Tafuta

Ushirikiano kati ya Masista wa Mpango wa Sisters Blended Value Project wa  Mfuko wa Hilton Fo na ACWECA. Ushirikiano kati ya Masista wa Mpango wa Sisters Blended Value Project wa Mfuko wa Hilton Fo na ACWECA. 

Mpango wa kubadilisha utume wa watawa barani Afrika

Mpango wa Watawa wa thamani uliochanganywa,unawapatia watawa Wakatoliki barani Afrika ujuzi wa kubadilisha utume wao kuwa biashara endelevu za kijamii.Mpango huu unalenga kujenga uwezo,upatikanaji wa fedha,masoko na ushirikiano ili kuimarisha kujiamini kwa masista na kuboresha usimamizi wa taasisi,unaoongozwa na Dkt.Angela Ndunge wa Chuo Kikuu cha ya Biashara cha Strathmore.

Na Sr. Christine Masivo, CPS

Dk. Angela Ndunge wa Chuo Kikuu cha Biashara cha Strathmore, mlei anayefanya kazi pamoja na watawa, na kuongoza mpango uitwao: “Sisters Blended Value Project” yaani,  “Mpango wa Watawa wa thamani uliochanganywa,” alieleza kuwa mpango huo "ulizinduliwa ili kuwasaidia watawa kufikiria upya uendelevu na kuimarisha taasisi zao." Mpango huo umekuwa ukiendeshwa kwa miaka sita na unaungwa mkono na Mfuko wa Conrad N. Hilton kwa kushirikiana na ACWECA (Umoja wa Mashirika ya Watawa wa Mashariki na Kati mwa Afrika). Ulianzia Kenya, Uganda, Tanzania, na Zambia na sasa umepanuka hadi Malawi. Akizungumza na Vatican News, Dk. Ndunge alisema kwamba,  "watawa wamekuwa nguzo ya matumaini kwa wengi, wakihudumu katika elimu, huduma za afya na uhamasishaji wa kijamii, mara nyingi miongoni mwa jamii zilizotengwa." Janga la Uviko -19 lilikuwa baya sana na lilionesha udhaifu wa huduma nyingi za watawa. Hivi ndivyo mpango ulivyoanza, ukilenga kuwasaidia watawa katika kubadilisha huduma zao za kijamii kuwa biashara endelevu za kijamii.

Janga la Uviko liliathii jamii zilizo hatarini

Janga la Ugonjwa wa Uviko  lilikuwa hatua ya mabadiliko katika mashirika ya watawa, wale waliokuwa wanafanya utume katika shule na hospitali walilazimika kufunga au kupunguza shughuli. "Watawa wengi katika kipindi hicho waliathiriwa na uhaba wa fedha," Dk. Ndunge alielezea. "Janga hili liliathiri jamii zilizo hatarini ambazo masista huhudumia, na kusisitiza hitaji la uendelevu wa muda mrefu na maandalizi bora kwa misiba ya siku zijazo." Hii ilizua maswali muhimu kuhusu uendelevu wa mipango hii tofauti na huduma za kijamii.

Kujenga watawa kwa kuwapa ujuzi

Mpango huu unalenga kujenga uwezo. Dk. Ndunge alibainisha kuwa watawa wengi huitwa kuchukua majukumu ya usimamizi, lakini mara nyingi huwana ujuzi wa kiufundi unaohitajika au maono ya kimkakati ya muda mrefu kwa huduma zao. Kupitia mafunzo, watawa wanajifunza kupanga bajeti, kuweka kumbukumbu, uongozi na kupanga mikakati. Ujuzi huu huwasaidia kuhama kutoka kwa mifumo ya kitamaduni ya hisani hadi ujasiriamali wa kijamii. "Hapo awali, watawa wamekuwa wakizingatia kufanya utume wao kwa upendo na kupokea msaada kutoka kwa wafadhili," alielezea. "Tunawasaidia kufikiria kuhusu ujasiriamali wa kijamii, na kuzalisha aina za mapato zinazotosha kusaidia huduma hizi za kijamii kila mara."

Upatikanaji wa ufadhili na masoko

"Watawa wamekabiliwa na changamoto kubwa sana katika kupata ufadhili," Dk. Ndunge alisema. Alibainisha kuwa hii ilisababisha hofu na kusita miongoni mwa mashirika mengi, wanapojitahidi kupata usaidizi wa kifedha na katika baadhi ya matukio, wametumiwa vibaya na wanaowasaidia. Mpango huu unawasaidia watawa kutambua ufadhili wa kimaadili na ubunifu huku pia wakiboresha uelewa wao wa kifedha, huku wakisaidiwa kupata masoko ya huduma na bidhaa zao. Mashirika mengi yana mashamba, shule na vituo vya afya ambavyo havina mikakati ya kuongeza uwezo wao wa kiuchumi.

Historia ya mafanikio

Mpango huu umebadilisha kwa kiasi kikubwa huduma ya ushonaji inayoendeshwa na watawa huko Kitui, Kenya. Hapo awali walikuwa wakitengeneza sare za shule kwa kiasi kidogo cha kujipatia kipato, baadaye walipata mafunzo ya uboreshaji wa bidhaa, usimamizi wa biashara na ukuaji wa kimkakati, ambayo yaliimarisha shughuli zao na ushindani. Matokeo yake, walipewa zabuni kutoka chuo kikuu ili kushona gauni za kuhitimu baada ya kufikia viwango vya juu vya ubora. Mafanikio haya yalionesha mabadiliko makubwa, yakibadilisha mpango wao wa ndani kuwa biashara ya kijamii yenye ushindani. Zaidi ya kuongeza uendelevu wa kifedha, mafanikio hayo yaliongeza kujiamini kwao kushirikiana na masoko makubwa, kuonyesha jinsi ujenzi wa uwezo unaolengwa unavyoweza kuwasaidia watawa kupanua huduma zao huku wakiendelea kuwa waaminifu katika utume wao.

Ushirikiano na motisha

Dk.  Ndunge alisisitiza kwamba watawa walihimizwa kushirikiana kama mashirika ya kitawa wakisaidiana kwa kujifunza kwa wengine na kutumia huduma za wao wenyewe, kama vile kununua mazao ya shambani au kupata huduma ya afya kutoka kwa taasisi zinazoendeshwa na watawa. Ushirikiano huu unaimarisha dhamira yao na uendelevu wa muda mrefu. Licha ya changamoto kama vile umbali na hali ngumu wanapofanya utume, intaneti ya chini na umeme unaopotea kila mara, watawa wengi wanabaki na hamu ya kujifunza na kuendeleza mbinu mpya za uendelevu huku wakiwezesha jamii zao.

Utume unaonawiri wa baadaye

Dk. Ndunge alisema wanatumaini kuona mpango huo ukiendelea kuimarisha huduma za watawa ili waweze kufanya vema katika utume wao, alisisitiza. "Wanapaswa kukumbuka wito na karama zao kila wakati, haijalishi wanachofanya ni kidogo au kikubwa kiasi gani." Pia alisisitiza umuhimu wa kusawazisha utume na ustawi wa kibinafsi na kutunza mahitaji ya msingi, huku akielezea matumaini ya usaidizi mkubwa kutoka kwa washirika. Mpango huu unafufua kujiamini na kujenga ujuzi, mitandao na uwezo wa uongozi ili kuhakikisha huduma endelevu na uinjilishaji.

MPANGO WA WATAWA AFRIKA

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.

05 Juni 2026, 09:19