Tafuta

2024.03.18 Vincent Gélot- directeur Syrie/Liban de l'Œuvre d'Orient 2024.03.18 Vincent Gélot- directeur Syrie/Liban de l'Œuvre d'Orient 

L’Œuvre d'Orient:Ni miaka 170 tangu kuwa karibu na Jumuiya za Kikiristo za Mashariki

Chama cha upendo cha Ufaransa kinasaidia watu katika nchi 20.Katika kumbukizi ya miaka 170 iliyofanyika Dominika tarehe 10 Mei 2026,Ibada ya misa iliadhimishwa huko Paris katika Kanisa Kuu la Mama Yetu,iliyoongozwa na Kardinali Claudio Gugerotti,Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Makanisa ya Mashariki.Katika ujumbe kutoka kwa Papa,uliosainiwa na Kardinali Parolin,alitoa shukrani na kutia moyo kwa kazi iliyofanywa.

Janvier Yameogo na Francesco Ricupero – Vatican.

“Kila mwaka, L'Œuvre inasaidia mamia ya mipango muhimu ya maisha ya Jumuiya, shukrani kwa maelfu ya wafadhili ambao ningependa kuwapongeza kwa ukarimu wao usio  choka. Msaada wenu katika elimu ya watoto na vijana, pamoja na watawa na mapadre wa siku zijazo, msaada wenu wa thamani wa kibinadamu,na uhifadhi wa urithi wa Kikristo unawakilisha chanzo kisichopimika na muhimu cha msaada kwa watu hawa ambao, kutokana na migogoro na vita, hukata tamaa na wakati mwingine huhisi wamesahaulika.” Haya ni maneno yaliyomo katika ujumbe kutoka kwa Papa Leo XIV, uliosainiwa na Katibu Mkuu wa Vatican  Kardinali Pietro Parolin, uliotumwa na kusomwa wakati wa Ibada ya  Misa iliyoadhimishwa Dominika tarehe 10  Mei 2026  katika Kanisa Kuu la Notre Dame jijini Paris, nchini Ufaransa  wakati wa maadhimisho ya miaka 170 ya chama cha Ufaransa cha “L'Œuvre” kwa ajili ya Mashariki, ambacho kinawaunga mkono Wakristo wa Mashariki na watu wa eneo hilo katika zaidi ya nchi 20.

Misa hiyo iliongozwa na Kardinali Claudio Gugerotti, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Makanisa ya Mashariki, mbele ya Askofu Mkuu wa Paris, Laurent Ulrich, na Monsinyo Hugues de Woillemont, Mkurugenzi Mkuu wa chama hicho. Katika ujumbe wa Papa uandelea "Jueni kwamba sala na matendo yenu yana thamani kubwa machoni pa Mungu, kama vile wale wanaofaidika nayo na ambao, bila msaada wenu, wangehatarisha kutoweka kutoka katika nchi hizi zilizobarikiwa."

Nyakati za Udhaifu Mkubwa

Haja ya kutoa msaada, lakini zaidi ya yote kujenga uhusiano na Makanisa ya Mashariki, ambayo yanakabiliwa na nyakati za udhaifu mkubwa, ilijadiliwa katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Jumatatu tarehe 11  Mei 2026, huko Paris. Haya  yalielezwa na Askofu Mkuu wa Aleppo, Hanna Jallouf, Vincent Gelot, mkurugenzi wa kikanda wa  Chama hicho cha “Œuvre d'Orient “kwa Lebanon na Siria, na Sr Magda Smet, wa Shirika la  Dada Wadogo wa Nazareti wanaotoa huduma katika kambi ya Dbayeh ya Lebanon. Kwanza kabisa, kuwashukuru waandishi wa habari kwa mchango wao mkubwa katika "kuongeza uelewa wa umma kuhusu hali ya Makanisa ya Mashariki, ambayo yanakabiliwa na nyakati za udhaifu mkubwa, ikiakisi idadi ya waliokimbia makazi yao, waliokufa, waliojeruhiwa, na waliopotea," Mkurugenzi mkuu wa chama hicho, Monsignor Hugues de Woillemont, aliendelea, "Wakristo wa Mashariki hawahitaji huruma yetu, bali shukrani zetu kwa ushuhuda wanaotoa na ambao tunaweza kujifunza kutokana nao." Kisha alisisitiza kwamba maadhimisho haya ni fursa ya kutoa shukrani za dhati kwa wafadhili binafsi na taasisi. "Ni urafiki tunaoshiriki.

Wakristo ni chumvi,chachu na nuru katika jamii

Katika hotuba yake kwa Kiarabu, Askofu Jallouf alitoa shukrani zake kwa ‘L’Œuvre d’Orient’ kabla ya kushirikisha ushuhuda wake. "Huko Aleppo, kulikuwa na Wakristo zaidi ya 300,000; ni 30,000 pekee waliosalia kutokana na vita na hofu." Hata hivyo, Askofu huyo alilaani taarifa potofu zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii, akibainisha kuwa idadi ya hivi karibuni ya "vifo 3,000 vya Wakristo, wakati kiukweli idadi hiyo ni 13." Ushuhuda wake pia ulionesha jukumu la Wakristo kama chumvi, chachu, na nuru katika jamii, akisema kwamba "haogopi waamini wa kweli wa Kiislamu, bali wale wenye msimamo mkali."

Wakati wa mkutano na waandishi wa habari, Kardinali Gelot alifafanua uchunguzi wa Askofu Jallouf kuhusu hali nchini Siria, akizungumzia nchi iliyoathiriwa na kiwewe, ya idadi ya watu walioharibiwa kabisa, na akibainisha kuwa katika miaka 15, asilimia 80 ya Jumuiya ya Wakristo wa asili ya Siria imetoweka." Kisha akazindua wito wa haraka kwa jumuiya ya kimataifa "kusaidia kuhifadhi mchanganyiko huu wa utofauti wa kikabila na kidini na wingi unaounda jamii za Siria.”

Vurugu nchini Lebanon

Sr Magda alilenga mawimbi mapya ya vurugu nchini Lebanon. "Kelele kubwa za ndege ni ngumu sana kuvumilia na huongeza msongo wa mawazo kwa idadi ya watu. Jumuiya yetu," alisema, "ni mahali ambapo kila mtu anakaribishwa; kila mtu anatafuta muda wa kupumzika, mahali ambapo wanaweza kuomba msaada bila aibu, watu waliokimbia makazi yao na wakimbizi. Shukrani kwa L'Œuvre d'Orient, tunaweza kusaidia na kutoa msaada. Hali hii inazilemea familia sana; kuna visa vya mfadhaiko, mzigo ni mzito sana. Tunashukuru sana kwa msaada na maombi, kwa matumaini ya kuishi katika ulimwengu wa amani." Mkutano huo na waandishi wa habari pia ulijumuisha utafiti uliofanywa na Ifop (Taasisi ya Maoni ya Umma ya Ufaransa) ambao uligundua kuwa Ufaransa inabaki kuwa "chanzo muhimu cha msaada" kwa Wakristo katika Mashariki ya Kati.

Imesasishwa tarehe 15 Mei 2026 saa 6.30 mchana na Angella Rwezaula 

 

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.

 

15 Mei 2026, 10:50