Tafakari Dominika 13 Ya Mwaka A: Gharama na Thawabu za Ufuasi
Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.
Utangulizi: Wapendwa Familia ya Mungu, ni Dominika ya 13 mwaka A wa Kanisa. Liturujia ya Neno la Mungu inatutafakarisha juu ya, “Gharama na Thawabu ya Ufuasi wa kweli” Masomo ya Dominika ya hii yanatupatia picha kamili ya nini maana ya kuwa kweli Mfuasi wa Kristo. Kumfuata Kristo kweli, si kazi rahisi, yatudai sadaka na gharama kubwa. Yatudai kujikana wenyewe, kuchukua kila mmoja msalaba wake kila siku na kumfuata Kristo katika njia yake. Matokeo ya kuishi kiaminifu ufuasi wetu ni neema na baraka tele na thawabu katika uzima wa milele. Katika Dominika hii, tuombe neema ya kupokea wito wa Kristo na kuishi kiaminifu ufuasi wetu kila siku ya maisha yetu, ili tustahilishwe kupata tuzo Mbinguni katika uzima wa milele pamoja naye. Somo la Injili: Ni Injili ya Mathayo 10:37-42. Katika somo la Injili Takatifu Dominika iliyopita, dominika ya 12 mwaka A, Kristo akiendelea na hotuba yake juu ya utume kwa wanafunzi wake katika sura hii ya 10 ya Injili ya Mathayo, aliwaalika “Wasiogope” Alifahamu kuwa ufuasi na utume wao kwake hautakuwa rahisi, hivyo aliwaandaa nao kisaikolojia kuupokea na kuuelewa ukweli na uhalisia huo hata kabla yeye mwenyewe hajaingia katika mateso yake, na hata kabla hajawatuma bado. Kristo anaendelea na sehemu ya mwisho ya hotuba yake hii ndefu kuhusu utume, na katika dominika hii ya 13 anawafundisha Mitume wake nasi sote juu ya gharama au masharti ya ufuasi na thawabu ya ufuasi huo wa wa kweli kwake. Katika somo hili la Injili ningependa tutafakari kwa kina juu ya mambo yafuatayo yatakayotusaidia kuelewa ujumbe mkuu ambao Mama Kanisa anatutafakarisha katika dominika hii ya 13 mwaka A wa Kanisa.
Jambo la kwanza: Ufuasi wa kweli, kwanza unatudai kufanya maamuzi magumu katika maisha kwa ajili ya Kristo: Kumpa Mungu daima nafasi ya kwanza. Katika somo hili la Injili Kristo anaanza kwa kutoa fundisho ambalo sio tu lilionekana gumu kwa wanafunzi wake bali hata kwetu sasa laweza kuonekana pia kuwa ni gumu kwa kiasi fulani. Tukumbuke aya mbili nyuma, kabla ya sehemu hii tuliyoisikia leo Kristo alikwisha sema, “Sikuja kuleta amani duniani, bali upanga (aya ya 34-36)”. Upanga huu unamaanisha kuwa Habari njema ya Ufalme wa Mungu iliyohubiriwa na Kristo na wanafunzi wake, ni wazi kwamba ingetenganisha na kuleta mgawanyiko kati ya wale waliyoipokea na wale wanaoikataa. Kristo anaeleza wazi kwamba Injili italeta upinzani mkubwa kiasi kwamba maadui wa mtu watakuwa ni wale wale wa nyumbani mwake mwenyewe (baba dhidi ya mtoto, mama dhidi ya binti, ndugu dhidi ya ndugu nk). Kwa nini? Kwa sababu ya kutofautiana kiimani, na kupokea au kutokupokea Injili. Aya hizi tunaweza kusema ndizo zinazofungua sehemu hii tuliyoisikia leo. Kristo Anasema sasa, “Apendaye Baba au Mama kuliko mimi, hanistahili; au apendaye mwana au binti kuliko mimi, hanistahili” (aya ya 37). Katika tamaduni za Wayahudi kama ilivyo pia katika tamaduni zetu sisi Waafrika, Familia ilikua ni taasisi muhimu sana katika jamii. Familia ilikua ndio kila kitu, ni utambulisho, ni utajiri, ni hadhi, ni ulinzi, ni heshima, ilikuwa ni mustakabali wa mtu na jamii kwa ujumla. Katika muktadha au uelewa huo, Kristo anatoa fundisho hilo gumu kwamba, “Asiyeichukia familia yake, huyo hanistahili” Je, Kristo alitaka tuzichukie familia zetu? Je, anaenda kinyume na Amri ya nne ya Mungu inayotudai kuwapenda na kuwaheshimu Wazazi na amri kuu ya mapendo inayotudai kumpenda Mungu na kupendana sisi kwa sisi? La hasha. Yesu hapingi upendo wa kifamilia wala hatufundishi kuwachukia wazazi na ndugu zetu, wala hatufundishi pia kuwaacha na kuwatelekeza. Anachokifundisha Kristo kwa wanafunzi wake hapa ni kufanya maamuzi magumu katika kumfuasa kweli, yaani au kuchagua au kuacha. Au kumpa Mungu nafasi ya kwanza, au kuwapa ndugu, jamaa na familia na mambo mengine ya kidunia nafasi ya kwanza.
Ndugu mpendwa, ni wazi kuwa maisha yetu/uhai wetu, familia zetu, fedha na mali, elimu na urithi mbalimbali tulio nazo kwa namna ya vitu hai na visivyo hai, yote haya yana thamani kubwa. Lakini hayo yote ni zawadi za Mungu tu kwa mwanadamu na tena ni mambo yanayodumu kwa kitambo kidogo tu. Kuna jambo la thamani zaidi kuliko haya nalo ni kumchangua kwanza Mungu na kubaki daima katika ufalme wa Mungu, kubaki katika muunganiko na Mungu aliye mtakatifu sana na chanzo cha mambo hayo yote hata sisi wenyewe. Hakuna kitu chochote hapa duniani kinachoweza kuchukua nafasi yake. Ifahamike kuwa katika sehemu hii ya Injili Yesu hatuambii tutupe vitu tulivyonavyo au kuziacha familia zetu, au kuyaacha maisha yetu na kadhalilika. Anachotuambia hapa ni kwamba vyote ni vya thamani lakini kuna kitu cha thamani zaidi kuliko vyote nacho ni Ufalme wa Mungu na kwamba tunapaswa kuwa tayari kuachilia mambo mengine yote kama yanakuwa kikwazo cha kubaki katika ufalme wa Mungu.
Jambo la pili: Ufuasi wa kweli kwa Kristo unatudai kuchukua msalaba wetu kila siku na kumfuta Kristo katika njia yake. Kristo anaendelea kwa kutoa sharti la pili la kuwa mfuasi wake kwamba, “Na wala mtu asiyechukua msalaba wake akanifuata, hanistahili.” Katika utawala wa Warumi katika wakati huu wa Yesu, msalaba ulikuwa na ulijulikana kama chombo cha adhabu ya kifo, fedheha, maumivu na aibu kubwa. Msalaba ulikuwa ni adhabu kwa wale waliokuwa wahalifu, waliohukumiwa adhabu ya kifo, wakishurutishwa kuubeba msalaba baada ya mateso makali, kabla ya kusulibiwa na kufa. Kumbe, mtu aliyebeba msalaba alikuwa njiani kuelekea kwenye kifo chake na kawaida asingeweza mtu yeyote kukubali adhabu hiyo kwa hiyari yake mwenyewe, isipokuwa Bwana wetu Yesu Kristo aliyefanya hivyo kwa ajili ya ukombozi wetu. Kristo sasa hapa anawaambia wanafunzi wake, yeye asiyeuchukua Msalaba wake, akanifuata, huyo hanistahili. Ndugu mpendwa, Neno lililotumika katika lugha ya kigiriki “Kuchukua Msalaba” (kai hos ou lambanei ton stauron autou) linamaanisha tendo la hiyari, kuchukua kwa makusudi, pasipo shuruti, au kuchagua kubeba kwa kupenda. Halimaanishi kulazimishwa kama ilivyokuwa adhabu hii mbaya katika dola ya Kirumi. Kwa fundisho hili, Yesu anamaanisha, kuwa ufuasi, kuchukua msalaba, ni tendo la mwanafunzi au Mfuasi wake kuitikia wito kwa utayari wa moyo, akijua gharama yake, na kuamua bado mwenyewe kwa hiyari yake kuubeba msalaba wake kila siku na kumfuata yeye.
Mwanataalimungu maarufu kutoka Ujerumani Dietrich Bonhoeffer, katika kitabu chake kinachoitwa “Gharama ya Ufuasi” anasema, “Wakati Kristo anapomwita mtu awe mfuasi wake, anamwamuru aje na afe.” (When Christ calls a man, he bids him come and die.) Kulingana na Bonhoeffer, kifo hiki si lazima kiwe cha kumwaga damu kama alivyokufa yeye Kristo Msalabani kwa kuwa hakuna awezaye kutoa sadaka kama ya Kristo, bali ni kifo cha kujikana nafsi. Ni kifo cha kuua matamanio na tamaa za utu wa kale, ubinafsi, vilema na udhaifu wetu mbalimbali, kuacha usalama wa kidunia, na kusalimisha mipango yote ya maisha mbele ya Kristo. Ni kukubali fedheha, matusi, dharau, mateso, kwa ajili ya Imani, kwa ajili ya Injili. Kumfuata Yesu ndugu mpendwa kunamtoa mtu kwenye maisha ya usalama wa kijamii na kumwingiza kwenye maisha yasiyo na usalama, yenye mahangaiko, changamoto na hatari nyingi, lakini yenye tegemeo kamili kwa Mungu.
Kubeba Msalaba ni kushiriki Mateso ya Kristo kila siku ya maisha yetu. Msalaba unamaanisha kusimama upande wa wanyonge, maskini, waliosahaulika na kutupwa nje na jamii, na wanaoteseka kwa dhuluma na uonevu, hata kama kufanya hivyo kutakuletea upinzani kutoka kwa wenye nguvu na mamlaka. Kubeba Msalaba ni kupokea majukumu yote yatokanayo na miito yetu. Kila mbatizwa anatolea maisha yake kuiishi kiaminifu Injili na kuwa shuhuda wa Kristo kwa maneno na matendo. Kisha kwa miito mingine mbalimbali. Wazazi wanatoa uhai wao, nguvu, sadaka na jitihada zao kwa ajili ya kulea na kutunza familia kama wachungaji pamoja na Kristo kwa hiyari yao. Hiyo ni sadaka kubwa. Wamisionari wanatolea maisha yao, mapadre, watawa wanatolea maisha yao kwa ajili ya Kristo kwa nadhiri, ufukara, utii na usafi wa moyo, si kwa kulazimishwa bali kwa hiyari yao kwa ajili ya Ufalme wa Mungu. Huu ni wito wa kila siku, ni wito wa maisha yetu yote. Ndiyo kuishi kama Kristo Yesu mwenyewe.
Fundisho la Tatu: Anayempokea Mjumbe wa Kristo, kwa sadaka ya Upendo, huyo ampokea Kristo mwenyewe. Matokeo yake ni baraka tele na thawabu. Katika sehemu ya mwisho ya Injili hii, Kristo anasema, “Awapokeaye ninyi, anipokea mimi; naye anipokeaye mimi ampokea yeye aliyenituma. Katika utamaduni wa kale wa Mashariki ya Kati na wa Kiyahudi, kulikuwa na sheria ya uwakilishi iliyoitwa “Shaliach” kwa Kiebrania. Kanuni hii inasema: “Mjumbe wa mtu ni kama mtu huyo mwenyewe.” Kumbe Kristo kwanza kabisa anawakumbusha Mitume wake kwamba, hakuna utengano kati yao wao wanaotumwa, na yeye Mchungaji mwema anayewatuma kwenda kutangaza Injili. Wao kama wajumbe wa Kristo, wanamwalikilisha na wanabeba ujumbe wa Kristo Mwenyewe. Aliyewapokea, alimpokea Kristo mwenyewe. Na ampokeaye Kristo, huyu ampokea yeye aliyemtuma Kristo. Hali kadhalika anayewakataa amkataa Kristo, amkataa Mungu mwenyewe. Ndugu mpendwa wanafunzi wengi wa Yesu walikuwa ni watu wa kawaida, wavuvi wa samaki, watoza ushuru, na watu wasio na elimu kubwa au ushawishi mkubwa sana wa kijamii na wa kisiasa. Walipokuwa wakienda ulimwenguni kuhubiri Injili, walikabiliwa na hatari ya kudharauliwa na kutokupokelewa na kutokusikilizwa. Kristo anawapa moyo kwamba, hawaitendi kazi yao, wala hawakwendi peke yao. Kumbe Kristo anawafundisha na anatufundisha sisi sote aliotuita, akatustahilisha na anatutuma kila siku kumshuhudia kwamba, yeye ndiye Kichwa nasi sote tu viungo vya mwili wake yaani Kanisa. Kristo hatengani kamwe na Kanisa lake, wala wajumbe wa Habari Njema ya Ufalme wake. Na hivyo hatupaswi kuogopa hata pale watu watakapoukataa ujumbe wa Kristo, kwa kuwa hawatukatai sisi bali wamkataa Mungu mwenyewe.
Tunapohubiri Injili lazima tukumbuke kuwa si Injili yetu, bali ni Injili ya Kristo. Hatupaswi kuwahubiria watu mambo yetu, wala kutumia Injili kwa faida na manufaa yetu, wala kuhubiri kuwafurahisha watu, yale tu wanayopenda kuyasikia, bali kumtangaza Kristo, wakati ufaao na wakati usiofaa. Ni wazi upinzani utakuwepo kama walivyomkataa Kristo mwenyewe au kama walivyowakataa manabii katika Agano la Kale, nasi tujue kuwa kuna nyakati ujumbe na wajumbe wote hawatapokeleka. Lakini Kristo anaendelea kwa kutukumbusha kuwa ipo thawabu kwa wote wanaoipokea Injili na wanaowapokea wajumbe wa Injili ya Kristo. Anasema, “Na mtu awaye yote ayakayemnywesha mmojawapo wa wadogo hawa walau kikombe cha maji ya baridi kwa kuwa ni mwanafunzi, huyo haitampotea kamwe thawabu yake. Israeli ni nchi iliyoko Mashariki ya Kati yenye maeneo makubwa ya jangwa, miamba, na joto kali. Katika mazingira hayo, kupata maji ya baridi haikuwa jambo rahisi kama kufungua jokofu au bomba la kisasa. Maji yalipaswa kutekwa mapema asubuhi sana kutoka visima vyenye kina kirefu, au kuhifadhiwa kwa ustadi mkubwa kwenye mitungi maalum ya udongo iliyowekwa chini ya ardhi ili yabaki na ubaridi. Kumbe kutoa maji ya baridi kulihitaji jitihada, maandalizi, na nia thabiti ya kutaka kumfariji mgeni aliyechoka kwa jua. Kwa kuweka msingi kwenye kikombe cha maji, kiasi kidogo tu ambacho mtu yeyote angeweza kutenda kuonesha ukarimu, Yesu anaondoa kisingizio cha umaskini. Kila mtu, hata maskini wa mwisho asiye na sarafu hata moja ya fedha au dhahabu walau anamiliki maji. Kwa hiyo ni kusema kwamba, kila mtu ana uwezo wa kutoa msaada na kupokea thawabu ya mbinguni si kwa kuwa anavyo vingi, bali kwa kuwa anatoa kidogo kwa upendo mkubwa. Hakuna asiyestahili kupata thawabu, kama matokeo ya ufuasi wetu kwa Kristo kwa sababu yoyote ile.
Somo la 1: Ni kitabu cha Pili cha Wafalme 4:8-11, 14-16. Katika somo la kwanza kutoka kitabu cha pili cha Wafalme, tunaona bado namna tukishirikiana na Mungu na wajumbe wake tunavyoweza kupata baraka na thawabu. Somo hili linatupa simulizi ya Mwanamke Mshunemi na Nabii Elisha. Mwanamke huyu alimtendea wema Mtu wa Mungu kwa kumkaribisha na kumfanyia chumba nabii Elisha na matokeo yake alipata baraka ya mtoto ingawa yeye na mumewe walikua wazee. Kumbe hapa tunaona Fundisho la Kristo wazi kabisa aliposema “Naye ampokeaye Nabii kwa kuwa ni Nabii, atapata thawabu ya Nabii” Mwanamke Mshunemi alimpokea Elisha kama Nabii na matokeo yake akapata thawabu ya Nabii. Somo hili linaendelea na kutufundisha kwamba: Ndungu mpendwa, ukarimu unalipa na ni chanzo cha thawabu na baraka tele. Thawabu na baraka ni matokeo ya ukarimu na kutengezea nafasi kwa ajili ya Mungu na kwa ajili ya wajumbe wake. Tunapowatendea wengine wema, hasa wale wanaofanya kazi ya Mungu, tunajifungulia milango ya baraka ambazo hukutarajia maishani. Mwanamke Mshunemu alitambua kuwa Elisha alikuwa mtu mtakatifu wa Mungu. Tumwombe Mungu atujalie nasi daima kuwa na macho ya kiroho ili kuwatambua na kuwaheshimu watu wa Mungu na wahitaji wanaotuzunguka katika jamii yetu. Mwanamke huyu alitoa chumba na chakula kwa upendo safi bila kujua kama atapewa zawadi ya mtoto. Alitoa huduma ya upendo kwanza pasi na kutafuta faida au fidia. Mwenyezi Mungu anaangalia usafi wa nia yetu tunapojitoa kuwasaidia wengine. Haangalii wingi wala ukumbwa, bali nia ya ndani kabisa ya moyo kwenye kila sadaka tunayotoa kwa ajili ya wengine na kwa ajili ya Mungu. Kumbe kama Kristo alivyotufundisha katika somo la Injili Takatifu, kila mmoja wetu kadiri ya Mungu alivyomjalia, ana kila sababu ya kupata thawabu ikiwa ataamua kumpa Mwenyezi Mungu nafasi, na kufungua moyo pia katika huduma ya upendo kwa wengine. Haituhitaji fedha nyingi ili tuwe watakatifu, haihitaji utajiri mkubwa ili tupate thawabu kutokana na utumishi na ufuasi wetu kwa Kristo. Tunahitaji moyo uliofunguka kwa ajili ya Mungu na kwa ajili ya wengine. Mwenyezi Mungu mwenye anayetambua haja za mioyo yetu, atajaza kile kinachopungua kwetu kwa namna yake vile kama alivyoijaza familia ile kwa neema na baraka zake kama thawabu ya ukarimu wao.
Somo la Pili: Ni Kutoka Katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi 6:3-4, 8-11. Katika somo hili la Pili Mtume Paulo anatukumbusha nini maana ya ufuasi wetu kama Wakristo. Kwa njia ya Ubatizo tumekufa na kufufuka pamoja na Kristo, na kupokea wito wa maisha mapya ya utakatifu ndani ya Kristo. Ni wito wa kila siku ya maisha yetu, kama anavyotualika Kristo, kujikana nafsi, kuchukua msalaba na kumfuata yeye katika njia yake. Hivyo hatupaswi tena kutawaliwa na maisha ya kale, kwa kuwa kifo wala mauti havina nguvu tena juu yetu. Matokeo ya kuuishi kweli na kwa uaminifu wito wetu huu wa kuwa wafuasi wa Kristo ni thawabu na tuzo ya kuishi na Kristo katika uzima wa milele baada ya maisha yetu ya hapa duniani. Tukikubali kila siku ya maisha yetu kufa kwa ajili ya Kristo, kwa kuuishi vyema na kwa uaminifu mkubwa ufuasi wetu basi tutakuwa daima hai kwa Mungu katika Kristo Yesu. Hitimisho: Katika Dominika ya Kumi na tatu ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa tuombe neema ya kupokea wito wa Kristo Yesu na kuishi kiaminifu ufuasi wetu kila siku ya maisha yetu, ili tustahilishwe kupata tuzo Mbinguni katika uzima wa milele pamoja na Kristo Yesu.