Tafuta

Mama Kanisa anaadhimisha, Sherehe Ya Utatu Mtakatifu: “Fumbo la Upendo na Umoja.” Mama Kanisa anaadhimisha, Sherehe Ya Utatu Mtakatifu: “Fumbo la Upendo na Umoja.”   (©Renáta Sedmáková - stock.adobe.com)

Tafakari Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu: Upendo na Umoja!

Mama Kanisa anaadhimisha, Sherehe Ya Utatu Mtakatifu: “Fumbo la Upendo na Umoja.” Mababa wa Kanisa wanasema, Imani Katoliki mintarafu Fumbo la Utatu Mtakatifu ndiyo hii: “Tunamwabudu Mungu Mmoja katika Utatu na Utatu katika Umoja, bila kugawanyika nafsi, wala kutenganisha uwamo; kwani ni Nafsi ya Baba, ya Mwana na Roho Mtakatifu. Ni umungu mmoja wa Baba, na wa Mwana na wa Roho Mtakatifu, utukufu ulio sawa, ukuu wa pamoja wa milele.”

Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.

Utangulizi. Wapendwa Familia ya Mungu, Dominika baada ya Sherehe ya Pentekoste, Mama Kanisa anaadhimisha, Sherehe Ya Utatu Mtakatifu: “Fumbo la Upendo na Umoja.” Mababa wa Kanisa wanasema, Imani Katoliki mimntarafu Fumbo la Utatu Mtakatifu ndiyo hii: “Tunamwabudu Mungu Mmoja katika Utatu na Utatu katika Umoja, bila kugawanyika nafsi, wala kutenganisha uwamo; kwani ni Nafsi ya Baba, ya Mwana na Roho Mtakatifu. Ni umungu mmoja wa Baba, na wa Mwana na wa Roho Mtakatifu, utukufu ulio sawa, ukuu wa pamoja wa milele.” KKK 266. Katekisimu ya Kanisa Katoliki namba 234, 253 na 256 yatufundisha kuwa, Mungu ni mmoja anayeishi katika nafsi tatu, Baba, Mwana na Roho Mtakatifu, wote ni Mungu kweli, na bado tuna Mungu mmoja. Lakini, Baba sio Mwana, Mwana sio Roho Mtakatifu na Roho Mtakatifu sio Baba. Hata hivyo, tofauti hii ya Nafsi haitengi Uungu wao. Mungu ni Mmoja tu kwa asili, nguvu, mamlaka, na utukufu. Hawagawani uungu, bali kila mmoja ni Mungu kamili, nao wanaishi katika umoja mkamilifu wa upendo. Ukweli huu wa Imani yetu ni Fumbo kwa kuwa hatuwezi kwa akili, maarifa na upeo wetu wa kibinadamu wenye ukomo, kumwelezea Mungu asiye na ukomo. Mtakatifu Agustino wa Hippo, mmoja wa Mababa wa Kanisa, aliyekua akijaribu kutaka kuelewa na kuelezea Fumbo ili kwa akili yake anatufundisha hivi, “Ikiwa unamwelewa Mungu kwa akili yako yote, basi huyo unayemwelewa si Mungu tena. Kumbe, tunamwelewa Mungu kwa mioyo yetu kupitia mahusiano ya sala. Pia, tunatambua uwepo wake kwa kuangalia jinsi anavyotenda kazi na kujifunua kwetu hatua kwa hatua katika historia yetu yote (Economy of Salvation). Baba ndiye Muumbaji, Mwana ni Mkombozi, na Roho Mtakatifu ni Mfariji na analitaka Kanisa. Katika Sherehe ya Utatu Mtakatifu tunaadhimisha nini? Neno “Utatu Mtakatifu halipo katika Maandiko Matakatifu, kuanzia Mwanzo mpaka Ufunuo wa Yohane. Lakini Ukweli wa kiutendaji wa Fumbo hili takatifu, kwamba Mungu ni mmoja katika Nafsi tatu zinazoshirikiana unatajwa na kuoneshwa wazi kabisa katika matukio na mistari mingi ya Agano Jipya, pamoja na vidokezo vya wazi katika Agano la Kale.

Fumbo la Utatu Mtakatifu: Umoja; upendo na mshikamano wa dhati
Fumbo la Utatu Mtakatifu: Umoja; upendo na mshikamano wa dhati   (@Vatican Media)

Mwenyezi Mungu amejifunua kwetu hatua kwa hatua katika Nafsi Tatu katika historia yote ya mwanadamu, kuanzia uumbaji mpaka safari nzima ya ukombozi, hili linadhihirika wazi kabisa katika Maandiko Matakatifu. Mafumbo yote ya ukombozi wetu ni kazi ya Utatu Mtakatifu. Maadhimisho yote ya Mafumbo haya, kuanzia Fumbo la Umwilisho, kuzaliwa Bwana, Tokeo la Bwana, Ubatizo wa Bwana, Utume wa wazi wa Bwana wetu Yesu Kristo, Mateso, kifo, na Ufufuko wake; Kupaa kwake mbinguni na Pentekoste, yanaonesha uwepo na ushirikiano wa umoja huu Mtakatifu usiogawanyika. Kumbe Dominika hii tunasherehekea maisha ya ndani ya Mungu, Mungu ambaye anaishi katika Umoja, katika jumuiya, katika ushirika na Mwana na Roho Mtakatifu. Ni Fumbo la umoja na Upendo. Katika maisha na utume wa Kanisa, Maadhimisho yote katika Kanisa, kuanzia Adhimisho la ibada ya Misa Takatifu, maadhimisho ya Sakramenti zote, sala mbalimbali tunazosali, yanaadhimishwa katika Utatu Mtakatifu. Tunabatizwa katika Utatu Mtakatifu, tunaondolewa dhambi katika Utatu Mtakatifu, na sakramenti nyingine zote zinaadhimishwa kwa jina la Utatu Mtakatifu. Kila mara tunapofanya ishara ya Msalaba tunajikumbusha juu ya ukweli huu wa Imani yetu. Tunahitimisha sala zetu kwa kuutukuza Utatu Mtakatifu tunaposema, atukuzwe Baba, na Mwana na Roho Mtakatifu…Kumbe Mungu ameamua kutushirikisha maisha yake, kwa kutupenda, kutuumba na kwa kutukomboa tulipoanguka katika dhambi. Sherehe hii inatualika nasi sote kuishi daima katika umoja, upendo na ushirika wa kudumu na Mungu, ili tuweze kudumisha upendo, umoja ushirika na mahusiano ya kweli kati yetu sisi kwa sisi katika safari yetu ya maisha hapa duniani.

Mafumbo ya Ukombozi ni Kazi ya Utatu Mtakatifu
Mafumbo ya Ukombozi ni Kazi ya Utatu Mtakatifu   (@Vatican Media)

Chimbuko la Fundisho la Utatu Mtakatifu katika Kanisa: Ufafanuzi wa kale kabisa wa mafundisho ya imani yetu juu ya Utatu Mtakatifu yanapatikana katika Kanuni ya Imani ya Mitume, iliyotumika kama mafundisho msingi kwa ajili ya Wakatekumeni na kama Ungamo la Ubatizo (Baptisimal confession) katika karne ya kwanza. Baadaye, Kanuni ya imani ya Nicea (Nicene Creed) iliyotokana na Mtaguso wa Nicea mwaka 325 AD yaeleza fumbo hili kwa upana na kwa wazi zaidi. Baadaye Kanuni hii iliingizwa rasmi katika liturujia ya Kanisa la Magharibi, yaani Kanisa Katoliki katika Mtaguso wa Toledo mwaka 589 AD. Ili kuonesha kuwa Mwana ana hadhi na Umungu uleule sawa kabisa na Baba, Mtaguso huu ulitamka kuwa Roho Mtakatifu hatoki tu kwa Baba, bali “anatoka kwa Baba na kwa Mwana” (Filioque), nasi tunakiri hata sasa katika kanuni ya imani yetu. Mababa wa Kanisa katika Mitaguso yote hii wanatufundisha kwamba, Mwenyezi Mungu amefunua kwetu kazi tatu, ambazo zahusishwa na nafsi tatu za Mungu. Mungu Baba ndiye Muumbaji, Mungu Mwana ni Mkombozi na Mungu Roho Mtakatifu atokaye kwa Baba na Mwana, ni Mfariji. Maarifa yetu kuhusu Mungu yawezeshwa na Mungu mwenyewe aliyeamua kujifunua kwetu hatua kwa hatua katika nafsi tatu katika historia yote ya maisha ya mwanadamu. Mungu kama Baba ndiye Muumbaji, aliyemfanya mtu kwa sura na mfano wake (Mwa 1:26-27). Mungu kama Mwana ndiye Mkombozi, aliyetwaa mwili akaingia katika historia ya Mwanadamu (Yn 1:14) na Mungu kama Roho Mtakatifu, ameamua kubaki nasi daima, akitufundisha, akitutakasa, akitufariji na akitukumbusha yale yote tuliyojifunza kwa Kristo Yesu. (Yn 14:26).

Fumbo la Utatu Mtakatifu: Umoja na Upendo
Fumbo la Utatu Mtakatifu: Umoja na Upendo   (@Vatican Media)

Fumbo la Utatu Mtakatifu katika Agano la Kale. Mafundisho ya Imani juu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu hayapo wazi sana katika Agano la Kale kama nilivyotangulia kusema. Licha ya hivyo, wataalamu mbalimbali wa taalimungu wanatueleza kuwa, katika Agano la Kale yapo matukio yanayotueleza uwepo wa Utatu Mtakatifu. Kwa akili zetu hatuwezi kueleza fumbo hili kwa kuwa kwa akili zetu hatuwezi kumwelewa na kumwelezea Mungu katika ukamilifu wake kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Agustino alipojaribu kuelezea kuhusu utatu Mtakatifu. Lakini Maandiko Matakatifu yanatusaidia kuelewa Utatu Mtakatifu katika utendaji, namna nafsi zote tatu zinavyoonekana hatua kwa hatua katika historia nzima ya ukombozi wa Mwanadamu. Katika Agano la Kale katika sehemu mbalimbali twaelezwa namna Utatu Mtakatifu unavyodhihirika kama ifuatavyo: Kwanza: Matumizi ya Lugha ya wingi kwa Mungu (Mwanzo 1:26). Matumizi ya lugha ya wingi katika baadhi ya aya katika Agano la kale yanatueleza kuwa Mungu kwa asili ni Mungu anayehusiana, si Mungu anayeishi peke yake, si Mungu aliyejitenga nasi, si Mungu aliye mbali nasi, ni Mungu katika jumuiya na ushirika. Katika kitabu cha Mwanzo 1:26, Mwenyezi Mungu anasema, “Na tumwumbe Mtu kwa sura na mfano wetu” Aya hii yatuonesha kwa hakika kuwa kazi ya uumbaji ilikua ni kazi ya Utatu Mtakatifu. Mwenyezi Mungu hakuumba peke yake, Mwana alikuwepo tangu Mwanzo hali kadhalika na Roho Mtakatifu.  Wazo hili laonekana pia katika Kitabu cha Mwanzo 11:7, katika simulizi la Mnara wa Babeli. Mwenyezi Mungu anaposema, “Haya, na tushuke huko, tuwachafulie usemi wao ili wasisikilizane maneno wao kwa wao” Matumizi haya ya lugha ya wingi yatupa picha kwamba Mungu anaishi katika jumuiya, anaishi katika umoja, nao ndio Utatu Mtakatifu. Somo la kwanza katika Sherehe hii kutoka kitabu cha kutoka sura ya 34 latuonesha asili ya Mungu, Mungu anayehusiana na taifa lake teule, Mungu mwenye upendo, Mungu mwenye huruma isiyo na mipaka, Mungu wa haki, anayesamehe, si mwepesi wa hasira, mwingi wa Fadhili na rehema, anayewapa wanadamu licha ya udhaifu wao nafasi ya kuanza tena kila kila kitu upya. Taifa la Israeli walivunja Agano na Mungu kwa kuabudu sanamu, lakini Mungu anajidhihirisha kwao tena kama Mungu anayewapenda, Mungu anayewajali, Mungu anayewatafuta na kuwahurumia. Mungu tangu katika Agano la kale hatua kwa hatua amejifunua kwetu kama Baba mwenye upendo na huruma.

Utatu Mtakatifu umejifunua hatua kwa hatua
Utatu Mtakatifu umejifunua hatua kwa hatua

Pili: Uwepo wa Roho wa Bwana katika uumbaji (Ruach Elohim) Mwanzo 1:2. Uwepo wa Roho wa Bwana watupa picha ya kuwa kazi ya uumbaji ni kazi ya Utatu Mtakatifu. Katika kitabu cha Mwanzo 1:2 tunaambiwa, “Na Roho ya Bwana ilikua juu ya uso wa maji” Roho wa Mungu (Ruach Elohim) ni pumzi ya Mungu, ni Roho itiayo uhai na uzima, inayobadilisha na yenye mamlaka ya kufanya kila kitu upya. Ni uwepo wa Mungu anayetenda kazi kwa nguvu na uweza. Ndugu mpendwa Roho huyu wa Mungu ndiye aliyewashukia Mitume siku ya Pentekoste, akawaimarisha Mitume na akapuliza pumzi yake ya uhai ndani ya Kanisa ili liwe hai na imara katika kuishuhudia Injili. Ndiye Roho huyu huyu ambaye sisi sote tumempokea katika ubatizo, roho atokaye kwa Baba na Mwana, na tukaimarishwa kwa mapaji yake katika sakramenti ya Kipaimara. Ni roho anayefanya hata sasa kila kitu upya ndani ya mioyo yetu, awekaye moyo wa nyama na kutoa moyo wa jiwe ndani mwetu. Kwa njia ya Roho Mtakatifu, Kristo ametupatia karama mbalimbali za kiroho ambazo zote kama tulivyotafakarishwa Dominika iliyopita ni kama viungo vingi ambayo vyote vinafanya mwili mmoja. Roho Mtakatifu anatupa nguvu ya kuujenga mwili wa Kristo kwa njia ya karama na vipaji mbalimbali vya Roho Mtakatifu.

Roho Mtakatifu ni Nafsi ya Tatu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu
Roho Mtakatifu ni Nafsi ya Tatu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu

Tatu: Uwepo wa Neno wa Mungu (Divine Logos) Zab 33:6. Mzaburi katika Zaburi hii ya 33:6 anatuambia, “Kwa Neno la Bwana, Mbingu zilifanyika” Hii yatuonesha kuwa Neno wa Bwana amekuwapo tangu milele yote na kwa njia yake mbingu zilifanyika. Neno huyu (Divine Logos) ndiye Bwana wetu Yesu Kristo ambaye alitwaa mwili akakaa kwetu, kama anavyoeleza Mwinjili Yohane katika utangulizi wa Injili ya nne (Yn 1:14). Mwinjili Yohane anatuambia tena katika somo la Injili Takatifu katika shehere hii, kwamba ni kwa sababu ya upendo usio na mipaka, sifa hii ya Mungu, ndiyo sababu Mungu aliamua kumtuma kwetu mwanaye wa pekee, Neno wake wa milele, ili kwa njia yake tusipotee bali tuwe na uzima wa milele (Yn 3:16-18). Jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanaye wa pekee, ili kila amwaminiye asipotee bali awe na uzima wa milele.” Ndiye Mungu aliyetwaa hali yetu ya kibinadamu ili atuumbe upya baada ya anguko la wazazi wetu wa kwanza na kupoteza neema ya utakaso yaani uzima wa kimungu ndani mwetu. Kazi ya ukombozi hivyo ni kazi ya utatu Mtakatifu. Mungu Baba aliyeupenda hivyo ulimwengu alimtuma mwanaye wa pekee ambaye kwa njia ya Roho Mtakatifu akatimiza kazi ya baba ya kuuletea ulimwengu ukombozi wa milele. Tunapokataa kumsadiki Mungu, tunajihukumu wenywe kwa sababu tutajitenga Mungu. Nne: Hekima kama nafsi pamoja na Mungu (Mit 8). Katika kitabu cha Mithali, hekima yajionesha kama nafsi aliyekuwa pamoja na Mungu kabla ya kuumbwa ulimwengu. Mababa wa Kanisa wanaeleza hekima hii kuwa ndiye Bwana wetu Yesu Kristo, tukirejea katika 1 Kor 1:23-24, Mtume Paulo anaposema: “Bali sisi tunamhubiri Kristo aliyesulibiwa; kwa Wayahudi ni kikwazo na kwa Wayunani ni upuuzi. Bali kwao waitwao Wayahudi kwa Wayunani, Kristo ni nguvu ya Mungu na Hekima ya Mungu”. Hebu tutazame Fumbo hili katika Agano jipya.

Yesu Kristo, Nafsi ya Pili Katika Fumbo la Utatu Mtakatifu
Yesu Kristo, Nafsi ya Pili Katika Fumbo la Utatu Mtakatifu   (@Vatican Media)

Fumbo la Utatu Mtakatifu katika Agano Jipya: Fumbo la Utatu Mtakatifu, kama ilivyokuwa katika Agano la kale, halielezwi pia wazi wazi kama “Utatu Mtakatifu” pia hata katika Agano jipya. Hakuna maelezo ya moja kwa moja kutoka katika Maandiko Matakatifu yanayoeleza juu ya Fumbo hili Takatifu. Licha ya hayo, katika Agano Jipya, tunaona jinsi Mungu ambaye hatua kwa hatua, katika matukio mbalimbali ya historia ya ukombozi, alianza kufunua fumbo hili kuanzia uumbaji, sasa tunaona namna kazi ya ukombozi wa mwanadamu ilivyo tunda la umoja huu Mtakatifu, inavyokamilishwa katika Agano jipya. Fumbo hili linadhihirika namna gani katika Agano jipya? Kwanza: Utatu Mtakatifu katika Fumbo Takatifu la Umwilisho. Katika fumbo la umwilisho tunamshangilia Neno wa Mungu aliyetwaa mwili akakaa kati yetu. Ni neno aliyekuwa kwa Baba tangu milele yote kama tunavyokiri katika kanuni ya Imani yetu. Malaika Gabrieli anavyompasha Habari Maria anawambia, “Roho Mtakatifu atakujilia juu yako na nguvu zake aliye juu zitakufunika kama kivuli, na hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu Mwana wa Mungu” Lk 2:35. Kumbe Mungu Baba, “Yeye aliye juu” anaanzisha mpango huu wa ukombozi, wa kumleta kwetu Neno wake wa milele kwa njia ya Roho Mtakatifu. Nafsi zote zinaonekana katika fumbo hili takatifu la Umwilisho. Kupitia umwilisho wa Neno wa Mungu, nafsi ya pili ya utatu Mtakatifu, tunajifunza umuhimu wa utii na ukubali (kama wa Bikira Maria) ili kuruhusu mapenzi ya Utatu Mtakatifu yatimie maishani mwetu, kila siku ya maisha yetu. Mapenzi ya Mungu si mapenzi yetu na hivyo tunapaswa kuomba maongozi yake.

Kristo Yesu Ni Ufunuo wa Huruma na Upendo wa Baba wa Milele
Kristo Yesu Ni Ufunuo wa Huruma na Upendo wa Baba wa Milele   (@Vatican Media)

Pili: Utatu Mtakatifu katika Ubatizo wa Bwana wetu Yesu Kristo. Katika ubatizo wa Yesu, Fumbo la Utatu Mtakafu ladhihirika. Mtoni Yordani, sauti ya Baba ilisikika kutoka mbinguni ikisema, “Huyu ni mwanangu mpendwa wangu, ninayependezwa naye (Mt 3:17.” Sauti ya Mungu Baba inasikika kutoka mbinguni, Mungu Mwana anabatizwa mtoni Yordani kabla ya kuanza rasmi utume wake wa wazi, na hapo Roho Mtakatifu anashuka kwa mfano wa hua na kukaa juu yake, ishara kwamba utume wake utaongozwa na Roho Mtakatifu. Tatu: Utatu Mtakatifu katika Utume wa Bwana wetu Yesu Kristo. Kristo anapoanza utume wake wa wazi, akiwa katika sinagogi huko Nazareti anasoma kutoka katika chuo cha Nabii Isaya, “Roho wa Bwana yu juu yangu, kwa maana amenitia mafuta kuhubiri maskini Habari Njema” (Lk 4:16). Yesu, Mwana wa Mungu anahubiri Habari Njema na kuponya, akitiwa nguvu na Roho Mtakatifu. Anafanya kazi aliyotumwa na Baba kwa ajili ya ukombozi wa ulimwengu. Kristo anatuambia katika Injili ya Yohane 8:29, “Yeye aliyenipeleka yu pamoja nami, hakuniacha peke yangu, kwa sababu nafanya siku zote yale yampendezayo. Kumbe kazi ya ukombozi ni kazi ya utatu Mtakatifu. Kazi ya utume wa Kristo ni kumfunua kwetu Baba kwa njia ya Roho Mtakatifu nasi tumemjua Baba. Nne: Utatu Mtakatifu katika Mateso na Kifo cha Bwana wetu Yesu Kristo. Kristo kwa njia ya Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na mawaa, sadaka iliyokubaliwa na Mungu Baba, tunasoma katika waraka kwa waebrania 9:14). Mungu Baba kwa upendo mkubwa anamtoa Mwanaye wa pekee Yesu Kristo kama sadaka ya upatanisho kati yake na sisi. Akiwa Getsemane katika mateso, Yesu anasali, akimwomba Baba, ishara ya ukaribu na muunganiko wake wa pekee na Mungu Baba yake. Mwinjili Yohane anatuamba kuwa, pale msalabani Yesu alitoa roho (Yoh 19:30), ishara kwamba, Kristo kwa kifo chake anatoa Roho Mtakatifu kwa ulimwengu.  Hivyo hapa twaona ushiriki wa nafsi zote tatu za Mungu katika mateso na kifo cha Bwana wetu Yesu Kristo.

Ufufuko wa Kristo Yesu ni ushindi wa mateso, dhambi na mauti
Ufufuko wa Kristo Yesu ni ushindi wa mateso, dhambi na mauti

Tano: Utatu Mtakatifu katika Ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo ni ushindi dhidi ya kifo na mauti.  Paulo anaandika, “Lakini ikiwa Roho wake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani yenu.” Rum 8:11. Ufufuko wa Kristo hautuoneshi tu ya kuwa Kristo ni mzima, yu hai, bali unatuonesha jinsi Baba, Mwana na Roho Mtakatifu walivyoshiriki pamoja katika kuleta uumbaji mpya, ukombozi na uzima wa milele, tunda la ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo kutoka wafu. Ijapokuwa fundisho la Utatu Mtakatifu halitajwi wazi hapa, ufufuko wa Kristo watuonesha namna nafsi zote tatu zilivyoshiriki kwa namna ya pekee kabisa na katika uhusiano wa ajabu katika ufufuko wa Kristo. Sita: Utatu Mtakatifu katika Pentekoste. Bwana wetu Yesu Kristo alipokuwa bado pamoja na wanafunzi wake, aliwaahidi kwamba hatowaacha yatima. Atamtuma kwao Roho Mtakatifu, zawadi ya Baba. Kristo mwana wa Mungu akiisha kukamilisha kazi ya ukombozi aliyotumwa na Baba hapa duniani alipaa mbinguni (Mdo 2:33) Kisha Mungu Baba anatimiza ahadi ya zawadi aliyoisemea Yesu kwa Mitume wake, na Roho Mtakatifu anatumwa, anayewafundisha na kuwakumbusha yote ambayo Kristo alikwisha kuwafundisha alipokuwa bado pamoja nao. Wakiisha kupokea Roho Mtakatifu, waliimarishwa nao wakaenda kutoka ushuhuda. Saba: Utatu Mtakatifu katika Utume wa Mitume wa Kristo na Utume wa Kanisa. Kristo anawaachia Mitume wake utume kabla ya kupaa kwake kurudi kwa Baba yake wa mbinguni. Yesu anawapa utume, kwamba walipaswa kwenda kuwafanya watu wa mataifa yote kuwa wanafunzi wa Kristo, wakiwabatiza kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu (Mt 28:18). Kazi ya mitume ilikuwa kuusimikia ufalme wa Mungu kwa watu wa mataifa yote. Hii ni kazi ya utatu Mtakatifu. Ndiyo kazi na utume wa Kanisa hata sasa, kuhubiri Habari Njema na kusimika Ufalme wa Mungu kati ya watu wa Mataifa yote. Tunajifunza wajibu wetu wa kimishenari kama Mitume wa Kristo; kila mkristo ana wito wa kuhubiri Habari Njema kwa maneno na matendo yake ya kila siku.

Fumbo la Utatu Mtakatifu ni kielelezo cha umoja na upendo kamili.
Fumbo la Utatu Mtakatifu ni kielelezo cha umoja na upendo kamili.   (@Vatican Media)

Tunapoadhimisha sherehe ya Utatu Mtakatifu tuna mambo yafuatayo ya kujifunza. Fundisho la kwanza: Utatu Mtakatifu ni Mfano Bora wa Umoja na Upendo (Perichoresis). Katika taalimungu neno la Kigiriki “Perichoresis” laonesha na kumaanisha ushirikiano wa ndani kabisa wa kimungu). Kama tulivyotafakari hapo mwanzo, fundisho hili lina maana kwamba Nafsi tatu za Utatu Mtakatifu ziko katika muungano mkamilifu wa upendo hivi kwamba kila mmoja anaishi ndani ya mwenzake bila kupoteza utambulisho wake. Baba si Mwana, Mwana si Roho, lakini wote ni Mungu mmoja kwa sababu ya upendo wao kamili. Hakuna ushindani, wivu, au ubinafsi kati yao Ndugu mpendwa, katika maisha yetu ya kila siku, sherehe hii inatufundisha kuwa umoja wa kweli haumaanishi watu wote wafanane au wafikiri sawa. Katika familia zetu, katika jumuiya zetu, katika mahali pa kazi, tunaweza kuwa na vipaji tofauti, mitazamo tofauti, na majukumu tofauti, lakini bado tunaweza kuwa wamoja kupitia upendo, ushirikiano na kuheshimiana. Katika ndoa, katika mahusiano na urafiki, upendo wa Utatu unatufundisha kumpenda mtu jinsi alivyo, bila kujaribu kumfanya awe kama wewe au pengine kumtawala. Sherehe hii inatualika kuchukuliana kwa upendo licha ya tofauti zilizopo kati yetu, kwa kuwa ni dhahiri kwamba hatuwezi wote kuwa sawa. Je, tunapokeana? Tunavumiliana? Ni mara ngapi tofauti zetu, za vipato, mishahara, vyeo, itikadi na mitazamo vimekua vyanzo vya maanguko, mafarakano na mpasuko katika jamii yetu, katika familia zetu? Mara kadhaa huenda tunaona kama wenye mawazo tofauti nasi ni maadui. Tunakumbushwa leo kuchukuliana kwa upendo na upole licha ya tofauti zetu. Inatuhimiza kuachana na tabia za kuchafuana, kuharibiana majiana au kushindana, na badala yake kusaidiana ili kufikia malengo ya pamoja. Mara kadhaa tunaweza kuona waliopiga hatua kidogo kuliko sisi kama ni tishio na hivyo kupanga, kukusudia, kuratibu au hata kutelekeza mipango ya kuwaangusha, kuwafelisha, kuwarudisha nyuma au kuwaharibia hatma yao. Tofauti zetu ziwe daima utajiri wetu. Lakini pia tuepuke pia kufanya ushirika katika mambo yanayotutenga na Mungu.

Utatu Mtakatifu ni Fumbo la Imani
Utatu Mtakatifu ni Fumbo la Imani   (@Vatican Media)

Fundisho la pili: Fumbo la Utatu Mtakatifu linatukumbusha wajibu wetu wa unyenyekevu Mbele ya Fumbo la Imani. Mtakatifu Augustino anatufudhisha kuwa akili ya mwanadamu ni kama kijiko kidogo kinachojaribu kuzoa maji yote ya bahari; haina uwezo wa kumaliza kumwelewa Mungu aliye mkuu na wa milele. Sherehe ya Utatu inatukumbusha kuwa Mungu yuko juu sana ya mawazo yetu na hawezi kuwekwa katika sanduku la mantiki ya kibinadamu pekee. Kumbe sherehe hii ndugu mpendwa inatufundisha sisi sote unyenyekevu wa kutotafuta majawabu ya kiakili kwa kila fumbo la maisha. Kuna mambo mengi yanayotokea katika maisha yetu ya kila siku, kama vile mateso ya wasio na hatia au majanga, ambayo hatuwezi kuyatolea maelezo kamili. Unyenyekevu mbele ya fumbo unatusaidia kusema hata katikati ya kina cha maumivu yetu, "Sielewi kwa nini hili linatokea, lakini ninamwamini Mungu." Mara kadhaa tunaweza kuwaza, akili, fedha, mali, vyeo, madaraka vyaweza kujibu kila changamoto na maswali magumu ya maisha yetu, lakini kiuhalisia sivyo. Tunapaswa kujisalimisha kwa Mungu na kuamini kwamba Yeye anajua mwisho tangu mwanzo, hata pale njia zetu zinapokuwa na giza. Tuseme daima kama Musa, “Ikiwa nimepata sasa nimepata neema mbele zako, Bwana nakuomba, Bwana uende kati yetu...Enda nasi, katika familia zetu, katika kazi zetu za kila siku, katika mahangaiko yetu, katika maumivu yetu, ukatwae tuwe urithi wako” Fundisho la Tatu: Fumbo la Utatu Mtakatifu linatukumbusha kila mara thamani ya alama ya Msalaba. Kama nilivyotangulia kusema, kila mara tunapofanya ishara ya msalaba tunakiri Fumbo hili la Utatu Mtakatifu. Alama ya Msalaba ni sala fupi zaidi lakini yenye nguvu kubwa zaidi katika imani yetu. Tunapoweka ishara hii, tunafanya mambo mawili kwa wakati mmoja; kwanza, tunakiri Msalaba wa Kristo kama njia ya ukombozi, na pili, tunakiri Majina ya Utatu Mtakatifu (utambulisho wetu). Si tu ishara ya nje, bali ni tangazo la kiroho la umiliki, kwamba sisi ni mali ya Mungu Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu. Kuna namna maisha yaweza kutusahaulisha, tukakimbia na kutoka kwenye umiliki wa Mungu, na kutafuta ulinzi na usalama katika mambo mengine. Bwana yu daima katikati yetu, nasi tumeitwa kwa jina lake, hatotuacha (Yer 14:9).

Fumbo la Utatu Mtakatifu ni ushuhuda wa utukufu
Fumbo la Utatu Mtakatifu ni ushuhuda wa utukufu   (@Vatican Media)

Ndugu mpendwa, kila mara unapoanza siku yako, unapoamka, unapoingia kwenye gari, unapoanza safari au usiku unapoenda kulala na kuweka ishara ya msalaba, unajizungushia ukuta na ulinzi wa kimungu. Unatangaza kuwa mazingira yako yanatawaliwa na Utatu Mtakatifu na sio na nguvu za giza au hofu sio mashaka au nguvu zingine. Kumbe tunapoanza kila jambo na Mungu kwa sala tunaposema, "Kwa jina la Baba..." kabla ya kuanza biashara au masomo, safari, mikutano, tunamaanisha kuwa jambo hilo tunalifanya kwa sifa utukufu wa Mungu, jambo linalokuzuia kufanya udanganyifu au uovu katika kazi hiyo, na kukuepusha na hatari mbalimbali zinazoweza kutupata.  Tutakua daima na hofu ya Mungu katika kila tutendalo, lakini pia yote tunayofanya yatajazwa neema na Baraka za Mungu mwenyewe. Je, ni mara ngapi ninakumbuka kuanza na ishara ya Msalaba kila ninapoamka? Mara nyingi tunawahi simu, mitandao ya kijamii, kuona dunia inasema nini na kusahau kumsikia kwanza Mungu anasema nini na sisi katika sala hiyo fupi na rahisi kabisa kusali. Tuombe neema ya kukumbuka kila mara kuanza na Mungu. Fundisho la nne: Sherehe hii inatukumbusha Wito wetu wa Utakatifu. Sisi sote tumeumbwa kwa mfano na sura ya Mungu (Mwanzo 1:26). Kwa sababu Mungu wetu ni Utatu unaoishi katika utakatifu, na sisi tuna asili hiyo ndani yetu. Utakatifu si kwa ajili ya viongozi wa dini pekee, bali ni wito wa kila mwanadamu kuishi maisha yanayoakisi tabia za Mungu: wema wa Baba, huruma ya Mwana, na usafi wa Roho Mtakatifu.

Kristo Yesu ni Ufunuo wa huruma na upendo wa Baba wa Milele
Kristo Yesu ni Ufunuo wa huruma na upendo wa Baba wa Milele   (@VATICAN MEDIA)

Ndugu mpendwa, Fumbo la utatu Mtakatifu linatusaidia sisi sote daima kuelewa hadhi na thamani kubwa tuliyo nayo mbele za Mwenyezi Mungu kama tulivyotafakari katika kitabu cha mithali. Wewe si kiumbe cha bahati mbaya; sisi ni hekalu linalokaliwa na Utatu Mtakatifu. Kumbe Sherehe hii inatualika daima tutunze miili yetu na roho zetu kama hekalu, kama makazi safi ya Mungu. Tunaalikwa kuomba nguvu na Roho Mtakafiu ili tuweze kuachana na vilema vyetu mbalimbali na mambo yote yanayoweza kuchafua hadhi hiyo ya Utakatifu tuliyoipata katika ubatizo wetu, na tunayoendelea kuipata kila mara kwa njia ya Mama Kanisa Mtakatifu kwa njia ya Sakramenti mbalimbali. Lakini pia katika maisha yetu ya kila siku, tunaitwa kuwaonyesha watu wengine sura ya Mungu. Tunapotoa msamaha, tunaonyesha upendo wa Mwana; tunapofariji anayelia, unaonyesha kazi ya Roho Mtakatifu; na unapotunza na kulinda wengine, unaonesha malezi ya Baba. Hitimisho: Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, na upendo wa Mungu Baba, na ushirika wa Roho Mtakatifu viwe nanyi nyote.

Fumbo Utatu Mtakatifu 2026
29 Mei 2026, 10:23