Tafuta

Maadhimisho ya Kongamano la 27 la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Italia yanakita mizizi yake katika: Umoja, Ushiriki na Utume wa Kanisa. Maadhimisho ya Kongamano la 27 la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Italia yanakita mizizi yake katika: Umoja, Ushiriki na Utume wa Kanisa. 

Kongamano la 27 la Ekaristi Takatifu Kitaifa Italia, 25 Septemba

Maadhimisho ya Kongamano la 27 la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Italia kuanzia tarehe 22 hadi tarehe 25 Septemba 2022, huko Matera, yananogeshwa na kauli mbiu: "Turudi Kwenye Ladha ya Mkate kwa Kanisa la Kiekaristi na Kisinodi" yanakita mizizi yake katika: Umoja, Ushiriki na Utume wa Kanisa mintarafu wongofu wa kiikolojia, kichungaji na kitamaduni. Muhimu Injili ya Matumaini

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tume ya Kipapa ya Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kimataifa ilianzishwa rasmi na Papa Leo XIII kunako mwaka 1876 ili kusaidia mchakato wa kumwezesha Kristo Yesu: kufahamika, kupendwa na kutumikiwa kwa njia ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Kumbe, Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kitaifa na Kimataifa katika maisha na utume wa Kanisa ni katekesi endelevu inayogusa: Fumbo la Ekaristi Takatifu, kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ekaristi Takatifu ni Fumbo la Mwanga linalobubujika kutoka katika Neno la Mungu linalohitaji: kutangazwa na kushuhudiwa kama kielelezo cha imani tendaji. Lina hitaji usikivu wa kiibada na ukimya wa kitafakari uwezeshao Neno la Mungu kugusa akili na nyoyo za waamini. Ekaristi Takatifu ni chakula cha maisha ya kiroho na kielelezo cha uwepo endelevu, fungamani na angavu wa Kristo Yesu kati pamoja na waja wake.  Ekaristi takatifu ni shule ya upendo, ukarimu, umoja na mshikamano wa dhati kati ya watu wa Mungu. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti na shule ya Upendo; ni zawadi na sadaka ya Kristo Yesu Msalabani; kielelezo cha huduma inayomwilishwa na kuwasha mapendo kwa Mungu na jirani. Hili ni Fumbo kubwa linalopaswa kuadhimishwa vyema; Kuabudiwa na Kutafakariwa kikamilifu.

Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa Italia 22-25 Septemba 2022
Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa Italia 22-25 Septemba 2022

Mtakatifu Yohane Paulo II katika Waraka wake wa Kitume, “Kaa Nasi Bwana”: Mane, Nobiscum Domine”, anawaalika waamini kujenga utambuzi hai wa uwepo halisi wa Kristo Yesu, katika adhimisho la Ibada ya Misa Takatifu na katika Ibada nje ya Ibada ya Misa Takatifu. Maadhimisho ya Kongamano la 27 la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Italia kuanzia tarehe 22 hadi tarehe 25 Septemba 2022, huko Matera, yananogeshwa na kauli mbiu: “Torniamo al gusto del pane. Per una Chiesa eucaristica e sinodale” "Turudi Kwenye Ladha ya Mkate kwa Kanisa la Kiekaristi na Kisinodi." Ni katika muktadha wa maadhimisho haya, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuhudhuria na hatimaye kuadhimisha Ibada ya kufunga rasmi maadhimisho haya, Dominika tarehe 25 Septemba 2022, kwenye Uwanja wa Michezo wa “XXI Settembre.” Yaani “Septemba 21.” Pamoja na mambo mengine, Baba Mtakatifu atakutana na kuzungumza na kundi la wakimbizi na wahamiaji; ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na hatimaye, kuongoza Sala ya Malaika wa Bwana.

Maadhimisho ya Kongamano la 27 la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Italia yanakita mizizi yake katika: Umoja, Ushiriki na Utume wa Kanisa mintarafu wongofu wa kiikolojia, kichungaji na kitamaduni. Baba Mtakatifu anatarajiwa pia kubariki na kuzindua rasmi Jengo Bwalo la Don Giovanni Melle, ambalo limejengwa kama kielelezo cha mshikamano wa udugu wa upendo na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kwa upande wake, Kardinali Matteo Maria Zuppi, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Bologna ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, anamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuamua kusindikizana na watu wa Mungu nchini Italia katika hija ya maisha yao ya kiroho, ili kuonja ladha ya Mkate kwa Kanisa la Kiekaristi na Kisinodi. Hii ni fursa ya kuadhimisha kumbukizi la Miaka 60 tangu Mababa wa Kanisa walipoadhimisha Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Haya yatakuwa ni mapambazuko ya Pentekoste mpya, ili kuonja: uzuri na utakatifu wa maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Haya ni mapambazuko ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi linalosimikwa katika Injili ya matumaini na Amani.

Umoja, ushiriki na utume ni muhimu katika kujenga Kanisa la Kisinodi
Umoja, ushiriki na utume ni muhimu katika kujenga Kanisa la Kisinodi

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa kufunga Kongamano la 51 la Ekaristi Takatifu Kimataifa huko nchini Ufilippini aliwatakia wajumbe wote imani thabiti na upendo kwa Kristo Yesu anayeendelea kuwepo katika Ekaristi Takatifu, ili kweli waweze kuwa ni Wamisionari na wafuasi amini wa Kristo; kwa kujenga na kudumisha umoja wa Kanisa sanjari na kuendeleza ari na mwamko wa kimisionari katika Makanisa mahalia. Ekaristi Takatifu iwe ni chachu ya: haki, upatanisho na amani duniani kote. Ekaristi Takatifu iwe ni shule ya huduma ya unyenyekevu, tayari kujisadaka kwa ajili ya wengine; kiini cha umisionari na ufuasi wa Kristo. Waamini wawe mstari wa mbele kuonesha mshikamano wa udugu wa upendo na wema; wapanie daima kujenga maisha yao, kielelezo cha nguvu ya Ekaristi Takatifu inayopyaisha maisha na kubadili mioyo ya waamini, tayari kuwahudumia na kuwalinda maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Ni mwaliko kwa waamini kujitahidi kuwa wakamiliifu kama Baba yao wa mbinguni alivyo mkamilifu kwa kupinga ukosefu wa haki kwa kusimama kidete dhidi ya rushwa na ufisadi; mambo yanayovuruga umoja, mshikamano na mafungamano ya kijamii na matokeo yake ni kusigina, utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Papa Francisko tarehe 25 Septemba 2022 anafunga Kongamano la 27 la Ekaristi Takatifu Italia
Papa Francisko tarehe 25 Septemba 2022 anafunga Kongamano la 27 la Ekaristi Takatifu Italia

Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu iwasaidie waamini kuwa ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake; mahali pa katekesi endelevu katika maisha ya kiroho, kama ilivyokuwa kwa wale wanafunzi wa Emau, waliobahatika kufafanuliwa Maandiko Matakatifu na hatimaye, wakamtambua Kristo Yesu kwa kuumega Mkate. Mama Kanisa anatukumbusha kwamba, Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Sadaka; Shukrani na masifu kwa Mungu Baba; Ni kumbukumbu ya sadaka ya Kristo na ya Mwili wake; Kanisa ni kielelezo cha uwepo wa Kristo kwa nguvu ya Neno na Roho wake Mtakatifu. Ekaristi Takatifu ni Fumbo la Imani na kutokana na ukuu wake, tunaweza kuthubu kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Thoma, Bwana wangu na Mungu wangu! Mama Kanisa anataka kuwa kweli ni chombo cha haki, amani, umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Maadhimisho ya Makongamano ya Ekaristi Takatifu katika ngazi mbalimbali za maisha na utume wa Kanisa yawe ni chachu ya kupyaisha maisha na utume wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Ekaristi Takatifu ni kumbu kumbu endelevu ya Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu, changamoto na mwaliko kwa waamini kuifia dhambi na kuanza kujikita katika mchakato wa wongofu na utakatifu wa maisha.

Kongamano la Ekaristi Takatifu Italia
09 July 2022, 16:26