Padre Wabanhu, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha SAUT, Tanzania
Martine Nyoni - SAUT DIGITAL., - Mwanza, Tanzania
Askofu Wolfgang Pisa, OFM Cap, wa Jimbo Katoliki la Lindi, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), ambaye pia ni Kansela wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino cha Tanzania (SAUT), amemteua Padre Emmanuel Charles Wabanhu kuwa Makamu Mkuu wa Chuo cha SAUT kuanzia tarehe 1 Agosti 2026. Uteuzi huo umefanyika kwa mujibu wa Ibara ya 11 ikisomwa pamoja na Kanuni ya 10 ya Hati ya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino Tanzania ya mwaka 2012, iliyochapishwa kupitia Tangazo la Serikali Na. 580 la mwaka 2020 chini ya Sheria ya Vyuo Vikuu, Sura ya 346, Toleo Lililofanyiwa Marejeo la mwaka 2023.
Prof. Wabanhu ni Padre wa Jimbo Katoliki la Geita na Profesa Mshiriki mwenye tajiriba kubwa katika taaluma ya Taalimungu Maadili, akibobea katika Maadili Tetezi (Applied Ethics). Amekuwa Mhadhiri mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki (CUEA), Nairobi nchini Kenya kwa zaidi ya miaka 13, kabla ya kuhudumu kwa miaka miwili kama Naibu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Utawala na Fedha katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Mihayo cha Tabora (AMUCTA).
Mbali na uzoefu wake wa kitaaluma, Prof. Wabanhu ameandika vitabu vitano na kuchapisha zaidi ya makala 20 za kitaaluma katika majarida yanayotambuliwa kimataifa. Kitaaluma, anashikilia Shahada ya Kwanza ya Taalimungu kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana, Roma nchini Italia, Shahada za Uzamili katika Masomo ya Dini na Taalimungu, Shahada ya Uzamivu ya Taalimungu (STD), pamoja na Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Maadili ya Jamii na Biashara kutoka Chuo Kikuu cha “Katholieke Universiteit Leuven” nchini Ubelgiji. Katika taarifa iliyotolewa Julai 15, 2026, na Ofisi ya Uhusiano wa Umma ya SAUT imempongeza Prof. Wabanhu kwa uteuzi huo na kueleza imani kuwa atalitekeleza vyema jukumu lake jipya. Chuo hicho pia kimewataka wanajumuiya wa SAUT na wadau wote kumpa ushirikiano na msaada anapoanza majukumu yake mapya.