Tafakari Utatu Mtakatifu: Fumbo la Imani & Msingi wa Maisha ya Kikristo!
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu, katika sherehe ya Utatu Mtakatifu. Mababa wa Kanisa wanasema, Imani Katoliki mintarafu Fumbo la Utatu Mtakatifu ndiyo hii: “Tunamwabudu Mungu Mmoja katika Utatu na Utatu katika Umoja, bila kugawanyika Nafsi, wala kutenganisha Uwamo; kwani ni Nafsi ya Baba, ya Mwana na Roho Mtakatifu. Ni umungu mmoja wa Baba, na wa Mwana na wa Roho Mtakatifu, utukufu ulio sawa, ukuu wa pamoja wa milele.” Wimbo wa mwanzo unaweka wazi dhamira ya Sherehe hii ukisema hivi; “Asifiwe Mungu Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; kwa sababu ametufanyizia huruma yake.” Ni sherehe ya Fumbo kuu halisi la imani, msingi wa mafumbo mengine na wa maisha ya kikristo. Katekisimu ya Kanisa Katoliki inafundisha hivi kuhusu hili fumbo; Utatu Mtakatifu ni fumbo la imani kwa maana halisi kwa kuwa limefichika ndani ya Mungu, ni fumbo la Mungu ndani yake mwenyewe. Fumbo hili haliwezi kujulikana, kufahamika, wala kuelezeka kwa akili ya kibinadamu peke yake kwa kuwa liko juu ya uwezo wake wa kuelewa. Lakini Mungu kwa upendo wake ametufunulia, kutuelewesha na kutufahamisha kuwa yeye ni mmoja katika nafsi tatu, yaani, Mungu Baba, Mungu Mwana, na Mungu Roho Mtakatifu. Nafsi zake hizi tatu, zina uwamo, uwapo, na asili moja ya kimungu, kwa maana kwamba hazigawani umungu wake mmoja, bali kila mmoja wao ni Mungu kamili katika asili hiyo hiyo, Baba ni vile alivyo Mwana, Mwana ni vile alivyo Baba, Baba na Mwana ni vile alivyo Roho Mtakatifu. Uhusiano wa mmoja kwa wengine ndio unaoonyesha tofauti yao: Baba si Mwana, Mwana si Baba, wala Roho Mtakatifu si Baba wala si Mwana. Baba ndiye anayezaa, Mwana ndiye aliyezaliwa, Roho Mtakatifu ndiye anayetoka (Rej. KKK 234, 237, 251-254, na 261).
Hivyo sisi tunasadiki na kuamini juu ya fumbo hili la utatu Mtakatifu, siyo kwa sababu ya utambuzi wa akili zetu, bali kwa kuwa Mungu mwenyewe ametufunulia hivyo. Mtakatifu Augustino anatuasa akisema; “Inatupasa kusadiki kwa sababu Mungu ametufunulia”. Ni katika mukatadha huu mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi; “Ee Mungu Baba, uliwafumbulia watu fumbo lako la ajabu, hapo ulipompeleka Neno wako na Roho Mtakatifu ulimwenguni. Utujalie kuutambua utukufu wa Utatu Mtakatifu wa milele katika kuungama imani ya kweli na kuabudu Umoja wa Mungu katika enzi ya fahari yake.” Fumbo hili la Utatu Mtakatifu ni moyo, na kiini cha imani na maisha ya Kikristo. Ndiyo maana zetu sala zote lazima zianze na kumalizika kwa ishara ya Msalaba inayoambata na kutamka maneno haya: “Kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu.” Hii ni namna fupi na rahisi ya kukiri kile tunachokiamini na kukikiri katika Kanuni ya Imani katika sehemu kuu tatu tukisema: “Nasadiki kwa Mungu mmoja Baba Mwenyezi, mwumba wa mbingu na Dunia… na kwa Yesu Kristo, Mwana wa pekee wa Mungu, aliyeshuka toka mbinguni kwa ajili yetu sisi wanadamu na kwa ajili ya wokovu wetu…na kwa Roho Mtakatifu, Bwana mleta uzima…” Ni katika ufahamu huu, Mama Kanisa katika sala ya utangulizi wa Sherehe hii anasali hivi; “Ee Bwana, Baba mwema, Mungu Mwenyezi wa milele. Wewe pamoja na Mwanao wa pekee na Roho Mtakatifu, u Mungu mmoja na Bwana mmoja, siyo katika umoja wa nafsi, ila katika Utatu wa umungu mmoja. Mambo tunayoyasadiki juu ya utukufu wako kwa sababu ya ufunuo wako, tuna yasadiki pia juu ya Mwanao na juu ya Roho Mtakatifu pasipo tofauti ya kutengana. Nasi tunapoungama Umungu wa kweli na wa milele, tunaabudu nafsi zilizo mbalimbali za Mungu mmoja zenye utukufu ulio sawa.”
Somo la kwanza ni la Kutoka katika Kitabu cha Kutoka (Kut. 34:4b-6, 8-9). Nalo linatueleza kuwa kama Mungu angekuwa Bwana mwenye haki tu, hatungekuwa na tumaini la wokovu. Lakini Yeye ni mwingi wa huruma na fadhili. Kwa hiyo tunatumaini kwamba ingawa sisi tu watu wadhambi tena wenye shingo ngumu, atatusamehe uovu wetu tunapoukiri na kuomba msamaha kwa moyo wa majuto na kutustahilisha kuingia katika utukufu wa ufalme wake mbinguni. Ni katika tumaini hili Danieli alipoutafakari ukuu wa huruma ya Mungu aliishia kutamka maneno haya ya wimbo wa katikati akisema; “Umehimidiwa, Ee Bwana, Mungu wa baba zetu: Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele. Limehimidiwa jina lako takatifu, tukufu; Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele. Umehimidiwa katika hekalu la fahari yako takatifu; Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele. Umehindiwa juu ya kiti cha ufalme wako; Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele. Umehimidiwa utazamaye vilindi, uketiye juu ya makerubi; Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele. Umehimidiwa katika anga la mbinguni; Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele” (Dn. 3:52-56). Somo la Pili ni la Waraka wa Pili wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (2Kor. 13:11-14). Ni hitimisho la Waraka huu, ambapo mtume Paulo anawaasa Wakorinto waachane na tofauti zinazowafanya watengane na wajitahidi kuishi kwa umoja akisema; “Hatimaye ndugu kwa herini; mtimilike, mfarijike, nieni mamoja, mkae katika amani; na Mungu wa upendo na amani atakuwa pamoja nanyi. Salimianeni kwa busu takatifu…Neema ya Bwana Yesu Kristo, na pendo la Mungu Baba…na ushirika wa Roho Mtakatifu vikae nanyi nyote.” Salamu hii ya mwisho inaukiri Utatu Mtakatifu kwa kuonyesha kuwa pendo la Mungu limedhihirika kwetu katika neema ya Yesu Kristo, inayofanya kazi yake katika Kanisa kwa njia ya Roho Mtakatifu. Hivi ukombozi wetu ni kazi ya Utatu Mtakatifu, na mapato yake ni furaha, amani, upendo, mshikamanoo na umoja.
Injili ni kama ilivyoandikwa na Yohane (Yn. 3:16-18). Ni mazungumzo kati ya Yesu na Nikodemu. Katika mazungumzo haya Yesu anatufunulia kuwa fumbo la ukombozi wetu ni tunda la upendo wa kazi ya Utatu Mtakatifu kwamba; “Mungu aliupenda ulimwengu hivi, hata akamtoa Mwanae wa pekee, ili kila amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwengu ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwamimiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa.” Kumbe, tunaona kuwa sehemu hii ya Injili inatoa ufunuo kuwa; Mipango yote ya Mungu inayohusu fumbo la wokovu ni kazi ya pamoja ya nafsi tatu za Mungu. Lakini, kila nafsi inatekeleza kazi yake ya pamoja kufuatana na hali yake kama nafsi (rej. KKK 258). “Katika kazi moja moja za Mungu kila nafsi huonyesha kile kilicho chake katika Utatu na hasa katika utume wa Mungu wa Umwilisho wa Mwana na utume wa paji la Roho Mtakatifu” (KKK 267). “Na maisha yote ya kikristo ni ushirika wa kila nafsi ya Mungu bila kuzitenganisha kwa namna yoyote. Anayemtukuza Baba hufanya hivyo kwa njia ya Mwana, katika Roho Mtakatifu; anayemfuata Kristo, anafanya hivyo kwa sababu Baba anamvuta na kwa sababu Roho Mtakatifu anamwongoza” (KKK 259).
Kwa kuhitimisha, Sherehe hii ya Utatu Mtakatifu inatuhimiza nasi tuwe na umoja katika maisha yetu tukisaidiana katika taabu na raha. Basi tumwombe Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu, watukirimie fadhila ya umoja na mapendo zitusaidie kuishi vyema hapa duniani, ili mwisho wa yote tukaunganike nao na watakatifu wote na kuishi pamoja nao kwa upendo huko mbinguni kama sala baada ya komunyo inahitimsiha maadhimisho haya ikisema; “Ee Bwana Mungu wetu, sakramenti hii tuliyoipokea ituletee afya ya mwili na roho, na kutuwezesha kuungama Umoja wa Mungu katika Utatu Mtakatifu wa milele”. Na hili ndilo tumaini letu. Tumsifu Yesu Kristo!