Tafuta

Kanisa nchini Cyprus limekuwa mstari wa mbele kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za wakimbizi na wahamiaji. Kanisa nchini Cyprus limekuwa mstari wa mbele kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za wakimbizi na wahamiaji. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Cyprus na Ugiriki: Kanisa Na Huduma Kwa Wakimbizi

Changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani linahitaji majibu muafaka kutoka kwa Jumuiya ya Kimataifa. Ujenzi wa kuta za umeme ni kielelezo cha hofu isiyokuwa na mashiko. Dhamana na utume wa Kanisa kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji ni kuhakikisha kwamba, Kanisa linasimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha: utu, heshima na haki zao msingi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Cyprus amewakumbusha waamini kwamba, Kristo Yesu anaendelea kupita hata katika barabara za Cyprus. Anasikiliza na kujibu kilio chao! Anagusa nyoyo zao, jambo la msingi kwa waamini hawa ni kuwa na imani kwa Kristo Yesu ili aweze kuwakirimia mwanga, hatimaye aweze kuwaganga na kuwatibu katika upofu wao ili watembee katika mwanga. Kristo Yesu anaweza kuganga, kuponya na kupyaisha udugu wa kibinadamu, kwa kuwanogeshea furaha ya maisha. Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Cyprus kuanzia tarehe 2-4 Desemba 2021 inanogeshwa na kauli mbiu “Tufarijiane Katika Imani”. Haya ni maneno yanayotokana na jina na Mtume Barnaba, maana yake Mwana wa Faraja! Ni yule Mtume aliyekuwa na shamba akaliuza, akaileta fedha, akaiweka miguuni pa Mitume! Rej. Mdo 4: 36. Baba Mtakatifu katika hija hii ya kitume anapenda kukazia umuhimu wa watu wa Mungu kufarijiana katika imani, kama sehemu ya nyenzo muhimu katika mchakato wa kukuza na kudumisha majadiliano, ujenzi wa madaraja yanayowakutanisha watu sanjari na ukarimu; amali za jamii nchini Cyprus.

Askofu mkuu Pierbattista Pizzaballa, Msimamizi wa kitume wa Upatriaki wa Yerusalemu, katika salam zake za kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko kushiriki katika Sala ya Kiekumene kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji, Ijumaa tarehe 3 Desemba 2021 amegusia kuhusu madonda ya mwanadamu kutokana na vifo vya wakimbizi na wahamiaji katika Bahari ya Mediterrania. Hawa ni watu wanaokimbia vita, machafuko na mipasuko ya kijamii; njaa, umaskini na hali ngumu ya maisha. Ni watu wanaotafuta: Usalama, hifadhi na maisha bora zaidi. Huu ni umati mkubwa wa watu ambao kamwe hauwezi kufichika machoni pa watu. Ni watu wanaotafuta maisha bora zaidi Barani Ulaya. Changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani linahitaji majibu muafaka kutoka kwa Jumuiya ya Kimataifa. Ujenzi wa kuta za umeme ni kielelezo cha hofu isiyokuwa na mashiko wala masilahi mapana ya watu wa Mungu. Wakimbizi na wahamiaji ni muhimu sana kwa ustawi, maendeleo na mafao ya Bara la Ulaya katika ujumla wake.

Dhamana na utume wa Kanisa kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji ni kuhakikisha kwamba, Kanisa linasimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha: utu, heshima na haki zao msingi. Kanisa nchini Cyprus linamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kujali na kusikiliza shuhuda za wakimbizi na wahamiaji, ili kujenga na kudumisha misingi ya amani, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki nchini Cyprus, Caritas Cyprus limekuwa ni sauti ya wale wasiokuwa na sauti kwa kutoa huduma kwa wakimbizi na wahamiaji kutoka Mashariki ya Kati, Afrika na Mashariki ya mbali. Hawa ni watu ambao wameteswa na kunyanyaswa utu, heshima na haki zao msingi. Caritas Cyprus imekuwa ni chombo cha faraja, imani na matumaini kwa wale waliokuwa wamekata tamaa kwa kuwapatia mahitaji msingi. Caritas Cyprus itaendelea kuwa ni chombo na shuhuda wa Injili ya upendo na matumaini.

Wakimbizi na wahamiaji katika shuhuda zao, wanasisitiza umuhimu wa wao kutambulika kama binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, ndugu, rafiki, mwamini na jirani mwema. Hakuna sababu ya kujenga chuki na uhasama dhidi ya wageni wanaotafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Wakimbizi na wahamiaji ni watu ambao wameathirika sana kutoka na vita, chuki na mipasuko ya kijamii. Hawa ni wahanga wa athari za mabadiliko ya tabianchi na sasa wanatafuta usalama zaidi pamoja na matumaini ya kupata maisha bora zaidi. Hii ni safari katika mwanga wa imani, maarifa na udugu wa kibinadamu. Vijana hawa wana ndoto ya amani, uhuru wa kweli, mahali ambapo utu, heshima na haki msingi za binadamu zinalindwa. Wana ndoto za kufahamiana na wengine, ili kujenga na kurutubisha mafungamano ya kijamii.

Kanisa na Wakimbizi
04 December 2021, 15:34