Sherehe ya Pentekoste: Roho Mtakatifu! Kanisa na Dhamana ya Waamini Walei
Na Padre OCTAVIAN O. HINJU CP. MOROGORO, Tanzania
Siku hamsini baada ya ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo Mama Kanisa anatuita kuadhimisha Sherehe ya Pentekoste. Ni siku ya kuadhimisha tukio adhimu na la kipekee sana; ndilo la msingi kwani Kanisa linazaliwa kwake kwa njia ya Roho Mtakatifu yaani kuumbwa upya kwa Taifa jipya la Mungu. Sherehe ya Pentekoste ni kilele cha maadhimisho ya sherehe ya Pasaka ya Bwana. Ni mwanzo wa kuutumia utajiri wote tuliochiwa na Yesu Mfufuka ili uanze kuonekana wazi katika mioyo na maisha ya Mitume. Roho Mtakatifu ni ishara ya umoja wa Kanisa; leo ni Sherehe ya waamini walei wanaoitwa na kutumwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kwa kuyatakatifuza malimwengu kwa uwepo wao angavu na endelevu. Mama Kanisa anasadiki na kufundisha kwamba, Roho Mtakatifu, Bwana mleta uzima, atokaye kwa Baba na Mwana. Anayeabudiwa na kutukuzwa, pamoja na Baba na Mwana aliyenena kwa vinywa vya manabii. Kanisa, ushirika hai katika imani ya Mitume ambayo linaiendeleza, ni mahali muafaka kabisa pa kumjua Roho Mtakatifu: Katika Maandiko Matakatifu ambayo ameyavuvia; Katika Mapokeo ambayo Mababa wa Kanisa siku zote ndio Mashuhuda wake halisi, Katika Mamlaka fundishi ndani ya Kanisa “Magisterium”; katika Liturujia ya Sakramenti za Kanisa kwa maneno na alama zake ambamo Roho Mtakatifu anawaingiza waamini katika ushirika na Kristo Yesu, Katika sala ambako anawaombea; katika karama na huduma zinazolijenga Kanisa; Katika Ishara na maisha ya kitume na kimisionari; Katika ushuhuda wa watakatifu, ambamo anadhihirisha utakatifu wake na kuendeleza kazi ya ukombozi. Rej. KKK 683-730.
Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Juma la “Laudato si”, Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumamosi tarehe 23 Mei 2026 amefanya hija ya kichungaji eneo la Acerra, maarufu kama "Terra dei Fuochi" yaani “Ardhi ya moto” eneo ambalo limeathiriwa sana na taka maalum na hatari zilizotupwa eneo hili kinyume cha sheria, taratibu na kanuni za nchi na mashirika pamoja na makampuni ya uhalifu. Hili ni eneo linalopatikana katika Majimbo ya Napoli na Caserta. Uchafuzi huu wa mazingira nyumba ya wote, kimekuwa ni chanzo kikuu cha kusambaa na kuenea kwa magonjwa ya Saratani sanjari na uchafuzi mkubwa wa mazingira. Baba Mtakatifu Leo XIV amepata nafasi ya kukutana na kusalimiana na watu wa Mungu, kama sehemu ya kumbukizi ya Miaka kumi na moja; yaani tarehe 24 Mei 2015, Baba Mtakatifu Francisko alipochapisha Waraka wa Kitume wa “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote.” Huu ni Waraka unaozungumzia kwa muhtasari mambo yanayotokea katika mazingira; Injili ya Uumbaji; Vyanzo vya mgogoro wa ikolojia vinavyohusiana na watu; Ikolojia msingi; Njia za kupanga na kutenda na mwishoni ni elimu ya Ikolojia na maisha ya kiroho. Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuunganisha athari za uchafuzi wa mazingira nyumba ya wote, magonjwa ya kijamii; vita na kinzani; wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi pamoja na baa la umaskini linalopekenya utu, heshima na haki msingi za binadamu. Lengo ni kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inaunda mfumo wa uchumi na masuala ya kijamii yanayokita misingi yake katika haki, heshima na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, daima: utu, heshima na haki msingi za binadamu zikipewa kipaumbele cha kwanza.
Tafakari ya Neno la Mungu katika Sherehe ya Pentekoste. Ni siku ya hamsini baada ya ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Ni siku ambayo Roho Mtakatifu aliwashukia Mitume ili kuwaangaza katika moyo, maisha na utume wao baada ya kupaa kwa Kristu. Siku ya Pentekoste ni kilele cha Sherehe ya Pasaka ya Bwana, kwa sababu utajiri wote aliotufunulia Yesu mfufuka unaanza kuonekana katika mioyo na maisha ya Mitume. Kumbe tunasherehekea utimilifu wa fumbo la ukombozi wetu kwa nguvu ya Roho Mtakatifu aliye ishara ya umoja wetu na Mungu kama tunavyo injilishwa na wimbo wetu wa mwanzo siku ya leo unaoimba; “Roho ya Bwana imeujaza ulimwengu, nayo inaviunganisha viumbe vyote, hujua maana ya kila sauti” (Hek.1:7). Naye Paulo Mtume anasisitiza juu ya ujumbe wa masomo ya leo akisema “na pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi, Aleluya” (Rum. 5:5). Kumbe katika muktadha huo, Pentekoste ni sherehe ya waamini walei wote. Kwa hakika sherehe hii inapata chimbuko lake kutoka katika sherehe na tamaduni za kiyahudi. Itakumbukwa kuwa katika jamii ya kiyahudi sherehe ya Pentekoste iliitwa pia Shavuot neno lenye maana ya sherehe ya majuma. Ilisherehekewa siku ya 49/50 yaani majuma saba ama siku moja baada ya pasaka ya kiyahudi. Sherehe hii ilibeba dhana kuu mbili; mosi ni kuhitimisha mavuno ya zao la ngano katika ardhi ya Israeli na pili ni tendo takatifu la Mwenyezi Mungu kuwapatia wana wa Israeli Torati kupitia mtumishi wake Musa mlimani Sinai. Sherehe hii kwa asili ilisherehekewa kufurahia mazao ya nchi. Ni wakati ambao wana wa Israeli walileta bikkurim yaani mazao ya kwanza ya ardhi katika hekalu la Yerusalemu ili kumtolea Mungu sadaka ya shukrani. Vilevile, katika siku hii tamaduni za kiyahudi zinatanabaisha kuwa watu kwa pamoja walikusanyika ili kula vyakula vya maziwa, kukesha usiku kucha kusoma torati na kuzipamba nyumba zao kwa kijani kibichi.
Kumbe pentekoste iliadhimishwa siku ya Hamsini baada ya Pasaka ya Kiyahudi. Pasaka kwa Wayahudi ilibeba ujumbe wa ushindi toka utumwani mwa Farao na jeshi lake huko Misri. Waliisherehekea kutukuza ukuu wa mwenyezi Mungu juu ya adui zao ndio maana walipovuka pakavu kwenye Bahari ya shamu Musa na wana wa Israeli wakamwimbia BWANA wimbo huu wakanena, na kusema, ‘Nitamwimbia BWANA, kwa maana ametukuka sana; Farasi na mpanda farasi amewatupa baharini. BWANA ni nguvu zangu, na wimbo wangu Naye amekuwa wokovu wangu. Magari ya Farao na jeshi lake amewatupa baharini, Maakida yake wateule wamezama katika bahari ya Shamu. Vilindi vimewafunikiza, Walizama vilindini kama jiwe. BWANA, mkono wako wa kuume umepata fahari ya uwezo (Kut. 15:1-2, 4-6). Sisi katika sikukuu hii ya Pentekoste tunaadhimisha kuwekwa kwa Agano Jipya na la milele kati ya Mungu na binadamu kwa njia ya Yesu Kristo na kuthibitishwa kwa ujio wa Roho Mtakatifu. Nasi kwa njia ya Kristo tumepewa Amri kuu mpya ya mapendo, kiini cha Agano jipya na la milele. Pentekoste kwetu pia ni “sikukuu ya mavuno” ya waamini waliobatizwa siku hiyo yapata watu elfu tatu, mavuno yanayoendelea kuongezeka kila inapoadhimishwa Sakramenti ya ubatizo. Katika kanisa kadhalika likifuata mtazamo wa Agano la Kale leo zinatimia siku Hamsini baada ya ufufuko wake Bwana. Katika muda wa siku hizo Hamsini kanisa lilimshangilia Kristo Mfufuka, lilifurahia uzima mpya ambao lilipewa kwa ufufuko wa Bwana. Katika siku hii ya Pentekoste fumbo la pasaka linakamilishwa.
Kwa kufa na kufufuka kwake, Kristo ametupatanisha tena na Mungu, ametushirikisha uzima wake kama anavyo sisitiza Paulo Mtume anaposali hivi “tukijua ya kuwa Kristo akiisha kufufuka katika wafu hafi tena, wala mauti haimtawali tena.” (Rom. 6:9). Leo Roho wa Mungu, yaani Roho Mtakatifu anaye mwagika ndani yetu ni uthibitisho wa umoja wetu na Mungu. Pentekoste inatufanya kuwa jamaa moja ya Mungu, taifa jipya teule yaani Kanisa kwa kuwa Roho wake hukaa ndani yetu, akituunganisha na Mungu na pia hutuunganisha sisi kwa sisi. Kwa maana nyingine leo ni sherehe pia ya kuzaliwa kwa Kanisa ambapo waamini kote duniani wanaalikwa kubeba kwa moyo wa shukrani na utayari wajibu wa msingi wa uinjilishaji. “Ilipofika Siku ya Pentekoste, waamini wote walikuwa wameku tana mahali pamoja. Ghafla, sauti kama mvumo mkubwa wa upepo uliwashukia kutoka mbinguni, ukaijaza nyumba yote walimokuwa wamekaa. Pakatokea kitu kama ndimi za moto ambao uligawanyika ukakaa juu ya kila mmoja wao. Wote walijazwa Roho Mtakatifu wakaamza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kusema (Matendo 2:1-4). Kumbe Roho wa Mungu alimwagwa juu ya wanadamu wote bila kujali rangi, sura, kabila au jamaa. Sote kwa uwezo tendaji wa Roho Mtakatifu tumepewa Roho yule ndani mwetu “Kwa kuwa hamkupokea tena roho wa utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba. Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu (Rom. 8:15-16).
Pentekoste ni ukumbusho ya kuwa watu wote wameitwa kwa namna ya pekee kushiriki katika kazi ya kanisa ya kitume kumtangaza Kristo kwa mataifa yote. Kama taifa teule la Mungu wote wameitwa kila mmoja kwa lugha yake lakini wenye lengo moja. Paulo Mtume alipoyatafakari hayo alisali hivi pamoja na wafilipi “Lakini hata ikitokea nini, hakikisheni kuwa mwenendo wenu unalingana na Injili ya Kristo. Ili kama nikija kuwaona au hata nisipojaliwa kufika, nipate habari kuwa mnasimama imara katika roho ya umoja, mkiwa na nia moja huku mkipambana kwa pamoja kwa ajili ya imani ya Injili, bila kuwaogopa wale wanaowapinga” (Wafilipi 1:27-28). Pentekoste ni ukaribisho wa Agano Jipya ambalo sio kwa ajili ya kundi fulani bali ni kwa ajili ya watu wote. Katika utimilifu wa fumbo la Pasaka, tutambue kwamba Kristu alikufa kusudi wanadamu wote wapate kukombolewa. Kwa maneno hayo, tunataka kusema kwamba Pentekoste ni adhimisho la mwanzo wa Agano Jipya na la milile linalofungwa kwa kufa na kufufka kwake Kristo. Ni mwanzo wa kanisa taifa jipya la Mungu lililojaa Roho wake Mtakatifu kama tunavyo fundishwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa pili wa Vatican.Somo la kwanza ni la Kitabu cha Matendo ya Mitume (Mdo. 2:1-11). Somo hili linasimulia jinsi “upepo wa nguvu” na “ndimi za moto” vilivyotokea siku ya Pentekoste ya kwanza zikiwa ni alama ya uwepo wa Roho Mtakatifu aliyewajaza mitume nguvu na ujasiri wa kuhubiri habari za Kristo Mfufuka na wongofu wa watu. Pia umoja na uelewano uliopotea sababu ya dhambi ulivyoletwa tena kwa watu wa Mataifa mbalimbali kuwasikia mitume wakiwahubiria kwa lugha yao ya kuzaliwa. Kwa nguvu na mwangaza wa Roho Mtakatifu, tunasali kuomba tunaposema “Ee Mungu, wewe unalitakasa Kanisa lako lote lililo kati ya makabila na mataifa yote kwa fumbo la sikukuu ya leo. Eneza mapaji ya Roho Mtakatifu popote duniani; na zile karama ulizozitoa tangu mwanzo wa kuhubiri Injili, hata sasa uzieneze kwa juhudi ya waamini wako.”
Somo la pili ni la Waraka wa Kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (1Kor. 12:3b-7, 12-13). Somo hili linatueleza kuwa Roho Mtakatifu ni msingi wa karama na hudumu mbalimbali katika Kanisa. Yeye ndiye anayefanya karama hizo zilete umoja katika kuihudumia jumuiya nzima ya waamini kama viungo mbalimbali vya mwili vinavyosaidiana kwa faida ya mwili mmoja. Injili inayo tamatisha tafakari yetu ni kama ilivyoandikwa na Yohane (Yn. 20:19-23). Sehemu hii ya Injili inaeleza jinsi Roho Mtakatifu alivyofanya kazi ya kuwaunganisha mitume na Yesu mfufuka na sasa anawaunganisha watu na Mungu kwa kuwaondolea dhambi zao. Zao la kazi hii ya Roho Mtakatifu ni upatanisho na amani kati ya Mungu na watu. Kabla ya kuhitimisha tafakari yetu katika sherehe hii ya pentekoste ningelipenda kuwakumbusha kuwa kwa sherehe ya Pentekoste tunahitimisha kipindi cha Pasaka. Hivyo kuna mambo muhimu ya kiliturujia tunayo paswa kuyazingatia: Kwanza kabisa Mshumaa wa Pasaka unatolewa mahali pa patakatifu karibu na Altare uliposimikwa usiku ule wa vijilia vya Pasaka na kuweka karibu na kisima cha ubatizo kama kipo au sehemu nyingine. Mshumaa huo utakuwa unawashwa wakati wa ubatizo ili mishumaa ya wabatizwa iwashwe kutokea katika mshumaa huu kama ishara ya kufa kuhusu dhambi na kufufuka pamoja na Kristo na wakati wa mazishi unawekwa kando ya jeneza ishara ya ufufuko kwa mkristo aliyekufa akiwa na muunganiko na Kristo mfufuka. Pili, kuanzia Jumatatu baada ya Jumapili ya Pentekoste, tunaacha kusali sala ya Malkia wa mbingu na tunaanza kusali sala ya Malaika wa Bwana na tunaendelea na Liturujia ya kipindi cha Kawaida cha mwaka A. Itakumbukwa kuwa kabla ya kuanza kipindi cha Kwaresima siku ya Jumatano ya Majivu mwaka huu 2026 A wa kiliturujia tuliishia wiki ya saba katika kipindi cha kawaida. Hivyo tutaendelea na wiki ya juma la nane. Tunapoendelea kuyatafakari hayo, tunamwomba huyo Roho tunaye mpokea aangaze moyo, akili na utashi wetu ili tuweze kujitoa kwa sadaka ya maisha yetu ili Kristo awe yote katika yote. Tumsifu Yesu Kristo.