Tafuta

Padre Walter Ihejirika Rais wa SIGNIS Afrika Padre Walter Ihejirika Rais wa SIGNIS Afrika 

SIGNIS iko tayari kwa ajili ya Kongamano la Kimataifa Kigali,Rwanda,kuanzia Agosti 3–8

Padre Walter Chikwendu Ihejirika,Rais na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Afrika kwa ajili ya Kongamano SIGNIS duniani litakalofanyika huko Kigali,Rwanda,kuanzia tarehe 3 hadi 8 Agosti 2026,alithibitisha kuwa "bara liko tayari kuwakaribisha wajumbe na wageni kutoka ulimwenguni kote.Hata kama taratibu za kujisajiri zimefungwa lakini unaweza kuwasiliana moja kwa moja na Signis Afrika."

Na Paul Samasumo – Vatican.

Kuanzia tarehe 3 hadi 8 Agosti 2026 litafanyika jijini Kigali, Rwanda Kongamano la SIGNIS duniani. Padre Walter Chikwendu Ihejirika, Rais na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Afrika kwa ajili ya Kongamano hilo akizungumza na Radio Vatican -Vatican News, alibainisha: "Tumebakiza chini ya mwezi mmoja kabla ya Kongamano Ulimwenguni la SIGNIS, na ninataka kuthibitisha kwamba tuna kila kitu chini ya udhibiti. Tumekuwa tukifanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kwamba kila kitu kuhusu kila kipengele cha Kongamano kinatunzwa vizuri." "Kamati ya Maandalizi ya Bara, pamoja na Kamati ya Maandalizi Mahalia huko Kigali, nchini Rwanda wamefanya kazi kwa bidii na bado wanaendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha Kongamano linafanikiwa. Tovuti ya Kongamano limekuwa ikifanya kazi, na imesaidia katika usajili wa Wazungumzaji Wakatoliki wanaokusudia kushiriki katika Kongamano," alisema Padre .

Kukaribishwa wawakilishi wote 

Kulingana na Padre Walter, Kongamano litafanyika katika Hoteli ya Familia Takatifu(Sainte Famille,) iliyoko ndani ya jiji la Kigali. Akizungumzia zaidi kuhusu maandalizi, Padre Walter alisema, "Tuna idara tofauti zinazofanya kazi katika maeneo kadhaa, mapokezi, malazi, vifaa, usafiri, kuhakikisha kwamba watu wanaokuja hawatakuwa na tatizo lolote uwanja wa ndege. Tumekuwa tukitoa barua za mwaliko kwa wanachama wote wa SIGNIS wanaosafiri, kwa Wazungumzaji Wakatoliki wa kawaida wanaotaka kushiriki, na kwa wageni wengine Wakatoliki. Lengo letu ni kufanikisha Kongamano hili la Dunia na watu wakumbuke hii kumbukumbu nzuri nyumbani," alisema Padre Walter.

Nembo ya Kongamano la SIGNIS Kimataifa,Kigali Rwanda 3-8 Agosti.
Nembo ya Kongamano la SIGNIS Kimataifa,Kigali Rwanda 3-8 Agosti.

Hakuna Ebola nchini Rwanda

Alipoulizwa kuhusu Ugonjwa wa Virusi vya Ebola uliozuka katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, nchi inayoshiriki mpaka na Rwanda, Padre Walter alipunguza hofu, alisema kwamba Kamati ya Maandalizi ya Ndani ilikuwa ikiwasiliana mara kwa mara na Maafisa wa Wizara ya Afya ya Rwanda. Hali ni kwamba hakuna Ebola nchini Rwanda. "Kuhusu suala la Ugonjwa wa Virusi vya Ebola uliozuka yapata miezi miwili iliyopita katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), mwanzoni tulikuwa na wasiwasi sana. Kwa bahati nzuri, ugonjwa huo umezuiliwa kwa DRC, ambapo ulizuka, na Shirika la Afya Duniani halijatoa tahadhari yoyote ya kusafiri kwa Rwanda. "Mamlaka ya nchi hiyo yanachukulia masuala ya kiafya kwa uzito mkubwa, na ndiyo maana Serikali ya Rwanda imetuambia hakuna sababu ya kuwa na wasiwasi kuhusu ugonjwa huo. Wametuambia kuwa tuwahakikishie kila mtu anayekuja Kigali kwa ajili ya Kongamano la Dunia,  mlipuko wa Ebola hautaleta tatizo la kiafya kwa washiriki. Ebola haijaingia Rwanda, na hakuna sababu ya kuwa na wasiwasi wowote kwa yeyote anayekuja," Padre Walter alirudia kusema.

Usajili wa dakika za mwisho

Ingawa usajili rasmi umefungwa, waandaaji wanasema, hawataki kumzuia mtu yeyote. "Ikiwa kuna mtu ambaye hajajiandikisha, na ndio, tulionyesha kwamba usajili ulifungwa tarehe 30 Juni, tunajua kwamba kuna watu ambao wanaweza kuwa na maelezo ya kutatua au walikabiliwa na changamoto za usafiri, kwa mfano, ruhusa kutoka kazini, n.k. Tumeweka masharti ya usajili wa dakika za mwisho. Kwa watu kama hao, tunasema, wawasiliane nasi ili tuweze kuona jinsi ya kukabiliana na hali yao. Wawasiliane nasi kupitia mawasiliano haya: info@signiscongresskigali2026.rw au Namba ya Katibu wa Kongamano – Bwana Daniel: +250 789 061 605,” alithibitishwa Padre Walter.  Kisha aliongeza, “Kongamano la Dunia la SIGNIS liko wazi kwa wawasilianaji wote Wakatoliki duniani kote kwa kuwa SIGNIS ni chombo cha wataalamu wote wa Mawasiliano Katoliki, iwe ni wanachama wa SIGNIS au la.”

Kongamano na Magnifica Humanitas

Padre Walter pia alibainisha kwamba waraka wa hivi karibuni wa Papa Leo XIV, wa Magnifica Humanitas, kuhusu kumlinda binadamu katika enzi ya akili unde, unaendana vyema na mada ya Kongamano la Kimataifa la SIGNIS huko Kigali 2026: “Mawasiliano ya kidijitali kwa ajili ya ushirika, usawa, na ustawi wa mazingira.” Ili kurahisisha usafiri hadi Rwanda, “Tumewasiliana na baadhi ya mashirika ya ndege barani Afrika, na wametupatia punguzo na kutoa msimbo kwa wale watakaokuja kwenye Kongamano. Mashirika ya Ndege ni, Rwanda, Ethiopia na Kenya. Ikiwa mshiriki yeyote atasafiri na yoyote kati ya mashirika haya ya ndege, tafadhali apate msimbo  kutoka kwetu ili aweze kupata punguzo la 15%,” alishauri Rais wa SIGNIS Africa.

Bi Helen Osman,Rais wa SIGNIS
Bi Helen Osman,Rais wa SIGNIS

Maafisa kutoka Vatican na sehemu nyingine huko Kigali

Wanaotarajiwa kufika mjini Kigali kwa ajili ya Kongamano, mbali na wazungumzaji Wakatoliki, ni baadhi ya Makardinali na Maaskofu Wakuu kutoka bara la Afrika, Mapadre na maafisa wa Kiti Kitakatifu, EWTN, Mfuko wa Conrad N. Hilton,  Chama cha Bibilia Marekani, mashirika mbalimbali  na washirika wengine wengi wa Kikatoliki.

"Kongamano limejaa shughuli nyingi. Pia itakuwa wakati wa wawasilianaji Wakatoliki kutoka  ulimwenguni kote kuungana na kubadilishana mawazo, kushiriki uzoefu, na kujikita katika utamaduni mpya. Tunataka kila mtu, hata Waafrika, apate uzoefu wa uzuri wa Afrika zaidi ya vichwa vya habari, ukarimu wa Kiafrika na utofauti wa Kiafrika katika lugha yake, chakula, mila na tamaduni," Padre Walter alisisitiza.

SIGNIS

SIGNIS ni Chama cha Vyombo vya Mawasiliano Katoliki Duniani. Ni shirika lisilo la kiserikali la Kimataifa linalowaunganisha wataalamu wa Mawasiliano kutoka zaidi ya nchi 100 wa radio, televisheni, sinema, uandishi wa habari, na mitandao yote ya kijamii.

Mkutano wa SIGNI Kimataifa huko Afrika 2026

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.

07 Julai 2026, 10:54