaliwa kwa mtakatifu, na mkutano wa Jubilei Kuu ya 2000, wakati katika kuadhimisha miaka mia moja ya kutangazwa kwake mtakatifu ambapo masalia ya Rita yaliletwa kwenye Uwanja wa Mtakatifu Petro.

Kitanda cha Mtakatifu Rita wakati akiwa mdogo

Kitanda cha Mtakatifu Rita wakati akiwa mdogo

Kardinali Dziwisz alinukuu maneno ambayo Yohane Paulo II alielezea "jeraha la mwiba" kwenye paji la uso la Rita kama muhuri wa mateso yake ya ndani na zaidi ya yote uthibitisho wa ushiriki wake wa moja kwa moja katika Mateso ya Kristo. Na alikumbuka jinsi ambapo Mtakatifu Yohane Paulo II alivyomjumuisha mtakatifu miongoni mwa wanawake Wakristo walio na ushawishi mkubwa katika maisha ya Kanisa, akisisitiza jinsi Rita alivyotafsiri vyema 'kipaji cha kike,' akikiishi kwa bidii katika umama wa kimwili na kiroho: "Nina uhakika, hata  leo pia Papa Mtakatifu anaungana kiroho nasi hapa Cascia, anafurahia uwepo wetu na sala zetu hapa, na anatubariki kutoka juu," alisisitiza.

Wanawake wawe na tumaini wanapokumbana na changamoto kama Rita

Kardinali  mwishoni  aliwaalika waamini kumfanya Mtakatifu Rita kuwa ishara ya matumaini, hasa kwa wanawake wanaopambana na magumu, mateso, na changamoto za maisha ya kila siku.  Kardinali aidha alimkabidhi Bwana Kanisa la ulimwengu wote, ambalo mchungaji wake amekuwa Baba Mtakatifu Leo XIV kwa mwaka mmoja huku akisisitiza ukaribu kati ya roho ya kiagostino na Papa kwa, ambayo inawaunganisha na Mtakatifu Rita, na kile ambacho watawa wa Kiagostiniani wote wanashiriki. Ombi la amani lilikuwa kwamba: "Tumwombe Bwana amani, hasa katika Ukraine inayoteswa na Mashariki ya Kati." Sherehe  kwa hiyo ilihitimishwa kwa  maombi kwa Mama wa Upendo Mzuri, kwa Mtakatifu Rita wa Cascia, na kwa Mtakatifu Yohane Paulo II,  kwa kuwaomba waombee mahitaji ya Kanisa na ulimwengu.

“Leo, mtakatifu wa yasiyowezekana amekusanya kuzunguka Patakatifu pake Kanisa la mahujaji, lililojeruhiwa na vita vya wakati wetu lakini bado lina uwezo wa matumaini, akifuata mfano wa mwanamke huyo rahisi lakini mkuu ambaye akiwa na mizizi ndani ya upendo wa Kristo, alipata katika imani yake isiyotikisika nguvu ya kuwa mwanamke wa amani katika kila hali."

Maandamano wakati wa sherehe za Mtakatifu Rita

Maandamano wakati wa sherehe za Mtakatifu Rita   (ANSA)

Ushuhuda wa Askofu Mkuu Renato kuhusu Gereza la Spoleto

"Gereza daima ni mahali pa mateso lakini pia pa matumaini, na kuwa na ishara ya uwepo wa Mtakatifu Rita miongoni mwa wanadamu waliojeruhiwa wakijaribu kurekebisha makosa yao kulikuwa jambo la kugusa moyo kweli." Hivi ndivyo Askofu  Mkuu Renato Boccardo, wa Jimbo Kuu la  Spoleto-Norcia, alivyokumbusha akizungumza na vyombo vya habari vya Vatican wakati wa tafakari na sala alioyoongoza Novemba mwaka 2025, wakati wa Jubilei Kuu ya Matumaini, ndani ya gereza la Spoleto kwamba: “Ilikuwa fursa kwa wafungwa kukabidhi kwa maombezi ya Mtakatifu,  kila kitu walichokuwa nacho mioyoni mwao. Waliguswa sana na mkutano huo, ambao ulikuwa chanzo cha matumaini hata kwa wale wanaotumikia kifungo cha maisha."

Ujumbe wa mtawa wa Kiagostino kwa walionyimwa uhuru wa kibinafsi

Uhuru wa ndani, unaoeleweka kama uwezo wa kukuza hamu ya mema bila kuathiriwa na shinikizo la nje au kumbukumbu za zamani: Huu ni ujumbe wa wakati unaofaa ambao Mtakatifu Rita anawapa wafungwa, kulingana na Askofu mkuu: "Mwanadamu si tu uhalifu wake, kama vile yeye si tu matendo yake: kuna hisia nzuri ndani ya moyo wa kila mtu, hata wale wanaoonekana kuwa waovu zaidi au wamefanya matendo mabaya zaidi. Mtakatifu huonyesha mema ndani ya kila mmoja wetu."

Mtakatifu wa mambo yasiyowezekana

Labda hii pia ndiyo sababu wafungwa wengi gerezani wamejitolea sana kwa mtawa wa Kiakostininai wakikaribisha masalia yake kama "ziara kutoka kwa mmoja wa familia:"Katika vyumba vingi niliwaona wafungwa wakiwa wameshika sanamu ndogo ya Mtakatifu," Askofu Mkuu  Boccardo aliendelea: "Wengi wao waliniambia walizungumza naye ili awakabidhi watoto wao, wajukuu, au wanafamilia ambao hawawaoni mara nyingi kwake, au waliomba waweze kudumisha nafasi yao katika familia, ingawa walikuwa mbali." Miaka michache iliyopita, picha katika kalenda iliyotengwa kwa ajili ya Mtakatifu zilikuwa zimejazwa na waridi za plastiki zilizotengenezwa na mfungwa. Waridi hizi zilipamba maeneo yanayohusiana na Rita kwa muda na sasa zimehifadhiwa katika vyumba vya mahali Patakatifu.

Sherehe za Mtakatifu Rita

Sherehe za Mtakatifu Rita

Huduma ya Kichungaji Gerezani:Uwepo wa Kusikiliza

Askofu Mkuu Boccardo alieleza kwamba Jimbo Kuu  lina Padre ambaye anajali gereza la ndani kwa kushirikiana na Caritas: "Uwepo wetu ni zaidi ya yote kusikiliza, kwa sababu wafungwa wanahitaji kushiriki hadithi zao na kusikilizwa, sio kuhukumiwa," anafichua. Ni wazi, pia kuna mahitaji ya kimwili yanayopaswa kutimizwa.

Kwa Papa na Mwenge wa Msamaha na Amani

Jumatano tarehe 20 Me 2026 Askofu Mkuu  Boccardo alipeleka Mwenge wa Msamaha na Amani kwa Papa mara baada ya Katekesi katika Uwanja wa Mtakatifu Petro. Mwenge huo uliwashwa huko Chicago katika Parokia iliyotengwa kwake ambaye inahudumiwa na Wanashirika Waagostiniani na pia ulipitishwa mahali alipozaliwa Papa Leo XIV mnamo mwezi Machi iliyopita. "Papa alituhimiza kutekeleza ujumbe tulioachiwa na Mtakatifu, ambaye, licha ya kuwa mbali na wakati, bado yuko karibu sana na wengi waliojitolea kwake," Askofu mkuu. Kabla ya kuwa mtawa, alikuwa mke na mama na alipitia matukio ya vurugu, kama vile vifo vya watoto wake, na mivutano ya kifamilia. Anatushirikisha haya yote leo.  Mahujaji wanaotembelea Cascia na Roccaporena kila mwaka hujitambulisha naye na kujifunza kutoka kwake jinsi ya kukabiliana na magumu haya ya maisha."

Kikanisa cha Kilimani alipokuwa akisali Mtakatifu Rita

Kikanisa cha Kilimani alipokuwa akisali Mtakatifu Rita   (Opera di Santa Rita)

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.

23 Mei 2026, 13:35