Tafuta

Hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Ugiriki: kuanzia tarehe 4 hadi 6 Desemba 2021: Kauli mbiu: Jiwekeni wazi kwa mshangao wa Mungu. Hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Ugiriki: kuanzia tarehe 4 hadi 6 Desemba 2021: Kauli mbiu: Jiwekeni wazi kwa mshangao wa Mungu. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Cyprus na Ugiriki: Mshangao wa Mungu

Baba Mtakatifu Francisko alipowasili kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Athens, Ugiriki amepokelewa na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na kupokea shada la maua kutoka kwa watoto waliokuwa wameandaliwa kwa tukio hili. Baba Mtakatifu amekagua gwaride la heshima lililoandaliwa kwa ajili ya heshima yake na hatimaye, wakatambulishana viongozi walioko kwenye msafara wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kuanzia Jumamosi tarehe 4 hadi Jumatatu tarehe 6 Desemba 2021 anafanya hija ya kitume nchini Ugiriki kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Jiwekeni Wazi Kwa Mshangao wa Mungu.” Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 36 ya Vijana Ulimwenguni. Huu ni ujumbe makini hasa katika kipindi hiki ambacho kuna maambukizi makubwa ya Virusi vya Korona, UVIKO-19 vinavyotishia maisha, ustawi na maendeleo ya wengi. Ugiriki ni nchi ambayo ilitikiswa sana na myumbo wa uchumi kitaifa na Kimataifa. Kumbe, hija hii ya kitume, ni kielelezo cha mwanga wa matumaini kwa nchi ya Ugiriki ambayo kimsingi ina utajiri mkubwa wa historia ya imani. Hiki ni kipindi kigumu sana cha maisha ya watu wengi nchini Ugiriki.

Watu wa Mungu nchini humo wanamwona Baba Mtakatifu Francisko kama rafiki anayewatembelea ili kuwaimarisha katika imani, matumaini na mapendo! Baba Mtakatifu baada ya kukagua gwaride la heshima kwa ajili yake na kuagana na wenyeji wake, aliondoka kuelekea nchini Ugiriki. Akiwa njiani, amemtumia salam na matashi mema Rais Nicos Anastasiades “Νίκος Αναστασιάδης”, Rais wa Cyprus. Kwa mara nyingine tena, Baba Mtakatifu amemshukuru Rais wa Cyprus pamoja na watu wake kwa makaribisho makubwa na ukarimu waliomwonesha wakati wa hija yake ya kitume nchini mwao. Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia sala zake kwa ajili ya kuombea amani, ustawi na maendeleo ya taifa la Cyprus. Mwishoni, amewapatia wote baraka zake za Kipapa.

Baba Mtakatifu Francisko alipowasili kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Athens, nchini Ugiriki amepokelewa na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na kupokea shada la maua kutoka kwa watoto waliokuwa wameandaliwa kwa tukio hili. Baba Mtakatifu amekagua gwaride la heshima lililoandaliwa kwa ajili ya heshima yake na hatimaye, wakatambulishana viongozi walioko kwenye msafara wake. Amekwenda moja kwa moja hadi kwenye Ikulu ya Athens ili kumtembelea Rais Katerina Sakellaropoulou wa Ugiriki na baadaye amekutana pia na Bwana Kyriakos Mītsotakīs (Kyriakos Mitsotakis) Waziri Mkuu wa Ugiriki aliyeanza kushika madaraka yake kunako tarehe 8 Julai 2019.

Papa Nchini Ugiriki
04 December 2021, 15:25