Tafuta

Askofu mkuu Ieronymos II wa Kanisa la Kiorthodox la Athene na Ugiriki nzima amewataka waamini kusima imara kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu pamoja na mazingira. Askofu mkuu Ieronymos II wa Kanisa la Kiorthodox la Athene na Ugiriki nzima amewataka waamini kusima imara kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu pamoja na mazingira. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Cyprus na Ugiriki: Waorthodox

Askofu mkuu Ieronymos II wa Kanisa la Kiorthodox la Athene na Ugiriki nzima anapenda kukazia umuhimu wa elimu makini, uhuru wa kuabudu na usawa kwa wakimbizi na wahamiaji. Waendeleze majadiliano ya kiekumene, ili siku moja, wote waweze kuwa wamoja chini Kristo Yesu. Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni tema inayopaswa kuvaliwa njuga na watu wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kuanzia Jumamosi tarehe 4 hadi Jumatatu tarehe 6 Desemba 2021 anafanya hija ya kitume nchini Ugiriki kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Jiwekeni Wazi Kwa Mshangao wa Mungu.” Ugiriki ni nchi ambayo imetikiswa sana na myumbo wa uchumi kitaifa na Kimataifa. Kumbe, hija hii ya kitume, ni kielelezo cha mwanga wa matumaini kwa nchi ya Ugiriki ambayo kimsingi ina utajiri mkubwa wa historia ya imani. Baba Mtakatifu baada ya kukutana na kuzungumza na viongozi wa serikali, vyama vya kiraia na wanadiplomasia, Jumamosi jioni tarehe 4 Desemba 2021 alipata nafasi ya kumtembelea Askofu mkuu Ieronymos II wa Kanisa la Kiorthodox la Athene na Ugiriki nzima.

Kwa upande wake Askofu mkuu Ieronymos II wa Kanisa la Kiorthodox la Athene na Ugiriki nzima amekumbushia kuhusu safari ya kwanza Mtakatifu Paulo Mtume huko Athene na alipokuwa anatoa hotuba yake ya mwanzo, akiwahubiria kuhusu Mungu wanayemwabudu bila kumjua. Rej. Mdo 17: 23. Amekumbushia hija yao pamoja kwenye Kisiwa na Lesvos kwa ajili ya kuwafariji wakimbizi na wahamiaji pamoja na kuendelea kuimarisha majadiliano ya kiekumene. Baba Mtakatifu anatembelea nchini Ugiriki wakati huu ambako maambukizi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 yanaendelea kupamba moto, kuna vitendo vingi vya jinai; ukosefu wa amani na utulivu; mambo yanayopelekea hofu na watu kukata tamaa na kwamba, binadamu wote ni sawa mbele ya Fumbo la Kifo. Jambo la msingi kwa Makanisa haya ni kuendelea kujikita katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia amani, kwa kuondoa hofu na mashaka na kukuza imani, sanjari na kusimama kidete kulinda na kutetea utu, heshima na uhai wa binadamu. Wakimbizi na wahamiaji ni watu wanaohitaji kuonjeshwa upendo, kupokelewa jinsi walivyo, kueleweka na kuwajali.

Askofu mkuu Ieronymos II wa Kanisa la Kiorthodox la Athene na Ugiriki nzima anapenda kumuunga mkono Baba Mtakatifu Francisko katika kukazia umuhimu wa elimu makini, uhuru wa kuabudu na usawa kwa wakimbizi na wahamiaji. Wanataalimungu wa Makanisa haya mawili wanapaswa kuendelea kujikita katika majadiliano ya kiekumene, ili siku moja, wote waweze kuwa wamoja chini Kristo Yesu. Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni tema inayopaswa kuvaliwa njuga na watu wote wa Mungu katika ujumla wao. Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii yanogeshwe na kanuni maadili, utu wema pamoja na uwajibikaji. Diplomasia katika ukweli na uwazi, isaidie kukuza mchakato wa mapambano kwa ajili ya watu kujipatia uhuru wa kweli. Anampongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuendelea kusimama kidete kulinda na kutetea misingi ya haki na amani; mazingira nyumba ya wote; pamoja na mapambano dhidi ya umakini duniani. Kanisa la Kiorthodox nchini Ugiriki litaendelea kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene katika ukweli, uwazi na upendo, ili Injili isonge mbele, Mwenyezi Mungu atukuzwe na mwanadamu aweze kutakatifuzwa.

Askofu mkuu
05 December 2021, 15:43