Tafuta

 Wamisionari wa Shirika la Maria Malkia wa Mbinguni nchini Ufilipino. Wamisionari wa Shirika la Maria Malkia wa Mbinguni nchini Ufilipino. 

Ufilipino:Watawa warejesha heshima ya wanawake wahanga wa unyonyaji

Nchini Ufilipino,Wamisionari wa Shirika la Maria Malkia wa Mbinguni(MQHM) kwa miongo mitatu wamekuwa wakifanya utume wa kuwaokoa na kuwarejesha hadhi ya mamia ya wanawake na wasichana walioathiriwa na biashara haramu ya ngono,ukahaba na unyanyasaji wa watoto.Shirika hili lilianza mwaka 1996 katika Jimbo Kuu la Cebu,Ufilipino.

Na Sr. Christine Masivo, CPS.

Kwa miaka 30 Wamisionari wa Shirika la Maria Malkia wa Mbinguni wamewasaidia wahanga kwa kuwapa makazi, ushauri nasaha, elimu na mafunzo ya ufundi ili kuwasaidia wahanga kujenga upya maisha yao na kurejesha heshima kwa wanawake ambao wameathiriwa na unyonyaji.

Utume wa huruma

Sr. Corazon J. Salazar, mwanzilishi na Mama Mkuu wa Shirika la Wamisionari wa Maria Malkia wa Mbinguni, walianzisha jumuiya hiyo pamoja na watawa wengine sita mwaka 1996 kutokana na kuongezeka kwa nyanyasi za kijinsia na Biashara haramu ya wasichana wadogo na vijana wanaoishi katika umaskini huko Ufilipino.

Kupitia utume wao, wanazingatia kujenga upya matumaini na mustakabali kwa waathiriwa wa nyanyaso na unyonyaji. Dhamira ni kuwaokoa wasichana wadogo na wanawake vijana, kuanzia umri wa miaka minane kutokana na ukahaba na biashara haramu ya binadamu, kuwapa makazi salama, utunzaji na upendo na kisha baadaye kutoa msaada wa kielimu kwa walionusurika na watoto kutoka jamii maskini za vijijini, ili kuvunja mzunguko wa umaskini kupitia elimu na mafunzo. Wao hufanya hivi kwa kuwapa wasichana mazingira salama, huduma na usaidizi ili wajiamini na kujitegemea.

Uponyaji na mwanzo mpya

Jumuiya inaendesha 'Nyumba ya Upendo' huko Tuburan, karibu na Cebu ambayo hutoa usaidizi kwa walionusurika kutokana na ukahaba na biashara haramu ya ngono. Shirika la Kipapa la Habari la Kimisionari Fides liliripoti kwamba, Askofu Mkuu Alberto S. Uy wa Cebu katika ziara yake ya hivi karibuni kwenye nyumba hiyo alisema: "Kwa kuona huduma ya Wamisionari wa Maria Malkia wa Mbinguni moja kwa moja kulinigusa sana. Hii ni kazi inayoendeleza  uhai." Alithamini kazi hiyo nzuri na kuelezea uungaji mkono wake kwa ajili ya  huduma hiyo, huku akiomba msaada zaidi ili kusaidia Shirika  kukamilisha vifaa vyake na kupanua huduma yake kwa watoto na wanawake vijana walio katika mazingira magumu.

‘My Bonita Girls’ Home’ yaani ‘Nyumba Yangu ya Wasichana ya Bonita’ huko Purok, katika manispaa ya Mtakatifu Jose pia huwasaidia watoto ambao wameathiriwa na nyanyaso. Vituo hivi viwili hutoa usaidizi na ushauri nasaha, elimu na mafunzo ya ufundi ili kuwasaidia manusura kuungana tena na jamii. Sr. Corazon alisema kuwa wanawake wengi ambao wameshiriki katika programu hii tayari wameunganishwa tena na jamii na kuonesha umuhimu wa usaidizi wa muda mrefu zaidi ya uokoaji.

Elimu kinga dhidi ya biashara haramu

Dhamira ya watawa katika kupunguza Biashara haramu wa binadamu na ukahaba ni kushughulikia sababu kuu ambayo ni umaskini. ‘Programu ya Usaidizi wa Elimu ya Regina Coeli’ inasaidia watoto na familia wanaoishi katika jamii maskini za vijijini kupitia mafunzo ya elimu. Pia inalenga kuwalinda wasichana wadogo na vijana kutoka kwa waajiri haramu wanaofanya kazi katika jamii zao, ikiahidi kazi za uwongo ili kuwadanganya wazazi na kuwashawishi wawapeleke watoto wao mbali nao.

Hili ni hitaji la dharura kwani kwa muda mrefu wamekabiliwa na changamoto zinazohusisha usafirishaji haramu wa binadamu na unyanyasaji wa kingono wa wanawake na watoto. Tatizo hili pia limebadilika katika miaka ya hivi karibuni na kuongezeka kwa kuhama kutoka eneo halisi hadi majukwaa ya kidijitali.

Nyumbani kwa wote

Cebu imekuwa ikitumika kama mahali pa asili, usafiri na mahali pa mwisho kwa waathiriwa wa biashara haramu ya binadamu, wanaoathiriwa na umaskini katika maeneo ya vijijini na shughuli kubwa za watalii. Makadirio ya kimataifa yanaonesha kuwa kati ya watoto 60,000 na 100,000 nchini Ufilipino hulazimishwa kufanya ukahaba au biashara haramu ya ngono kila mwaka.

Kulingana na Idara ya Sheria ya Ufilipino, unyonyaji wa kijinsia ndio aina iliyoenea zaidi ya biashara haramu ya binadamu. Miongoni mwa waathiriwa waliotambuliwa kote nchini, wanawake na wasichana wanachangia idadi kubwa ya visa. Katika ngazi ya kitaifa, zaidi ya 70% ya hatia za biashara haramu ya binadamu zinahusishwa haswa na unyonyaji wa ngono haramu ya kibiashara.   Kwa Wamisionari wa Maria Malkia wa Mbinguni, mwitikio unazidi kuwaokoa waathiriwa. Kupitia makazi, uponyaji, elimu na fursa za ajira, dada hao hutafuta kuwapa manusura zana za kujenga upya maisha yao na kusaidia jamii zilizo katika mazingira magumu kuzuia unyonyaji kabla haujatokea.

UFILIPINO: WATAWA

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku. Just click here.

11 Agosti 2026, 15:43