Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 15 ya Mwaka A wa Kanisa sanjari na Maadhimisho ya Dominika ya Utume wa Bahari kwa Mwaka 2026. Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 15 ya Mwaka A wa Kanisa sanjari na Maadhimisho ya Dominika ya Utume wa Bahari kwa Mwaka 2026.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Tafakari Dominika ya 15 ya Mwaka A wa Kanisa: Nguvu ya Neno la Mungu: Utume wa Bahari

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu: “Nguvu ya Neno la Mungu" Mungu amepanda mbegu ya Neno lake ndani ya mioyo yetu. Ni Neno hai, tena lina nguvu (Ebr 4:12), ndiyo Habari Njema ya Ufalme wa Mbinguni iliyofunuliwa kwetu kwa njia ya Yesu Kristo (Yn 1:14). Kama vile mbegu inayooteshwa inavyohitaji udongo wenye rutuba ili iweze kukua na kuzaa matunda mengi, Neno la Mungu lahitaji mioyo iliyo tayari, si tu kulipokea Neno; kuliishi. kulitangaza na kulishuhudia!

Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.

Utangulizi: Wapendwa wanafamilia ya Mungu, ni Dominika ya 15 Mwaka A wa Kanisa. Mama Kanisa tarehe 12 Julai 2026 anaadhimisha Dominika ya Utume wa Bahari, fursa makini kwa Familia ya Mungu sehemu mbalimbali za dunia: Kumwomba, kumtukuza, kumsifu na kumshukuru Mungu, kwa huduma na mchango mkubwa unaotolewa na mabaharia pamoja na wavuvi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Ni siku maalum ya kutambua na kuthamini: mchango na sadaka ya watu hawa, ambao wakati mwingine, utu na heshima yao vinahatarishwa kutokana na changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo wakati wa kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa jamii. Maadhimisho haya kwa Mwaka 2026 yananogeshwa na kauli mbiu: “Zaidi ya bidhaa na biashara: sura ya kibinadamu ya bahari” ni kauli mbiu inayokumbushia dhamana na wajibu mkubwa unaotekeleza na mabaharia na wavuvi sehemu mbalimbali za dunia. Mlango Bahari wa Hormuz (Strait of Hormuz) ni moja ya njia muhimu na nyeti zaidi za Bahari kwa uchumi na biashara ya kimataifa, kwani inakadiriwa kupitisha zaidi ya asilimia 20% ya mafuta na gesi asilia duniani. Kufungwa kwa Mlango wa Bahari wa Hormuz kunachochea mfumuko wa bei na kupunguza ukuaji wa uchumi wa Dunia na katika hali mbaya zaidi kusababisha ongezeko la umaskini kwa watu milioni 32 na njaa kali kwa watu zaidi ya milioni 45. Baraza la Kipapa la Maendeleo Fungamani ya Binadamu linasema, hii inaonesha ni kwa jinsi gani binadamu kwa asilimia kubwa anategemea huduma ya bahari kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Katika Maadhimisho ya Utume wa Bahari, Mama Kanisa anawakumbuka na kuwaombea mabaharia na wavuvi walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; wana utu, heshima na haki zao msingi wanavyotekeleza dhamana na utume wao katika mazingira yenye matumaini na hofu, mizigo na ustahimilifu, mahusiano na ndoto zinazostahili kuonekana, kuheshimiwa, na kuthaminiwa.

Maadhimisho ya Dominika ya Utume wa Bahari kwa Mwaka 2026
Maadhimisho ya Dominika ya Utume wa Bahari kwa Mwaka 2026   (AFP or licensors)

Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika hii inatutafakarisha juu ya, “Nguvu ya Neno la Mungu” Mwenyezi Mungu amepanda mbegu ya Neno lake ndani ya mioyo yetu. Ni Neno hai, tena lina nguvu (Ebr 4:12), ndiyo Habari Njema ya Ufalme wa Mbinguni iliyofunuliwa kwetu kwa njia ya Mwanaye mpenzi Yesu Kristo (Yn 1:14). Kama vile mbegu inayooteshwa inavyohitaji udongo mzuri wenye rutuba ili iweze kukua na kuzaa matunda mengi, Neno la Mungu lahitaji mioyo iliyo tayari, si tu kulipokea Neno hilo, bali pia kuliishi, kulitangaza na kulishuhudia, ili liweze kuleta mabadiliko ya kweli na kuzaa matunda mengi ya utu wema, ukamilifu na utakatifu kwa ajili ya utukufu wa Mungu na wokovu wetu. Somo la Kwanza: Ni kutoka katika Kitabu cha Nabii Isaya 55:10-11. Somo la kwanza ni kutoka sehemu ya mwisho ya Kitabu cha Pili cha Nabii Isaya 55:10-11. Kitabu cha Pili cha Nabii Isaya kinaanzia kimsingi katika ile sura ya 40-55. Hebu tuanze kutafakari somo hili na kuona jinsi linavyotusaidia kuelewa ujumbe ambao Mama Kanisa amependa kututafakarisha katika dominika hii ya 15 ya mwaka A wa kanisa. Fundisho la kwanza: Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, kwa kuwa ni Nafsi na pumzi ya Mungu aliye daima Mwaminifu. Somo hili linaanza wazi kabisa kutuonesha nguvu ya Neno la Mungu. Mazingira ya somo hili ni wakati taifa la Israeli walipokuwa ugenini, utumwani huko Babiloni ambapo walikaa kwa muda mrefu sana. Hekalu lao kule Yerusalemu, ambalo lilikuwa ni kiini na ishara ya uwepo wa Mungu katikati yao lilikwisha bomolewa na kuharibiwa vibaya sana. Hivyo walipoteza matumaini kabisa. Walikua wakavu kabisa kiroho, wakihisi Mungu amewasahau. Waliona kana kwamba Ahadi za Mungu zinachelewa kutimia, au hazitatimia kabisa.

Dominika ya Utume wa Bahari: Mabaharia, Wavuvi na Familia zao
Dominika ya Utume wa Bahari: Mabaharia, Wavuvi na Familia zao   (Erika Santelices)

Kwa upande mwingine, Babeli ulikuwa mji mkuu wenye utajiri mkubwa, biashara, na miungu mingi ya sanamu. Wayahudi wengi walianza kushawishika kuachana na imani yao ya kweli na kufuata tamaduni na anasa za Babeli ili kufanikiwa kimaisha. Waliona kama Neno la Mungu linawachelewesha kupata mafanikio, faraja na amani ya kudumu, wengine walianza hata kupingana na utabiri kuhusu kurejea kwao kutoka utumwani. Na hapo ndipo katika somo hili Mwenyezi Mungu ananena nao tena kwa kinywa cha Nabii Isaya, kuwakumbusha nguvu ya Neno lake. Anawafariji katika mazingira yao ya ukavu na ukame wa kiroho na kukata tamaa, akiwathibitishia kuwa kama vile mvua na theluji visivyoshuka bure, bali huinywesha ardhi na kuchipusha, ikampa mtu apandaye mbegu, na mtu alaye chakula, ndivyo na Neno lake halitarudi bure, bali litatimiza daima mapenzi yake. Litatenda daima alichosema. Ndugu mpendwa, somo hili la kwanza linatufundisha kuwa, Neno la Mungu li hai tena lina nguvu kama tunavyosoma pia katika kitabu cha waraka kwa waebrania 4:12. Lina nguvu na linachoma kama upanga ukatao kuwili kwa kuwa ni pumzi ya Mungu mwenyewe. Ni neno la Uzima linalopandwa ndani ya mioyo yetu na Mungu mwenyewe. Ni nafsi hai, yenye nguvu ya kuleta mageuzi, faraja na uponyaji wa kweli ndani ya moyo wa yule anayelipokea. Taifa la Israeli wakiwa huko utumwani Babeli walikuwa wamekauka kabisa kiroho kwa sababu ya nyakati mbaya za kuumiza na za kukatisha tamaa walizopitia. Hawakuona tena tumaini na nguvu katika Neno la Mungu juu ya utimilifu wa Ahadi zake. Nabii analifananisha Neno la Mungu na mvua na theluji ambavyo vikishatoka mawinguni hairudi bure mpaka imeinyeshea ardhi na imechipusha vyote vimeavyo ndani yake. Na kama vile ambavyo mvua ikishatoka ni lazima idondoke chini, vivyo hivo na Neno la Bwana likishatoka kinywani mwake lazima litekeleze kile lilichoadhidi. Anawahakikishia kuwa unabii wa Bwana ambao ameutoa kwa hakika utatimia kwa sababu Neno la Mungu ni la kuaminika. Kwetu sisi tunaolikiliza Neno la Mungu leo tunavutwa kuwa na imani na matumaini. Kuliamini Neno la Mungu na kuzitumainia ahadi zake kwetu kwani yeye ni mwaminifu na Neno lake lina nguvu ya kutekeleza kile anachoahidi.

Kkristo Yesu ni Neno wa Mungu aliyefanyika Mwili
Kkristo Yesu ni Neno wa Mungu aliyefanyika Mwili   (@Vatican Media)

Somo la Pili ni kutoka katika Waraka wa Mtume Paulo Kwa Warumi 8:18-23. Somo la Pili kutoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi 8:18-23, linatutafakarisha kuhusu tumaini la utukufu ujao katikati ya mateso tunayopitia wakati wa sasa, kama ilivyokuwa kwa Taifa la Israeli.  Mtume Paulo anatufundisha kuwa madhila, magumu na mateso tunayopitia sasa duniani hayawezi kufananishwa hata kidogo na ule utukufu mkubwa ambao Mungu atatufunulia baadaye. Sio wanadamu pekee wanaoteseka, bali viumbe vyote vinalia na kuugua vikitafuta kukombolewa kutoka katika uharibifu uliosababishwa na dhambi, ili viingie katika uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu. Licha ya hayo, bado lipo tumaini imara. Sisi tulio na malimbuko ya Roho Mtakatifu tunatakiwa kusubiri kwa subira na tumaini kubwa ukombozi kamili wa miili yetu, tukijua kuwa maumivu ya sasa ni kama uchungu wa uzazi unaofungua mlango wa maisha mapya yenye baraka. Hatupaswi kuogopa kwa kuwa Kristo amefufua upya matumaini yetu. Somo la Injili: Ni Injili ya Mathayo 13:1-23. Katika Dominika hii ya 15 A tunaanza rasmi sehemu nyingine muhimu ya Injili ya Mathayo, ambapo Kristo Yesu Mwalimu wetu anatufundisha juu ya “Siri za Ufalme wa Mbinguni” kwa Mifano. Sura hii ya kumi na tatu ina mifano 8 katika aya zake zote 52, mifano tutakayoisikia kuanzia dominika hii ya 15 hadi ya 17. Kwa nini Kristo anafundisha kwa mifano? Moja ya sababu kuu ni kwamba Ufalme wa Mungu sio kitu kinachoelezeka kwa urahisi, kuonekana wazi au kushikika. Hivyo alitumia mifano ya mazingira na vitu ambavyo watu walivifahamu vyema ili aweze kuwafunulia siri hizi za ufalme wa Mbinguni, si wote, bali wale waliokuwa tayari, kwa unyenyekevu na upole kuyapokea mafundisho yake kama alivyotualika katika dominika ya 14 ya Mwaka A wa Kanisa. Katika dominika hii ya Kumi na tano ya Mwaka A wa Kanisa tunaanza na mfano wa kwanza, mfano wa Mpanzi aliyekwenda kupanda Mbegu. Katika somo la kwanza na la pili tumetafakari juu ya nguvu ya Neno la Mungu. Katika Injili Takatifu, ningependa tutafakari namna sasa Mwenyezi Mungu anavyopanda mbegu ya Neno lake la uzima ndani mwetu na wajibu wetu wa kuipokea mbegu hiyo na kuitunza ili iweze kuzaa matunda mengi.

Neno la Mungu lina nguvu
Neno la Mungu lina nguvu   (@Vatican Media)

Fundisho pili: Mwenyezi Mungu anapanda mbegu ya Neno lake, mbegu njema isiyo na dosari, bila upendeleo, Neno lenye nguvu ile ile kwa kila aina ya udongo.  Mfano wa mpanzi katika Mathayo 13:3-9 unataja mazingira halisi ya kilimo ya karne ya kwanza huko Galilaya. Yesu alitumia mazingira ambayo kila msikilizaji wake, kuanzia mkulima maskini hadi mtu wa mjini alikuwa anayafahamu vyema ili kufikisha ujumbe wa kiroho. Katika kilimo cha kale cha Kiyahudi, mara baada ya kuchagua mbegu zilizo bora, mpanzi kawaida alipanda kwa kuzitawanya mbegu kwa kuzirusha zianze kuanguka chini kabla ya kulima ardhi kwa jembe la ng’ombe. Kwa sababu hiyo, mbegu zilianguka kwenye maeneo tofauti tofauti ndani ya shamba lile lile moja, nyingine karibu na njia, kwenye miamba, penye miiba na penye udongo mzuri. Kumbe mpanzi hakuchagua, hakubagua wala hakupanda mbegu kwa upendeleo. Alipanda mbegu njema na nzuri, zote zenye uwezo wa kuzaa matunda mengi. Ndugu mpendwa, Mwenyezi Mungu, Mpanzi, anapanda mbegu yaani Neno lake, mbegu njema sana kwa ukarimu mkubwa sana, mbegu isiyo na dosari yoyote, mbegu yenye nguvu, yaani pumzi yake mwenyewe ndani ya shamba yaani ndani ya moyo wa kila mmoja pasipo na upendeleo wowote. Haangalii nani anastahili na nani hastahili, wala haangalii hali ya udongo wetu yaani hali mbalimbali zilizo ndani yetu mithili ya lile shamba lenye aina mbalimbali za udongo. Injili hii inatolewa bure kwa ulimwengu mzima bila ubaguzi, kwa tajiri na maskini, mdhambi na mwenye haki. Kumbe tunaposhindwa kutoa matunda mema, hatuwezi kumlaumu mpanzi, kwa kuwa mpanzi, Mwenyezi Mungu mwenyewe ni mkarimu daima, amekwisha panda mbegu njema ndani mwetu, na anaendelea kila siku bila kuchoka kupanda mbegu hiyo ndani ya mioyo yetu, pale tunapolisikia Neno lake. Injili haiuzwi wala hainunuliwi, hivyo twapaswa kuwa makini na wale wanaochukua nafasi ya mpanzi, kwa kupanda mbegu mbaya ndani mwetu, kwa jina la Injili ya Kristo. Hao ndio manabii wa uwongo ambao wanahubiri Injili yao badala ya Injili ya Kristo. Tuombe neema ya kutofautisha mbegu mbaya na Neno la kweli la uzima, mbegu njema yenye kutia uzima roho zetu. Tunapopokea mbegu njema ndipo nasi tutaweza kuzaa matunda bora na kuwasaida wengine pia kuipokea nao waweze kuzaa vile vile matunda mengi, tukitambua kuwa kila mbatizwa aliyepokea mbegu njema kutoka kwa mpanzi ana wajibu wa kuwa shuhuda wa Injili hiyo kwa wengine.

Neno la Mungu ni faraja kwa waamini
Neno la Mungu ni faraja kwa waamini   (@Vatican Media)

Fundisho la Tatu: Licha ya kwamba Neno linapandwa bure bila upendeleo, Moyo wa Mwanadamu una hiari na uhuru wa kuchagua, kuwa na kuishi hali hizi mbalimbali za udongo. Katika somo hili la Injili Takatifu tunaweza kufikiri pengine mpanzi alipanda mbegu katika mashamba tofauti. La hasha. Mpanzi alipanda mbegu katika shamba moja vile tu kama wakati wa sasa kila mkulima anavyopanda mbegu katika shamba lake. Lakini shamba hili lina aina hizi mbalimbali za udongo ambazo kila aina inapokea mbegu hii kwa namna yake. Hali kadhalika moyo wa mwanadamu ndiyo shamba hili lenye hizi hali mbalimbali za udongo. Kimsingi Mwenyezi Mungu alimuumba mwanadamu akiwa na uhuru wa kuchagua (free will). Haingii mioyoni mwetu kwa nguvu au kwa kulazimisha utii. Mfano huu unaonyesha jinsi hiari ya binadamu inavyotengeneza mazingira manne tofauti katika upokeaji wa Neno la Mungu. Hapa kila mmoja wetu aweza kujiuliza, moyo wangu una mazingira gani kwa sasa kati ya haya? Au ni mazingira gani yamekuwa yakitawala zaidi ndani mwangu yanayoweza kunifanya au nipokee Neno la Mungu lizae matunda au lisizae matunda. Je ni mwamba, au nipo njiani, au nimezingirwa na miiba au ni udongo mzuri?

Neno la Mungu linahitaji udongo mzuri ili liweze kumea na kukua
Neno la Mungu linahitaji udongo mzuri ili liweze kumea na kukua   (@Vatican Media)

Kwanza: Mioyo yetu inaweza kuwa daima karibu na njia, ikakosa utulivu, Neno la Mungu lisipate kabisa nafasi ndani yake. Mbegu zilizoanguka karibu na njia zinawakilisha yule alisikiaye Neno la Mungu wala asilielewe. Njia kwa kawaida ni mahali ambao watu na magari vinapita kila mara na kufanya ardhi kuwa ngumu. Mara kadhaa mioyo yetu inaruhusu mambo mengi yapite juu yake na kufanya moyo kuwa mgumu na Neno la Mungu linashindwa kabisa kupenya ndani yake. Huenda muda mwingi tunatumia katika kazi, mitandao ya kijamii, kutazama mambo mbalimbali ya kidunia na muda mchache sana tunatenga kwa ajili ya kusoma na kutafakari kwa kina kile Mungu anataka kusema nasi kila siku. Mbegu inapoanguka njiani inabaki wazi juu ya ardhi, na ndege wanaiona na kuila kwa urahisi. Kumbe nasi tunapokosa ulinzi wa sala, tafakari, na sakramenti matokeo yake ni kwamba shetani anatumia nafasi hiyo kuondoa lile Neno tulilolisikia hata kabla halijafanya kazi ndani mwetu. Mara kwa mwara tunaweza kusoma Biblia kwa mazoea tu bila utayari wa dhati wa moyo. Neno linaingia sikio hili na kutokea lile lingine, bila kutafakariwa wala kupewa nafasi ya kubadilisha tabia zetu. Je, ninasoma na kutafakari mara ngapi Neno la Mungu? Matokeo yake ni kwamba shetani anatupa daima options au machaguo mengine na kulinyakua lile Neno Jema liliopandwa ndani mwetu.

Mwaliko kwa waamini ni kulisoma, kulitafakari na kulimwilisha Neno la Mungu
Mwaliko kwa waamini ni kulisoma, kulitafakari na kulimwilisha Neno la Mungu   (@Vatican Media)

Pili: Moyo kupokea Neno la Mungu kwa mihemko ya muda mfupi, au kwa kufuata mkumbo. Kristo Yesu anaeleza kuwa hawa ni wale ambao hulipokea Neno kwa furaha, lakini hawana mizizi ndani yake, bali hudumu kwa muda, ikitokea dhiki au udhia kwa ajili ya Neno lile mara huchukizwa. Hawa ndio waliopandwa penye miamba. Nini kinafanya ugumu katika kulipokea Neno na likadumu ndani ya moyo? Moyo huu una mwamba mgumu ndani yake, nao ni mwamba wa kutotaka kuacha ubinafsi. Tamaa hii inapotawala moyo, inafanya Neno la Mungu lionekane kama jambo la ziada au lisilo na faida ya haraka, na hatimaye imani yetu inanyauka. Mara kwa mara tunapenda Ahadi za Mungu, uponyaji, mafanikio, amani ya roho, utulivu wa ndani, ahadi ambazo tunazipata tulisikiapo Neno la Mungu linapohubiriwa kwetu. Moyo huo huo waweza kukataa gharama ya ufuasi, yaani toba, kuliishi neno kweli kwa vitendo, kujikana nafsi na kuchukua msalaba kwa uaminifu kila siku. Matokeo yake ni kuwa na udongo dhaifu ambao mizizi ya Neno la Mungu inashindwa kustawi na kudumu.  Mateso, kejeli, dhihaka, maumivu na maradhi au changamoto za kimaisha (jua kali) zinapotokea kwa sababu ya imani yetu, tunanakosa unyevu, rutuba na mizizi imara na kukauka upesi. Ni imani inayotegemea mazingira yawe mazuri tu; mazingira yakiharibika, basi na imani inapotea kabisa. Ndio maana kunakua na kishawishi cha kuhama hama na kutanga tanga kiimani, ninakwenda kwa mchungaji anayehubiri mafanikio pekee, nakwenda kanisa lile wanayehubiri ahadi pekee, naenda kwa mwinjilisti huyu anayehubiri uponyaji na utukufu bila maumivu, mateso na msalaba. Ni hali ya kukosa msimamo katika kulipokea Neno la Mungu.

Familia zijenge utamaduni wa kusoma, kutafakari na kuliishi Neno la Mungu
Familia zijenge utamaduni wa kusoma, kutafakari na kuliishi Neno la Mungu   (@Vatican Media)

Tatu: Moyo unaozidiwa na kazi, mahangaiko na unaozongwa zongwa na mali anasa na mambo mengi ya kidunia. Kristo anatufundisha kuwa hawa ni wale ambo wanalisikia Neno, mimi na wewe nyakati fulani, na shughuli za kidunia na udanganyifu wa mali hulisonga lile Neno; likawa halizai. Hawa ndio waliopandwa katika miiba. Mara kwa mara tunatoa kipaumbele kikubwa sana kwa mambo ya ulimwengu huu yanayotusongasonga kila siku, hofu kuhusu kesho yetu, tutakula nini, tutavaa nini, tunahangaikia vyeo, biashara, masomo, tunatafuta kuwa mamlaka, umaarufu na matokeo yake kukosa muda wa kusali, kuhudhuria ibada ya Misa Takatifu, kusoma Neno la Mungu na tafakari binafsi, na kupokea Sakramenti. Matokeo yake ni kwamba, miiba hii inazuia mbegu kukuwa na kustawi, mengine yaweza kuwa magugu yanayochukua hata rutuba njema iliyopaswa kupata mbegu nzuri ya Neno la Mungu ndani mwetu, yanatuchukulia muda wetu mwingi wa kusali, yanatupotezea nguvu na jitihada nyingi badala ya kutenda mema, yanatuziba kuendelea kupokea neema na baraka za Mungu ambazo tunazihitaji sana ili tukuwe na tuzae matunda, yanatuzuia kuona uzuri wa Mungu ndani mwetu na ndani ya wengine. Matokeo yake, tunashindwa kutoa matunda stahiki.

Neno la Mungu linapaswa kutangaza na kushuhudiwa kwa watu wa Mataifa
Neno la Mungu linapaswa kutangaza na kushuhudiwa kwa watu wa Mataifa   (@Vatican Media)

Nne: Udongo mzuri, ni Moyo msikivu, ulio tayari kupokea, kulishika na kuliishi Neno la Mungu. Kristo anatufundishwa kwamba yule aliyepandwa kwenye udongo mzuri, huyo ndiye alisikiaye Neno na kuelewa nalo. Ni mtu anayesikia Neno, analielewa, analitafakari kwa kina, na analitunza na analinda kwa gharama kubwa sana lisiondoke. Yuko tayari kuruhusu Neno liuguse moyo wake na kufanya mabadiliko ya kweli ndani yake. Anaruhus neno litulize njaa na kiu ya moyo wake na hivyo kupata kitulizo, faraja na pumziko la kweli kwa Kristo Yesu pekee. Anaruhusu Neno la Mungu limuunde na kumfinyanga ili aendane daima na mpango pamoja na mapenzi ya Mungu ndani mwake. Matokeo yake Mtu huyu anadumu na kuzaa matunda. Viwango vya mia, sitini, na thelathini vinaonyesha kuwa hata kati ya Wakristo waaminifu, uwezo na nafasi zetu za kuzaa matunda zinatofautiana kulingana na karama na neema tulizopewa, lakini jambo la msingi ni kwamba kila mmoja anazaa matunda. Hatupaswi kushindana kuzaa matunda, kwa kuwa hatujapewa sawa. Lakini tunaweza kusaidiana na kutegemezana ili sote katika umoja wetu, ndani ya familia, ndani ya jumuiya, ndani ya ndoa, ndani ya kanisa tuweze kuwa udongo wenye rutuba, unaoweza kuzaa matunda mengi. Kwa njia ya sala, kuombeana sisi wenyewe, kupokea sakramenti za kanisa, kusoma daima Neno la Mungu, kutenda mema, tunazidi kuweka rutuba ndani mwetu ili tuzae matunda zaidi na zaidi.

Neno la Mungu ni chemchemi ya imani, matumaini na mapendo
Neno la Mungu ni chemchemi ya imani, matumaini na mapendo   (@Vatican Media)

Fundisho la Nne: Sote tuna uwezekano wa kuwa udongo mzuri. Na Kipimo cha kweli cha Imani yetu ni kuzaa matunda. Ndugu mpendwa, dominika ya leo inatukumbusha, kila mmoja wetu ana uwezekano wa kuwa udongo mzuri na hivyo kipimo hali na cha kweli cha ukristo na imani yetu ni kuzaa matunda. Mwenyezi Mungu kama nilivyotangulia kusema, amepanda mbegu ndani mwetu bila upendeleo na anataka kweli kila mmoja hata kwa kidogo alicho nacho kadiri Roho Mtakatifu alivyomjalia azae matunda na matunda hayo yapate kudumu. Ndugu mpendwa, Yesu haisifu mbegu kwa kuota haraka (kama ile iliyoanguka kwenye miamba), bali anaisifu ile inayofika hatua ya kutoa mazao, thelathini, sitini na mia moja. Mara kadhaa watu wengi wanapenda kupima Ukristo kwa ishara za nje. Lakini leo Kristo anatuuliza nasi kila mmoja wetu, je, umezaa matunda gani? Lakini swali hili lapaswa kututafakarisha pia kwamba, je, ni mbegu gani ipo ndani ya moyo wangu? Huenda moyo wangu umejazwa daima na wivu, chuki, visasi, majivuno, roho mbaya, uvivu, ubinafsi, ulafi na vilema vingine mbalimbali. Lakini pia wakati fulani sipo tayari kuondoa mizizi iliyosababishwa na mbegu hiyo mbaya ndani ya moyo wangu na matokeo yake, nayo itakua na kuzaa matunda mabaya.  Ndio maana wakati mwingine tunakuwa warahisi kuwatendea wenzetu mambo ya kuumiza, kwa kuwa ndiyo mbegu tuliyopanda ndani mwetu. Lakini matunda ya kweli yanayotajwa hapa ni yale ya Wagalatia 5:22-23 (upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi) pamoja na matunda ya kuwaleta wengine kwa Kristo. Matunda haya yanahitaji muda, yanahitaji kuvumilia dhoruba, na yanahitaji moyo uliounganishwa kikamilifu na shina ambalo ni Yesu Kristo (Yohana 15:5). Hitimisho: Katika dominika hii tumshukuru Mungu ambaye amepanda mbegu ya Neno lake bila upendeleo ndani ya kila mmoja wetu. Tuombe neema ya kulipokea Neno hilo na kuruhusu lifanye kazi ndani mwetu, ili tuweze kuzaa matunda.

Tafakari Dominika 15 Mwaka A
10 Julai 2026, 11:29