Tafuta

2026.05.20 Padre Luigi Pugliese,Msimamizi wa Madhabahu ya Kijimbo ya ‘Ave Maria Gratia Plena’ huko Giugliano Jimbo la Aversa,katika moja ya sherehe za Maria 2026.05.20 Padre Luigi Pugliese,Msimamizi wa Madhabahu ya Kijimbo ya ‘Ave Maria Gratia Plena’ huko Giugliano Jimbo la Aversa,katika moja ya sherehe za Maria 

Madhabahu ya Ave Maria Gratia Plena:moyo wenye hofu unaokuja kwa Maria,unapata faraja na amani

“Giugliano inapitia mwezi wa Maria unaoendelea mwaka mzima.Naweza kutambua uhusiano uliopo kati ya mtu na Yeye ni sawa na ule wa mtoto kwa Mama yake.Siku chache baada ya Pompei na Napoli,Papa atatembelea Acerra.Kwa wale tunaoishi janga la ardhi hii,kujua jinsi masuala fulani yanavyothaminiwa na Baba Mtakatifu yanatujaza matumaini na furaha.Alisema hayo Padre Luigi Pugliese,Msimamizi wa Madhabahu ya Ave Maria Grazie Plena katika mahojiano na Vatican News.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Mwezi wa Mei kwa kawaida huwekwa wakfu kwa ajili ya Bikira Maria, kwa hivyo watu wa Mungu ulimwenguni kote husali sala rahisi ya Rosari Takatifu kila siku, wakifanya hija nyingi kwenye madhabahu mbalimbali ya kijimbo, kitaifa, na kimataifa na kufanya sherehe za kiutamaduni. Kuna madhabahu mengi yanayojulikana ulimwenguni kote,  lakini pia yale ambayo hayajulikani sana, bali katika ngazi za kijimbo. Katika ulimwengu ambapo tunahitaji amani, Vatican News ilimhoji Msimamamizi wa Madhabahu ya  kijimbo ya Maria "Ave Maria Gratia Plena" huko Giugliano Jimbo la  Aversa, Napoli, Mkoa wa Campagna.

Madhabahu ya Ave Maria Gratia Plena
Madhabahu ya Ave Maria Gratia Plena

Katika mahojiano hayo alieleza jinsi ambavyo mwaka huu anasherehekea miaka 25 ya ukuhani, na pia uzoefu wa madhahabu hiyo kwamba, "Maria anahisiwa kama mama, tunamgeukia katika milima ya furaha na huzuni ya maisha yetu binafsi na ya jamii, tunajikabidhi kwake kwa kila hatua ya maisha yetu." Msimamizi  huyo pia  anaelezea mahali hapo patakatifu kama "mwanga wa matumaini katika nchi iliyo na uwepo wa mtandao wa wahalifu," wakati huo huo, "nchi inayoitwa ya moto, bila ukosefu  wa visa vya saratani katika kila nyumba, vile vile kuna ugumu mkubwa wa kiuchumi kutokana na ukosefu wa kazi na matarajio ya siku zijazo, na lazima pia tukubali kuanguka kwa urahisi katika mtandao wa wahalifu kwa vijana wengi sana, wasio na uhakika mbele ya mustakabali wa ajabu kama huo." Hapa chini runachapisha mahojiano kamili.

Ndani ya Madhabahu ya Ave Maria Gratia Plena
Ndani ya Madhabahu ya Ave Maria Gratia Plena

Ni mwezi wa Maria, na katika parokia yako kuna utamaduni wa kale unaohusishwa na Madhabahu ya Mama wa Amani. Je, unaweza kuelezea kwa ufupi asili ya historia yake? Je, Madhabahu iko sehemu gani ya Italia?

Habari za asubuhi, mimi ni Padre Luigi Pugliese, Mkuu wa Madhabahu ya Maria Kijimbo ya "Ave Maria Gratia Plena" huko Giugliano, jimbo la Aversa, Napoli Mkoa wa Campagnia. Ninajiandaa kusherehekea maadhimisho yangu ya mika ishirini na tano ya ukuhani wangu, na ninaweza kushuhudia kwa moyo wote kwamba, kama mzaliwa wa Giugliano, katika asili yangu na ile ya familia yangu, sina kumbukumbu ya safari yangu ya imani ambayo haihusiani na maisha ya Madhabahu hii hapa, na kwa uso wa Bikira Maria, anayeitwa hapa kama Malkia wa Amani. Kumbukumbu ambazo zinalindwa kwa wivu, kama hazina ya kweli ya watu wa Giugliano. Giugliano inauishi mwezi wa Maria katika mwelekeo  ndani ya mwaka mzima. Leo hii ninapokuwa ninatoa huduma yangu kama Msimamizi wa mahali hapa palipobarikiwa na uwepo wa Maria kwa miaka mitatu, ninaweza kutambua kwamba uhusiano tulionao naye ni sawa na ule wa mtoto kwa Mama yake. Hapa Maria anahisiwa kama mama, tunamgeukia katika nyakati za furaha na huzuni za maisha yetu binafsi na ya kijamii, tunajikabidhi kwake kwa kila hatua ya maisha yetu. Historia ya mahali hapa ni ya kale sana.

Maadalizi makubwa ya sherehe ya Mama wa Amani huko Giugliano
Maadalizi makubwa ya sherehe ya Mama wa Amani huko Giugliano

Matukio yanayomzunguka Bikira Mtakatifu yameashiria historia ya ardhi hii kwa zaidi ya karne sita. Hasa: Asili ya ibada ya Bikira Maria wa Amani (iliyoitwa hivyo kwa sababu iliwezesha upatanisho wa familia mbili za kifalme zenye uadui) inahusishwa na ibada ya kale maarufu inayohusiana na ugunduzi wa sanamu inayomwonesha Bikira, ambayo kuna maoni tofauti kuihusu. Kulingana na baadhi ya wasomi, kiukweli, sanamu ya Mama ilikuwa mojawapo ya  nyingi zilizotupwa baharini mwaka 1453, kufuatia na kuanguka kwa Ufalme wa  Constantinople kwa Waturuki. Kwa kuokotwa na malaika (yaani wavuvi), ilibebwa hadi ufukweni mwa Cumae na, ikipatikana na baadhi ya mabaharia, ilibebwa mabegani mwao hadi mjini ili kuwekwa katika Kanisa la kwanza walilokutana njiani, lile la Annunziata. Kwa hivyo, kulingana na historia hii, sanamu ina asili ya Byzantine, ikianzia mwanzoni mwa karne ya 15 na ilifika Giugliano miaka michache baada ya 1450.

Maandalizi ya sherehe ya madhabahu ya Ave Maria Gratia Plena
Maandalizi ya sherehe ya madhabahu ya Ave Maria Gratia Plena

Hata hivyo, wengine, waliofuata toleo la mafunzo zaidi, wanaamini sanamu ya Bikira ilisafirishwa na kundi la mabaharia na kupatikana na wakulima wawili walipokuwa wakilima ardhi yao. Baada ya kupakia sanamu hiyo kwenye mkokoteni ili kuipeleka Giugliano, wakulima walilazimishwa na ng'ombe kusimama katika kile ambacho sasa ni Uwanja wa  Annunziata. Na ndiyo maana hapo palijengwa madhabahu ya Annunziata, ambapo Kanisa liliwekwa wakfu kwa ajili ya Maria Mtakatifu sana wa Amani  na mahali  ambapo sanamu yenye rangi ya udongo inaonyesha Mama akiwa na Mtoto magotini mwake, imehifadhiwa. Leo, si kila kitu kiko wazi katika historia ya Chama cha Mama Yetu wa Amani na Kanisa Kuu; maswali mengi, mashaka, na kutokuwa na uhakika bado yanabaki, yakichochewa na mapengo yaliyoachwa na wakati katika Hati.  Karibu bila shaka, vifungu vingi ambavyo hatuvielewi kwa sasa vingekuwa wazi ikiwa kumbukumbu za kihistoria za madhabahu ya  Annunziata hazingepotea kutokana na moto mbaya wa mnamo 1662.

Siku Kuu ya Mama wa Amani ni tukio kubwa katika eneo hilo la Giugliano
Siku Kuu ya Mama wa Amani ni tukio kubwa katika eneo hilo la Giugliano

Siku kuu ya Mama Yetu wa Amani huadhimishwa lini?

Sherehe za kiutamaduni, zilizoandaliwa na Chama cha  Mama Yetu wa Amani na kamati yake, huanza usiku wa kuamkia Pentekoste na kumalizika Dominika  inayofuata, ya sherehe ya Utatu Mtakatifu. Jumatatu baada ya Pentekoste, Mama Yetu hubebwa kwa maandamano na waamini kupitia mitaa ya kituo cha kihistoria, juu ya gari la kukokotwa na ng'ombe, wakati mwingine umbo la meli. Mojawapo ya nyakati za dhati za sherehe hiyo ni kile kinachoitwa "Kushuka  kwa Malaika," wakati katika Uwanja wa  Annunziata, msichana mdogo aliyevaa nguo kama malaika, akiwa ameshikiliwa kwenye nyaya imara, ananing'inizwa hewani kati ya majengo mawili yapata mita thelathini juu ya ardhi. Msichana huyo, akiimba wimbo wa kiutamaduni kwa heshima ya Mama Yetu wa Amani, anaachilia njiwa na kushushwa kwenye gari la Mama Yetu wa Amani, ambapo anaweka shada la maua.

Gari mfano wa Meli  inayobeba sanamu ya Bikira Maria
Gari mfano wa Meli inayobeba sanamu ya Bikira Maria

Kwa hakika hatuwezi kupuuza marejeo ya maandiko matakatifu kuhusu Maria pamoja na wanafunzi waliokusanyika katika sala katika Chumba cha Juu  cha Karamu Kuu wakati Roho Mtakatifu alishuka ghafla, akitulia juu yao kama miali ya moto. Kile kinachoadhimishwa siku ya Pentekoste kimeashiria maisha ya imani ya watu wetu, kikiwa kimeunganisha sherehe hizo kwa heshima ya Mama Yetu na Jumatatu inayofuata Sherehe. Katika Wosia wa Baba Mtakatifu Francisko ulikuwa wa furaha kubwa wakati, mwaka 2018, alipoanzisha siku kuu ya Maria, Mama wa Kanisa, akiiweka katika kalenda ya kiliturujia Jumatatu ya Pentekoste, huku akifufua jina la Maria lililopewa na Mtakatifu Paulo VI mwaka 1964.

Siku kuu hii inamsherehekea Maria si tu kama Mama wa Kristo, bali kama mama wa kiroho wa waamini wote na wa mwili mzima wa fumbo ambalo ni Kanisa. Hatuwezi kushindwa kusisitiza uhusiano wa karibu kati ya kuzaliwa kwa Kanisa, ambao ulitokea siku ya Pentekoste na kushuka kwa Roho juu ya wanafunzi katika Chumba cha Juu cha Karamu Kuu, na uwepo wa mama Maria, kama ilivyoelezwa katika Matendo 1:14: “Wote kwa moyo mmoja walidumu katika kusali, pamoja na wanawake na Maria mama yake Yesu, na ndugu zake.” Tunawezaje kushindwa kutafsiri upya historia yetu na ile ya eneo letu, hasa kwa kuzingatia kukumbu kumbu ya kibiblia, tamaduni ya Kanisa, na uchaji wa watu wengi? Tamko rasmi la Baba Mtakatifu hakika lilizingatia haya yote, na sisi, katika tamaduni ya madhabahu yetu, ndiyo ya kwanza kushuhudia hili.

Mtoto mdogo kama Malaika hushuka kuweka shada la Maria
Mtoto mdogo kama Malaika hushuka kuweka shada la Maria

Ni namna gani wakazi wanaendeleza utamaduni huu mzuri wa Mama Yetu wa Amani?

Leo, hii katika madhabahu ni mahali pa kurejea watu wacha Mungu, ambapo mioyo isiyotulia, inayopelekwa kwa Maria, hupata faraja na amani. Katika madhabahu ni mwanga wa matumaini katika nchi iliyoharibiwa na uwepo wa mtandao wa wahalifu. Kazi ya kichungaji inayofanyika ndani ya mahali Patakatifu inalenga kabisa kumtazama Maria kama mama na mfano wa maisha yaliyotimizwa, inayolenga kuelekea Wema Mkuu. Kufanya kazi na vizazi vichanga, usaidizi kwa familia, na mazoezi ya sala, hasa Ibada ya Ekaristi, na kusali Rozari, vinabaki kuwa vipaumbele vya kupambana na uovu na kulea maisha ya kila mtu ili waweze kuitikia wito wa Tangazo: “Fanyeni  chochote atakachowambia.”

Ni kwa kumtii Mungu pekee tunaweza kuwa wajenzi wa amani, na kwa hivyo kubarikiwa. Katika Madhabahu palipojengwa kwa Mama Yetu wa Amani, tungependa kuendelea kuwa kama “wale mabaharia” waliovuta sanamu hiyo kutoka majini, ishara ya kutokuwa na uhakika, ili kuifikisha salama kwenye nchi kavu. Kisha ilikabidhiwa kwa wale wakulima walioandaa mashamba mazuri kwa ajili ya kupanda kweli matumaini na ambao, wakisaidiwa na ng'ombe, kwa nguvu ya kazi yao, waliiweka pale ambapo kila mtu, hata leo hii, baada ya karibu karne sita, inawezekana kuendelea kuomba msaada katika kazi ya ajabu ya kujenga ustaarabu wa haki na amani.

Mtoto kama Malaika akishuka wakati maua yakidondoshwa
Mtoto kama Malaika akishuka wakati maua yakidondoshwa

Duniani kote, vijana mara nyingi wamekuwa wazembe katika kuendeleza  mila  na tamaduni na, huku wazee na hata baadhi ya familia vijana kwa wazee, wakihusika sana; hali ikoje katika eneo lenu?

Kwa "zingarella"- kama vile Mama wa kweli wa Giugliano anavyoitwa kwa kilugha cha hapa, “Mama yetu wa Amani”, kutokana na rangi ya mbao, vizazi vyote vinavutiwa na kuhusika, hasa katika siku zake za sherehe. Hakika, uwepo wa kudumu zaidi katika mahali Patakatifu ni miongoni mwa watu wazima na wazee. Kwa bahati mbaya, ugumu wa ardhi yetu, kijamii, kiuchumi, na kutokana na afya mbaya, hulazimisha hata wengi  kwa wadogo kumkaribia, kama watu wangeweza kumkaribia mama yao. Tuko katika kile kinachoitwa "Ardhi ya Moto." 

Na hakuna uhaba wa visa vya saratani katika kila nyumba, kama vile kulivyo na ugumu mkubwa wa kiuchumi kutokana na ukosefu wa kazi na matarajio ya siku zijazo, na lazima pia tukubali kuanguka kwa urahisi vijana wengi sana wasio na uhakika kuhusu mustakabali wa ajabu kama huo, katika makucha ya ulimwengu wa wahalifu.  Hasa kwa sababu ya wasiwasi, usumbufu, hofu, na wasiwasi unaotawala mioyo ya wengi, watu humgeukia mama. Kwa Giugliano, Mama yetu wa Amani si sanamu, yeye ni uwepo. Madhabahu yake  si Kanisa miongoni mwa mengine; ni nyumbani kwa Mama yetu, na tunaingia kwake kwa ibada hiyo ambayo inakuwa uhakika wa kusubiriwa na kuhitajika, kupendwa na kulindwa. Macho yake "yanazungumza." Hakuna mkazi wa Giugliano, hata aliye mbali zaidi na mzembe maishani, ambaye hamgeukii...

Utamaduni wa sala na sherehe kwa Mama Maria
Utamaduni wa sala na sherehe kwa Mama Maria

Dunia inawaka moto na inahitaji amani. Papa Leo XIV analia kila siku jangwani. Mnamsaidiaje Papa katika hali hii ya kilio chake?

Mahali Patakatifu, Rozari inasaliwa kila siku kama jumuiya, na kila Alhamisi huadhimishwa na Ibada ya kibinafsi na ya kijumuiya, tukio linalohudhuriwa sana na kusubiriwa kwa hamu kwa waamini wengi. Miguuni pa Maria, taa inawaka kwa ajili ya nia ya Baba Mtakatifu, mahitaji ya Kanisa, na mahitaji ya ndani kabisa ya kila mtoto wa Mama Yetu. Kwa sababu ya historia na wadhifa uliopewa kwa  Mama Yetu hapa, maombi ya Amani yanaendelea... Yeye, ambaye alipofika, aliweza kurekebisha mpasuko kati ya familia za nchi yetu, hawezi kushindwa kusaidia mchakato wa kufikia “Amani isiyo silaha na inayopokonya  silaha,” inayokaa duniani kote. Tunatamani kusindikizana na kazi ya kitume ya Mrithi wa Petro kwa kutoa shukrani zetu za dhati kwa umakini wake kwa eneo la Campania. Siku chache baada ya Pompeii na Napoli, atatembelea Acerra wakati wa Juma lililotengwa kwa Laudato Si', Waraka wa Papa Francisko kuhusu ulinzi wa kazi ya uumbaji. Kwa wale kama sisi tunaoishi katika janga la ardhi hii, kujua jinsi masuala fulani yanavyothaminiwa na Baba Mtakatifu yanatujaza matumaini na furaha. Sisi tuko pamoja na Papa Leo XIV  kila wakati...

Waamini wengi katika mitaa wakiudhuria maandamano ya kila mwaka ya Mama Maria
Waamini wengi katika mitaa wakiudhuria maandamano ya kila mwaka ya Mama Maria

Hatimaye, una chochote ungependa kuongeza  kwenye kile ambacho ulikielezea?

Kardinali Angelo Comastri(Mkuu wa Zamani wa Basilika ya Mtakatifu Petro)  alitutumia ujumbe kwa njia ya  video wakati wa siku hizi za kuandaa sherehe, ambazo tunamshukuru sana. Akikumbuka thamani ya familia, sala, na kujitolea kuwa wapatanishi, Kardinali alituhimiza kuhakikisha kwamba jina "ardhi ya moto" halikumbushi uchafuzi unaosababisha magonjwa mabaya tu, bali pia kujitolea kuwasha moto wa upendo kila mahali, moto wa upendo ambao lazima uwe alama ya maisha ya Mkristo, akiitikia mwaliko wa Yesu wa kupendana kama alivyotupenda. Huu ni moto ambao lazima usambazwe  ulimwenguni kote, ukisaidiwa na Mama Yetu, ambaye ametufikia baada ya safari hii ndefu kuvuka maji ya Bahari ya Mediterania.

Ni zawadi kutoka kwa Mungu, baraka kwa nchi yetu, na mwaliko wa kufuata mfano wake. Kama Msimamizi wa Madhabahu, ninahisi jukumu kubwa la kutoa msaada na usaidizi kwa wale wanaokuja kwenye hifadhi yetu, nikijua kwamba sala yetu lazima ibadilishwe kuwa ya kuiga kweli. Historia tuliyokabidhiwa lazima itusaidie kukuza ndani yetu shauku ya kuboresha wakati wetu na ulimwengu wetu. Ninaota, kama Kardinali, aliyekuwa Askofu wa Kanisa Kuu la  Jiji la Vatican, alivyotutakia, kwamba mazingira yetu, yanayodumishwa na uwepo mpole na wenye kutia moyo wa Mama Yetu, yatakuwa kimbilio la amani ya kweli.

Padre Luigi msimamizi wa Madhabahu akivalisha Kofia sanamu ya Maria
Padre Luigi msimamizi wa Madhabahu akivalisha Kofia sanamu ya Maria
madhabahu ya amani

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.

20 Mei 2026, 11:22