Tafuta

Tafakari Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya 14 ya Mwaka A wa Kanisa: Wokovu ni kwa njia ya Kristo Yesu Mfalme wa amani Tafakari Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya 14 ya Mwaka A wa Kanisa: Wokovu ni kwa njia ya Kristo Yesu Mfalme wa amani  (@Vatican Media)

Tafakari Dominika ya 14 ya Mwaka A wa Kanisa: Wokovu Ni Kwa Njia ya Kristo Yesu Mfalme wa Amani

Ujumbe mkuu ni huu; Yesu Kristo ndiye Masiya aliyetabiriwa na manabii. Kumfuata Yeye na kuyaishi mafundisho yake, ndiyo msingi wa maisha ya furaha na Amani na uzima wa milele mbinguni. Ni katika tumaini hili, mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi: “Ee Mungu, kwa njia ya unyenyekevu wake Mwanao, umeuinua ulimwengu uliokuwa umeanguka. Uwajalie waamini wako furaha takatifu; uwapatie furaha za milele hao uliowaondoa katika utumwa wa dhambi.”

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya 14 ya mwaka A wa kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumamosi tarehe 4 Julai 2026 amefanya hija ya kichungaji Kisiwani Lampedusa kwa kutembelea Makaburi na kutoa heshima kwa Marehemu waliolazwa mahali hapa! UNHCR inasema tangu mwaka 2014 wakimbizi na wahamiaji zaidi ya 32, 700 wamefariki dunia wakijaribu kutafuta hifadhi, usalama na maisha bora Barani Ulaya. Kunako mwezi Oktoba 2013 watu zaidi ya 368 walifariki dunia kwenye Kisiwa cha Lampedusa. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Leo XIV amepata nafasi ya kukutana na kuzungumza na wakimbizi na wahamiaji, baadaye kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na kutoa heshima yake kwa Sanamu ya Bikira Maria Bandari Salama “Portosalvo.” Amekutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali, watoto wagonjwa pamoja na watu wa kujitolea. Katika maadhimisho ya Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya 14 ya Mwaka A wa Kanisa ujumbe mkuu ni huu; Yesu Kristo ndiye Masiya aliyetabiriwa na manabii. Kumfuata Yeye na kuyaishi mafundisho yake, ndiyo msingi wa maisha ya furaha na Amani na uzima wa milele mbinguni. Ni katika tumaini hili, mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi: “Ee Mungu, kwa njia ya unyenyekevu wake Mwanao, umeuinua ulimwengu uliokuwa umeanguka. Uwajalie waamini wako furaha takatifu; uwapatie furaha za milele hao uliowaondoa katika utumwa wa dhambi.” Na zaburi ya wimbo wa mwanzo inasema hivi; “Tumezitafakari fadhili zako, ee Mungu, katikati ya hekalu lako. Kama lilivyo jina lako, ee Mungu, ndivyo na sifa yako hata miisho ya dunia. Mkono wako wa kuume umejaa haki” (Zab. 48:9-10).

Wokovu ni kwa njia ya Kristo Yesu Mfalme wa Amani
Wokovu ni kwa njia ya Kristo Yesu Mfalme wa Amani   (@Vatican Media)

Somo la kwanza ni la kitabu cha Nabii Zekaria (Zek. 9:9-10). Nabii huyu alifanya utume wake wakati wa utawala Dario, kuanzia mwaka 520, baada ya uhamisho wa Babeli. Maana ya jina ni “Bwana amekumbuka.” Somo hili ni utabiri wa ujio wa Masiha, mfalme wa amani, mkombozi wa Israeli. Ishara kuu ni unyenyekevu wake wa kutumia mwana-punda. Tunasoma hivi; “Furahi sana, Ee binti Sayuni; Piga kelele, Ee binti Yerusalemu; Tazama, mfalme wako anakuja; Ni mwenye haki, naye ana wokovu; Ni mnyenyekevu, amepanda punda, Naam, mwana-punda, mtoto wa punda. Na gari la vita nitaliondoa liwe mbali na Efraimu, na farasi awe mbali na Yerusalemu, na upinde wa vita utaondolewa mbali; naye atawahubiri mataifa yote habari za amani; na mamlaka yake yatatoka bahari hata bahari, na toka mto hata miisho ya dunia.” Ni ujumbe wa matumaini wa mpango wa Mungu wa ukombozi kupitia kwa Masiya, Yesu Kristo Mkombozi wa ulimwengu. Ni katika muktadha huu zaburi ya wimbo wa katikati inasema hivi; “Ee Mungu wangu Mfalme nitakutukuza, nitalihimidi jina lako milele na milele. Kila siku nitakuhimidi, nitalisifu jina lako milele na milele. Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma, si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema. Bwana ni mwema kwa watu wote, na rehema zake zi juu ya kazi zake zote. Ee Bwana, kazi zako zote zitakushukuru, na wacha Mungu wako watakuhimidi. Wataunena utukufu wa ufalme wako, na kuuhadithia uweza wako. Bwana ni mwenye haki katika njia zake zote, na mwenye fadhili juu ya kazi zake zote. Bwana huwategemeza wote waangukao, huwainua wote walioinamia chini” (Zab. 144:1-2,8-11,14,17).

Bwana anafadhili ni mwingi wa huruma, si mwepesi wa hasira
Bwana anafadhili ni mwingi wa huruma, si mwepesi wa hasira

Somo la pili ni kutoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi (Rum. 8:9, 11-13). Ujumbe mkuu ni kuwa kuishi kwa ajili ya mwili tu, kunatupelekea kuishi katika dhambi, na hivi kupoteza uzima wa milele. Lakini kuishi kwa roho ni kuishi katika imani na ubatizo na kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Na tukiishi kwa roho tutaokoka kwa kuwa Roho wa Mungu anakuwa ndani mwetu, hivyo anatuwezesha kuishi kitakatifu na kumpendeza Mungu. Huku ndiko kufufuliwa pamoja na Kristo kwa sakramenti ya ubatizo, na hivyo hatufungwi na maisha ya kimwili kwa kuwa tunaongozwa na Roho Mtakatifu, na tuna uwezo wa kuzisulubisha tamaa za kimwili kwa maongozi ya Roho Mtakatifu na kuweza kuishi kwa upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi (rej. Gal 5:22-25). Na matokeo yake ni kuishi milele na Kristo Mbinguni. Injili ni kama ilivyoandikwa na Mathayo (Mt. 11:25-30). Sehemu hii ya Injili ni wimbo wa sifa na shukrani kwa Mungu Baba. Nao una mashairi matatu. Shairi la kwanza ni shukrani ya Mungu Mwana kwa Mungu Baba, kwa kuzificha siri za mafumbo ya ufalme wa mbingu kwa wanaofikiri na kujiona ni wenye akili na ufahamu wa yote yamhusu Mungu, na kujaa kiburi na majivuno. Anguko lao ni kubwa. Lakini Mungu kwa huruma na upendo wake amewafunulia siri za mafumbo ya uzima wa milele watoto wachanga. Hawa ni wale wanaojua kuwa siri za ufalme wa Mungu zinajidhihirisha kwa maskini wa roho na wanyenyekevu wa moyo; “Heri walio maskini wa roho, maana ufalme wa mbingu ni wao… Heri walio wapole na wanyenyekevu wa moyo, maana hao watairithi nchi” (Mt. 5:3, 5).

Njooni kwangu wote wenye kuelemewa na mizigo, jifunzeni kutoka kwangu
Njooni kwangu wote wenye kuelemewa na mizigo, jifunzeni kutoka kwangu

Shairi la pili ni ufunuo wa uhusiano uliopo kati ya Mungu Baba na Mungu Mwana. Naye anasema hivi; “hakuna amjuaye Mwana, ila Baba; wala amjuaye Baba, ila Mwana, na ye yote ambaye Mwana apenda kumfunulia.” Huu ni ufunuo wa muungano wa kiupendo uliopo kati ya Mungu Baba na Mungu mwana ambao Yesu peke yake amepewa mamlaka na uwezo wa kuwafunulia wanyenyekevu wa moyo na maskini wa roho, kwa kuwa Yeye yuko ndani ya Baba na Baba yuko ndani yake, Yeye na Baba ni kitu kimoja, na hivyo kumuona Yeye ni kumuona Baba (rej. Yn. 10:30,38; 14:9). Ukweli huu tunautambua na kuuelewa kwa imani, kama ilivyo katika Ekaristi Takatifu, kwa anayeipokea kwa imani, anampokea Yesu mwenyewe na yale yote anayoahidi. Lakini yeye asiye na imani, hata kama akiipokea Ekaristi, hampokei Yesu Kristo, na wala hapokea yale anayoahidi.

Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu
Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu   (@Vatican Media)

Na shairi la tatu ni mwaliko wa Yesu kwa wote wanaosumbuka na kulemewa na mizigo na matatizo ya kimaisha, kujipumzisha kwake, akisema; “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu.” Katika magumu na matatizo ya kimaisha; Yesu anasema, njoni kwangu mpumzishe. Mapumziko hayo yamejikita katika kujifunza upole na unyenyekevu wa moyo kutoka kwake, Yeye “alipotukanwa hakujibu kwa tukano; alipoteseka, hakutoa vitisho, bali aliyaweka matumaini yake kwa Mungu, hakimu mwenye haki” (1Pet 2:23). Tujifunze kuuishi upendo kwake. Upendo ndio winchi la kutulia mizigo na masumbuko yanayosababishwa na makovu ya kutunza hasira na sumu ya kutaka kulipiza kisasi kwa sababu ya kutendewa vibaya. Unyenyekevu, upole na umaskini wa roho, ni fadhila zinazotupa nafasi ya kupokea matunda ya Sakramenti ya Kitubio kwa kusamehewa na kutuondolea dhambi zetu, kupokea na kupata matunda ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, kutiwa nguvu za kiroho za kupambana na nguvu ya dhambi na udhaifu wa kimwili kwa uzima wa milele Mbinguni. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali; “Ee Bwana, sadaka tunayotoa kwa heshima ya jina lako itutakase, na ituwezeshe siku kwa siku kutenda yafaayo kutuletea uzima wa mbinguni.” Na katika sala baada ya Komunyo anasali hivi; “Ee Bwana, sisi tuliojaliwa thawabu zako nyingi sana, tunakuomba utujalie fadhili zako za wokovu; tena tusichoke kamwe kukusifu.” Na hili ndilo tumaini letu. Tumsifu Yesu Kristo!

Dominika 14 ya Mwaka A
04 Julai 2026, 11:36