Tafuta

2026.05.13 Padre Nathaniel Asuwaye 2026.05.13 Padre Nathaniel Asuwaye 

Nigeria:Padre aliyetekwa nyara aachiliwa huru baada ya miezi 3

Jimbo Katoliki ya Kafanchan nchini Nigeria lilitangaza kuachiliwa huru kwa Padre Nathaniel Asuwaye, ambaye alitekwa nyara mnamo tarehe 7 Februari 2026 kutoka makazi yake ya Parokia katika Jimbo la Kaduna.

Vatican News

Katika taarifa iliyotolewa tarehe 12 Mei, Jimbo Katoliki ilionesha "shukrani kubwa kwa Mungu" kwa kurejea salama kwa Padre Nathaniel Asuwaye baada ya miezi mitatu ya kutekwa nyara. "Tunafurahi kuwajulisha kwamba Padre Nathaniel sasa yuko salama na anapokea huduma muhimu ya kimatibabu," taarifa hiyo ilisema. "Hali yake ni nzuri, na anawashukuru kwa maombi na usaidizi wenu." Padre Nathaniel wa Parokia ya Kanisa la Utatu Mtakatifu huko Karku, Kaunti ya Kaura ya Jimbo la Kaduna, alitekwa nyara tarehe 7 Februari 2026 wakati washambuliaji wenye silaha walipovamia makazi ya mapadre. Kulingana na ripoti wakati huo, waamini kumi wa Parokia pia walitekwa nyara wakati wa shambulio hilo, huku watu watatu wakiuawa.

Sala

Kumbukizi miezi iliyofuata baada ya kutekwa nyara, Jimbo ilisema imewahimiza waamini kuendelea kumwombea Padre huyo aachiliwe. "Mwishoni mwa mwezi Aprili 2026, tuliikabidhi mwezi wa Mei kwa Mungu kupitia kwa sala wakati wa ibada zetu za kila mwaka za Maria na sala zingine, hasa Misa Takatifu. Mungu, ambaye hawaachi wale wanaoitwa kwa jina lake na kumwita, amesikia maombi yetu na kumpa Padre Nathaniel kurudi salama," taarifa hiyo ilibainisha. Askofu Julius Yakubu Kundi, pamoja na Mapadre na waamini wa Jimbo la Kafanchan, pia walitoa shukrani kwa wote waliounga mkono Kanisa wakati wa kipindi kigumu, hasa wale waliojali familia ya Padre na kuandamana na jamii kupitia sala na mshikamano. "Tunapofurahia wakati huu wa kujibiwa kwa maombi, tuendelee kuwa imara katika imani, tukiwa na umoja kama familia moja, na kusaidiana," Jimbo lilisema, huku likiwahimiza waamini kuwa macho na wenye huruma kwa kila mmoja.

Wasiwasi kuhusu ukosefu wa usalama ulioenea

Kulingana na Shirika la Kipapa la Habari la Kimisionari Fides, hakuna taarifa iliyotolewa bado kuhusu hatima ya waamini kumi waliotekwa pamoja na Padre Nathaniel. Kuachiliwa kwa Padre huyo kunakuja huku kukiwa na wasiwasi unaoendelea kuhusu kutekwa nyara kwa mapadre na ukosefu wa usalama katika sehemu kadhaa za Nigeria. Shirika la Fides liliripoti kwamba mapadre wawili Wakatoliki bado wako mikoni mwa watekaji: Padre Joseph Igweagu wa Jimbo la Aguleri katika mji wa Anambra, aliyetekwa nyara tarehe 12 Oktoba 2022, na Padre Emmanuel Ezema wa Jimbo la Zaria wa jiji la Kaduna, aliyetekwa nyara tarehe 2 Desemba 2025. Kanisa Katoliki nchini Nigeria limekuwa likiomba mara kwa mara hatua kali za usalama na juhudi mpya za kulinda maisha ya binadamu na kurejesha amani katika jamii zilizoathiriwa na vurugu na mashambulizi ya jinai.

Imesasishwa tarehe 15 Mei 2026 saa 9. 53 alasri na Sr Christine Masivo.

Padre wa Nigeria aachiliwa huru

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.

15 Mei 2026, 15:49