Tafuta

2026.07.11 Tamasha la Flores nchini Indonesia. 2026.07.11 Tamasha la Flores nchini Indonesia. 

Indonesia:Hija ya Maria huko Flores yahamasisha utunzaji wa uumbaji

Askofu wa Labuan Bajo katika kisiwa cha Flores cha Indonesia alizindua hija ya Juma moja kwa ajili ya Mama Yetu wa aliyepalizwa Mbinguni,kabla ya Tamasha ya kila mwaka la Golo Koe mwezi Agosti.Hija ya mwaka 2026 inalenga kuunganisha ibada ya Maria na uwajibikaji wa kutunza mazingira.

Na Br. Kasmir Nema, SVD - Labuan Bajo, Indonesia

Hija ya Mama Maria itakayovuka vilima na vijiji vya Kisiwa cha Flores cha Indonesia inawaalika Wakatoliki kuimarisha sio tu kujitolea kwa Bikira Maria bali pia kujitolea kwao kutunza uumbaji. Mnamo tarehe 10 Julai 2026, Askofu Maksimus Regus wa Labuan Bajo, alizindua Maandamano Makubwa ya Maria Mpalizwa Mbinguni(Nusantara) katika Parokia ya Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi huko Lengkong Cepang, akizindua ziara hii ya Juma moja ya kutembeza sanamu ya Mama Yetu Mpalizwa Mbinguni kupitia Parokia kadhaa kabla ya Tamasha la kila mwaka la Golo Koe kufikia kilele chake mwezi Agosti.

Tamasha la Flores nchini Indonesia kabla ya Sherehe ya Mama Mpalizwa
Tamasha la Flores nchini Indonesia kabla ya Sherehe ya Mama Mpalizwa

Hija ya mwaka huu 2026 ina ujumbe tofauti. Kwa kuongozwa na kauli mbiu "Hija ya Kijumuiya katika Ushirika wa Pamoja ili Kutunza Uadilifu wa Uumbaji," Jimbo la Labuan Bajo linaunganisha kujitolea kwa Mama Maria na uwajibikaji wa mazingira, ikirudia wito wa Papa Francisco wa Laudato Si' kwa ajili ya ubadilishaji wa mazingira unaotokana na imani.

Hija yenye dhamira ya ikolojia/mazingira

Mkazo wa mazingira ulikuwa tayari dhahiri wakati tamasha hilo lilipozinduliwa rasmi tarehe 4 Juni 2026 sanjari na Siku ya Mazingira Duniani. Akizungumza katika Ufukwe wa Sudamala huko Labuan Bajo, Askofu Regus alisema ubinadamu unakabiliwa na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira, akiwataka watu wa kila imani kukumbatia ubadilishaji wa ikolojia ya mazingira unaooneshwa kwa vitendo halisi. Uzinduzi huo ulijumuisha usafi wa ufukwe, upandaji wa miti ya nazi kando kando ya pwani, na kurushwa  kwa Njiwa kama ishara za amani na utunzaji wa kazi ya  uumbaji. Kiongozi wa West Manggarai Edistasius Endi pia aliwahimiza washiriki kuhakikisha kwamba ujumbe wa ikolojia/mazingira wa tamasha hilo unakuwa ahadi iliyo hai badala ya mada ya sherehe tu.

Ushuhuda wa udugu

Hija pia iliakisi utamaduni wa eneo hilo wa maelewano kati ya dini mbalimbali. Sanamu ya Maria ilipopita katika kijiji cha Nanga Lili, wakazi wa Kiislamu waliikaribisha maandamano hayo kwa ngoma ya kiutamaduni ya Manggarai, wakitoa ishara ya ukarimu iliyoaonesha uhusiano wa karibu ulioshirikiwa na jamii tofauti za kidini. Sanamu hiyo kisha ilibebwa kwa maandamano hadi Parokia ya Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi huku kukiwa na maombi ya nyimbo za Mama Maria na kusali rozari, ambapo waamini waliikaribisha kwa kitambaa cha kitamaduni cha nyimbo, ishara ya heshima mahalia.

Tamasha la Flores nchini indonesia
Tamasha la Flores nchini indonesia

"Maria humleta Kristo kila wakati"

Wakati wa Misa ya ufunguzi, Askofu Regus alitafakari kuhusu Ziara hiyo, akiwakumbusha waamini kwamba popote Mama Maria anapokwenda, anawaongoza watu kwa Mwanawe. Akikumbuka ziara ya Mama Maria kwa Elizabeth, alisema hija hiyo inaalika familia na jamii kumkabidhi matumaini yao kwa Kristo, akiongeza kwamba Wakristo pia wameitwa kuwa wabebaji wa matumaini, furaha na upendo duniani. Misa Takatifu iliadhimishwa kwa pamoja na mapadre kutoka kwenye nyumba ya Jimbo na dinari ya Wae Nakeng.

Br. Ivan Selman, mwenyekiti wa kamati ya Tamasha la Golo Koe, alisema hija ya Marian ndiyo moyo wa kiroho wa tamasha hilo. Kabla ya maelfu kukusanyika Labuan Bajo kwa ajili ya sherehe za mwisho, alielezea, kuwa sanamu ya Mama Maria hutembelea kila parokia kwanza, akielezea wito wa Kanisa wa kutembea pamoja katika ushirika.

Imani, utamaduni na utunzaji wa nyumba ya pamoja

Katika toleo lake la tano, Tamasha la Golo Koe limekuwa mojawapo ya sherehe kuu za kidini na kiutamaduni nchini Indonesia na limejumuishwa miongoni mwa Matukio 10 Bora ya Kharisma Event Nusantara nchini, mpango wa kitaifa wa utalii. Ikiwa karibu na Hifadhi la wanyama la Kitaifa ya Komodo, Labuan Bajo imeshuhudia ukuaji wa haraka wa utalii katika miaka ya hivi karibuni. Jimbo hilo linaona tamasha hilo kama fursa ya kuunganisha imani, utamaduni wa ndani na utunzaji wa mazingira, ikiwahimiza wageni kukutana sio tu na uzuri wa Flores bali pia jukumu la kulinda mifumo yake tete ya ikolojia.

Sherehe za kilele cha tamasha hilo, zilizopangwa kufanyika kuanzia tarehe 10 – 15 Agosti 2026, zitajumuisha maonesho ya kiutamaduni, ngoma ya kitamaduni ya Manggarai Caci, kuadhimisha Misa Takatifu, na mipango ya mazingira inayowahusisha vijana, shule na jamii za wenyeji, ikiwa ni pamoja na upandaji miti na shughuli za usafi wa ufukweni.

Tamasha la Flores
Tamasha la Flores

Wakati huo huo, sanamu ya Mama Yetu Mpalizwa itaendelea na hija yake kupitia dinari ya Wae Nakeng, Pacar na Labuan Bajo kabla ya kufika katika Kanisa Kuu la Roho Mtakatifu mapema Agosti kwa ajili ya Maandamano ya Grand Marian. Kwa Askofu Regus, ziara hii ni kipindi cha  maombi na upyaishaji unaoanza katika mioyo ya waamini na kuenea nje kwa upendo kwa kila mmoja na kwa ajili ya nyumba ya pamoja iliyokabidhiwa kwa wote.

Indonesia hija ya Flores

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.

 

13 Julai 2026, 11:58