Tafuta

Jumamosi jioni tarehe 4 Desemba 2021 Baba Mtakatifu Francisko alipata nafasi ya kumtembelea Askofu mkuu Ieronymos II wa Kanisa la Kiorthodox la Athene na Ugiriki nzima. Jumamosi jioni tarehe 4 Desemba 2021 Baba Mtakatifu Francisko alipata nafasi ya kumtembelea Askofu mkuu Ieronymos II wa Kanisa la Kiorthodox la Athene na Ugiriki nzima.  

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Cyprus na Ugiriki: Roho Mtakatifu: Madonda ya Utengano

Umuhimu wa kuendelea kurutubisha ushirika kwa kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kuwapaka mafuta ya ushirika. Wakristo wawe wanyenyekevu ili Roho Mtakatifu aweze kuwapaka mafuta ya hekima, awakirimie mafuta ya faraja ili waweze kushirikiana kikamilifu ili kukabiliana na changamoto daima wakidumu katika imani kwa Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 4-6 Desemba 2021 anafanya hija ya kitume nchini Ugiriki kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Jiwekeni Wazi Kwa Mshangao wa Mungu.” Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa maadhimisho ya Siku ya 36 ya Vijana Ulimwenguni. Baba Mtakatifu baada ya kukutana na kuzungumza na viongozi wa serikali, vyama vya kiraia na wanadiplomasia, Jumamosi jioni tarehe 4 Desemba 2021 alipata nafasi ya kumtembelea Askofu mkuu Ieronymos II wa Kanisa la Kiorthodox la Athene na Ugiriki nzima. Katika hotuba yake amekumbushia hija yake ya kitume aliyoifanya Kisiwani Lesvos; Umuhimu wa kuendelea kurutubisha ushirika kwa kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kuwapaka mafuta ya ushirika, ili kunogesha ushirika wa kidugu unaovuta neema ya Mungu. Wakristo wawe wanyenyekevu ili Roho Mtakatifu aweze kuwapaka mafuta ya hekima inayomwilishwa katika huduma. Roho Mtakatifu awakirimie mafuta ya faraja ili waweze kushirikiana kikamilifu ili kukabiliana na changamoto mamboleo, daima wakidumu katika imani kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu!

Baba Mtakatifu Francisko amesema, nia ya kumtembelea ni kutoa heshima yake kwa unyenyekevu kwa Wakristo wa Kanisa la Kiorthodox, ili kupyaisha ushirika wa kitume, ili hatimaye, kuimarisha udugu wa upendo. Baba Mtakatifu amekumbushia hija yake ya kitume Kisiwani Lesvos walipokwenda kuwatembelea na kuwafariji wakimbizi na wahamiaji kama kielelezo cha ushirika wa kitume. Ukanda wa Mediterrania umekuwa maarufu sana kutokana na matatizo na changamoto zinazoendelea kujitokeza, lakini pia ni mahali pa kuwakutanisha watu kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Ikumbukwe kwamba, Wakristo wote wanaunganishwa kwa sababu wamejengwa juu ya msingi wa Mitume na Manabii na Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni. Rej. Efe 2:20. Huu ndio mzizi wa Habari Njema ya Wokovu iliyoanza kuzaa matunda katika utamaduni wa Kigiriki na matokeo yake ni kuibuka kwa umati mkubwa wa Mababa wa Kanisa sanjari na Maadhimisho ya Mitaguso mikuu ya Kanisa.

Utengano wa Kanisa ulipotokea, Wakristo wakashindwa kurutubisha ushirika, aibu kubwa kwa Kanisa Katoliki. Uchu wa madaraka, ukadhohofisha ushirika na matokeo yake Kanisa likameguka! Kumbe, huu ni wakati wa kuomba msamaha kwa Mwenyezi Mungu na kwa Wakristo wa Kanisa la Kiorthodox, kwa makosa yaliyotendwa na Wakatoliki. Lakini jambo la msingi ni kukumbuka kwamba, ule mzizi wa kitume uliopandwa na Mwenyezi Mungu unaendelea kuzaa matunda kwa njia ya Roho Mtakatifu, mwaliko ni kukiri na kutambua matunda mema kutoka kwa wengine. Kwa njia ya nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu, Kanisa lilizaliwa. Na kwa njia ya mafuta ya Roho Mtakatifu anaweza kuiangazia safari ya ushirika wa Kanisa. Baba Mtakatifu anasema, Roho Mtakatifu ni mafuta ya ushirika yanayowawezesha waamini kuona mng’ao wa ubinadamu, tayari kuanza mchakato wa ujenzi wa ushirika wa Kanisa na hivyo kuondokana na chachu ya ubinafsi pamoja na ugumu wa kitaasisi. Tofauti miongoni mwa Wakristo zinapaswa kupewa uwiano na ushirika.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, ushirika wa kidugu unavuta neema ya Mungu na kuwataka kujikita zaidi katika ujenzi wa udugu wenye mwelekeo mpana zaidi, ili kukuza na kudumisha uhuru wa kuabudu. Ni sala ya Baba Mtakatifu kwamba, Wakristo watashinda vikwazo vyao na kuwa ni wajenzi wa ushirika unaosimikwa katika upendo wa kidugu unaofukuzia mbali hofu na kuigeuza kuwa ni sehemu ya mchakato wa upendo na kwa njia hii, waamini wataweza kugundua kwamba, wote wanaokolewa na umoja. Wakristo wamwombe Roho Mtakatifu awajalie ujasiri wa kufuata maongozi yake ili ushirika wao uweze kujengwa katika msingi wa Fumbo la Utatu Mtakatifu na wala si kwa mahesabu, sera, mipango na uzoefu wao. Roho Mtakatifu ni chemchemi ya hekima, wito na mwaliko kwa Wakristo wote kuonesha unyenyekevu, utakaowawezesha kukua na kukomaa katika ufahamu wa Mungu. Kanisa la Kiorthodox limepiga hatua kubwa katika mchakato wa utamadunisho wa imani nchini Ugiriki. Hii inatokana na Kanisa kutoa kipaumbele cha pekee katika malezi na majiundo ya kitaalimungu.

Kumekuwepo na ushirikiano mkubwa kati ya Huduma ya Kitume “Apostoliki Diakonia” ya Kanisa la Kiorthodox pamoja na Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo. Maadhimisho ya Tamasha la Kitaalimunhu kati ya Kitivo cha Taalimungu Chuo Kikuu cha Salonica na Chuo Kikuu cha Kipapa cha Antonianum kilichoko Roma. Matukio yote haya mawili yamesaidia kujenga uhusiano mwema kati ya wanataalimungu wa Makanisa haya mawili kiasi hata cha kubadilishana mawazo. Ushiriki wa Kanisa la Kiorthodox katika Tume ya Pamoja ya Kiekumene Kimataifa ya Majadiliano ya Kitaalimungu kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiorthodox ni jambo la kutia moyo! Roho Mtakatifu ni mafuta ya faraja anayeganga na kuponya madonda ya utengano na hali ngumu ya maisha. Baba Mtakatifu anasema, kuna haja ya kushirikiana na kushikamana katika utekelezaji wa matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Lengo ni kuweza kukabiliana na changamoto za kimaadili na kijamii, ili kuwaokoa watu wa nyakati hizi kwa faraja ya Injili. Roho Mtakatifu anawataka Wakristo pengine kuliko wakati mwingine wowote kuganga na kuponya madonda ya binadamu kwa mafuta ya upendo na sala kama alivyofanya Kristo Yesu alipokuwa pale kwenye Bustanini Gethsemane.

Roho Mtakatifu awapatie mafuta ya faraja ili kuganga mahusiano na mafungamano yao yaliyojeruhiwa, lakini jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, wanatakasa kwanza kumbukumbu zao za kale ili waweze kusameheana na hatimaye, kupatana. Yale yaliyojitokeza miaka kadhaa iliyopita hata leo hii yanaweza kujitokeza pia. Wakristo wote wanahimizwa kujizatiti zaidi katika imani yao kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Roho Mtakatifu awajalie utulivu, mwanga angavu na mwono wa ukweli ili kuona huruma na upendo wa Mungu unaokoa. Kanisa Katoliki kwa wakati huu linaendelea kujielekeza katika mchakato wa kumwilisha dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa, ili kudumisha ushirika na utume wa Kanisa miongoni mwa waamini, ili hatimaye, Roho Mtakatifu aweze kuwashukia na kuijaza nyoyo zao. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake, amewaomba watakatifu, mashuhuda na waungama imani walioungana huko mbinguni waweze kuwaombea, ili Roho Mtakatifu aweze kuwashukia na kukaa juu yao, ili zaidi na zaidi watamani ushirika na kuendelea kuwakirimia hekima na faraja!

Kanisa la Kiorthodox
05 December 2021, 16:01