Tafuta

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 15 ya Mwaka A wa Kanisa: Nguvu, uweza na umuhimu wa Neno la Mungu katika maisha ya waamini. Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 15 ya Mwaka A wa Kanisa: Nguvu, uweza na umuhimu wa Neno la Mungu katika maisha ya waamini.  (@Vatican Media)

Tafakari Dominika 15 Mwaka A wa Kanisa: Nguvu ya Neno la Mungu

Ujumbe mkuu umejikita katika nguvu, uweza na umuhimu wa Neno la Mungu kwa maisha ya mwanadamu, kwa maana “li hai tena lina nguvu, tena lina makali kuliko upanga uwao wote wenye makali kuwili, tena linachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, viungo na mafuta yaliyo ndani yake, tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo” (Ebr. 4:12). Hivyo linaonya, linakaripia, linafundisha, linarekebisha na ana heri yule aonywaye na kuonyeka!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya 15 ya mwaka A wa kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Mama Kanisa tarehe 12 Julai 2026 anaadhimisha Dominika ya Utume wa Bahari, fursa makini kwa Familia ya Mungu sehemu mbalimbali za dunia: Kumwomba, kumtukuza, kumsifu na kumshukuru Mungu, kwa huduma na mchango mkubwa unaotolewa na mabaharia pamoja na wavuvi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Ni siku maalum ya kutambua na kuthamini: mchango na sadaka ya watu hawa, ambao wakati mwingine, utu na heshima yao vinahatarishwa kutokana na changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo wakati wa kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa jamii. Maadhimisho haya kwa Mwaka 2026 yananogeshwa na kauli mbiu: “Zaidi ya bidhaa na biashara: sura ya kibinadamu ya bahari” ni kauli mbiu inayokumbushia dhamana na wajibu mkubwa unaotekeleza na mabaharia na wavuvi sehemu mbalimbali za dunia. Mlango Bahari wa Hormuz (Strait of Hormuz) ni moja ya njia muhimu na nyeti zaidi za Bahari kwa uchumi na biashara ya kimataifa, kwani inakadiriwa kupitisha zaidi ya asilimia 20% ya mafuta na gesi asilia duniani. Kufungwa kwa Mlango wa Bahari wa Hormuz kunachochea mfumuko wa bei na kupunguza ukuaji wa uchumi wa Dunia na katika hali mbaya zaidi kusababisha ongezeko la umaskini kwa watu milioni 32 na njaa kali kwa watu zaidi ya milioni 45. Baraza la Kipapa la Maendeleo Fungamani ya Binadamu linasema, hii inaonesha ni kwa jinsi gani binadamu kwa asilimia kubwa anategemea huduma ya bahari kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Katika Maadhimisho ya Utume wa Bahari, Mama Kanisa anawakumbuka na kuwaombea mabaharia na wavuvi walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; wana utu, heshima na haki zao msingi wanavyotekeleza dhamana na utume wao katika mazingira yenye matumaini na hofu, mizigo na ustahimilifu, mahusiano na ndoto zinazostahili kuonekana, kuheshimiwa, na kuthaminiwa.

Maadhimisho ya Siku ya Dominika ya Utume wa Bahari: Mabaharia na Wavuvi
Maadhimisho ya Siku ya Dominika ya Utume wa Bahari: Mabaharia na Wavuvi   (ANSA)

Ujumbe mkuu katika Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya 15 ya Mwaka A wa Kanisa umejikita katika nguvu, uweza na umuhimu wa Neno la Mungu kwa maisha ya mwanadamu, kwa maana “li hai tena lina nguvu, tena lina makali kuliko upanga uwao wote wenye makali kuwili, tena linachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, viungo na mafuta yaliyo ndani yake, tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo” (Ebr. 4:12). Hivyo linaonya, linakaripia, linafundisha, linarekebisha na ana heri yule aonywaye na kuonyeka, akaripiwapo na kukaripika, afundishwapo na kufundishika, arekebishwapo na kurekebeshika, kwani ataishi kwa furaha maisha ya hapa duniani na kupata heri ya milele mbinguni, kumwona Mungu jinsi alivyo na kufurahi naye milele yote. Ni katika muktadha huu zaburi ya wimbo wa mwanzo inasema hivi; “Mimi nikutazame uso wako katika haki, niamkapo nishibishwe kwa sura yake” (Zab. 17:15). Na mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi; “Ee Mungu, wawaonyesha mwanga wa ukweli wako wale wanaodanganyika, ili waweze kurudia haki. Uwawezeshe wote wanaoshika imani ya kikristo, wayakatae mambo yanayopingana na jina hilo, na kuyafuata yale yanayopatana nalo.”

Neno la Mungu lina nguvu, uweza na ni muhimu katika maisha ya waamini
Neno la Mungu lina nguvu, uweza na ni muhimu katika maisha ya waamini   (@Vatican Media)

Somo la kwanza ni kutoka katika Kitabu cha Nabii Isaya (Isa. 55:10-11). Ni hitimisho la Kitabu cha Pili cha Nabii Isaya kinachoanzia sura ya 40 mpaka 55. Katika sehemu hii ya somo hili Nabii Isaya anatueleza nguvu na uweza wa Neno la Mungu akililinganisha na mvua inyeshayo na umande ushukao kutoka juu, kuwa ni lazima vilainishe ardhi, na kuzifanye mbegu ziote, mimea ichipue, istawi, izae na kumpa mwanadamu na viumbe vingine chakula. Ndivyo lilivyo Neno la Mungu, likitoka kinywani mwake na kutangazwa na watumishi wake, lazima litimize aliyoyakusudia na kuahidi kuyatenda. Huu ni ujumbe wa faraja na matumaini kwa Waisraeli wakiwa uhamishoni Babeli kuwa watarudi katika nchi yao kwa sababu Mungu aliahidi hivyo. Ni katika muktadha wimbo wa katikati ni wa kipindi cha mavuno unaosifu na kuushukuru wema na ukarimu wa Mungu kwa kuelezea mafanikio ya mavuno yatokayo katika mashamba ukisema hivi: “Mbegu nyingine zikaanguka penye udongo mzuri; zikamea, zikazaa. Umeijilia nchi na kuisitawisha, Mto wa Mungu umejaa maji; Wawaruzuku watu nafaka, maana ndiwe uitengenezaye ardhi. Matuta yake wayajaza maji; Wapasawazisha palipoinuka; Wailainisha nchi kwa manyunyu; Waibariki mimea yake. Umeuvika mwaka taji ya wema wako; Mapito yako yadondoza unono. Huyadondokeza malisho ya nyikani. Na vilima vyajifunga furaha. Na malisho yamevikwa kondoo; Na mabonde yamepambwa nafaka. Yanashangilia, naam, yanaimba kwa furaha” (Lk. 8:8; Zab. 64: 9-13).

Neno la Mungu ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa
Neno la Mungu ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa   (@Vatican Media)

Somo la pili ni la Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi (Rum. 8:18-23). Ujumbe wake unasisitiza kuwa mateso na mahangaiko ya maisha kwa viumbe vyote ni matokeo ya dhambi. Udhalimu, uchoyo na ulafi wa mwanadamu, na kutaka kuwa kama Mungu, ili kuutawala badala ya kuutiisha ulimwengu ndiko kunavifanya viumbe vyote viugue na kuteseka, pamoja na yeye mwenyewe, ikiwemo matokeo ya mabadiliko ya tabia nchi – ongezeko la joto, ukame na mafuriko, baadhi ya viumbe hai kutoweka, mahusiano yao na binadamu kuwa hatarishi, na kuibuka kwa magonjwa yasiyo na tiba. Lakini kikomo chao wote, mtu na ulimwengu mzima ni kimoja. Kwa kadiri ile Mungu atakavyotukuza miili yetu, ndivyo atakavyofanya kwa ulimwengu mzima, viumbe vyote vitarudi na kushiriki uhuru na utukufu wa watoto wa Mungu, kwa njia ya Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wa ulimwengu wote, ambaye kwa Yeye viumbe vyote “vitawekwa huru na kutolewa katika utumwa wa uharibifu; hata viingie katika uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu.” Huu ni ujumbe wa furaha na matumaini kwa kuwa na sisi wenyewe tulio na malimbuko ya Roho, tutafanywa wana, na kupata ukombozi wa mwili na roho.

Neno la Mungu liwe ni chachu ya mabadiliko chanya katika maisha
Neno la Mungu liwe ni chachu ya mabadiliko chanya katika maisha   (@Vatican Media)

Injili ni kama ilivyoandikwa na Mathayo (Mt. 13:1-23). Ni simulizi la mpanzi kutoka na kwenda kupanda mbegu, na katika kupanda mbegu zilianguka sehemu tofauti tofauti, zikamea na kutoa mavuno kulingana na sehemu na mazingira zilipoanguakia na kuota. Maana ya mfano huu anautoa Yesu mwenyewe kuwa mpanzi ni Mungu, mbegu ni Neno lake, ardhi ni mioyo yetu, na matunda yake yanategemea namna tunavyoliishi licha ya uwepo wa vizuizi, na vishawishi vya shetani vya kutuingiza katika taabu na mateso, matokeo ya dhambi. Mtakatifu Yohane Christostom anasema kuwa katika mfano huu wa mpanzi; Yesu anaeleza upendo na huruma ya Mungu inayojidhihirisha katika kazi na matendo yake katika kumkomboa mwanadamu kutoka katika mahangaiko na utumwa wa dhambi. Hivyo Yesu anaposema mpanzi alitoka, maana yake ni kile kitendo cha Mungu muweza wa yote na aliyeko mahali pote kujishusha, kuchukua hali yetu ya kibinadamu katika fumbo la umwilisho, akawa mwanadamu na kuja kukaa nasi, kwa kuwa sisi hatukuwa na uwezo wa kumwendea yeye aliye mkatatifu kwa sababu ya dhambi zetu. Hivyo Yeye kwa upendo wake, huruma yake na uvumilivu wake, akashuka, akaja kukaa nasi na kupanda ndani mwetu Neno la uzima.

Meza ya Neno la Mungu ina nguvu katika maisha ya waamini
Meza ya Neno la Mungu ina nguvu katika maisha ya waamini   (@Vatican Media)

Kama mkulima asivyokata tamaa ya uwepo wa ndege wanaovamia na kula mbegu kabla ya kuota, miamba kuzuia mizizi ya mimea iliyoota kukua na hivyo mimea inapigwa na jua na kukauka, miiba kuisonga mimea iliyoota hata kushindwa kuzaa matunda yake, bali kwa matumaini, anapanda mbegu, na hivyo kwa bahati kukawa na sehemu ndogo ya udongo mzuri ambapo mbegu zilimea na kuzaa mazao mazuri na mengi. Ndivyo ilivyo kwa Mungu, anapanda Neno lake katika mioyo ya wote bila ubaguzi, bila kuangalia mapungufu na madhaifu yetu. Kwa kuheshimu uhuru wa kila mmoja, anaendelea kututangazia huruma yake, akitumaini kuwa, mda utatoa hukumu, wa sisi kuongoka na kuingia katika uzima wa milele mbinguni. Na kama ilivyo kwa mbegu bora inavyotegemea udongo mzuri wenye rutuba ili imee, ikuu, ikomae na kuzaa mazao mengi na mazuri, ndivyo ilivyo kwa neno la Mungu, ili liingie na kupenye mioyo yetu, likue, likomae na kuzaa matunda bora ndani ya maisha yetu, linahitaji utayari wetu, imani yetu, upendo wetu, matumaini yetu na ujasiri wetu katika kulipokea, kulipa nafasi ndani mwetu na kuliacha litubadilishe. Neno hili linapita uwezo wa ufahamu wetu. Kumbe imani, matumaini, upendo, uvumilivu na usikivu vinahitajika ili liweze kuzaa matunda. Ndiyo maana Yesu anasisitiza umuhimu wa kusikiliza akisema; “Mwenye masikio na asikie.”

Mbegu zilizoanguka kwenye udongo mzuri zilizaa matunda mengi.
Mbegu zilizoanguka kwenye udongo mzuri zilizaa matunda mengi.

Katika ulimwengu mamboleo, kuna sauti nyingi nzuri, tamu na za kupendeza masikioni. Hizi zinaweza kutufanya tusikie, lakini tusisikilize na hivyo tusilielewe Neno la Mungu. Mazuri ya ulimwengu, yanaweza kutuhadaa na kuyafumba macho yetu yasiuone wema wa Mungu kwa kuifanya mioyo yetu iwe mizito na migumu. Hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuwa na bidii, kulisoma, kulisikiliza, kulitafakari na kulitunza Neno la Mungu, ili ndege wa dunia hii wasilile, miamba ya ulimwengu huu isilizuie kuzama, jua lake lisiikaushe na miiba isilisonge na kulizuia lisizae matunda yake. Kwa nguvu zetu hatuweze lolote. Tunahitaji neema na msaada wa Mungu Roho Mtakatifu. Ndiyo maana mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anatuombea akisali hivi; “Ee Bwana, tazama dhabihu za Kanisa lako liombalo. Nasi waamini wako utujalie tuzile tupate kuzidishiwa utakatifu.” Na katika sala baada ya Komunyo anasali; “Ee Bwana, baada ya kuzipokea fadhili zako, tunaomba utuzidishie mapato ya wokovu wetu, kila tunapopokea fumbo hili.” Na hili ndilo tumaini letu. Tumsifu Yesu Kristo!

Dominika 15 Mwaka A
09 Julai 2026, 16:33