Tafuta

Watu wa Haiti wanahitaji msaada wa kila kitu. Watu wa Haiti wanahitaji msaada wa kila kitu.  (World Food Programme)

Haiti:Maelfu ya wakimbizi na vurugu mpya wakati wa mgogoro wa kibinadamu

Maelfu ya watu wamekimbia makazi yao katika mlipuko mpya wa vurugu za kutumia silaha nchini Haiti katika maeneo ya Artibonite na Magharibi na kuongeza upungufu mkubwa wa misaada wa dharura ya kibinadamu.Ukosefu wa usalama umevuruga huduma za afya na raia kukimbia makazi yao,huku Kanisa na mashirika ya kibinadamu yakilazimika kuingilia kati,wakiendelea kudumisha elimu, uhamasishaji wa kichungaji na shughuli za kibinadamu.

Na Sr. Christine Masivo, CPS – Vatican.

Kuna mgogoro mkubwa wa kibinadamu nchini Haiti, na unaendelea kuwa mbaya zaidi huku vurugu mpya za kutumia silaha zikilazimisha familia nyingi kukimbia makwao na kuzidisha mzigo wa huduma za umma ambazo tayari ni dhaifu. Shirika la Kimataifa la Wahamiaji (IOM) liliripoti kwamba watu 2600 walikimbia makazi yao katika eneo la Artibonite kufuatia mapigano kati ya vikundi vyenye silaha siku chache zilizopita.

Zaidi ya robo tatu ya waliokimbia makazi yao walitafuta hifadhi katika manispaa ya Marchand Dessalines. Mapigano mapya katika manispaa ya Cité Soleil, katika eneo la Magharibi, ambayo yalianza tarehe 13 Juni 2026, yalilazimisha zaidi ya watu 5,000 kukimbia kwa ajili ya usalama kutoka majumbani mwao, kulingana na shirika la IOM, na kuongeza maelfu ya watu waliokimbia makazi yao kati ya Machi na Mei kutokana na vurugu za kutumia silaha katika eneo hilo.

Mahitaji ya wakimbizi na kibinadamu yanaongezeka

Vurugu hizi mpya zimesababisha kuzorota kwa usalama katika sehemu nyingi za Haiti, huku kukiwa na uhaba wa huduma muhimu pamoja na mahitaji ya kibinadamu, ikiwa ni pamoja na chakula, maji safi, na huduma za afya. Kulingana na Shirika la Kipapa la Habari za Kimisionari, Fides, nchi hiyo inakabiliwa na ongezeko la watu kulazimishwa kurudi makwao, na iliripoti kwamba kulingana na IOM, zaidi ya watu 25,000 walilazimika kurudi Haiti mnamo Mei 2026. Kati ya Januari na Juni mwaka 2026, idadi ya waliorudi ilizidi 11,700, huku wanawake wakiwakilisha robo ya idadi ya watu na asilimia nane ikiwa ni ya watoto, na kuongeza changamoto iliyopo kuhusu ukosefu wa usalama na rasilimali chache.

Huduma ya afya iko hatarini

Huduma ya afya imeathiriwa na kukatizwa sana, hasa kwa wale wanaohudumia wanawake na watoto. Madaktari Wasio na Mipaka (Médecins Sans Frontières (MSF) wamesimamisha shughuli katika kituo chake cha uzazi huko Cité Soleil kutokana na ukosefu wa usalama unaowanyima maelfu ya wanawake huduma ya afya ya uzazi. Basi upatikanaji wa huduma ya afya unabaki kuwa moja ya wasiwasi wa dharura kwa jamii zilizoathiriwa na vurugu zinazoendelea.

Hata hivyo, mashirika ya Kikanisa yanaendelea na uwepo wao wa kichungaji na kibinadamu licha ya kufanya kazi chini ya hali ngumu zaidi, kutoa makazi, kutoa msaada wa kibinadamu, na kusaidia familia zilizo katika mazingira magumu katika maeneo ambayo huduma za serikali ni chache. Viongozi wa kanisa wamekuwa wakiomba amani, mazungumzo, na heshima kwa maisha ya binadamu kila mara.

Utume wa Parokia unaendelea katikati ya mgogoro

Katika eneo la milimani la Pourcine Pic Makaya, Parokia ya Mama Yetu, wa Msada wa Daima (Notre-Dame-du-Perpétuel-Secours) inaendelea kusaidia Jumuiya za wenyeji kupitia mpango wake wa KIWO, unaoongozwa na mmisionari wa Shirika la Wacamillian,  Padre Massimo Miraglio. Akitafakari kuhusu dhamira ya chama cha KIWO, Padre Miraglio alisema kwamba watoto sitini, vijana, na watu wazima walikusanyika kwa shughuli ya hivi karibuni ya parokia kwa ajili ya siku ya maombi, huduma ya jamii na ushirika karibu na mto ulio karibu na Parokia. Walisafisha eneo hilo na kushiriki mlo pamoja kabla ya kurudi parokiani.

Padre Miraglio alitoa maoni zaidi kwamba katika mwaka wa shule uliomalizika hivi karibuni katika shule ya Parokia ya Mama Yetu wa Msaada wa Daima, licha ya changamoto nyingi zinazowakabili walimu na wanafunzi, kuna maendeleo katika mahudhurio, kuchelewa, usafi wa kibinafsi, na ushiriki katika shughuli za shule. Pia alisisitiza kukamilika kwa mafanikio kwa programu ya kusoma na kuandika ya parokia, ambayo iliwakusanya washiriki kutoka jamii kadhaa za wenyeji baada ya miezi sita ya masomo. Maandalizi sasa yanaendelea kwa mwaka wa masomo wa 2026-2027 huku Parokia ikiendelea na utume wake ya kielimu na kichungaji huku changamoto za kibinadamu na usalama zinazoendelea nchini.

HAITI

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.

04 Julai 2026, 15:10