Tafuta

Juma la 55 la Kuombea Umoja wa Wakristo kuanzia tarehe 18-25 Januari 2022 linanogeshwa na kauli mbiu "Tuliiona Nyota yake Mashariki, Nasi Tumekuja Kumsujudia" Mt 2:2. Juma la 55 la Kuombea Umoja wa Wakristo kuanzia tarehe 18-25 Januari 2022 linanogeshwa na kauli mbiu "Tuliiona Nyota yake Mashariki, Nasi Tumekuja Kumsujudia" Mt 2:2. 

Juma la 55 la Kuombea Umoja wa Wakristo: 18-25 Januari 2022: Nyota

Papa Francisko anawaalika Wakristo wote watambue kwamba, wao ni mahujaji kuelekea kwenye umoja kamili wa Wakristo. Wataweza kufikia lengo hili, ikiwa kama watayaelekeza macho yao kwa Kristo Yesu. Katika kipindi hiki cha Kuombea Umoja wa Wakristo, waamini watolee kama sadaka shida na mahangaiko yao kwa ajili ya mchakato wa umoja na mshikamano wa Kikristo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, mchakato wa majadiliano ya kiekumene kati ya Makanisa na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo unafumbatwa katika: Uekumene wa damu, maisha ya kiroho, sala na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kielelezo cha ushuhuda wa Injili ya Kristo inayotangazwa, kushuhudiwa na hatimaye , kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu wa Mungu. Juma la 55 la Kuombea Umoja wa Wakristo kuanzia tarehe 18-25 Januari 2022 linaongozwa na kauli mbiu “Tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia.” Mt 2:2. Tafakari ya kuombea umoja wa Wakristo kwa Mwaka 2022 imeandaliwa na Baraza la Makanisa Mashariki ya Kati na linahitimishwa kwa Sikukuu ya kuongoka kwa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa hapo tarehe 25 Januari 2022. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika, tarehe 16 Januari 2022 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amewaalika Wakristo wote katika tofauti zao msingi, Mapokeo na tamaduni zao, watambue kwamba, wao ni mahujaji kuelekea kwenye umoja kamili wa Wakristo. Wataweza kufikia lengo hili, ikiwa kama watayaelekeza macho yao kwa Kristo Yesu. Katika kipindi hiki cha Kuombea Umoja wa Wakristo, waamini watolee kama sadaka shida na mahangaiko yao kwa ajili ya mchakato wa umoja  wa Wakristo.

Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuongoza Masifu ya Jioni kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo nje ya kuta za Roma kuanzia saa 11:30 jioni kwa saa za Ulaya, sawa na saa 1:30 Usiku kwa Saa za Afrika Mashariki. Hili ni tukio la kiekumene linaloyashirikisha Makanisa na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo. “Tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia.” Mt 2:2. Katika kipindi hiki chenye changamoto nyingi za kiafya, kiuchumi, kijamii na kisiasa, watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia wanaona kuna haja ya kutafuta mwanga angavu utakaoshinda giza linalomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Kristo Yesu ndiye Mwanga wa Mataifa, “Lumen Gentium” na hivyo Kanisa ni Sakramenti, Ishara na Chombo kinachowaunganisha watu kiundani na Mwenyezi Mungu na hivyo kuleta umoja kati ya wanadamu wote. Rej. LG 1. Kumbe, watu wa Mungu wanahimizwa kuuangalia mwanga wa nyota angavu, inayopyaisha: imani, matumaini na mapendo hasa katika eneo la Mashariki ya Kati ambalo linakabiliwa na changamoto pevu: Kisiasa, kiuchumi, kijamii na hata kidini.

Mlipuko wa Lebanon uliotokea mwezi Agosti 2020 umeacha madhara makubwa katika maisha ya watu wa Mungu nchini Lebanon. Wakristo kutoka Lebanon, Siria na Misri wameandaa muswada wa tafakari na sala zinazotumika kwa ajili ya Juma la 55 la Kuombea Umoja wa Wakristo kwa mwaka 2022. Tafakari hizi zimehaririwa na hatimaye, kupitishwa na Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC., kwa kushirikiana na Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo, dhamana inayotekelezwa tangu mwaka 1966 mara tu baada ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Katika shida na mahangaiko makubwa ya watu wa Mungu, waamini wanatafuta Mwanga angavu. Katika dhambi na maovu mengi yanayomwandama mwanadamu, waamini wanatafuta uzuri na utakatifu wa maisha. Pale ambapo wameelewa sana na udhaifu wao, wanataka kuweka matumaini yao kwa Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo, wanayemwabudu na kumtukuza. Nyota angavu iliwaongoza Mamajusi kutoka Mashariki hadi mjini Bethlehemu na huko wakamwona Mtoto pamoja na Mariamu mamaye, wakaanguka wakamsujudia, wakamtolea tunu: dhahabu, uvumba na manemane. Rej. Mt. 2: 1-12.

Hizi ni tunu ambazo Makanisa na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo yanazo, kumbe, Wakristo katika ujumla wao, wanawezesha kushirikishana tunu hizi katika maisha yao ya kila siku. Kwa namna ya pekee kabisa, Ukanda wa Mashariki ya Kati unahitaji mwanga wa amani, matumaini na mshikamano, ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Mashariki ya Kati ni uwanja wa watakatifu, mashuhuda na waungama dini. Lakini, leo hii, idadi ya Wakristo huko Mashariki ya Kati ni ndogo sana, kiasi cha kutia mashaka makubwa. Ushuhuda wa umoja wa Wakristo ni cheche za Uinjilishaji unaoweza kuzaa matunda kwa wakati, lakini, kinzani na migawanyiko ni sumu katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaosimikwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Hii ni changamoto ya kushikamana, ili kulinda na kudumisha utu, heshima, haki msingi za binadamu; umoja na udugu wa kibinadamu.

Umoja wa Wakristo 2022
16 January 2022, 14:47