Tafuta

Wito wa Mapadre katika Jimbo Kuu la Arusha -Tanzania. Wito wa Mapadre katika Jimbo Kuu la Arusha -Tanzania.  

Ask.Mkuu Amani:Wito ni zawadi ya Imani na Ujasiri

Mapadre wanalo jukumu la kuwaongoza watu katika kumfuata Mungu kwa uchaji, kwa kufanya kazi na kuwaongoza katika toba ya kweli.Kwa kuwa upadre ni kujitoa sadaka,wanapaswa kuwa tayari kujisadaka kwa ajili ya mambo yamhusuyo Mungu.Alisema hayo Askofu Mkuu Amani wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha,Tanzania,wakati wa kutoa Daraja Takatifu la Upadre kwa mashemasi,Julai 9,katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu.

Na Sr Ernestina Patrikck Lasway,SCA - Arusha,Tanzania.

Wito wa Upadre unaongozwa na Imani na Upendo, sawa na miito mingine ilivyo. Askofu Mkuu Isaac Amani alibainisha hayo, katika adhimisho la Misa Takatifu ya upadrisho iliyofanyika  tarehe 9 Julai 2026 katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu Jimboni Arusha nchini Tanzania. Katika homilia yake, Askofu Amani alibainisha kuwa wito wa upadre unalenga kuwaongoza wengine kwa Mungu kama mchungaji afanyavyo kuwaongoza katika malisho yaliyo sahihi na salama.

Jimbo kuu la Arusha Tanzania na miito ya kipadre
Jimbo kuu la Arusha Tanzania na miito ya kipadre

Wajibu wa Padre katika Kanisa

Akiendelea na homilia yake, Askofu aliwaalika mapadre kuwalisha kondoo kwa maarifa na busara, kwa fahamu na usahihi. “Mapadre wanalo jukumu la kuwaongoza watu katika kumfuata Mungu kwa uchaji, kwa kufanya kazi na kuwaongoza katika toba ya kweli,” alikazia. Kwa kuongozwa na mfano wa  Nabii Yeremia (Yer.23:4),   anatuongoza kutupatia wachungaji ambao hawataleta hofu miongoni mwa watu  na hilo ndilo kusudi la Mungu.  Mapadre ni sawasawa na manabii, makuhani na wafalme, wanatengwa kwa kupakwa mafuta ili kumtolea Mungu sadaka na kumpatanisha mwanadamu na muumba wake. Katika historia ya wokovu, Mungu aliwatuma manabii kwa nyakati tofauti kuwaongoza watu katika utumishi adimilifu na kufanya Ibada adilifu,” alisisitiza.

Umuhimu wa kuwatii manabii

Manabii na mitume waliposikilizwa na watu,walipokea baraka, walipoenda kinyume na ujumbe wa manabii na mitume, waliadhibiwa. Katika Injili ya siku (Yh. 10:11-21) Yesu anajitambulisha kama Mchungaji Mwema. Mchungaji mwenye kuwaongoza kondoo katika malisho yaliyo salama. Walio wake wanamfuata katika njia sahihi na salama. Kumfuata mcunhuja sahihi kama Kristo alivyofanya Kristo kwa kumfuata Baba na kwa njia hii kumkomboa mwanadamu “Nami nautoa uhai wangu kwa ajili ya Kondoo zangu.”

Mapadre wapya wa Jimbo Kuu la Arusha.
Mapadre wapya wa Jimbo Kuu la Arusha.

Yesu Kristo Mchungaji Mkuu

“Mungu anamthibisha Bwana wetu Yesu Kristo kama Mchungaji mkuu. Kwa upendo wake kwa Mwanadamu, anaudhihirisha kwa njia ya Kristo. Kwa njia hii anawaita wengine kuwa wachungaji, walimu, manabii ili kuujenga mwili wa Kristo kwa majitoleo katika nafasi mbalimbali,” alibainisha Askofu Mkuu Amani. Kwa njia hii padre analo jukumu la kujifunza kila mara kutoka kwa mchungaji mkuu Yesu Kristo kwa ufanisi katika utume wa kila siku.

Umuhimu wa kusoma alama za nyakati

“Ili kuwa mchungaji mwema,” Askofu Mkuu  Amani aliwataka mapadre wapya “kusoma vyema alama za nyakati. Kwa kuwa upadre ni kujitoa sadaka, mapadre wanapaswa kuwa tayari kujisadaka kwa ajili ya mambo yamhusuyo Mungu (Ebr. 5:1-14).” Katika utume wa kikuhani, mapadre wanapaswa kufanya kazi kwa ajili ya ufalme wa Mungu kwa kuwatumilkia watu wa Mungu katika hali zote. Kwa njia hii lazima padre kutumia katika utume na kuwahudumia watu wa Mungu kwa upendo na majitolea ya dhati.

Wanaitwa na Kutumwa

Mapadre wapya, mara baada ya upadrisho, walitumwa kufanya utume sehemu mbalimbali ndani na nje ya Tanzania. Miongoni mwao ni mapadre watatu wa Shirika la Wafransiskani Wakapuchini(OFMcap) na Kumi na moja wa Jimbo Kuu Katokili Arusha.

Mapadre Mapya wa Jimbo Kuu la Arusha mbele ya Altare
Mapadre Mapya wa Jimbo Kuu la Arusha mbele ya Altare

Mapadre hawa ni:

Padre Aplhonse Bahati, wa Parokia ya Mashati Rombo

Padre  Epiphany Joseph  Mushi wa Uru Shimbwe,

Padre Juvenalis Donasian Mwendapole wa Parokia ya Mt.Fransisco wa Assisi- Kwangulelo,

Padre Joseph Kweyemamu wa Parokia ya Mtakatifu Theresa Arusha,

Padre Vedastus Method  Waziri wa Mkuu Rombo na Parokia ya Roho Mtakatifu Ngarenaro,

Padre Emmanuel Lazaro Mollel wa Parokia ya Polisingisi,

Padre Joseph Josephat wa Parokia ya Mtakatifu Ambrosi Kibuka – Sinoni,

Padre Emmanuel Mazoya Peter wa Parokia ya Maji ya Chai,

Padre Gido Adolfu Kimario wa Parokia ya Mtakatifu  Karoli Lwanga- Usa River,

Padre Priva Julian Kirango kutoka Parokia ya Kristo Mfalme Chekereni,

Padre Erasto Otto Lekule wa Parokia ya Mtakatifu Simon Mtume Loruvani,

Padre Elton  Njau wa Parokia ya Mtakatifu Yoseph Mume wa Bikira Maria- Patandi,

Padre Joseph Salvatory Chuwa OFMCap, Padre Adelardi Shirima OFMCap, na

Padre Jackson Noel Swai, OFMCap.

 Tuwaombee mapadre wapya ili wadumu katika wito wao.

Wakati wa Misa ya Upadrisho Jimbo Kuu la Arusha Tanzania.
Wakati wa Misa ya Upadrisho Jimbo Kuu la Arusha Tanzania.

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.

10 Julai 2026, 12:43