Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko katika mazungumzo yake na watu wa Mungu nchini Ugiriki amekazia umuhimu wa kudumisha mchakato wa utamadunisho wa imani katika uhalisia wa maisha ya watu. Baba Mtakatifu Francisko katika mazungumzo yake na watu wa Mungu nchini Ugiriki amekazia umuhimu wa kudumisha mchakato wa utamadunisho wa imani katika uhalisia wa maisha ya watu. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Cyprus na Ugiriki: Utamadunisho

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba hii alikazia kuhusu umuhimu wa hija yake nchini Ugiriki ili kushangaa mchakato wa utamadunisho wa Injili; mtazamo wa Mtakatifu Paulo, Mtume katika kujiamini na kujikubali na kwamba, uinjilishaji mpya unajikita katika ujenzi wa mahusiano na mafungamano mapya yanayoletwa na Kristo Yesu. Waamini wajiamini na kujipokea kutangaza Injili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko baada ya kukutana na kuzungumza na viongozi wa serikali, vyama vya kiraia na wanadiplomasia, Jumamosi jioni tarehe 4 Desemba 2021 alipata nafasi ya kumtembelea Askofu mkuu Ieronymos II wa Kanisa la Kiorthodox la Athene na Ugiriki nzima, alibahatika kukutana na kuzungumza na wakleri, watawa, majandokasisi pamoja na makatekista kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Dionisio “St. Dionysius.” Amesikiliza kwa makini shuhuda na hatimaye, akawapatia hotuba yake. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba hii alikazia kuhusu umuhimu wa hija yake nchini Ugiriki ili kushangaa mchakato wa utamadunisho wa Injili; mtazamo wa Mtakatifu Paulo, Mtume katika kujiamini na kujikubali na kwamba, uinjilishaji mpya unajikita katika ujenzi wa mahusiano na mafungamano mapya yanayoletwa na Kristo Yesu. Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru watu wote wa Mungu nchini Ugiriki kwa ushuhuda wa imani yao kwa Kristo Yesu, katika huduma kwa watu wa Mungu; imani inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya waamini ndani ya familia. Ugiriki ni nchi ambayo imebahatika kuwa na wasomi katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu, waliojitahidi kutegua kitendawili cha maisha, upendo, mateso na fumbo la kifo.

Imani thabiti ya Mababa wa Kanisa imeiwezesha Ugiriki kuwa ni “maabara ya imani yanayosimikwa katika utakatifu wa maisha, kazi na utume uliotekelezwa na Mtakatifu Paulo, Mtume alipokutana na wanafalsafa wa Athene waliokuwa na haki ya kutoa maamuzi mazito kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wote kwa ujumla. Mtakatifu Paulo Mtume ni mfano bora wa kuigwa katika mchakato wa kuitamadunisha imani. Rej. Mdo 17:16-34. Paulo Mtume, alikuwa na mtazamo wa kujiamini kiasi cha kuwahubiria wanafalsafa kuhusu Kristo Yesu na Ufufuko wa wafu, kiasi kwamba, hotuba hii ikaonekana kuwa ni elimu mpya inayosheheni mambo mapya na Paulo Mtume, akawekwa majaribuni. Katika maisha na utume wake alipambana kikamilifu na kinzani, kwa kufungwa na kufunguliwa; kwa kusimama imara katika imani mjini Thesalonike. Alijitahidi kuinjilisha katika hali na mazingira magumu. Licha ya kuwa peke yake, lakini hakukata wala kukatishwa tamaa, bali alisonga mbele kwa ari na moyo mkuu kwa kujiamini haswa na kumtegemea Mwenyezi Mungu, akalimweka Neno la Mungu kuwa ni nguzo na dira yake ya maisha na utume.

Katika udogo wake, akawa ni chombo makini cha uinjilishaji wa watu. Udogo wa mtu au uchache wa waamini si mali kitu, jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, waamini wanakuwa karibu zaidi na Kristo Yesu kwa kujishusha na kujiaminisha kwa Kristo Yesu “Kenosis” na hivyo kujifanya kuwa hana utukufu, na kutwaa namna ya mtumwa. Rej. Flp 2:7. Hii pia inajitokeza katika Ufalme wa Mungu. Kumbe, kuna haja ya kuwa na moyo mkuu na hivyo kuendelea kudumu katika uinjilishaji. Mtakatifu Paulo Mtume, mbele ya wanafalsafa alionesha tabia na hali ya kujikubali, kama sehemu muhimu sana ya uinjilishaji. Akathamini mbegu ya Neno la Mungu iliyopandwa katika akili na nyoyo za watu, akaona ukweli wa Kimungu ndani mwao na huo ukawa ni msingi thabiti wa uinjilishaji na utamadunisho wa Neno la Mungu. Alitambua ile karama ya uchaji wa Mungu ndani mwao na kuitumia kama njia ya kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu. Alitambua na kuthamini kazi na nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu katika maisha ya waamini na hivyo kujitambua kwamba, yeye ni chombo cha ujenzi wa umoja na udugu wa kitume. Daima mwanadamu amesimika maisha yake katika utamaduni na kwamba, uasili na utamaduni vimeungana kwa karibu sana. Neema hutegemea kuwepo kwa utamaduni, na paji la Mungu humwilishwa na kutamadunishwa na wale wanaolipokea. Rej. Evangelium gaudium, 115.

Katika mchakato wa uinjilishaji mpya, anasema Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto wa kumi na sita,alisema kwamba, kuna haja ya kuwa makini na watu wasioamini wasidhani kwamba, wao ndio walengwa wa mchakato wa uinjilishaji mpya, kwani wanahofia kupokonywa  uhuru wa mawazo pamoja na utashi wao. Mchakato wa uinjilishaji mpya hauna budi kujikita katika ukarimu na ushirika katika ulimwengu mamboleo wenye changamoto kibao. Ni mwaliko wa kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikilizana kama ndugu wamoja, ili kujenga udugu wa kitume katika majadiliano kama njia ya kukabiliana na changamoto mamboleo. Kwa kujiaminisha kwa Mungu, Paulo Mtume, aliweza kupokelewa, wakamkejeli, lakini kuna baadhi ya waamini walimwamini na kujiunga naye na kati yao ni Dionisio, Mwareopago pamoja na mwanamke mmoja jina lake Damari. Baba Mtakatifu anawataka watu wa Mungu nchini Ugiriki kuwa mstari wa mbele katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, ili kuendeleza ile kazi ya kutengeneza maabara ya imani kihistoria kwa kujikita katika mtazamo wa kujiamini, kujipokea ili kuboresha mchakato wa kutangaza Injili kwa chachu ya furaha na udugu wa kitume.

Watu wa Mungu
05 December 2021, 16:28