Tafuta

Maadhimisho ya Siku ya 108 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani, Dominika tarehe 25 Septemba 2022 Maadhimisho ya Siku ya 108 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani, Dominika tarehe 25 Septemba 2022  

Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani 25 Septemba, 2022: Mshikamanano wa Kidugu

Waamini wadumishe Ufalme wa Mungu kadiri ya mpango wa Mungu, ambamo kila mtu anapata nafasi ya kushiriki na kuheshimiwa. Hapa ni mahali ambapo wakimbizi, wahamiaji watu wasiokuwa na makazi maalum; waathirika wa biashara ya binadamu; waathirika wa mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo, wanaweza kuishi kwa amani na utu wao kuheshimiwa na wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Siku ya 108 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani, Dominika tarehe 25 Septemba 2022 yananogeshwa na kauli mbiu “Kujenga mustakabali wa wakimbizi na wahamiaji” kwa “Maana hapa hatuna mji udumuo, bali twautafuta ule ujao.” Ebr 13:14. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa maadhimisho haya anakazia kuhusu: Hatima ya maisha ya mwanadamu, mbingu na nchi mpya, kujenga mustakabali wa wakimbizi na wahamiaji; mchango wao; Yerusalemu mpya ni kwa wote pasi na ubaguzi; mchango maalum wa vijana na mwishowe ni sala kwa ajili ya waamini. Baba Mtakatifu mara baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, Kongamano la 27 la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Italia kuanzia tarehe 22 hadi tarehe 25 Septemba 2022, huko mjini Matera, ambayo yamenogeshwa na kauli mbiu: “Torniamo al gusto del pane. Per una Chiesa Eucaristica e Sinodale” "Turudi Kwenye Ladha ya Mkate. Kwa Kanisa la Kiekaristi na Kisinodi" amezungumzia kuhusu Siku ya 108 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani.

Siku ya 108 ya wakimbizi na wahamiaji duniani 2022
Siku ya 108 ya wakimbizi na wahamiaji duniani 2022

Baba Mtakatifu anawataka waamini kujenga na kudumisha Ufalme wa Mungu kadiri ya mpango wa Mungu, ambamo kila mtu anapata nafasi ya kushiriki na kuheshimiwa. Hapa ni mahali ambapo wakimbizi, wahamiaji na wale wote wanaotafuta hifadhi ya kisiasa; watu wasiokuwa na makazi maalum; waathirika wa biashara ya binadamu na viungo vyake; waathirika wa mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo, wanaweza kuishi kwa amani na utu wao kuheshimiwa na wote. Hii ni kutokana na sababu kwamba, Ufalme wa Mungu unajengwa kwa kuwahusisha wote bila kuwatenga wala kuwabagua. Ni kwa njia ya uwepo na ushiriki wao, jumuiya mahalia anasema, Baba Mtakatifu Francisko, zinaweza kukua na kushamiri kama “mtende wa Lebanon” katika masuala ya kijamii, kiuchumi, kitamaduni na maisha ya kiroho. Amana ya mila, desturi na tamaduni njema kutoka kwa wakimbizi na wahamiaji ni chachu muhimu sana ya maboresho ya maisha ya watu wa Mungu. Huu ni mwaliko kwa watu wote kujibidiisha kujenga jamii shirikishi na inayosimikwa katika udugu wa kibinadamu. Sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji inajikita katika mambo makuu manne yaani: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi na usalama wa maisha!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, mwanadamu hapa duniani ni msafiri anayeuendea Ufalme wa Mungu ulioanzishwa na Kristo Yesu na utimilifu wake ni pale atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu. Lakini Ufalme huu, uko kati ya waja wake lakini utapata utilimifu wake katika utukufu wa Kristo. Huu ni mji ambao umejengwa na Mwenyezi Mungu na kila mtu anashirikishwa kwa namna ya pekee. Lakini bado kuna changamoto kubwa kuweza kuifikia Yerusalemu mpya; maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu. Rej Ufu 21:3. Ni katika muktadha wa machafuko ya kisiasa yaliyojitokeza katika miaka ya hivi karibuni, watu wa Mungu wanahimizwa kujibidiisha kujenga mji wa Mungu kadiri ya mpango wa Mungu, ili watu waweze kuishi kwa amani na utu wema. Kama ilivyo ahadi ya Mwenyezi Mungu, tunatazamia mbingu mpya na nchi mpya, ambayo haki yakaa juu yake. Rej 2Pet 3: 13. Haki ni kati ya vifaa muhimu sana vya ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Hii ni haki inayosimikwa katika: uvumilivu, sadaka na uthubutu ili wale wenye njaa na kiu ya haki waweze kutoshelezwa, kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, ndiye asili ya wema wote na hivyo binadamu anarejea tena kuwa mwema.

Waamini wajenge na kudumisha mshikamano wa upendo na udugu
Waamini wajenge na kudumisha mshikamano wa upendo na udugu

Lakini jambo la msingi, ni kukubali wokovu ulioletwa na Kristo Yesu na kusimikwa katika Injili ya Upendo, ili “kufyekelea mbali” mifumo yote ya ukosefu wa haki na ubaguzi. Mpango wa Mungu ni shirikishi na hasa kwa wale wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya kijamii, kati yao anasema Baba Mtakatifu ni wakimbizi, wahamiaji na wale wote wanaotafuta hifadhi ya kisiasa; watu wasiokuwa na makazi maalum pamoja na waathirika wa mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo. Hawa ndio wale watakaourithi Ufalme wa mbinguni ambao umeandaliwa kwa ajili yao. Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanamwilisha ndani mwao matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kama kielelezo cha imani tendaji. Kwani katika hukumu ya mwisho, waamini wataulizwa jinsi walivyojibidiisha: kuwalisha wenye njaa, kuwanywesha wenye kiu, kuwakaribisha wageni; kuwavika walio uchi, kuwatazama wagonjwa na kuwatembelea wafungwa kifungoni. Rej Mt 25: 34-36. Baba Mtakatifu Francisko anasema “Kujenga mustakabali wa wakimbizi na wahamiaji” ni kutambua na kuthamini mchango unaoweza kutolewa na wakimbizi na wahamiaji katika ujenzi wa nchi inayowapatia hifadhi, kwani hawa pia ni wajenzi wa Yerusalemu mpya inayoangazwa na Mwenyezi Mungu na wageni watajenga kuta zake na malango yake yatakuwa wazi daima, ili watu wote wapate kuleta utajiri wa Mataifa yao. Rej Isa 60: 10-11.

Utabiri huu, uzoefu na mang’amuzi yanaonesha kwamba, wakimbizi na wahamiaji wamechagia kwa kiasi kikubwa katika mchakato wa ukuaji wa kiuchumi na kijamii.  Ni watu ambao wamechangia nguvu kazi, ujana wao, ari na mwamko mpya. Wanaweza kuendelea kuchangia zaidi, ikiwa kama watapatiwa fursa. Baba Mtakatifu Francisko anakiri kwamba, wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji ni changamoto na fursa ya ukuaji kitamaduni na kiroho, kwa watu wote; kwa kutambua na kuheshimu tofauti msingi zinazojitokeza; ili kujenga na kuimarisha ushirika. Kwa kuendelea kuwa wazi kati yao ili kupata maono na mapokeo tofauti na hatimaye, kuwa na mwelekeo mpya; kwa kutambua na kuthamini amana na utajiri unaofumbatwa katika dini za waamini wengine, tasaufi ambazo pengine ni mpya, kiasi cha kusaidia kuzamisha mizizi ya imani yao. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Yerusalemu mpya ni kwa ajili ya watu wote. Uzoefu unaonesha kwamba, wakimbizi na wahamiaji wakatoliki wamesaidia sana kupyaisha jumuiya za Kikristo zilizowapokea na kuwakaribisha kwa upendo. Wamekuwa ni chachu ya maboresho ya maadhimisho ya Mafumbo mbalimbali ya Kanisa, kiasi cha waamini wote kujisikia kuwa ni sehemu ya ukatoliki wa watu wa Mungu.

Wakimbizi na wahamiaji wanachangia katika ustawi na maendeleo ya wengi
Wakimbizi na wahamiaji wanachangia katika ustawi na maendeleo ya wengi

Ikiwa kama waamini wanataka kushiriki na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya ujenzi wa mustabakali wa mwanadamu kwa siku za usoni, hawana budi kushirikiana na wakimbizi na wahamiaji na kwamba, kipaumbele cha pekee, wapewe vijana wa kizazi kipya. Mustakabali wa kesho, unaanza leo kwa kufanya maamuzi, ili kutekeleza mpango wa Mungu katika mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika haki, udugu wa kibinadamu na amani. Baba Mtakatifu katika sala yake kwa waamini anawataka wawe vyombo na mashuhuda wa matumaini na haki katika mchako wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu na kwamba, inapendeza kuishi vyema kama ndugu wamoja!

Wakimbizi 2022
25 September 2022, 15:24