Nigeria:Vurugu Jimbo la Wukari zasababisha mamia ya vifo!
Na Sr. Christine Masivo,CPS –Vatican.
Jimbo Katoliki la Wukari nchini Nigeria linakabiliwa na moja ya mawimbi mabaya zaidi ya vurugu katika historia yake ya hivi karibuni. Katika taarifa iliyotolewa baada ya Mkutano Mkuu wa Tatu wa Jimbo hilo, Askofu Mark Maigida Nzukwein alifichua athari mbaya ambayo shambulio hilo limesababisha kwa Kanisa na jamii za wenyeji.
Hasara kubwa za kiroho na kibinadamu
"Tangu Septemba, zaidi ya watu 98,000, wakiwemo mapadre 16, wamefukuzwa na kuhama makazi yao kutokana na vurugu zinazoendelea kusini mwa Jimbo la Taraba," alisema Askofu Mark. Kwa mujibu wa Shirika la Kipapa la Habari za Kimisionari Fides, Askofu alisema kuwa, Makanisa 217 yameharibiwa kabisa huku nyumba za mapadre wanane zikiporwa wakati wa mashambulizi hayo. Vurugu hizo pia zimesababisha vifo vya zaidi ya watu 100. Miongoni mwa Makanisa yaliyoshambuliwa hivi karibuni ni Kanisa Katoliki la Mtakatifu Yakobo, mwezi Machi ikiwa ni pamoja na Kanisa Kuu la Kupalizwa kwa Bikira Maria lililoteketezwa moto na kuongeza maumivu na kutokuwa na uhakika unaowakabili waamini Wakatoliki katika eneo hilo. Vurugu hizo zimeathiri zaidi Wilaya ya Chanchanji ya eneo la Serikali za Mitaa za Takum, na pia katika jamii za Ussa na Donga, ambapo wakazi wengi wamelazimika kukimbia nyumba zao kutafuta usalama.
Jumuiya ya Wakristo wakulima zikiwa zimezingirwa
Viongozi wa Kanisa mahalia na wakazi wanaamini mashambulizi hayo yanafanywa kwa kiasi kikubwa na magenge ya wafugaji wa Fulani wenye silaha yanayolenga vijiji vingi vya Wakristo, vingi vikiishiwa na watu wa kabila la Tiv. Kulingana na ripoti kutoka kwenye Jimbo, washambuliaji mara nyingi huharibu nyumba, makanisa, na majumba ya jamii kabla ya kumiliki ardhi zilizotelekezwa kinyume cha sheria. Uvamizi huo umezidisha mvutano wa muda mrefu kuhusu umiliki wa ardhi kati ya jamii za kabila la Tiv na Jukun, mgogoro ambao umeendelea kwa vizazi vingi katika Jimbo la Taraba. Ukosefu wa usalama unaozidi kuwa mbaya pia umeathiri shughuli za kilimo, na kuziacha familia nyingi bila riziki na hofu kubwa ya njaa na mateso makubwa ya kibinadamu katika jamii zilizoathiriwa.
Wito wa usaidizi bado haujaonesha matokeo
Mgogoro unaoongezeka umesababisha wito wa mara kwa mara wa kuchukua hatua kutoka kwa viongozi wa Kanisa. Mnamo Februari 12, Mapadre kutoka jimbo la Wukari na Jalingo walifanya maandamano ya umma wakitaka serikali iingilie kati mara moja ili kukomesha mauaji, utekaji nyara, na uharibifu wa jamii za wakulima wa Kikristo kusini mwa Taraba. Wakati huo, Jimbo la Wukari iliripoti kwamba zaidi ya watu 80 waliuawa, zaidi ya makanisa na jamii 200 ziliharibiwa, na zaidi ya Wakristo 90,000 walikimbia makazi yao. Karibu miezi mitatu baadaye, takwimu hizo zimeongezeka sana, zikisisitiza kile ambacho viongozi wa Kanisa wanakielezea kama kushindwa kwa mamlaka kurejesha amani na usalama. Kwa familia nyingi zilizokimbia makazi yao, maisha bado hayana uhakika. Maelfu sasa wanaishi bila makazi ya kutosha, chakula, huduma ya afya, au ulinzi, huku vituo vya ibada ambavyo hapo awali vilikuwa mahali pa matumaini na umoja vikiwa magofu. Huku vurugu zikiendelea kuenea katika sehemu za Jimbo la Taraba, viongozi wa Kanisa wanarudia ombi lao la kuingilia kati haraka ili kulinda jamii zilizo hatarini na kuzuia vifo zaidi.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.