Tafuta

Hija ya Kitume ya Papa Francisko nchini Cyprus na Ugiriki: Huduma ya Kiekumene kwa wakimbizi na wahamiaji Hija ya Kitume ya Papa Francisko nchini Cyprus na Ugiriki: Huduma ya Kiekumene kwa wakimbizi na wahamiaji 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Cyprus Na Ugiriki: Uekumene na Wakimbizi

Katika hotuba yake ya sala ya kiekumene kwa ajili ya kuwaombea wakimbizi, wahamiaji na wale wanaotafuta hifadhi ya kisiasa amekazia kuhusu: ukarimu wa watu wa Mungu, madonda ya chuki na uhasama na umuhimu wa jamii kujielekeza zaidi katika ushirika na ujenzi wa mshikamano na udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza vijana kwa shuhuda zao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kanisa Katoliki katika sera na mikakati yake kuhusu huduma kwa wakimbizi na wahamiaji linapenda kukazia kwa namna ya pekee umuhimu wa: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapatia hifadhi. Baba Mtakatifu Francisko, tangu mwanzo wa utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, ameguswa sana na matatizo, changamoto na fursa zinazowakabili wakimbizi, wahamiaji na watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa sehemu mbalimbali za dunia. Hawa ni watu wanaokimbia vita, dhuluma, nyanyaso, majanga asilia na umaskini, changamoto na mwaliko kwa familia ya binadamu kusoma alama za nyakati, ili kujenga utamaduni wa upendo na mshikamano wa kidugu. Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Cyprus kuanzia Alhamisi tarehe 2 hadi Jumamosi tarehe 4 Desemba 2021 inanogeshwa na kauli mbiu “Tufarijiane Katika Imani.” Baba Mtakatifu wakati wa hija yake ya Kitume nchini Cyprus Ijumaa tarehe 3 Desemba 2021 alikutana na kuzungumza na viongozi wa Sinodi Takatifu ya Kanisa la Kiorthodox na kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, jioni alipata nafasi ya kushiriki sala ya kiekume na hivyo kuzungumza na wakimbimbizi na wahamiaji kwenye Parokia ya Msalaba Mtakatifu mjini Nicosia.

Baba Mtakatifu alisikiliza shuhuda zilizotolewa na viongozi wa Kanisa, Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Cyprus pamoja na wakimbizi na wahamiaji. Katika hotuba yake ya sala ya kiekumene kwa ajili ya kuwaombea wakimbizi, wahamiaji na wale wote wanaotafuta hifadhi ya kisiasa amekazia kuhusu: ukarimu wa watu wa Mungu, madonda ya chuki na uhasama na umuhimu wa jamii kujielekeza zaidi katika ushirika na ujenzi wa mshikamano na udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza vijana kwa shuhuda zao. Kwa namna ya pekee amemshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwa mambo haya aliwaficha wenye hekima na akili, akawafunulia watoto wachanga juu ya Ufalme wake unaosimikwa katika: upendo, haki na amani. Baba Mtakatifu amewafariji wakimbizi na wahamiaji hawa kwa kusema kwamba ndani ya Kanisa hakuna wageni wala wapitaji, bali wote ni wenyeji pamoja na watakatifu, kielelezo makini cha ndoto ya Mungu anayewatakia watoto wake amani na ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Wahamiaji na wakimbizi, katika shida na mahangaiko yao, wanajikuta hata wakipoteza utu, heshima, haki msingi za binadamu na utambulisho wao.

Baba Mtakatifu amewataka waamini na watu wenye mapenzi mema kukumbuka kwamba, wao ni ndugu, rafiki, waamini na majirani wema. Ubinafsi, uchoyo, uchu wa mali na madaraka vimepelekea watu wengi duniani kutumbukizwa katika mifumo mbalimbali ya utunwa mamboleo. Kinyume chake, waamini wajenge na kudumisha Injili ya upendo inayowaweka huru dhidi ya chuki na uhasama. Watu wengi wamejeruhiwa kutoka katika undani wa maisha yao. Chuki na uhasama vimeathiri pia mahusiano na mafungamano miongoni mwa Wakristo. Chuki ni ni mwelekeo potofu wa maisha unaoshindwa kutambua wengine kuwa kama ndugu na badala yake, wanageuzwa na kuthaminishwa kama bidhaa sokoni inayoweza kuuzwa au kununuliwa kwa ajili ya masilahi ya mtu binafsi. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuanza mchakato wa kutoka katika kinzani na mipasuko ya kijamii na kuanza kujielekeza katika ujenzi wa ushirika, ni safari ndefu lakini haitishi hata kidogo.

Watu waogope tabia ya kutaka kujifungia katika ubinafsi wao, maamuzi mbele yanayogumisha mchakato wa watu kukutana na kuanza kutembea kwa pamoja. Chuki na maamuzi mbele ni chanzo cha ujenzi wa kuta yaani uadui ambao Kristo Yesu alikwisha kuubomoa. Rej. Efe 2:14. Majadiliano ya kiekumene ili kuweza kufikia umoja kamili, yanawezekana ikiwa kama Wakristo wote watamwangalia Kristo Yesu ambaye ni amani ya watu wake. Kristo Yesu ni jiwe kuu la pembeni anayekuja kukutana na ndugu zake wanaonyanyaswa, kudharauliwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii. Uhamiaji unapaswa kuwa ni safari ya matumaini, amani na utulivu. Kuna haja ya watu bado kuendelea kuota ndoto ya Mungu inayosimikwa katika amani, ushirika na udugu wa kibinadamu. Hata katika tofauti zao msingi, watu watambuane kuwa ni ndugu wamoja. Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, Cyprus ni nchi ambayo imegawanyika na kumeguka kutokana na kinzani za kisiasa na za kidini. Lakini ni nchi ambayo imeonesha dalili kwamba, inaweza kuwa ni maabara ya ujenzi wa udugu wa kibinadamu kutokana na ukarimu wake, licha ya changamoto na matatizo mbalimbali yanayoikabili nchi hii. Ili kuweza kufikia lengo hili, kuna haja kwa Cyprus kusimama kidete kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Huu ni msingi wa kanuni maadili na utu wema. Baba Mtakatifu anakaza kusema, hiki ni kiini pia cha Mafundisho Jamii ya Kanisa. Kumbe, ni mwaliko wa kuondokana na chuki na uhasama na kuanza kujielekeza zaidi kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo; kwa kukazia ujenzi wa madaraja ya watu kukutana na wala si kukimbiana wala kukimbizana. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, kuna maelfu ya wakimbizi na wahamiaji waliofariki dunia wakijaribu kutafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi. Kuna watu ambao wametumbukizwa katika mifumo ya biashara ya binadamu na viungo vyake pamoja na mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo. Kuna wakimbizi na wahamiaji ambao wamefariki dunia kwa baridi, njaa na utupu, kutokana na mipaka kufungwa. Kuna watu wanauwawa kutokana na tabia ya ubaguzi wa rangi, nyanyaso na dhuluma za kidini. Baba Mtakatifu anakaza kusema, ni wajibu wake wa kimaadili kutangaza hali halisi inayowakabili wakimbizi na wahamiaji kutokana na vita, chuki na uhasama. Kuna kuta za nyaya za umeme zinazoendelea kujengwa katika baadhi ya nchi Barani Ulaya. Mipasuko ya kisiasa hata katika nchi husika ni chanzo cha utengano. Kuta za nyaya za umeme sehemu nyingi zinajengwa ili kuwazuia wakimbizi na wahamiaji wasipate hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Lakini ikumbukwe kwamba, wakimbizi na wahamiaji ni watu wanaotafuta: hifadhi, usalama, maisha bora; uhuru, riziki katika maisha, msaada na ujenzi wa udugu wa kibinadamu, lakini kwa bahati mbaya, wanakutana na mkono wa nyuma, hakuna kuingia. Mbele ya changamoto, matatizo na fursa zote hizi, watu waamshe dhamiri njema ili kuwalinda na kuwasaidia.

Wakimbizi
04 December 2021, 15:55