Tafuta

Wamisionari wazee huko Papua New Guinea. Wamisionari wazee huko Papua New Guinea.  (©Photo by Fr. Christian Sieland)

Urithi wa wamisionari wazee na kuiweka Papua New Guinea mioyoni mwao

Baada ya miongo kadhaa ya utume wa wamisionari wazee waliostaafu huko Papua New Guinea, sasa wamerudi Ulaya na wanaendelea kusimulia historia ya ajabu ya imani,kujitole na upendo usioyumba kwa watu wa Papua New Guinea. Padre Sieland,Mkurugenzi wa PMS nchini Papua New Guinea anatafakari jinsi unyenyekevu,kujitolea kwao kwa utamaduni na ya huduma vinavyobaki kuwa msukumo wa kudumu kwa Kanisa la leo na vizazi vijavyo vya wamisionari.

Na Sr. Christine Masivo, CPS – Vatican.

Kustaafu kutoka kwa utume hai kwa wamisionari wengi waliohudumu kwa kujitolea kwa zaidi ya miongo mitano ya maisha yao huko Papua New Guinea hakujafuta roho yao ya umisionari. Kwasababu ya umri na matatizo ya kiafya walilazimika kurudi katika nchi zao za asili barani Ulaya, huku mioyo yao ikibaki imara katika jamii walizohudumia. Ingawa wengi wa wamisionari hawa wangependa kukaa katika nchi zao za umisionari na kuzikwa huko walikotoa utume wao.

Utume usio na mwisho

Padre Christian Sieland, Mkurugenzi wa Kitaifa wa PMS nchini Papua New Guinea, hivi karibuni aliwatembelea Shirika la wamisionari la Neno la Mungu (SVD)  na masista wa shirika la Wamisionari wa Roho Mtakatifu (SSpS) wazee wanaoishi katika nyumba zao za kustaafu Uholanzi na Ujerumani. Akizungumza na Shirika la Kipapa la Habari za Kimisionari, (Fides), Padre Christian Sieland Mkurugenzi wa Shirika la Kipapa la Utume wa Kimisionari(PMS) nchini Papua New Guinea(PNG)alielezea jinsi unyenyekevu wao, kujitolea kwao kwa utamaduni, na utume vinavyobaki kuwa msukumo mstakabali kwa Kanisa na vizazi vijavyo vya wamisionari. Askofu Mstaafu Henk Te Maarssen, (SVD,) ni miongoni mwao, alikuwa mmisionari kwa karibu miaka sitini nchini Papua New Guinea.

Wajenzi wa Kanisa na taifa

Shirika la wamisionari la Neno la Mungu (SVD)  walichukua jukumu la msingi katika kuinjilisha Papua New Guinea (PNG) baada ya kufika Madang mnamo 1896. "Kilichonishangaza zaidi," Padre Sieland alikumbuka, "ni kwamba hakuna hata mmoja wao anayejuta kuwa mmisionari, na wakipewa fursa nyingine, wangefanya chaguo lile lile." Wamisionari hawa wanakumbuka Papua New Guinea kwa shukrani na upendo na sio magumu waliyopitia walipoanza utume. Mazungumzo yao yamejaa historia za watu walioandamana nao, urafiki waliojenga, na jumuiya za imani walizolea. Padre Sieland alibainisha kuwa mchango wao ulikuwa zaidi ya uinjilishaji. Walipokuwa wakieneza injili, waliweka misingi wa shule, hospitali, parokia, na taasisi za kijamii ambazo zimesaidia kuunda PNG ya kisasa, na licha ya mafanikio haya, unyenyekevu wao ni mfano wa kuigwa. Padre Sieland alisisitiza kwamba, "Hawakuzungumza kwa fahari kuhusu walichotimiza, kwani kila kitu walichofanya kilikuwa kwa ajili ya utukufu wa Mungu."

Kujifunza injili katika tamaduni mbalimbali

Wamisionari hawa walijikita kikamilifu katika utamaduni wa wenyeji. Walifika miaka ya 1950 na 1960 walijifunza lugha za wenyeji, waliishi miongoni mwa watu, wakakumbatia mtindo wao wa maisha, na kuelewa mila zao kabla ya kuhubiri Injili. "Hawakupuuza mila za wenyeji bali walitambua maadili ambayo tayari yalikuwepo ndani yao," Padre Sieland alitoa maoni, "kwa kutofautisha kwa uangalifu desturi za kitamaduni zilizoangazia maadili ya Injili kutoka kwa yale yaliyohitaji mabadiliko kupitia imani." Baadhi ya wamishonari waliandika kamusi na miongozo ya sarufi kwa lugha ambazo hapo awali walizungumza tu bila maandishi, wakihifadhi urithi wa kitamaduni usio na thamani.

Utume katika urahisi na unyenyekevu

Wamisionari hawa walihudumu katika vijiji vya mbali bila barabara, vifaa vya kisasa, au starehe za msingi kwa uvumilivu na urahisi. Kuchanganyika na jamii za wenyeji kuliwafundisha kwamba utajiri wa mali haumaanishi ustawi wa binadamu. "Waligundua kwamba hawa ni watu waliounganishwa kwa undani na ardhi yao, utamaduni, na maisha ya pamoja, ambapo maadili mengi ya Injili yalikuwa tayari yamekuwepo muda mrefu kabla ya Ukristo kufika," alisema Padre Sieland. Alielezea uzoefu huu wa mabadiliko kama "kuambukizwa virusi vya New Guinea" upendo mkubwa kwa watu unaobadilisha moyo wa wamishonari milele.

Urithi wa wamisionari na mstakabali

"Ushahidi wa wamisionari hawa wazee unabaki kuwa muhimu sana, kwani Kanisa linategemea zaidi uongozi wa wenyeji," Padre Sieland alitoa maoni. Alisema kuwa, "Ninahisi kwamba roho na msukumoo huu wa umisionari wa hapo awali wakati mwingine haipo miongoni mwa wamisionari wengi wapya wanaofika leo, hasa kwa sababu msingi mwingi tayari umewekwa." Wamisionari wa kisasa wanaendelea kujenga juu ya misingi iliyoanzishwa na waanzilishi hawa wa mapema, lakini bidii na nguvu thabiti ya wamisionari wa kwanza ilikuwa kitu cha kipekee kabisa.

Aliwatia moyo wamisionari wapya na mapadre kupokea kila utamaduni kwa uwazi, heshima, na nia ya kujifunza. Uinjilishaji halisi hauanzii kwa kulazimisha utamaduni wa mtu mwenyewe bali kwa kutambua uwepo wa Mungu tayari unafanya kazi ndani ya maisha ya watu anaowahudumia. Kwa Padre Sieland, maisha ya wamisionari hawa wastaafu ni ukumbusho kwamba urithi mkubwa zaidi wa kimisionari haupimwi kwa majengo au takwimu bali kwa maisha yaliyohamishwa. kupitia huduma ya unyenyekevu, upendo unaodumu, na Injili inayoishi kwa uhalisia. Ushuhuda wao unaendelea kulitia moyo Kanisa la PNG kukumbatia utume unaoashiriwa na heshima, utamadunisho, na kujitolea bila ubinafsi kwa watu wa Mungu.

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.

09 Julai 2026, 12:55